read

Aya 5 – 8 : Huufunika Mchana Juu Ya Usiku

Lugha

Neno Huuzongazonga limefasiriwa kutokana na neno la kiarabu yukawwir, lenye maana ya kufunika kitu kilicho mviringo; kama mtu anavyozongazonga kitambaa kichwani kufanya kilemba.

Maana

Ameumba mbingu na ardhi kwa Haki. Huuzongazonga usiku kwenye mchana, na Huuzongazonga mchana kwenye usiku.

Huko nyuma tumesema kuwa Mwenyezi Mungu ana vitabu viwili: Kitabu kinachotamka kwa mistari amabacho ni Qur’an na kitabu kilichonyamaza cha kuangaliwa, ambacho ni ulimwengu. Na kwamba yaliyomo katika kitabu hiki; kama vile umoja wenye kuthibiti na hekima iliyopangika, ni dalili mkataa ya umoja wa mwenye kuthibiti na hekima ya mwenye kupangalia. Ama sadfa, kama itatokea, basi hutokea kwenye kitu kimoja wala haikaririki mara nyingi kwenye kitu kimoja.

Mwenye Tafsir Adhilal akizungumzia Aya hii anasema: “Hakika ibara ya kuzongazonga inanilazimisha niangalie vizuri suala la ardhi kuwa ni mviringo, kwamba hiyo yenyewe inazunguka katika kulielekea jua. Kwa hiyo sehemu inayoeleka jua inafunikwa na mwanga na kuwa mchana, lakini sehemu hiyo haitulii kwa vile ardhi inazunguka.

Kila inavyozidi kuendelea ndio usiku nao unaanza kufunika sehemu iliyokuwa mchana. Kufunika huko kunakuwa kwa namna ya kuzongazonga. Kwa hiyo mchana unazongwazongwa na usiku na usiku nao unazongwazongwa”

Kwa hiyo neno kuzongazonga, haliko mbali kuwa linafahamisha mviringo. Ndio maana tunaungana na mwenye Dihilal aliposema ibara ya kuzongzonga inapelekea kuangalia kuwa ardhi ni mviringo. Mustafa Mahmud, katika gazeti la sabahulkhayr amesema kama alivyosema mwenye Dhilal, lakini hakumtaja. Sijui hii ni sadfa ya kuoana mawazo?

Umetangulia mfano wake katika Juzuu hii (36:37), lakini huko halikuja nen o kuzongazonga; bali tulipofafanua tuliashiria kuhusu mzunguko wa ardhi na kwamba upande uanaolelekea jua wakati wa kuzunguka unakuwa mchana na upande wa pili unakuwa usiku.

Na amelitiisha Jua na Mwezi, kila kimoja kinapita mpaka muda uliotajwa. Ehe! Yeye ndiye Mwenye nguvu, Mwenye kughufiria .

Umetangulia mfano wake katika Juz. 13 (13:2), 21 (31:29) na 22 (35:13).

Amewaumba kutokana na nafsi moja, na katika hiyo akamjaalia mkewe.

Umetangulia mfano wake katika Juz. 4 (4:1) na Juz. 9 (7:143)

Na amewateremshia wanymahoa namna nane za madume na majike.

Umetangulia mfano wake katika Juz. 8 (6:143).

Anawaumba katika matumbo ya mama zenu, umbo baada ya umbo, katika viza vitatu. Huyo ndiye Mwenyezi Mungu Mola wenu. Ufalme ni wake. Hapana Mola isipokuwa Yeye. Basi nyinyi mnageuzwa wapi?

فَإِنَّا خَلَقْنَاكُمْ مِنْ تُرَابٍ ثُمَّ مِنْ نُطْفَةٍ ثُمَّ مِنْ عَلَقَةٍ ثُمَّ مِنْ مُضْغَةٍ {5}

‘Umbo baada ya umbo’ ni ishara ya kauli yake Mwenyezi Mungu: “Hakika tuliwaumba kutokana na udongo kisha kutokana na pande la damu, kisha kutokana na pande la nyama” Juz. 17 (22:5).

Viza vitatu ni tumbo, tumbo la uzazi na fuko la mtoto. Kuendelea huku kutoka hali moja hadi nyingine ndani ya viza vitatu ni dalili mkataa ya kuweko mpangiliaji mwenye kutengeneza.

Ikiwa kukua huku kunatokana na maumbile moja kwa moja, basi maumbile ni katika usanii wa anayesema ‘kuwa ikawa’ Hili hawezi kupofuka nalo isipokuwa kipofu.

Imam Ali (a.s.) anasema: “Ewe kiumbe uliyembwa sawa sawa na mwenye kutunzwa kwenye viza vya tumbo la uzazi na tabaka za sitara! Umeanzishwa Kutokana na asili ya udongo1.”

Na ukawekwa “mahali palipo madhubuti makini mpaka muda maalum,2 na muda maalum. Unataharaki tumboni ukiwa mchanga, huwezi kuita wala kusikia mwito.

Kisha ukatolewa kwenye makazi yako kwenda mahali ambapo hujapashuhudia wala hujui manufaa yake. Basi ni nani aliyekuongoza kutafuta chakula kutoka kwenye matiti ya mama yako na kukujulisha matakwa ya haja yako?”3

Mkikufuru basi Mwenyezi Mungu si mwenye haja nanyi

Hayamdhuru maasi ya mwenye kuasi, wala haumnufaishi utiifu wa mwenye kutii “lakini inamfikia takua kutoka kwenu” Juz. 17 (22:37); yaani anawaridhia mkiwa ninyi ni wenye takua;

Ashaira wanasema kuwa Mwenyezi Mungu ndiye mwenye kutaka yote yanayokuwa; hata kufuru ya kafiri, zina ya mzinifu na uuaji wa mwenye kuua kwa dhulma; kwa vile Yeye ni muumba wa kila kitu. Lakini wakati huohuo anakataza kufuru, zina na kuua.

Almawafiq Juz. 8 Uk. 173. Kwa hiyo kukalifishwa lisilowezekana inajuzu kwa Ashaira. Kwa sababu Mwenyezi Mungu hawajibikiwi na kitu chochote wala hakuna kibaya kwake. Almawaqif Juz. 8 Uk. 200.

Hakuna kitu kilicho wazi zaidi kufahamisha ubatilifu wa fikra hii kuliko kauli yake Mwenyezi Mungu:

Wala haridhii kufuru kwa waja wake.

Na mkishukuru atawaridhia.

Analoturidhia ni amani kwetu na rehema.

Wala hatabeba mbebaji mzigo wa mwingine.

Imetangulia kwa herufi zake katika Juz. 8 (6:164), 15 (17:15), 22 (35:18).

Kisha marejeo yenu ni kwa Mola wenu. Basi atawambia mliyokuwa mkiyafanya. Hakika Yeye ni Mjuzi wa yaliyomo vifuani.

Kwake Yeye Mwenyezi Mungu ndio marejeo ya viumbe na mikononi mwake ndio kuna malipo ya matendo na Yeye anajua siri zote na yale wanayoyakusudia.

Na dhara inapomfikia mtu humwomba Mola wake akielekea kwake. Kisha akimpa neema kutoka kwake, husahau yale aliyo kuwa akimwitia zamani, na akamfanyia Mwenyezi Mungu washirika ili apoteze njia yake.

Kumgusa ni kumpata, dhara ni tabu na maudhi na kuelekea kwake ni kurejea kwake. Maana ni kuwa mtu anapopatwa na shida ya nafsi yake au mali yake humkimbila Mwenyezi Mungu kwa kumnyenyekea, lakini shida ikimwondokea basi anasahau unyenyekevu aliokuwa nao.

Sema: Starehe na kufuru yako kidogo, kwani hakika wewe mi miongoni mwa watu wa Motoni.

Hili ni kemeo na kiaga kwa yule anayeamini wakati wa shida na kukufuru wakati wa raha. Hakuna mwenye shaka kwamba starehe ya dunia pamoja kufuru ina mwisho mbaya.

أَمَّنْ هُوَ قَانِتٌ آنَاءَ اللَّيْلِ سَاجِدًا وَقَائِمًا يَحْذَرُ الْآخِرَةَ وَيَرْجُو رَحْمَةَ رَبِّهِ ۗ قُلْ هَلْ يَسْتَوِي الَّذِينَ يَعْلَمُونَ وَالَّذِينَ لَا يَعْلَمُونَ ۗ إِنَّمَا يَتَذَكَّرُ أُولُو الْأَلْبَابِ {9}

Je, Afanyaye ibada nyakati za usiku kwa kusujudu na kusimama akitahadhari na Akhera, na akitaraji rehema za Mola wake. Sema: Je, wanalingana sawa wale ambao wanajua na wale ambao hawajui? Hakika wanaokumbuka ni wenye akili tu.

قُلْ يَا عِبَادِ الَّذِينَ آمَنُوا اتَّقُوا رَبَّكُمْ ۚ لِلَّذِينَ أَحْسَنُوا فِي هَٰذِهِ الدُّنْيَا حَسَنَةٌ ۗ وَأَرْضُ اللَّهِ وَاسِعَةٌ ۗ إِنَّمَا يُوَفَّى الصَّابِرُونَ أَجْرَهُمْ بِغَيْرِ حِسَابٍ {10}

Sema: Enyi waja wangu ambao mmeamini! Mcheni Mola wenu. Wale ambao wamefanya wema katika dunia hii watapata wema. Na ardhi ya Mwenyezi Mungu ni pana. Hakika si mengineyo, wenye subira watapewa ujira wao bila ya hisabu.

قُلْ إِنِّي أُمِرْتُ أَنْ أَعْبُدَ اللَّهَ مُخْلِصًا لَهُ الدِّينَ {11}

Sema: Hakika mimi nimeamrishwa nimuabudu Mwenyezi Mungu kwa kumsafia Yeye Dini.

وَأُمِرْتُ لِأَنْ أَكُونَ أَوَّلَ الْمُسْلِمِينَ {12}

Na nimeamrishwa niwe wa mwanzo wa Waislamu.

قُلْ إِنِّي أَخَافُ إِنْ عَصَيْتُ رَبِّي عَذَابَ يَوْمٍ عَظِيمٍ {13}

Sema: Hakika mimi ninahofia adhabu ya Siku Kubwa nikimuasi Mola wangu.

قُلِ اللَّهَ أَعْبُدُ مُخْلِصًا لَهُ دِينِي {14}

Sema: Mwenyezi Mungu ninamuabudu kwa kumsafia Yeye Dini yangu.

فَاعْبُدُوا مَا شِئْتُمْ مِنْ دُونِهِ ۗ قُلْ إِنَّ الْخَاسِرِينَ الَّذِينَ خَسِرُوا أَنْفُسَهُمْ وَأَهْلِيهِمْ يَوْمَ الْقِيَامَةِ ۗ أَلَا ذَٰلِكَ هُوَ الْخُسْرَانُ الْمُبِينُ {15}

Basi abuduni mpendacho badala yake. Sema: Hakika waliohasirika ni wale waliojihasiri nafsi zao na ahali zao Siku ya Kiyama. Ehe! hiyo ndiyo hasara iliyo dhahiri

لَهُمْ مِنْ فَوْقِهِمْ ظُلَلٌ مِنَ النَّارِ وَمِنْ تَحْتِهِمْ ظُلَلٌ ۚ ذَٰلِكَ يُخَوِّفُ اللَّهُ بِهِ عِبَادَهُ ۚ يَا عِبَادِ فَاتَّقُونِ {16}

Watakuwa na vivuli vya moto juu yao, na chini yao vivuli. Kwa hayo Mwenyezi Mungu anawahofisha waja wake. Enyi waja wangu! Nicheni.
  • 1. Qur’an (23:12)
  • 2. Qur’an (77:21 – 22)
  • 3. Nahjulbalagha hotuba 163