read

Aya 22 – 24: Ambaye Mwenyezi Mungu Amemfungulia Kifua Chake Kwa Uislamu

Maana

Je! Yule ambaye Mwenyezi Mungu amemfungulia kifua chake kwa Uislamu, na akawa kwenye nuru itokayo kwa Mola wake, ni sawa na mwenye moyo mgumu?

Mwenye kumtegemea Mwenyezi Mungu humtosha na mwenye kutafuta uongofu humwongoza. Mwenyezi Mungu akiona kheri kutoka kwa mja na kwamba yeye anataka kuijua haki na kuitumia, basi Mwenyezi Mungu humshika mkono na kumwongoza na humjaalia ubainifu kwenye jambo lake:

وَمَنْ يُرِدْ ثَوَابَ الدُّنْيَا نُؤْتِهِ مِنْهَا وَمَنْ يُرِدْ ثَوَابَ الْآخِرَةِ نُؤْتِهِ مِنْهَا ۚ {145}

“Na anayetaka malipo ya dunia tutampa humo na anayetaka malipo ya akhera tutampa huko” Juz. 4 (3:145).

Basi ole wao wenye nyoyo ngumu zisizomkumbuka Mwenyezi Mungu!

Pamoja na mawaidha, hadhari na bishara, lakini nyoyo zao zimesusuwaa na wala hazikuelekea kwenye uongofu.

Hao wamo katika upotofu wa dhahiri na adhabu ya kufedhehesha.
Amesema Al-Hafidh Muhammad Bin Ahmad Al-Kalabiy, katika kitabu Attas-hil liulumittanzil: “Imepokewa kwamba ambaye amefunguliwa kifua chake kwa Uislamu ni Ali bin Abu Talib na Hamza; na mwenye moyo mgumu ni Abu Lahab na watoto wake”

Kisha Mwenyezi Mungu ameisifu Qur’an kwa sifa zifuatazo:-

1. Mwenyezi Mungu ameteremsha hadithi nzuri kabisa, katika itiakadi yake, sharia yake, mawaidha yake, hekima zake, misingi yake na mafunzo yake yote.

2. Kitabu chenye kufanana kimfumo wala hakuna mgongano katika maana yake, kwa sababu kinatoka kwa Mwenye hekima aliye Mjuzi.

3. Chenye kuelezewa mara mbili mbili; yaani hukumu zake na mawaid- ha yake huja mara mbili mbili – kinachanganya kuamrisha na kukataza, ahadi na kiaga nk. Katika Kitabu ‘Annuwatu fi haqlil hayat’ cha Sheikh Al-Abidy anasema: “Katika Qur’an kuna Sura za kufanana na kinyume chake; kisha inavuma kwako, katika yanayohusiana na ubora, kwa sauti ya kuam- risha ya upole. Na katika yanayohusiana na ubaya kwa sauti ya mwenye kukemea mwenye nguvu. Na ndani ya Qur’an kuna tulizo la mwenye kuabudu na karipio la kiongozi. Imesemekana kuwa makusudio ni kukaririwa. Kwa vyote iwavyo, makusudio ya neno mathani hapa, sio kama ile iliyoko Juz. 14 (15:87).

4. Husisimka kwacho ngozi za wenye kumkhofu Mola wao. Hiki ni kinaya cha hofu ya waumini wanaposikia kiaga cha Mwenyezi Mungu na tishio la Moto. Mfano wake ni kama kauli ya Imam Ali (a.s.): “Wao na mtoto ni kama waliouona wakiwa ndani wanaadhibiwa.”

5. Kisha ngozi zao na nyoyo zao hulainika kwa kumkumbuka Mwenyezi Mungu. Kinaya cha kutulia kwao wanaposikia ahadi ya Mwenyezi Mungu na bishara yake ya neema: Imam Ali (a.s.) anasema: “Wao na Pepo ni kama waliyoiona wakiwa ndani wakineemeshwa.”

Huo ndio uwongofu wa Mwenyezi Mungu, na kwa huo humwongoza amtakaye. Na ambaye amepotezwa na Mwenyezi Mungu, basi hana wa kumwongoza.

Je! Ajilindae uso wake na adhabu mbaya Siku ya Kiyama ni sawa na asiyejilinda? Sio sawa yule iliyemvaa adhabu mpaka unyayoni na yule aliye katika amani. Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ametaja uso kwa vile ndio kiungo kitukufu kwa mtu na kinachompambanua na wengine.

Na wataambiwa wenye kudhulumu: Onjeni hayo mliyokuwa mkiy-achuma!

Sawa na “Kama utakavyofanya nawe utafanyiwa, utavuna utakachopanda na ulichokifanya leo kitakufanya kesho,” kama alivyosema Imam Ali (a.s.).

كَذَّبَ الَّذِينَ مِنْ قَبْلِهِمْ فَأَتَاهُمُ الْعَذَابُ مِنْ حَيْثُ لَا يَشْعُرُونَ {25}

Waliokuwa kabla yao walikadhibisha, na ikawajia adhabu kutoka pahali wasipo patambua.

فَأَذَاقَهُمُ اللَّهُ الْخِزْيَ فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا ۖ وَلَعَذَابُ الْآخِرَةِ أَكْبَرُ ۚ لَوْ كَانُوا يَعْلَمُونَ {26}

Basi Mwenyezi Mungu akawaonjesha hizaya katika uhai wa duniani. Na bila ya shaka adhabu ya Akhera ni kubwa zaidi; laiti wangelijua!

وَلَقَدْ ضَرَبْنَا لِلنَّاسِ فِي هَٰذَا الْقُرْآنِ مِنْ كُلِّ مَثَلٍ لَعَلَّهُمْ يَتَذَكَّرُونَ {27}

Na hakika tumewapigia watu kila mifano katika hii Qur’an ili wapate kukumbuka.

قُرْآنًا عَرَبِيًّا غَيْرَ ذِي عِوَجٍ لَعَلَّهُمْ يَتَّقُونَ {28}

Qur’an ya Kiarabu isiyo na upogo, ili wawe na takua.

ضَرَبَ اللَّهُ مَثَلًا رَجُلًا فِيهِ شُرَكَاءُ مُتَشَاكِسُونَ وَرَجُلًا سَلَمًا لِرَجُلٍ هَلْ يَسْتَوِيَانِ مَثَلًا ۚ الْحَمْدُ لِلَّهِ ۚ بَلْ أَكْثَرُهُمْ لَا يَعْلَمُونَ {29}

Mwenyezi Mungu amepiga mfano wa mtu mwenye washirika wanaohitalifiana, na wa mtu mwengine aliyehusika na mtu mmoja tu. Je! Wako sawa kiufananishi? Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu! (Alhamdu lillahi) Lakini wengi wao hawajui.

إِنَّكَ مَيِّتٌ وَإِنَّهُمْ مَيِّتُونَ {30}

Kwa hakika wewe utakufa, na wao watakufa.

ثُمَّ إِنَّكُمْ يَوْمَ الْقِيَامَةِ عِنْدَ رَبِّكُمْ تَخْتَصِمُونَ {31}

Kisha hakika mtahasimiana Siku ya Kiyama mbele ya Mola wenu.