read

Aya 69 – 70: Hatukumfundisha Mashairi

Maana

Maadui wa Mwenyezi Mungu walijaribu kwa nyenzo zote kumkadhibisha Muhammad (s.a.w.). Miongoni mwazo ni kauli yao kuwa ni mwenda wazimu, lakini mmoja wao, Walid bin Al-Mughira, aliyekufa akiwa kafiri, akasema: “Hapana, hakika kauli yake – yaani Qur’an – ina utamu na ina mvuto na kwamba juu yake kuna matunda na chini yake kumejaa. Hakika iko juu na haishindwi.” Basi wakabadilisha kumtusi na wazimu na kusema: “Huyu ni mchawi muongo” (38:4.) Ilipowabainikia kuwa wao ndio waongo wakasema ni kuhani anakosea na anapatia au ni malenga mwenye kutunga mashairi kwa mawazo.

Ilivyo hasa ni kuwa kutuhumu kwao kuwa Mtume (s.a.w.) ni mshairi kunafahamisha kwamba mashairi kwa waarabu si lazima yawe na vina na uzani, bali yana upana zaidi. Ni fani iliyo na uzuri wake; iwe na uzani au la. Hali ni hiyo hiyo hata kwa wanafalsafa wa kale.

Mwenye Tafsir Ruhul-bayani amesema: “Mashairi ya watu wa kale hayakuwa na uzani wala vina wala hivyo sio nguzo ya ushairi.” Fikra hii imeenea leo kwenye somo la fasihi na uchambuzi.
Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amewarudi wanaomtuhumu Mtume Mtukufu kuwa ni mshairi au kuhani kwenye Aya nyingi; miongoni mwazo ni:

إِنَّهُ لَقَوْلُ رَسُولٍ كَرِيمٍ {40}

وَمَا هُوَ بِقَوْلِ شَاعِرٍ ۚ قَلِيلًا مَا تُؤْمِنُونَ {41}

وَلَا بِقَوْلِ كَاهِنٍ ۚ قَلِيلًا مَا تَذَكَّرُونَ {42}

“Kwa hakika hiyo ni kauli ya Mtume mwenye heshima. Wala si kauli ya mshairi. Ni machache mnayoamini, wala si kauli ya kuhani. Ni machache mnayokumbuka. (69:40 42).

Na wewe kwa neema ya Mola wako si kuhani wala mwendawazimu. Au wanasema ni mshairi (52:29 – 30).

Na wakisema:

وَيَقُولُونَ أَئِنَّا لَتَارِكُو آلِهَتِنَا لِشَاعِرٍ مَجْنُونٍ {36}

“Hivi tuiache miungu yetu kwa ajili ya huyu mshairi mwendawazimu?” (37:36).

“Bali huyo ni mshairi.” Juz. 17 (21:5). Aya hizi tulizo nazo:

Wala hatukumfundisha mashairi, wala hayatakikani kwake hayo. Haukuwa huu ila ni ukumbusho na Qur’an inayobainisha. Ili imwonye aliye hai, na ihakikike kauli juu ya makafiri.

Makusudio ya aliye hai hapa, ni yule ambaye akili yake iko hai kiuzingatiaji, kutaamali na kufungua moyo wake kwa haki na kheri. Na makusudio ya kauli hapa ni adhabu; sawa na kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:

وَلَٰكِنْ حَقَّتْ كَلِمَةُ الْعَذَابِ عَلَى الْكَافِرِينَ {71}

“Lakini limekwishahakika neno la adhabu juu ya makafiri.” (39:71).

Washirikina walisema kuwa Qur’an aliyokuja nayo Muhammad si chochote ila ni mashairi yanayoelezea fikra yake na mawazo yake; na wala sio wahyi kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Ndipo Mwenyezi Mungu (s.w.t.) akawarudi, kwa kuwaambia, kuwa shairi linajikita zaidi kwenye fikra hawa na mapendeleo ya mshairi; anamtetea anayempenda hata kama hana haki na anapamabana na anayemchukia hata kama ana haki. Na Qur’an ni kauli yenye hadhi na ya upambanuzi, na wala si kauli ya hawa na mzaha.

Ni Kitabu cha itikadi na sharia, maadili na mawaidha, ndani yake mna ilimu na fikra. Sasa wapi na wapi ushairi na hayo.

Kama ingelikuwa Qur’an imetengenezwa na Muhammad (s.a.w.), angeliweka humo machungu yake na huzuni yake, maisha yake na maazimio; sawa na walivyo malenga.

Kilichobakia ni kudokeza kuwa; hata hivyo Mtume (s.a.w.) alikuwa akithamini na akiheshimu ushairi, kama fani iliyo na athari nzuri katika kuelezea mapendeleo na matakwa ya watu na amani yao.

Kuna kauli mshuhuri aliyoisema: “Katika baadhi ya ubainifu kuna uchwi na katika baadhi ya mshairi kuna hekima.” Alikuwa akiwaombea tawfiki malenga wanaoipigania haki na watu wa haki.

Aliwahi kumvulia kashida yake Ka’ab bin Zuheir kwa kumtuza, pale alipomsifu kwa kaswida yake iliyo maarufu kwa jina la Burda (kashida); miongoni mwa beti zake ni:

Haki ni nuru rasuli, kwaye twaangaziwa, Upanga wenye makali, wa Mola umechomozwa.

Tazama Juz. 22 (36:4) kifungu cha ‘Mdundo wa ndani katika Qur’an’ na Juz.19(26:224).

أَوَلَمْ يَرَوْا أَنَّا خَلَقْنَا لَهُمْ مِمَّا عَمِلَتْ أَيْدِينَا أَنْعَامًا فَهُمْ لَهَا مَالِكُونَ {71}

Je! Hawaoni kwamba tumewaumbia kutokana na iliyofanya mikono yetu wanyamahowa, na wao ni wenye kuwamiliki.

وَذَلَّلْنَاهَا لَهُمْ فَمِنْهَا رَكُوبُهُمْ وَمِنْهَا يَأْكُلُونَ {72}

Na tumewatiisha kwao. Basi baadhi yao wako wanaowapanda, na baadhi yao wanawala.

وَلَهُمْ فِيهَا مَنَافِعُ وَمَشَارِبُ ۖ أَفَلَا يَشْكُرُونَ {73}

Na wao wanapata kwao manufaa na vinywaji. Basi je, hawashukuru?

وَاتَّخَذُوا مِنْ دُونِ اللَّهِ آلِهَةً لَعَلَّهُمْ يُنْصَرُونَ {74}

Na wameishika miungu mingine badala ya Mwenyezi Mungu wapate kusaidiwa!

لَا يَسْتَطِيعُونَ نَصْرَهُمْ وَهُمْ لَهُمْ جُنْدٌ مُحْضَرُونَ {75}

Hawataweza kuwasaidia. Bali hao ndio jeshi lao watakaohudhurishwa.

فَلَا يَحْزُنْكَ قَوْلُهُمْ ۘ إِنَّا نَعْلَمُ مَا يُسِرُّونَ وَمَا يُعْلِنُونَ {76}

Basi isikuhuzunishe kauli yao, hakika Sisi tunayajua wanayoyaweka siri na wanayoyatangaza.