read

Aya 55 – 68: Watu Wa Peponi Na Watu Wa Motoni

Maana

Hakika watu wa Peponi leo wamo shughulini, wamefurahi. Wao na wake zao wamo katika vivuli wameegemea juu ya viti vya fahari. Watapata humo kila namna ya matunda na watapata kila watakachokitaka.

Anachotamani mtu zaidi ni siha, amani, utulivu wa moyo kutokana na tabu na mihangaiko na kupata kuburudika na chakula na kinywaji, maskani, mavazi, kustarehe na wanawake na kuwa na bustani yenye miti na mito. Haya yote yanapatikana Peponi.

Zaidi ya hayo ni Salaam! Ndiyo kauli itokayo kwa Mola Mwenye kurehemu.

Salaam ya Mwenyezi Mungu ni amani na rehema. Na radhi yake ndio ukomo wa wema na neema. Ndio maana Imam Ali (a.s.) akasema: “Kila neema isiyokuwa Pepo ni upuzi na kila balaa isiyokuwa moto ni faraja.”

Na jitengeni leo enyi wakosefu.

Wakosefu walikuwa duniani wakijionyesha ni watu wema, wakivaa nguo za utawa na kuchanganyika na watu wa takua na wa heri. Hali halisi haikuwa ikijulikana na watu wengi. Ama leo – siku ya hukumu na malipo, Mwenyezi Mungu atawaweka mbali na watu wema na kuwaambia, ingieni motoni pamoja na watakaoingia: “Watajulikana wakosefu kwa alama zao, basi watashikwa kwa nywele za utosi na kwa miguu” (55:41).

Je, sikuagana nanyi, enyi wanadamu, kuwa msimuabudu Shet’ani? Hakika yeye ni adui dhahiri kwenu.

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) aliwahadharisha waja kutokana na shetani na wasiwasi wake na akwakataza wasimtii; akawaongoza kwenye njia ya heri na uongofu. Lakini wengi wamemtii Shetani na kumuasi Mwingi wa rehe- ma. Hili ameliashiria kwa kusema:

Na ya kwamba mniabudu Mimi? Hii ndiyo Njia iliyonyooka.

Na hakika yeye amewapoteza viumbe wengi miongoni mwenu. Je, hamkuwa mkitia akili?

Kila mwenye kufuata njia ya walioangamia baada ya kuhadharishwa na kuonywa, basi huyo ni katika vipofu wa nuru ya akili na muongozo wake. Wala hakuna malipo ya mfano huu isipokuwa adhabu ambayo amaeiashiria Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kwa kusema:

Hii ndiyo Jahannamu mliyokuwa mkiahidiwa, kupitia midomoni mwa mitume; mkaidharau na mkawadharau. Basi Ingieni leo kwa vile mlivyokuwa mkikufuru, na huu ndio mwisho wa kila mpotevu na aliyepitukamipaka.

Leo tunaviziba vinywa vyao, na iseme nasi mikono yao, na itoe ushahidi miguu yao kwa waliyokuwa wakiyachuma.

Kila kiungo cha muasi kesho kitatamka kumtolea ushahidi mtu wake yale maovu aliyoyafanya. Mkono utatoa ushahidi kwa ulivyopiga, kuiba, kuandika na kuashiria. Mguu kwa ulivyohangaika. Jicho kwa lililoona n.k. Unaweza kuuliza: Utachanganya vipi kauli hii ‘Tutaziba vinywa vyao’ na ile isemayo:

يَوْمَ تَشْهَدُ عَلَيْهِمْ أَلْسِنَتُهُمْ{24}

“Siku ambayo zitawashuhudia ndimi zao” Juz. 18 (24:24).

Ambapo ya kwanza imekanusha kutamka na hii ikathibitisha.

Jibu: Kesho waja watakuwa wana hali tofauti, wengine wataruhisiwa kuzungumza na wengine hawataruhusiwa:

يَوْمَ يَأْتِ لَا تَكَلَّمُ نَفْسٌ إِلَّا بِإِذْنِهِ ۚ {105}

“Siku itakapofika, nafsi yoyote haitasema ila kwa idhini yake.” Juz. 13 (11:105).

Na lau tungelipenda tungeliyafutilia mbali macho yao, wakawa wanaiwania njia. Lakini wangeionaje? Na lau tungelitaka tungewageuza hapo hapo walipo, basi wasingeweza kwenda wala kurudi.

Makusudio ya kufutilia mbali macho yao ni kuwa kipofu. Maana ni lau Mwenyezi Mungu angelitaka kuwaadhibu wakosefu dunianai angeliwapofusha macho yao na wasingeweza kuongoka na angeliwageuza wakawa wameganda bila ya kuwa na harakati wala uhai.

Na tunayempa umri tunampindua katika umbo. Basi je! hawatii akilini?

Kupindua kitu ni kukifanya juu chini. Binadamu kila anavyoendelea kuwa na umri mrefu anarudi nyuma: anakuwa mdhaifu baada ya kuwa na nguvu.

Lengo la ubainifu huu ni kuashiria kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amempa maisha ya kutosha ili aongoke na afanye mambo mema. Na lau angelipewa umri zaidi ya kawaida, basi maradhi yangelimweka chini, na umri mrefu ungelikuwa ni balaa na shari:

أَوَلَمْ نُعَمِّرْكُمْ مَا يَتَذَكَّرُ فِيهِ مَنْ تَذَكَّرَ وَجَاءَكُمُ النَّذِيرُ ۖ فَذُوقُوا فَمَا لِلظَّالِمِينَ مِنْ نَصِيرٍ {37}

“Je, hatukuwapa umri wa kutosha kukumbuka mwenye kukumbuka, na akawajia mwonyaji? Basi onjeni Na madhalimu hawana wa kuwanusuru” Juz. 22 (35:37).

وَمَا عَلَّمْنَاهُ الشِّعْرَ وَمَا يَنْبَغِي لَهُ ۚ إِنْ هُوَ إِلَّا ذِكْرٌ وَقُرْآنٌ مُبِينٌ {69}

Wala hatukumfundisha mashairi, wala hayatakikani kwake hayo. Haukuwa huu ila ni ukumbusho na Qur’an inayobainisha.

لِيُنْذِرَ مَنْ كَانَ حَيًّا وَيَحِقَّ الْقَوْلُ عَلَى الْكَافِرِينَ {70}

Ili imwonye aliye hai, na ihakikike kauli juu ya makafiri.