Aya 25 – 31: Qur’ani Ya Kiarabu Isiyokuwa Na Upogo
Maana
Waliokuwa kabla yao walikadhibisha, na ikawajia adhabu kutoka pahali wasipopatambua. Basi Mwenyezi Mungu akawaonjesha hizaya katika uhai wa duniani. Na bila ya shaka adhabu ya Akhera ni kubwa zaidi; laiti wangelijua!
‘Kabla’ yao ni kabla ya hao washirikina wa Makka waliomkadhibisha MtumewaMwenyeziMungu(s.a.w.).Ayainawambiakuwamnamkadhibisha Muhammad na wala hampati mazingatio kwa kuanangamia umma zilizopita kutokana na kukadhibisha kwao Mitume wao? Maana haya yamekaririka kwenye Aya nyingi; ikiwemo ile ya Juz. 8 (6:148).
Na hakika tumewapigia watu kila mifano katika hii Qur’an ili wapate kukumbuka.
Qur’an imekusanya mafunzo ya kuwalea watu kwa maisha mema na ya amani, katika kila zama na kila mahali. Imewabainishia yaliyo na heri na masilahi na ikawaamuru kuyafanya hayo. Na ikawabainishia yaliyo na shari na ufisadi na ikawakataza kuyafnya. Imefanya hivyo kwa mifumo mbali mbali na mifano iliyowazi ili waweza kupata mawaidha na wanyooke sawasawa.
Umetangulia mfano wake katika Juz. 15 (18:54) na Juz. 21 (30:58)
Tarjuma Ya Qur’an
Qur’an ya Kiarabu isiyo na upogo, ili wawe na takua.
Qur’an ni ya kiarabu kilugha na ni ya watu wote kidini na kimsingi, haina mpaka wa wakati au mahali wala haibagui rangi au taifa:
وَمَا أَرْسَلْنَاكَ إِلَّا كَافَّةً لِلنَّاسِ بَشِيرًا وَنَذِيرًا وَلَٰكِنَّ أَكْثَرَ النَّاسِ لَا يَعْلَمُونَ {28}
Imenyooka haiko kombokombo, kwa sababu inatoka kwa Mjuzi Mwenye hekima, ikilenga kuwaongoza watu kwenye njia ya haki iliyo sawasawa. Umetangulia mfano wake katika Juz. 12 (12:2), Juz.13 (13:37) na Juz. 16 (20:113).
Unaweza kuuliza: Je, inajuzu kutarjumu Qur’an kwenye lugha nyinginezo? Kama inajuzu, je, tarjuma itakuwa na hukumu ya Qur’an, kwamba isi- guswe bila twahara?
Jibu: Hakuna shaka wala wasiwasi wowote kuhusu kutarjumu Qur’an kwenye lugha zote; bali hilo linatakikana litilwe mkazo, kwa sababu Qur’an ni risala ya Mwenyezi Mungu kwa watu wote, na tarjuma ni kazi ya msingi ya kueneza risala ya Mungu na kuieneza.
Kuna jamaa wengi wamesilimu au wamefahamu hakika ya Uislam kupitia tarjuma ya Qur’an. Ni hivi karibuni tu alisilimu msichana wa kingereza, msomi, baada ya kusoma tarjuma ya Qur’an kwenye lugha yake. Tazama kifungu cha ‘msichana wa kingereza na Uislamu,’ kwenye Juzuu hii.
Kwenye jarida la Arribat la mwezi January 1979, imeelezwa kuwa mpaka sasa Qur’an imetarjumiwa kwenye lugha 27 na tarjuma.
Hakuna shaka kwamba tarjuma ya Qur’an haina hukumu ya Qur’an kwa sababu zifuatazo:-
Kwanza, Kiarabu ndio mhimili wa Qur’an:
إِنَّا أَنْزَلْنَاهُ قُرْآنًا عَرَبِيًّا{2}
Pili, tarjuma sio Qur’an hasa, bali ni maana ya Qur’an. Kwa maneno mengine ni kuwa Qur’an ni fasihi ya kiarabu na maana yake ya kiuhakika. Kwa hiyo hakuna Qur’an bila ya kiarabu; bali inabaki ni kitu kingine tu. Kwa hiyo hukumu ya tarjuma ya Qur’an, ni sawa na hukumu ya tafsiri yake.
Hata hivyo hukumu ya jina la Mwenyezi Mungu na sifa zake ni hukumu ya Qur’an hasa, inakuwa haramu kugusa kwa lugha yoyote itakayokuwa.
Mwenyezi Mungu amepiga mfano wa mtu mwenye washirika wanaohitalifiana, na wa mtu mwengine aliyehusika na mtu mmoja tu. Je! Wako sawa kiufananishi?
Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amepiga mfano huu kwa washirikina wa waliokadhibisha risala ya Muhammad (s.a.w.). Ufafanuzi wake ni kuwa mshirikina anayeabudu waungu wengi ni sawa na mtumishi aliyemilikiwa na watu mbali mbali waliotofauti katika rai na hulka, hawaafikiani kwenye jambo lolote.
Kila mmoja anataka mtumishi atekeleze analolitaka yeye linalotofautiana na wenzake. Mtumishi naye hawezi kutekeleza matakwa ya kila mmoja na kumridhisha; wakati huo huo hataki kuwaudhi wote. Kwa hiyo siku zote anakuwa hajui afanye nini.
Ama mumin mwenye kumpwekesha Mungu mmoja anafanana na mtumishi aliyemilikiwa na mtu mmoja, wala hataki kumridhisha mwingine asiyekua bwana wake anayempangilia katika anayomwamuru na anayomkataza. Kila mmoja ana raha na mwenzake.
Bwana hamkalifishi mtumishi wake asiloliweza na mtumishi anamsikiliza na kumtii huku moyo wake ukiwa umetulia, kwa vile ana uhakika wa kumridhisha bwana wake.
Je, mtu huyu anayehusika na bwana mmoja tu Mwenye hekima na wala hamnyenyekei yeyote isipokuwa yeye tu na mtu yule mwenye mabwana wengi anayetaka kuwaridhisha wote, wako sawa? Hapana!
أَأَرْبَابٌ مُتَفَرِّقُونَ خَيْرٌ أَمِ اللَّهُ الْوَاحِدُ الْقَهَّارُ {39}
Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu! (Alhamdu lillahi) ambaye ametia nguvu dini na Mtume wake kwa nguvu za hoja na ubainifu unaofafanua na akawadhalilisha maadui zake wabatilifu, wakarudi nyuma wakiwa vichwa chini.
Lakini wengi wao hawajui.
Kwamba mshirikina ni kama mtumishi mwenye kumilikiwa na wachungaji wengi.
Kwa hakika wewe –Muhammad - utakufa, na wao watakufa.
Kwa sababu mauti ndio mwisho wa uhai wa kila mtu, awe Nabii au sio Nabii, wala hakuna atakayebakia isipokuwa dhati yake tukufu. Lakini maadui wa Muhammad (s.a.w.) watakufa kifo cha kikafiri na cha kijahili; haitabaki athari yao isipokuwa laana na matusi. Ama risala ya Muhammad (s.a.w.) itadumu wakati wote na jina lake linakutanishwa na rehema na amani mpaka Siku ya Mwisho.
Kisha hakika mtahasimiana Siku ya Kiyama mbele ya Mola wenu.
Makusudio ya kuhasimiana hapa ni kuwa Nabii (s.a.w.) atatoa ushahidi mbele ya Mwenyezi Mungu, Siku ya Kiyama, kuwa yeye amewafikishia risala ya Mola wao: “Na tutakuleta wewe uwe shahidi juu ya hawa. Juz. 14 (6:89)