Aya 9 – 16: Hadhari Ya Akhera Na Matarajio Ya Rehema Ya Mola
Maana
Hata Manabi Wana Shauku Na Hofu
Je, Afanyae ibada nyakati za usiku kwa kusujudu na kusimama akitahadhari na Akhera, na akitaraji rehema za Mola wake.
Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kutaja yule anayeamini wakati wa shida na kukufuru wakati wa raha, anafuatishia kumtaja yule anayeamini wakati wa shida na raha. Neema haimzidishii kitu isipokuwa imani, shukrani, kusujudu na kurukui wakati wa giza la usiku, watu wakiwa wamelala. Hafanyi kitu isipokuwa shauku ya thawabu za Mwenyezi Mungu na kuhofia adhabu yake.
Katika Aya hii kuna ishara kuwa mtu hafanyi ila kwa msukumo shauku na hofu, awe ni mwenye takua au muovu. Tofauti ni kuwa muovu anafanya na kuacha kwa shauku ya starehe za dunia na kuhofia tabu na machungu, lakini mwenye takua anafanya na kuacha kwa sahuku ya shamba la Akhera na neema zake na kuhofia adhabu yake na moto wake.
Hali hii iko hata kwa manabii walio maasumu ambao Mwenyezi Mungu Mtukufu amewasifu kwa kusema: “Wakituomba kwa shauku na hofu.” Juz. 17 (21:90).
Sema: Je, wanalingana sawa wale ambao wanajua na wale ambao hawajui? Hakika wanaokumbuka ni wenye akili tu.
Makusudio ya wanaojua hapa sio wale waliohifadhi sherehe na matini, wala sio wale waliogundua elektroni, mabomu ya masafa marefu na kupanda mwezini au kwenye Mars.
Hapana! Sio hao kabisa; isipokuwa makusudio ni wale wanaofanya kheri kwa binadamu wote na kuwakomboa wanaoadhibiwa ardhini na kuwaondoa watu kwenye tabu na mashaka.
Ama ulama wasiojali au wale ambao wameuza dini yao kwa mshetani na maibilisi kwa ajili ya kuwachapa watu na wakagundua silaha za maangamizi, hawa ni kama wanyama; bali wao wamepotea zaidi ya wanyama.
Hawawezi kuitambua hakika hii isipokuwa wale wenye akili na busara.
Sema: Enyi waja wangu ambao mmeamini! Mcheni Mola wenu, kwa sababu imani bila takua wala amali njema haina manufaa yoyote. Ndio maana baadhi ya maulama wamesema kuwa matendo mema ni sehemu ya kuamini haki.
Wale ambao wamefanya wema katika dunia hii watapata wema.
Haya ni maneno mapya hayaungani na yaliyotangulia. Maana yake ni kuwa mwenye kufanya hata chembe ya amali ya kheri ataiona.
Na ardhi ya Mwenyezi Mungu ni pana.
Kwa hiyo atayepata dhiki mjini kwake na akashindwa kutekeleza wajibu wake wa kidini au wa kidunia basi ahamie kwengine. Umetangulia mfano wake katika Juz. 5 (4:97).
Hakika si mengineyo, wenye subira watapewa ujira wao bila ya hisabu.
Yaani wenye kuvumilia shida kwa subira ya kiungwana na kukataa kusalimu amri kwenye ufukara na udhalili. Ama wale ambao wanawanyeyekea wenye nguvu na kuwa waoga mbele ya mataghuti, hao ndio waliohasirika duniani na akhera na huko ndiko kuhasrika waziwazi.
Sema: Hakika mimi nimeamrishwa nimuabudu Mwenyezi Mungu kwa kumsafia Yeye Dini.
Hakuna tofauti baina ya Nabii na mwenginewe. Yeye anaamrishwa kum- fanyia ikhlasi Mwenyezi Mungu katika kauli na matendo yake yote; kama binadamu mwingine.
Na nimeamrishwa niwe wa mwanzo wa Waislamu.
Mtume (s.a.w.) aliwapa watu mwito wa uislamu baada ya kutangulia yeye mwenyewe kwenye Uislamu, kwa sababu anafanya anayoyasema wala hasemi asiyoyafanya.
Sema: Hakika mimi ninahofia adhabu ya Siku Kubwa nikimuasi Mola wangu.
Muhammad (s.a.w.) anamhofia Mwenyezi Mungu kwa sababu Yeye hawezi kumwepuka Mwenyezi Mungu wala hana hoja naye, bali yeye ni hoja ya Mwenyezi Mungu kwa viumbe wake wote.
Utukufu zaidi kwa Muhammad (s.a.w.) ni kwamba yeye ni mtiifu kwa Mola wake, mwenye kumfanayia ikhlasi na mtangulizi wa mambo ya heri, akipata wahyi kutoka kwa Mola wake na akiutekeleza unavyotakikana:
قُلْ مَا كُنْتُ بِدْعًا مِنَ الرُّسُلِ وَمَا أَدْرِي مَا يُفْعَلُ بِي وَلَا بِكُمْ ۖ إِنْ أَتَّبِعُ إِلَّا مَا يُوحَىٰ إِلَيَّ وَمَا أَنَا إِلَّا نَذِيرٌ مُبِينٌ {9}
Sema: Mwenyezi Mungu ninamuabudu kwa kumsafiia Yeye Dini yangu.
Mara nyingine Muhammad (s.a.w.) anasisitiza, kwa amri ya Mwenyezi Mungu, kwamba Yeye ni mja mwenye kuamriwa. Mustshriq mmoja wa kingereza, Jeb Hamilton, mwalimu katika chuo kikuu cha Oxford, katika kitabu “Modern trends in Islam” anasema: “Qur’an inakataa fikra ya kuingiliwa kati, baina ya Mwenyezi Mungu na mtu. Unamweka mtu moja kwa moja mbele ya Mola wake bila ya kuweko wa katikati kiroho au kiutu.” Na hii ni tofuati kubwa inayoshindia Uislamu dini nyingine.
Basi abuduni mpendacho badala yake.
Huu ni ufasaha wa hali ya juu kuelezea hasira za Mwenyezi Mungu na makemeo kwa yule anayemfanya muabudia asiyekuwa Mwenyezi Mungu.
Sema: Hakika waliohasirika ni wale waliojihasiri nafsi zao na ahali zao Siku ya Kiyama. Ehe! hiyo ndiyo hasara iliyo dhahiri.
Wamezihasiri nafsi zao kwa sababu wamejiingiza kwenye Jahannam, marejeo mabaya kabisa, na wamewahasiri watu wao kwa sababu atakayekuwa mshirikina katika wao ataangamia. Na mumin ni adui wa mwenye kushirikisha duniani na akhera.
Watakuwa na vivuli vya moto juu yao, na chini yao vivuli.
Yaani adhabu ya kuungua itawazunguka kila mahali.
Kwa hayo Mwenyezi Mungu anawahofisha waja wake. Enyi waja wangu! Nicheni.
Mwenyezi Mungu amewabainishia adhabu ya akhera ili waweze kujiepusha nayo wakiwa duniani kwa kufanya utiifu na ikhlasi. Vinginevyo wataionja tu.
Msemaji mmoja alisema kuwa Pepo ni ladha za kiroho na moto ni machungu ya kinafsi na kwamba yote yaliyoelezwa kwenye Qur’an katika sifa za kihisia ni aina ya kupiga mfano na kuleta karibu kwenye akili. Kwa vile mabedui wanapenda sana asali, maziwa, pombe na wanawake mahurilaini. Msemaji wa maneno haya ametolea dalili kauli yake, kwa Aya hii tuliyo nayo: “Kwa hayo Mwenyezi Mungu anawahofisha waja wake.”
Kwamba inavyofahamika ni kuwa Mwenyezi Mungu ametaja matamshi ya adhabu kwa ajili ya kuhofisha tu, wala hakuna hakika1
Tunajibu: kila tamko lililokuja katika Kitabu cha Mwenyezi Mungu na sunna za Mtume wake ni wajibu kuchukulia dhahiri yake, ila ikiwa halingiliki akilini; na hapo tutalitumia kimajazi yanayokwenda na tamko lenyewe.
Hakuna tamshi katika matamshi ya sifa za Pepo na Moto yaliyotajwa na Qur’an, linalokataliwa na akili. Kwa hiyo ni wajibu kubakia tamko kwenye dhahiri yake, bila ya kuweko haja ya kuleta taawili.
Maana ya kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: “Kwa hayo Mwenyezi Mungu anawahofisha waja wake,” ni kuwa anawabainishia uhakika wa mambo, ili wachukue hadhari na wajiepushe na sababu zitakazopelekea hilo. Aya iliyotaja sifa za Moto ndio inayofahamisha maana haya:
إِنَّ ذَٰلِكَ لَحَقٌّ تَخَاصُمُ أَهْلِ النَّارِ {64}
Ama kauli ya kuwa huruma ya Mwenyezi Mungu haiafikiani na adhabu ya ya Moto kwa kiumbe huyu masikini aliye dhaifu, tunaijibu hivi:
Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amewandalia adhabu kali na chungu wale wanofanya ufisadi katika ardhi wakamwaga damu, kuwafanya waja wa Mungu kuwa watumwa wao, wakaangamiza watu kwa silaha za maangamizi na kuwaua kwa maelfu ndani ya dakika. Jahannam, pamoja na sifa zake zote, haitoshi kuwa ni malipo kwa hawa; bali wamehurumiwa pia. Amani imshukie yule aliyesema: “Ghadhabu haimshughulishi (asiwe) na huruma, wala huruma haimshughulishi (asiwe) na mateso.”
Tazama kifungu cha ‘Jahannam na silaha za maangamizi’ katika Juz.13 (14:46-52).
وَالَّذِينَ اجْتَنَبُوا الطَّاغُوتَ أَنْ يَعْبُدُوهَا وَأَنَابُوا إِلَى اللَّهِ لَهُمُ الْبُشْرَىٰ ۚ فَبَشِّرْ عِبَادِ {17}
الَّذِينَ يَسْتَمِعُونَ الْقَوْلَ فَيَتَّبِعُونَ أَحْسَنَهُ ۚ أُولَٰئِكَ الَّذِينَ هَدَاهُمُ اللَّهُ ۖ وَأُولَٰئِكَ هُمْ أُولُو الْأَلْبَابِ {18}
أَفَمَنْ حَقَّ عَلَيْهِ كَلِمَةُ الْعَذَابِ أَفَأَنْتَ تُنْقِذُ مَنْ فِي النَّارِ {19}
لَٰكِنِ الَّذِينَ اتَّقَوْا رَبَّهُمْ لَهُمْ غُرَفٌ مِنْ فَوْقِهَا غُرَفٌ مَبْنِيَّةٌ تَجْرِي مِنْ تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ ۖ وَعْدَ اللَّهِ ۖ لَا يُخْلِفُ اللَّهُ الْمِيعَادَ {20}
أَلَمْ تَرَ أَنَّ اللَّهَ أَنْزَلَ مِنَ السَّمَاءِ مَاءً فَسَلَكَهُ يَنَابِيعَ فِي الْأَرْضِ ثُمَّ يُخْرِجُ بِهِ زَرْعًا مُخْتَلِفًا أَلْوَانُهُ ثُمَّ يَهِيجُ فَتَرَاهُ مُصْفَرًّا ثُمَّ يَجْعَلُهُ حُطَامًا ۚ إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَذِكْرَىٰ لِأُولِي الْأَلْبَابِ {21}
- 1. Kauli hii ni ya zamani na watu wameachana nayo, lakini Mustafa Mahmud ametaka kuijibu kwa makala aliyoisambaza kwenye gazeti la Sabhul-khayr la 22-1-1970