read

Aya 41 – 48: Ayyub

Maana

Na mkumbuke mja wetu Ayyub

Ayyub ana kitabu maalum katika Biblia kwenye agano la kale. Zimetumika karibu kurasa arubaini. Kwenye kamusi ya Kitabu kitakatifu imeandikwa kuwa kitabu hicho cha Ayyub mwanzo kiliandikwa kwa mashairi na kwamba baadhi wanaona kuwa kiliandikwa karne ya nne kabla ya Milad (Bc). Na kuna uwezekano kuwa aliishi milenia ya pili kabla ya Milad (Bc). Kisha wakasema waliochangia kuweka Kamusi ya Kitabu kitakatifu kuwa Ayyub aliishi katika nchi ya Usi. Inaaminika kuwa nchi hii iko katika jang- wa la Syria na wengine wanaamini ni Huran.

Alipomwita Mola wake akasema: Kwa hakika Shetani amenifikishia tabu na adhabu.

Watu wamekua wakipiga mfano wa masaibu ya Ayyub katika karne nyingi zilizopita, huku wakiongeza vigano vingi. Aya hii na ile iliyo katika Juz. 17 (21: 83), zinafahamisha kuwa Ayyub alipata masaibu ya hali na mali na kwamba yeye aliyanasabishia yaliyomfika kwa shetani. Hii ndio iliyowafanya jamaa katika wafasiri kutunga riwaya ya ‘Ayyub na shetani.’

Ukiunganisha riwaya zao na yale yaliyoelezwa kwenye Biblia utaona kuwa wao wanaifasiri Qur’an kwa Hadith za kiisrail.

Kwa ufupi ni kuwa Biblia na baadhi ya wafasiri wanasema kuwa Mwenyezi Mungu alimsalitia Ayyub shetani ili amjaribu imani yake. Akaangamiza mali yake na familia yake. Aliposhindwa akauingilia mwili, lakini pia akashindwa.

Ni kweli Aya inaelezea kuwa shetani alimpa Ayyub tabu na mashaka, laki- ni haikusema ni tabu na adhabu ya aina gani? Nasi tunayanyamazia yale aliyoyanyamazia Mwenyezi Mungu, wala hatujikalifishi kuyafanyia utafiti. Lau Mwenyezi Mungu angelitukalifisha angelibainisha. Na kwa kuwa hakuna ubainifu basi hakuna taklifa. Tumeashiria kisa cha Ayyub katika Juz. 17 (21:83 – 91).

Akaambiwa: Piga-piga ardhi kwa mguu wako! Hapa mahali baridi pa kuogea na kinywaji.

Makusudio ya mahali pa kuogea hapa ni maji. Ayyub alikimbila kwa Mwenyezi Mungu kumshtakia yaliyomfika. Mwenyezi Mungu akamwitikia na akamwamrisha apige ardhi kwa mguu wake, yatatoka maji baridi ya kuoga na kunywa, atapona kwa idhini ya Mwenyezi Mungu. Na hivyo ndivyo ilivyokuwa.

Na tukampa ahali zake na wengine kama wao pamoja nao, kuwa ni rehema itokayo kwetu, na iwe kumbusho kwa watu wenye akili.

Mwenyezi Mungu alimponyesha na kumruzuku watoto na wajukuu zaidi ya aliowakosa. Umetangulia mfano wake katika Juz. 17 (21:83 – 91).

Na shika kitita cha vijiti mkononi mwako, kisha ndio upige kwacho, wala usivunje kiapo. Hakika tulimkuta mwenye subira, mbora wa waja, kwa hakika alikuwa mwingi wa kutubu.

Wafasiri wamesema kuwa Ayyub alipokuwa kitandani aliwahi kumkasirikia mkewe kwa jambo lililozuka baina yake na yeye. Akaapa kumpiga, mara kadha, akipona. Mwenyezi Mungu alipompa shafaa, alimwamrisha achukue vijiti kadhaa ampige navyo mara moja tu. Hapo kiapo chake kitakuwa kimefunguka.

Aya haiashiri hilo kwa mbali wala karibu, lakini pamoja na hayo hatupingi kauli ya wafasiri. Kwa sababu kwenye Aya kumetajwa kiapo na kupiga. Kukiweko kupiga, lazima kuwe na kilichopigwa. Mtu akiwa hoi kitandani huwa anaona dhiki hata kwa mambo madogo; hasa yakitokea kwa watu wake mwenyewe. Kwa hiyo basi kauli ya wafasiri haiko mbali.

Unaweza kuuliza kauli yake Mwenyezi Mungu: Na shika kitita cha vijiti…inafahamisha kuwa inafaa kufanya hila na ujanja katika sharia ya Qur’an na inajulikana kuwa Bani israil walikatazwa kufanya hila ya kuvua Jumamosi, kama ilivyobainisha Aya isemayo: “Na waulize habari za mji uliokuwa kando ya bahari walipokuwa wakivunja Sabato, samaki wao walipowajia juu juu siku ya Sabato na siku wasiyofanya Sabato hawakuwajia. Kama hivyo tuliwajaribu kwa sababu walikuwa wakifanya ufuska. Juz. 9 (7:163).

Jibu: kwanza aina hii inahusiana na Ayyub tu peke yake wala haienei kwa wengine wanaoapa; vinginevyo suna za Mtume zingeliweka wazi hilo na ulama wote wangelilitolea fatwa. Pili: Hila hii ni kwa ajili ya huruma ya kibinadamu sio kuifanyia hila haki na ubinadamu.

Na wakumbuke waja wetu, Ibrahim na Is-haqa na Ya’qub waliokuwa na nguvu na busara.

Wenye nguvu ni nguvu za matendo mema, na busara ni kinaya cha kumjua Mwenyezi Mungu na dini yake. Maana ni kuwa wakumbuke ewe Muhammad manabii walioijua dini ya Mwenyezi Mungu,wakaitumia kwa ikhlasi na wakafanya jihadi katika njia yake wakiwa na subira. Wakumbuke na uwe na subira kwa wanaokukadhibisha katika watu wako; kama walivyokuwa na subira mitume wengine.

Sisi tumewahusisha wao kwa sifa ya ukumbusho wa makao; yaani makao ya Akhera.
Neno sifa limefasiriwa kutokana na neno Khaliswa lenye maana ya sifa safi kabisa isiyo na doa; nayo ni kuwa wao wanafanya kwa ajili ya akhera na wameathirika na kila kitu.

Na hakika wao kwetu sisi ni wateuliwa walio bora.

Walimfanyia ikhlasi Mwenyezi Mungu akawahusisha na risala yake, na akawafanya ni katika bora ya viumbe wake.

Na mkumbuke Ismail na Alyasaa na Dhulkifl, na wote hao ni katika walio bora.

Sikupata katika faharasa ya Kamusi ya Kitabu kitakatifu kutajwa Alyasaa na Dhulkifil. Nililolikuta ni jina la la Yashuu bin Nun, khalifa wa Musa. Inasemekana kuwa ndiye Alyasaa. Vyovyote iwavyo, yeye na Dhulkifl ni kama Ismail, Is-haq na Ya’qub katika manabii wateuliwa.

Umetangulia mfano wake katika Juz. 7 (6:85) na Juz. 17 (21:83 – 91).

هَٰذَا ذِكْرٌ ۚ وَإِنَّ لِلْمُتَّقِينَ لَحُسْنَ مَآبٍ {49}

Huu ni ukumbusho. Na hakika wenye takua wana marudio mazuri.

جَنَّاتِ عَدْنٍ مُفَتَّحَةً لَهُمُ الْأَبْوَابُ {50}

Bustani za milele zitazofunguliwa milango kwa ajili yao.

مُتَّكِئِينَ فِيهَا يَدْعُونَ فِيهَا بِفَاكِهَةٍ كَثِيرَةٍ وَشَرَابٍ {51}

Humo wataegemea matakia, wawe wanaagiza humo matunda mengi na vinywaji.

وَعِنْدَهُمْ قَاصِرَاتُ الطَّرْفِ أَتْرَابٌ {52}

Na pamoja nao wapo wenye kutuliza macho, walio marika.

هَٰذَا مَا تُوعَدُونَ لِيَوْمِ الْحِسَابِ {53}

Haya ndiyo mliyoahidiwa kwa Siku ya Hisabu.

إِنَّ هَٰذَا لَرِزْقُنَا مَا لَهُ مِنْ نَفَادٍ {54}

Hakika hii ndiyo riziki yetu isiyomalizika.

هَٰذَا ۚ وَإِنَّ لِلطَّاغِينَ لَشَرَّ مَآبٍ {55}

Ndio hivi! Na hakika wenye kupituka mipaka bila ya shaka watapata marejeo maovu.

جَهَنَّمَ يَصْلَوْنَهَا فَبِئْسَ الْمِهَادُ {56}

Nayo ni Jahannamu! Wataingia humo. Nayo ni malalo movu mno.

هَٰذَا فَلْيَذُوقُوهُ حَمِيمٌ وَغَسَّاقٌ {57}

Ndio hivi! Basi na wayaonje maji ya moto na ya usaha!

وَآخَرُ مِنْ شَكْلِهِ أَزْوَاجٌ {58}

Na mengineyo ya namna hii.

هَٰذَا فَوْجٌ مُقْتَحِمٌ مَعَكُمْ ۖ لَا مَرْحَبًا بِهِمْ ۚ إِنَّهُمْ صَالُو النَّارِ {59}

Hili ndilo kundi litakaloingia pamoja nanyi. Hapana makaribisho kwao. Hakika hao wanaingia Motoni.

قَالُوا بَلْ أَنْتُمْ لَا مَرْحَبًا بِكُمْ ۖ أَنْتُمْ قَدَّمْتُمُوهُ لَنَا ۖ فَبِئْسَ الْقَرَارُ {60}

Waseme: Lakini nyinyi! Hamna makaribisho! Nyinyi ndio mliotutangulizia haya, napo ni pahala paovu kabisa!

قَالُوا رَبَّنَا مَنْ قَدَّمَ لَنَا هَٰذَا فَزِدْهُ عَذَابًا ضِعْفًا فِي النَّارِ {61}

Waseme: Mola wetu! Aliyetutangulizia haya mzidishie adhabu mara mbili Motoni.

وَقَالُوا مَا لَنَا لَا نَرَىٰ رِجَالًا كُنَّا نَعُدُّهُمْ مِنَ الْأَشْرَارِ {62}

Watasema: Mbona hatuwaoni wale watu ambao tukiwahisabu ni katika waovu?

أَتَّخَذْنَاهُمْ سِخْرِيًّا أَمْ زَاغَتْ عَنْهُمُ الْأَبْصَارُ {63}

Je, tuliwafanyia maskhara, au macho yamewakosa?

إِنَّ ذَٰلِكَ لَحَقٌّ تَخَاصُمُ أَهْلِ النَّارِ {64}

Hakika hayo ya kuhasimiana watu wa Motoni ni kweli.