read

Aya 1 – 10: Wanaojipanga Safu

Maana

Naapa kwa wanaojipanga safu-safu. Na kwa wenye kuzuia sana. Na kwa wenye kusoma Ukumbusho.

Wametofautiana wafasiri katika maana ya wanaojipanga safu, wenye kuzuia na wenye kusoma ukumbusho. Kuna waliosema kuwa ni Malaika.

Wengine wakasema ni waumini wanaokaa safu katika Swala ya jamaa na katika jihadi. Na wenye kuzuia ni makatazo ya Qur’an na Aya zake. Na wenye kusoma ni wasomaji wa Qur’an kwenye Swala na kwengineko.

Sio mbali kuwa makusudio ni aina tatu alizozitaja Imam Ali (a.s.) katika khutba ya kwanza kwenye Nahjul-Balagha, katika wasifu wa Malaika: “Miongoni mwao kuna ambao wamesujudu na wala hawarukui, na kuna waliorukuu na wala hawasimami, kuna waliosimama katika safu na wala hawatawanyiki.” Aliposema: ‘Kuna waliosimama katika safu na wala hawatawanyiki’ inawezekana kuwa ni ishara ya kauli yake Mwenyezi Mungu: “Naapa kwa wanao jipanga safu-safu.”

Kisha Imam Ali (a.s.) akaendelea kusema: “ Miongoni mwao kuna waaminifu wa wahyi wa Mungu, na ni ndimi zitamkazo kwa mitume Wake;” yaani wanaoshuka na wahyi kwa mitume wake; kama vile Jibril (a.s.). Kauli hii nayo ina uwezekano wa kuwa ni ishara ya kauli ya Mwenyezi Mungu: “Na kwa wenye kusoma Ukumbusho.” Kwa sababu wao wanasoma Kitabu cha Mwenyezi Mungu wakati wanapofikisha kwa Mitume.

Akaendelea kusema: “Na miongoni mwao kuna wahifadhi wa waja wake.” Sheikh Muhammad Abduh, katika kuwaelezea hawa, anasema: “Kama kwamba wao ni nguvu inayotiwa katika miili ya binadamu na katika nafsi zao; akiwahifadhi Mwenyezi Mungu binadamu wasiangamie kwa Malaika. Na lau si hivyo, maangamizi yangelikuwa yanamwandama mtu zaidi kuliko amani.”

Sheikh, katika kuleta picha hii, anakusudia kurahisisha kufahamu jinsi Malaika wanavyohifadhi waja; akisema: “Kama kwamba wao.”

Kwa hiyo basi inawezekana hilo linaashiria kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: “Na kwa wenye kuzuia sana,” ikiwa tutasema kuwa kuzia hapa maana yake ni kuzuia udhia kwa waja.

Hakika Mungu wenu bila ya shaka ni Mmoja. Mola wa mbingu na ardhi, na vilivyomo kati yake, na ni Mola wa mashariki zote.

Makusudio ya mashariki1 zote ni mashariki ya Jua kwa kuangalia kwamba kila siku linatokeza mashariki na kutua magharibi. Mwenyezi Mungu amekata kuwa Yeye ni mmoja hana mshirika katika kuumba na kupangilia.

Mwenyezi Mungu Na Kuapa Na Viumbe Vyake

Unaweza kuuliza: Kwa nini Mwenyezi Mungu ameapa kwa Malaika?

Wafasiri wamejibu kuwa Mwenyezi Mungu ameapa kwa Malaika kujulisha ukuu wa daraja na umuhimu wao. Hili ndio jawabu lao kwa kila alichoapia Mwenyezi Mungu; iwe ni wakati, mahali au chochote kilichoko juu au chini. Hata hivyo mwenye Dhilal ameunganisha kuapa huku na kauli ya watu wa jahiliya waliosema kuwa Malaika ni mabinti wa Mungu; kama alivyosema Mwenyezi Mungu:

أَفَأَصْفَاكُمْ رَبُّكُمْ بِالْبَنِينَ وَاتَّخَذَ مِنَ الْمَلَائِكَةِ إِنَاثًا ۚ إِنَّكُمْ لَتَقُولُونَ قَوْلًا عَظِيمًا {40}

“Je, Mola wenu amewachagulia waototo wa kiume na yeye akajichukulia watoto wa kike katika Malaika? Hakika nyinyi mnasema kauli kubwa.” Juz. 15 (17:40).

Akasema mwenye Dhilal: Lengo la kuapa kwa Malaika ni kuwarudi wenye kuamini upotofu huu alioita Mwenyezi Mungu ‘kauli kubwa.’

Tuanavyo sisi ni kuwa Mwenyezi Mungu anaapa na kitu chochote kile kwa lengo moja tu – kuwa kila kilichopo kwa asili yake kinafahamisha kuwa Mwenyezi Mungu ni mmoja hana mshirika.

Hakuna mwenye shaka kuwa Malaika wanaopanga safu na wasiopanga safu wanamwabudu Mwenyezi Mungu na kumtii kwa ujuzi na yakini na kwa utumishi wao. Kwa hiyo kujua kwao hivi ni dalili mkataa kuwa Yeye ni mmoja hana mshirika katika kuuumba umiliki na upangiliaji; sawa na kujua wataalamu hakika ya maudhui waliyoyagundua na kuyafanyia majaribio.

Hakika Sisi tumeipamba mbingu ya dunia (karibu) kwa pambo la nyota.

Makusudio ya mbingu ni anga ya juu na dunia ni dunia yetu sisi binadamu2, sio ulimwengu wote. Makusudio ya nyota ni zile zilizo kwenye anga iliyo karibu zaidi na sisi. Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amejaalia nyota, jinsi ziliyvo na mwanga wake katika anga yetu, kuwa ni pambo na urembo; mbali ya manufaa na faida zake:

وَهُوَ الَّذِي جَعَلَ لَكُمُ النُّجُومَ لِتَهْتَدُوا بِهَا فِي ظُلُمَاتِ الْبَرِّ وَالْبَحْرِ ۗ{97}

“Na yeye ndiye aliyewafanyia nyota ili muongoke kwazo katika viza vya bara na baharini. Juz. 7 (6:97).

Na kuilinda na kila shetani muasi wasiweze kuwasikiliza viumbe watukufu. Na wanafukuzwa huko kila upande, wakifurushwa. Na wanayo adhabu ya kudumu. Isipokuwa anayenyakua kitu kidogo, na mara humfuatia kimondo kinacho ng’ara.

Misamiati ya Aya hii iko wazi, isipokuwa miwili-Shetani asi na viumbe watukufu. Mwenyezi Mungu na Mtume wake wameinyamazia, hawaku- tubainishia. Nasi hatuwezi kufasiri bila ya ujuzi. Kwa hiyo tunasema kuwa Aya hizi ni katika zinazotatiza kwetu, lakini inawezekana kuwa ziko wazi kwa wenzetu.

Sio mbali kuwa sababu ya kunyamazia ni kuwa kumjua shetani huyu na kiumbe mtukufu hakuna uhusiano na maisha yetu au kuwa fahamu zetu zinashindwa kufahamu uhakika wake. Na mwenye elimu kadiri atakavyojitahidi, lakini hawezi kujua kila kitu; bali hawezi hata kujua kitu chochote katika vinavyomzunguka uhakika wake hasa kilivyo.

Kujua kwetu misamiati ya Aya; kama kimondo kinachong’ara, adhabu ya kudumu, kunyakua na kufuatiwa, hakuwezi kutosha kufasiri makusudio ya Aya kwa ujumla wake, maadamu hatujui uhakika wa shetani asi na viumbe watukufu.

Baadhi ya wafasiri wamesema makusudio ya shetani asi ni shetani jini. Wengine wakasema ni binaadamu ambaye hafikiri ukuu na utukufu wa nyota na kufahamisha kwake kuweko Mwenyezi Mungu. Masufi wanase- ma: Makusudio ya shetani ni picha na nguvu ya kuwazia. Yote hiyo ni kutupia kwa mbali. Ni afadhali kunyamaza kuliko kusema bila ya kujua. Mwenyezi Mungu anasema:

وَمَا أُوتِيتُمْ مِنَ الْعِلْمِ إِلَّا قَلِيلًا {85}

“Nanyi hamkupewa katika elimu ila kidogo tu.” Juz. 15 (17:85).

فَاسْتَفْتِهِمْ أَهُمْ أَشَدُّ خَلْقًا أَمْ مَنْ خَلَقْنَا ۚ إِنَّا خَلَقْنَاهُمْ مِنْ طِينٍ لَازِبٍ {11}

Hebu waulize: Je! Wao ni wenye umbo gumu zaidi au hao wengine tuliowaumba. Hakika Sisi tuliwaumba wao kwa udongo unaonata.

بَلْ عَجِبْتَ وَيَسْخَرُونَ {12}

Bali unastaajabu, na wao wanafanya maskhara.

وَإِذَا ذُكِّرُوا لَا يَذْكُرُونَ {13}

Na wanapokumbushwa hawakumbuki.

وَإِذَا رَأَوْا آيَةً يَسْتَسْخِرُونَ {14}

Na wanapoona Ishara, wanafanya maskhara.

وَقَالُوا إِنْ هَٰذَا إِلَّا سِحْرٌ مُبِينٌ {15}

Na husema: Haya si chochote ila ni uchawi ulio dhahiri.

أَإِذَا مِتْنَا وَكُنَّا تُرَابًا وَعِظَامًا أَإِنَّا لَمَبْعُوثُونَ {16}

Ati tukishakufa na tukawa udongo na mifupa ndio kweli tutafufuliwa?

أَوَآبَاؤُنَا الْأَوَّلُونَ {17}

Hata baba zetu wa zamani?

قُلْ نَعَمْ وَأَنْتُمْ دَاخِرُونَ {18}

Sema: Naam! Na hali nyinyi ni madhalili.

فَإِنَّمَا هِيَ زَجْرَةٌ وَاحِدَةٌ فَإِذَا هُمْ يَنْظُرُونَ {19}

Na hakika ni ukelele mmoja tu! Na hapo ndio wataona!

وَقَالُوا يَا وَيْلَنَا هَٰذَا يَوْمُ الدِّينِ {20}

Watasema: Ole wetu! Hii ndiyo Siku ya Malipo.

هَٰذَا يَوْمُ الْفَصْلِ الَّذِي كُنْتُمْ بِهِ تُكَذِّبُونَ {21}

Hii ndiyo Siku ya upambanuzi mliyokuwa mkiikadhibisha.

احْشُرُوا الَّذِينَ ظَلَمُوا وَأَزْوَاجَهُمْ وَمَا كَانُوا يَعْبُدُونَ {22}

Wakusanyeni waliodhulumu, na wenzao, na hao waliokuwa wakiwaabudu,

مِنْ دُونِ اللَّهِ فَاهْدُوهُمْ إِلَىٰ صِرَاطِ الْجَحِيمِ {23}

Badala ya Mwenyezi Mungu. Waongozeni njia ya Jahannamu!

وَقِفُوهُمْ ۖ إِنَّهُمْ مَسْئُولُونَ {24}

Na wasimamisheni. Hakika hao wataulizwa.

مَا لَكُمْ لَا تَنَاصَرُونَ {25}

Mna nini? Mbona hamsaidiani?

بَلْ هُمُ الْيَوْمَ مُسْتَسْلِمُونَ {26}

Bali leo, watasalimu amri.
  • 1. Neno mashariki ni la kiarabu lenye maana ya matokeo ya jua (mawiyo) na magharibi ni machweo - Mtarjumu
  • 2. Ndio maana wafasiri wengi wa Kiswahili wamelifasiri neno hilo kwa ‘karibu’ wakimaanisha karibu yetu sisi. - Mtarjumu