Aya 12 – 20: Subiri Juu Ya Hayo Wanayosema
Maana
Walikadhibisha kabla yao kaumu ya Nuh, na kina A’adi na Firauni mwenye vigingi Na Thamud na kaumu ya Lut na watu wa mwituni.
Wote hawa waliwakanusha mitume; baadhi yao wakaangamizwa kwa tufani; kama vile watu wa Nuh, wengine kwa kuzama baharini, kama Firauni.
Kuwa na vigingi ni kinaya cha kujikita ufalme wake kama linavyokitwa hema na vigingi kwenye ardhi.
“Basi Thamud waliangamizwa kwa balaa kubwa (la ukelele wa adhabu). Ama A’d waliangamizwa kwa upepo mkali usiozuilika” (69:5-6).
Kaumu ya Lut majumba yao yalipinduliwa juu chini. Tazama Juz. 12 (11:82). Watu wa mwituni Mwenyezi Mungu aliwaadhibu adhabu chungu. Tazama Juz.14 (15:78) na Juz. 19 (26:176).
Hayo ndiyo makundi. Wote waliwakadhibisha Mitume; basi wakastahili adhabu yangu.
Mwenyezi Mungu aliviadhibu vikosi vya shetani kwa sababu ya madhambi yao; ikiwa ni malipo ya yale waliyoyafanya. Je, wanaomkadhibisha Muhammad (s.a.w.) hawahofii kuwafika yaliyowafika hao.
Na hawa hawangojei ila ukelele mmoja tu usio na muda.
Hawa ni waliomkadhibisha Muhammad (s.a.w.). Maana ni; wanangoja nini kwa Mungu baada ya kukukadhibisha ewe Muhammad na hali Mwenyezi Mungu, kwa neno moja tu anaweza kuwapelekea adhabu itayowafyeka katika muda ambao hawataweza kuusia wala kurudi kwa watu wao.
Na wao husema: Mola wetu! Tuletee upesi sehemu yetu kabla ya Siku ya Hisabu.
Yaani sehemu yetu ya adhabu. Mwenyezi Mungu (s.w.t.) aliwatishia na adhabu ya Jahannam kupitia kwa Mtume wake mtukufu, lakini wao wakasema kwa madharau kuwa ikiwa ni kweli basi anangoja nini mpaka siku ya Kiyama? Basi na iwe duniani sio akhera.
Subiri kwa wayasemayo, kuwa wewe ni mwongo na mengineyo ya uzushi. Kwani mwisho wa mambo yao ni hasara na kusalimu amri.
Mtume (s.a.w.) alisubiri na kuvumilia adha ya washirikina kwa muda wa mika 13 na vitimbi vya wanafiki kwa miaka kadhaa huko Madina. Alivumilia muda huu mrefu akiwa na mategemeo ya mustkabali hata kama utachelewa. Hazikupita siku Muhammad (s.a.w.) akashinda kwa msaada wa Mwenyezi Mungu, na akaudhihirisha uislamu kuliko dini zote, wajapochukia washirikina.
Na umkumbuke mja wetu Daud.
Hili ni jina la kiebrania lenye maana ya mpendwa (mahboob). Yeye alikuwa mfalme wa pili wa Kiyahudi, wa kwanza alikuwa Talut:
إِنَّ اللَّهَ قَدْ بَعَثَ لَكُمْ طَالُوتَ مَلِكًا ۚ {247}
Tawrat imemwita Talut huyu kwa jina la Shaul (Saulo). Imeelezwa kwenye Kamusi ya Kitabu kitakatifu’ kwamba Shaul ndiye mfalme wa kwanza wa waisrail na kwamba Daud alipigana katika jeshi lake. Razi anasema kuwa Mwenyezi Mungu amemsifu Daud kwa sifa nyingi. Kisha akazifafanua kwenye kurasa nne. Tutazifupiliza kwenye mistari ifuatayo: Mwenyezi Mungu alimwambia Muhammad (s.a.w.):
Subiri kwa wayasemayo, na umkumbuke mja wetu Daud.
Hii ni karama kwa Daud.
Mwenye nguvu; yaani mwenye nguvu ya kumtii Mwenyezi Mungu.
Hakika yeye alikuwa mwingi wa kutubia; yaani akiyarudisha mambo yote kwa Mwenyezi Mungu.
Hakika tuliidhalilisha milima pamoja naye ikisabihi jioni na asubuhi pamoja naye. Na pia ndege waliokusanywa makundi; wote walikuwa wanyenyekevu kwake.
Mfano wake ni kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:
يَا جِبَالُ أَوِّبِي مَعَهُ وَالطَّيْرَ ۖ {10}
وَسَخَّرْنَا مَعَ دَاوُودَ الْجِبَالَ يُسَبِّحْنَ وَالطَّيْرَ ۚ {79}
Kwa maelezo zaid kuhusu Daud rejea huko.
Na tukautia nguvu ufalme wake.
Na tukampa hikima.
Ambayo ni kukiweka kitu mahali pake. Kwa ibara ya Razi ni elimu na kuitumia. Imeitwa hivyo kwa sababu hekima ni kupanga mambo na kuyaweka sawa.
Na kukata hukumu.
Razi anasema ni uwezo wa kudhibiti maana na kuyatolea tafsiri ya upeo wa juu. Hivi ni zaidi ya tunavyofahamu kuwa kukata hukumu ni elimu ya kuhukumu, kwa uadilifu, mambo ya wanaoteta.
Hivi ndivyo Qur’an ilivyomsifu Daud kwa sifa bora za ukamilifu, lakini Tawrat imemsifu kwa sifa mbaya mbaya; kama dhulma, ufuska, hadaa na kunyanyag’anya wanawake; kiasi amabacho waliochangia kuweka kamusi ya Kitabu Kitakatifu wakasema katika ukurasa 365, chapa ya mwezi Machi 1967, ninanukuu: “Mara nyingine Daud aliweza kufanya mambo ya kufedheheshanayaaibu.”
وَهَلْ أَتَاكَ نَبَأُ الْخَصْمِ إِذْ تَسَوَّرُوا الْمِحْرَابَ {21}
إِذْ دَخَلُوا عَلَىٰ دَاوُودَ فَفَزِعَ مِنْهُمْ ۖ قَالُوا لَا تَخَفْ ۖ خَصْمَانِ بَغَىٰ بَعْضُنَا عَلَىٰ بَعْضٍ فَاحْكُمْ بَيْنَنَا بِالْحَقِّ وَلَا تُشْطِطْ وَاهْدِنَا إِلَىٰ سَوَاءِ الصِّرَاطِ {22}
إِنَّ هَٰذَا أَخِي لَهُ تِسْعٌ وَتِسْعُونَ نَعْجَةً وَلِيَ نَعْجَةٌ وَاحِدَةٌ فَقَالَ أَكْفِلْنِيهَا وَعَزَّنِي فِي الْخِطَابِ {23}
قَالَ لَقَدْ ظَلَمَكَ بِسُؤَالِ نَعْجَتِكَ إِلَىٰ نِعَاجِهِ ۖ وَإِنَّ كَثِيرًا مِنَ الْخُلَطَاءِ لَيَبْغِي بَعْضُهُمْ عَلَىٰ بَعْضٍ إِلَّا الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ وَقَلِيلٌ مَا هُمْ ۗ وَظَنَّ دَاوُودُ أَنَّمَا فَتَنَّاهُ فَاسْتَغْفَرَ رَبَّهُ وَخَرَّ رَاكِعًا وَأَنَابَ ۩ {24}
فَغَفَرْنَا لَهُ ذَٰلِكَ ۖ وَإِنَّ لَهُ عِنْدَنَا لَزُلْفَىٰ وَحُسْنَ مَآبٍ {25}