read

Aya 50 – 68: Kwa Mfano Wa Haya Nawafanye Wafanyao

Maana

Tena watakabilaiana wao kwa wao wakiulizana.

Bado maneno yanaendelea kuhusu watu wa Peponi. Katika Aya iliyotangulia, Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amesema kuwa watu wa Peponi watakuwa na aina mbali mbali za starehe.

Katika Aya hii anasema kuwa watazungumziana wao kwa wao, huku wakiwa na furaha, kuhusiana na maisha yao ya duniani. Miongoni mwayo ni:

Aseme msemaji miongoni mwao: Hakika mimi nilikuwa na rafiki aliyekuwa akiniambia: Hivyo wewe ni katika wanaosadiki ati tukishakufa tukawa udongo na mifupa, ndio tutahisabiwa?

Mumin huyu atawazungumzia wenzake na jirani zake kuhusiana na vile waumini wa malipo ya kiyama walivyokuwa wakifanyiwa masikhara wakisema wasioamini, ati mamake fulani, kweli tukishakufa na kuisha kabisa tutafufuliwa tuwe hai?

Hivi ndivyo alivyo kila mlahidi. Na hiyo hasa inatokana na kuwa kuamini ufufuo ni sehemu ya kuamini wahyi wa Mwenyezi Mungu kwa yule aliyemteua katika waja wake. Ikiwa mlahidi haamini wahyi huu, ataweza kweli kuamini ufufuo baada ya mauti? Kwa maneno mengine ni kuwa ufufuo ni katika mambo ya ghaibu ambayo kwa mlahidi ni vigano tu.

Atasema: Je! Nyie mtachungulia?

Mumin ataendelea kuwaambia wenzake akiwaomba waangalie Jahnnam ili waone mwisho wa aliyekuwa na dharau.

Basi atachungulia amwone katikati ya Jahannamu.

Akishawaambia wenzake atachungulia kwenye Jahannam amwone jamaa yuko katikati ya Jahannam. Aseme - kwa kumtahayariza- Wallahi! Ulikaribia kuniangamiza. Yaani kunitia kwenye shaka kwa wasiwasi wako na shaka zako. Na lau si neema ya Mola wangu bila ya shaka ningelikuwa miongoni mwa waliohudhurishwa pamoja nawe katika moto.

Kisha mumin atawageukia wenzake awaambie:

Je! Sisi hatutakufa, isipokuwa kifo chetu cha kwanza? Wala sisi hatutaadhibiwa. Hakika huku, bila ya shaka, ndiko kufuzu kukubwa.

Atazungumza haya kwa furaha kutokana na aliyoyapata huku akisema alhamudulillah, tumepita mtihani vizuri, hakuna mauti tena wala tabu. Hakuna isipokuwa radhi za Mwenyezi Mungu na neema zake. Katika maana haya ni kauli yake Mwenyezi Mungu: “Hawataonja humo isipokuwa mauti ya kwanza na atawakinga na adhabu ya moto” (44:57).

Kwa mfano wa haya nawafanye wafanyao na washindane wanaoshindana.

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amewaachia waja matendo na amali, akawajibishia kufanya yale yaliyo na kheri nao na masilahi kwao; na akawakataza yale yaliyo na shari yao na ufisadi. Kisha akwaachia hiyari ya kufanya na kuacha. Mwenye kutii akamwahidi Pepo na mwenye kuasi akamwahidi adhabu ya kuunguza.

Hakuna mwenye shaka kuwa mwenye akili atajihurumia na kuchagua lililo na masilahi zaidi. Imeelezwa kwenye Nahjul-balagha: “Hakuna thamani ya nafsi zenu ispokuwa Pepo. Basi msiziuze ila kwayo.”

Je! Kukaribishwa hivi ni bora, au mti wa Zaqum? Hakika Sisi tumeufanya huo kuwa ni fitna kwa waliodhulumu.

Kukaribishwa hivi ni kukaribishwa kwenye neema. Makusudio ya fitna hapa ni adhabu. Ama mti wa Zaqum ameubanisha Mwenyezi Mungu kwa kusema:

Hakika huo ni mti unaotoka katikati ya Moto. Mashada yake ni kama vichwa vya mashetani. Basi hakika hao bila ya shaka wataku- la katika huo, na wajaze matumbo kwa huo.

Zaqqum ni kauli ya waarabu kwa chakula kinachochukiza kukila. Kwenye Tafsir Tabari kuna maelezo Haya: “Iliposhuka Aya hii Abu Jahl alisema kwa madharau: “Mimi nitawaletea Zaqqum.” Akaleta siagi na tende kisha akasema: Haya! Nyinyi kuleni Zaqqum. Basi hii ndio Zaqqum anayowatisha nayo Muhammad.

Vichwa vya mashetani, ni kinaya cha ubaya na mandhari ya kutisha ya huo mti. Yule anayesema kuwa Zaqqum ni nembo ya ubaya wa adhabu, hatuwezi kumpinga.

Kisha juu yake wapewe mchanganyiko wa maji ya moto.

Yaani watakula zaqqum na wanywe maji ya usaha; kama anavyosema Mwenyezi Mungu: “Nyuma yake iko Jahannam na atanyeshwa maji ya usaha uliochanganyika na damu” Juz.13 (14: 16).

Kisha hakika marejeo yao bila ya shaka yatakuwa kwenye Jahannamu.

Makusudio ya marejeo ni makazi ya mwisho na makao yao ya kudumu. Maana ni kuwa chakula chao ni Zaqqum na kinywaji chao ni maji moto. Ama kivazi chao, Mwenyezi Mungu amekiashiria kwa kusema:

سَرَابِيلُهُمْ مِنْ قَطِرَانٍ{50}

“Nguo zao zitakuwa za lami” Juz. 13 (14:50).

إِنَّهُمْ أَلْفَوْا آبَاءَهُمْ ضَالِّينَ {69}

Hakika waliwakuta baba zao wamepotea.

فَهُمْ عَلَىٰ آثَارِهِمْ يُهْرَعُونَ {70}

Na wao wakafanya haraka kufuata nyayo zao.

وَلَقَدْ ضَلَّ قَبْلَهُمْ أَكْثَرُ الْأَوَّلِينَ {71}

Na hakika walikwishapotea kabla yao wengi wa watu wa zamani.

وَلَقَدْ أَرْسَلْنَا فِيهِمْ مُنْذِرِينَ {72}

Na hakika tuliwapelekea waonyaji.

فَانْظُرْ كَيْفَ كَانَ عَاقِبَةُ الْمُنْذَرِينَ {73}

Basi tazama jinsi ulivyokuwa mwisho wa wale walioonywa.

إِلَّا عِبَادَ اللَّهِ الْمُخْلَصِينَ {74}

Isipokuwa waja wa Mwenyezi Mungu waliosafishwa.

وَلَقَدْ نَادَانَا نُوحٌ فَلَنِعْمَ الْمُجِيبُونَ {75}

Na hakika Nuh alituita, na Sisi ni bora wa waitikiaji.

وَنَجَّيْنَاهُ وَأَهْلَهُ مِنَ الْكَرْبِ الْعَظِيمِ {76}

Na tulimwokoa yeye na ahali zake kutokana na msiba mkubwa.

وَجَعَلْنَا ذُرِّيَّتَهُ هُمُ الْبَاقِينَ {77}

Na tuliwajaalia dhuriya zake ndio wenye kubakia.

وَتَرَكْنَا عَلَيْهِ فِي الْآخِرِينَ {78}

Na tukamwachia kwa walio baadaye.

سَلَامٌ عَلَىٰ نُوحٍ فِي الْعَالَمِينَ {79}

Amani kwa Nuh ulimwenguni kote!

إِنَّا كَذَٰلِكَ نَجْزِي الْمُحْسِنِينَ {80}

Kwa hakika hivyo ndivyo tunavyowalipa watendao mema.

إِنَّهُ مِنْ عِبَادِنَا الْمُؤْمِنِينَ {81}

Hakika yeye ni katika waja wetu walio waumini.

ثُمَّ أَغْرَقْنَا الْآخَرِينَ {82}

Kisha tukawagharikisha wale wengine.