read

Sura Ya Sitini Na Mbili: Al-Jum’a

Imeshuka Madina Ina Aya 11.

بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ 

Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema Mwenye kure­hemu.

يُسَبِّحُ لِلَّهِ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الْأَرْضِ الْمَلِكِ الْقُدُّوسِ الْعَزِيزِ الْحَكِيمِ {1}

Vinamsabihi vilivyo katika mbingu na vilivyo katika ardhi, Mfalme, Mtakatifu, Mwenye nguvu, Mwenye hiki­ma

هُوَ الَّذِي بَعَثَ فِي الْأُمِّيِّينَ رَسُولًا مِنْهُمْ يَتْلُو عَلَيْهِمْ آيَاتِهِ وَيُزَكِّيهِمْ وَيُعَلِّمُهُمُ الْكِتَابَ وَالْحِكْمَةَ وَإِنْ كَانُوا مِنْ قَبْلُ لَفِي ضَلَالٍ مُبِينٍ {2}

Yeye ndiye Aliyempeleka Mtume kwenye watu wasiojua kusoma, aliyetokana na wao, awasomee Aya zake, na awatakase, Na awafunze Kitabu na hikima, Japokuwa hapo kabla walikuwa katika upotofu uliodhahiri.

وَآخَرِينَ مِنْهُمْ لَمَّا يَلْحَقُوا بِهِمْ ۚ وَهُوَ الْعَزِيزُ الْحَكِيمُ {3}

Na kwa wengine ambao bado hawajaungana nao. Na Yeye ndiye Mwenye nguvu, Mwenye hikima.

ذَٰلِكَ فَضْلُ اللَّهِ يُؤْتِيهِ مَنْ يَشَاءُ ۚ وَاللَّهُ ذُو الْفَضْلِ الْعَظِيمِ {4}

Hayo ni fadhila ya Mwenyezi Mungu anayompa amtakaye. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye fadhila kubwa.

Aya 1-4: Ndiye Aliewapelekea Mtume

Maana

Vinamsabihi vilivyo katika mbingu na vilivyo katika ardhi, Mfalme, Mtakatifu, Mwenye nguvu, Mwenye hikima.

Kila kilicho katika ulimwengu kinafahamisha umoja wa Mwenyezi Mungu na uweza wake. Hii ni tasbihi na kutukuza, ni ufalme unaotawala, utakati­fu wa kuepuka na vile visivyolaikina naye, ni nguvu isiyoshindwa na hiki­ma katika matumizi yake. Umetangulia mfano wake katika Juz. 27 (57:1), na katika Juzuu hii tuliyo nayo mwanzo wa sura 59 na 61.

Yeye ndiye Aliyempeleka Mtume kwenye watu wasiojua kusoma, aliyetokana na wao.

Makusudio ya wasiojua kusoma hapa ni waarabu. Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amewasifu kuwa hawajui kusoma kwa vile siku hizo wengi wao walikuwa hawasomi wala hawaandiki.

Neno wasiojua ‘kusoma,’ tumelifasiri kutokana na neno la kiarabu ummiy, ambalo baadhi wamesema kuwa makusudio ya Ummiy hapa ni watu wa Makka, kwa sababu Makka pia inaitwa Ummulqura, hivyo ummiy liwe limetokana na ummu.

Lakini kauli hii tunaipinga kwa sababu zifuatazo:­

1. Neno la kutojua kusoma ndilo linalokuja kwanza kwenye ufa­hamu.

2. Kauli yake Mwenyezi Mungu kwa kutumia neno hilo hilo ummiy:

وَمِنْهُمْ أُمِّيُّونَ لَا يَعْلَمُونَ الْكِتَابَ إِلَّا أَمَانِيَّ وَإِنْ هُمْ إِلَّا يَظُنُّونَ {78}

“Na wako miongoni mwao wasiojua kusoma; hawajui kitabu isipokuwa matamanio tu.”
Juz. 1 (2:78).

Na Qur’an inajifasiri yenyewe.

3. Kauli yake Mtume (s.a.w.): Sisi ni umma usiosoma, hatuandiki wala hatuhisabu.”

Baaadhi ya watu wa Kitab wamesema kuwa kauli yake Mwenyezi Mungu: “Yeye ndiye Aliempeleka Mtume kwenye watu wasiojua kusoma, aliyeto­kana na wao, “ inajulisha kuwa Muhammad ni Mtume wa waarabu tu.

Hilo tumelijibu kwa ufafanuzi zaidi katika Juz. 7 (6:91-92) na katika Juz. 22 (33:36-40) kifungu cha: “Kwanini utume uliishia kwa Muhammad?

Kisha Mwenyezi Mungu (s.w.t.) akabainisha ufahamu wa risala ya Nabii wake Mtukufu, kama ifuatavyo:-Awasomee Aya zake. Awafikishie risala ya Mola wake ambayo watak­wenda nayo kwenye njia ya maisha na uokovu.

Na awatakase. Azisafishe nafsi zao na shirki, akili zao na ujinga na amali zao na uovu na madhambi.

Na awafunze Kitabu. Awagurishe kutoka kwenye giza la upofu na ujinga kwenda kwenye nuru ya ilimu na uongofu, kwa mafundisho yake ambayo yanaitukuza ilimu na kutupilia mbali upotofu; na yanayojikita kwenye akili na maumbile ya kibinadamu.

Na hikima. kila linaloongoza kwenye heri katika itikadi na maadili basi hilo ni hikima. Ibn Al-arabi anasema: Hikima ni sifa ya kuhukumia wala haihukumiwi; yaani inakua juu wala haikaliwi juu.

Kwa ufupi ni kuwa risala ya Muhammad (s.a.w.) ni risala ya ubinadamu kwa ujumla, ikizungumza na watu kwa mazungumzo ya kiakili.
Sifa muhimu ya uislamu inayoutofautisha na dini nyingine, ni kuwa inakaribisha somo lolote la kimaudhui lenye insafu.

Ijapokuwa hapo kabla walikuwa katika upotofu uliodhahiri, wa ushirikina, ujinga, dhulma, chuki na mengineyo mabaya na machafu.

Na kwa wengine ambao bado hawajaungana nao.

Makusudio ya wengine ni kila mwenye kuingia uislamu baada ya Muhammad (s.a.w.) mpaka siku ya Kiyama, awe mwarabu au sio mwarabu. Maana ni kuwa Muhammad (s.a.w.) ni Nabii wa rehema kwa vizazi vyote na mwito wake ni wa watu wote. Wameuamini waarabu na wasiokuwa waarabu katika wakati wake na wanaendelea kuaamini wanofuatia mpaka siku ya ufufuo.

Na Yeye ndiye Mwenye nguvu, Mwenye hikima. Na kwa nguvu yake ameupa nguvu uislamu, akaueneza mashariki mwa ardhi na magharibi yake na kwa hikima yake amemchagua Muhammad (s.a.w.) kwa risala yake yenye kuenea.

Hayo ni fadhila ya Mwenyezi Mungu anayompa amtakaye. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye fadhila kubwa.

Hayo ni hayo ya kumtuma Muhammad (s.a.w.). Ni fadhila kutoka kwa Mwenyezi Mungu na rehema kwa binadamu wote. Mfano ni kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:

وَمَا أَرْسَلْنَاكَ إِلَّا رَحْمَةً لِلْعَالَمِينَ {107}

“Na hatukukutuma ila uwe ni rehema kwa walimwengu.” Juz. 17 (21:107)

مَثَلُ الَّذِينَ حُمِّلُوا التَّوْرَاةَ ثُمَّ لَمْ يَحْمِلُوهَا كَمَثَلِ الْحِمَارِ يَحْمِلُ أَسْفَارًا ۚ بِئْسَ مَثَلُ الْقَوْمِ الَّذِينَ كَذَّبُوا بِآيَاتِ اللَّهِ ۚ وَاللَّهُ لَا يَهْدِي الْقَوْمَ الظَّالِمِينَ {5}

Mfano wa waliobebeshwa Tawrati kisha wasiibebe, ni mfano wa punda anayebeba vitabu vikubwa. Mfano muovu mno wa watu waliokadhibisha Ishara za Mwenyezi Mungu, na Mwenyezi Mungu hawaon­goi watu madhalimu.

قُلْ يَا أَيُّهَا الَّذِينَ هَادُوا إِنْ زَعَمْتُمْ أَنَّكُمْ أَوْلِيَاءُ لِلَّهِ مِنْ دُونِ النَّاسِ فَتَمَنَّوُا الْمَوْتَ إِنْ كُنْتُمْ صَادِقِينَ {6}

Sema: Enyi mlio Mayahudi! Ikiwa nyinyi mnadai kuwa ni vipenzi vya Mwenyezi Mungu pasipo kuwa watu wengine, basi yatamanini mauti, ikiwa mnasema kweli.

وَلَا يَتَمَنَّوْنَهُ أَبَدًا بِمَا قَدَّمَتْ أَيْدِيهِمْ ۚ وَاللَّهُ عَلِيمٌ بِالظَّالِمِينَ {7}

Wala hawatayatamani kabisa, kwa sababu ya iliyokwisha yatanguliza mikono yao. Na Mwenyezi Mungu anawajua madhalimu.

قُلْ إِنَّ الْمَوْتَ الَّذِي تَفِرُّونَ مِنْهُ فَإِنَّهُ مُلَاقِيكُمْ ۖ ثُمَّ تُرَدُّونَ إِلَىٰ عَالِمِ الْغَيْبِ وَالشَّهَادَةِ فَيُنَبِّئُكُمْ بِمَا كُنْتُمْ تَعْمَلُونَ {8}

Sema: Hakika mauti mnayoy­akimbia, bila ya shaka yatawakuta. Kisha mtarudish­wa kwa Mwenye kuyajua ya ghaibu yanayoonekana. Hapo atawaambia mliyokuwa mkiy­atenda.

Aya 5 – 8: Kama Mfano Wa Punda Waaliobeba Vitabu

Maana

Mfano wa waliobebeshwa Tawrati kisha wasiibebe, ni mfano wa punda anayebeba vitabu vikubwa.

Mayahudi wanasema sisi ni watu wa Tawrat na ndio kitabu chetu kitakati­fu, lakini pamoja na hayo wanamkana Muhammad aliyenukuliwa kwenye Tawrat. Kwa hiyo hali yao ni kama punda aliyebebeshwa mzigo wa vitabu vya ilimu kwenye mgongo wake, lakini hana akili ya kilichomo ndani yake wala kunufaika nacho.

Mayahudi wameipotoa Tawrat ya Musa na vitabu vingine vitakatifu kwao, hilo halina shaka. Tazama Aya 6 ya sura iliyopita. Kisha baada ya kuipotoa wakayafanyia kazi yale waliyoyapotoa. Tunataja mfano wa hayo katika kitabu walichokinasibisha kwa Ezekieli, ninanukuu:

“Na hao wengine aliwambia, nami nalisikia, Piteni kati ya miji nyuma yake; mkapige jicho lenu lisiachilie, wala msione huruma; waueni kabisa, mzee, na kijana, na msichana, na watoto wachanga, na wanawake…” Ezekili 9: (5-6)

Hii ndio Israil inayofuata misingi hii kila inapopata fursa, kuwaua wazee, vijana, watoto na wanawake, si kwa chochote ila kwa maangamizi na kumaliza.

Unaweza kuuliza: waislamu wengi hawaitumii Qur’an, je mfano wao ni kama mfano wa punda anayechukua mizigo?

Jibu: Waislamu hawakuipotoa Qur’an na kuondoa Aya zinazomkubali Musa, Isa, Tawrat na Injil za asili zilizo sahihi, kama walivyopotoa maya­hudi Tawrat na wanaswara Injil: “Semeni: Tumemwamini Mwenyezi Mungu na yale tuliyoteremshiwa na yale yaliyoteremshwa kwa Ibrahim na Ismail na Is’hak na Yaqub na wajukuu na aliyopewa Musa na Isa na pia yale waliyopewa Manabii (wengine) kutoka kwa Mola wao; hatutafautishi baina ya yeyote katika hao na sisi tumesilimu (tumenyenyekea) kwake.”Juz. 1 (2:136)

Kwa hiyo basi hakuna njia yoyote ya kufananisha wala kulaumu.

Mfano muovu mno wa watu waliokadhibisha Ishara za Mwenyezi Mungu.

Kila mwenye kukadhibisha haki anakuwa ametoa mfano kutoka kwenye nafsi yake juu ya ukafiri na ufisadi wake. Inafaa kila mtu kumwambia: Ni aibu kwako na huzuni.

Na Mwenyezi Mungu hawaongoi watu madhalimu.

Wataongoka vipi na hali upotevu umemea kwenye nyoyo zao.

Sema: Enyi mlio Mayahudi! Ikiwa nyinyi mnadai kuwa ni vipenzi vya Mwenyezi Mungu pasipo kuwa watu wengine, basi yatamanini mauti, ikiwa mnasema kweli. Wala hawatayatamani kabisa, kwa sababu ya iliyokwisha yatanguliza mikono yao. Na Mwenyezi Mungu anawajua madhalimu.

Mayahudi walidai kuwa wao ni taifa teule la Mwenyezi Mungu na kwam­ba ni vipenzi wa Mwenyezi Mungu na Pepo ni yao tu. Ndio akawarudi Mwenyezi Mungu kwamba wao ni waongo katika madai yao. Kama wan­gelikuwa wakweli katika madai yao wangelitamani kukutana na Mwenyezi Mungu. Kwa sababu yaliyoko kwake ni yenye kubaki na bora zaidi kuliko fedheha waliyo nayo.

Wapi! Wao wanachukia mauti na wanayahofia, kwa wingi wa madhambi yao. La kushangaza ni kuwa wao bado wanaendelea na kung’ang’ania yale wanayohofia mauti kwayo. Umetangulia mfano wake katika Juz. 1 (2:94).

Sema: Hakika mauti mnayoyakimbia, bila ya shaka yatawakuta. Kisha mtarudishwa kwa Mwenye kuyajua ya ghaibu yanayoonekana.

Hapo atawaambia mliyokuwa mkiyatenda duniani, yakupotoa Kitabu na mengineyo ya ufisadi na makosa na atawalipa adhabu kali ya Jahannam.

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِذَا نُودِيَ لِلصَّلَاةِ مِنْ يَوْمِ الْجُمُعَةِ فَاسْعَوْا إِلَىٰ ذِكْرِ اللَّهِ وَذَرُوا الْبَيْعَ ۚ ذَٰلِكُمْ خَيْرٌ لَكُمْ إِنْ كُنْتُمْ تَعْلَمُونَ {9}

Enyi mlioamini! Ikinadiwa Swala siku ya Ijumaa, nendeni upesi kwenye dhikri ya Mwenyezi Mungu, na wacheni biashara. Hayo ni bora kwenu, kama mnajua.

فَإِذَا قُضِيَتِ الصَّلَاةُ فَانْتَشِرُوا فِي الْأَرْضِ وَابْتَغُوا مِنْ فَضْلِ اللَّهِ وَاذْكُرُوا اللَّهَ كَثِيرًا لَعَلَّكُمْ تُفْلِحُونَ {10}

Na itakapokwisha Swala, tawanyikeni katika ardhi mtafute fadhila za Mwenyezi Mungu, na mkumbukeni Mwenyezi Mungu kwa wingi ili mpate kufaulu.

وَإِذَا رَأَوْا تِجَارَةً أَوْ لَهْوًا انْفَضُّوا إِلَيْهَا وَتَرَكُوكَ قَائِمًا ۚ قُلْ مَا عِنْدَ اللَّهِ خَيْرٌ مِنَ اللَّهْوِ وَمِنَ التِّجَارَةِ ۚ وَاللَّهُ خَيْرُ الرَّازِقِينَ {11}

Na wanapoiona biashara au pumbao wanayakimbilia hayo na wakakuacha umesi­mama. Sema: Yaliyoko kwa Mwenyezi Mungu ni bora kuliko pumbao na biashara. Na Mwenyezi Mungu ni Mbora wa watoa riziki.

Aya 9 – 11: Swala Ya Ijuma

Maana.

Enyi mlioamini! Ikinadiwa Swala siku ya Ijumaa, nendeni upesi kwenye dhikri ya Mwenyezi Mungu.

Kunadi swala ni kuadhini.

Swala ya Ijumaa ni wajibu kwa Kitabu, Sunna na Ijmai. Ina rakaa mbili kwa kutanguliwa na khutba mbili. Inaitosheleza swala ya Adhuhuri. Inahusika na wanaume. Hakuna tofauti baina ya waislamu katika hayo. Isipokuwa tofauti inakuwa ni: Je, ni wajibu bila ya masharti au ni lazima aweko kiongozi au naibu wake?

Hanafi na Shia Imamia wamesema, kuweko kiongozi (wa dini) au naibu wake ni sharti, lakini Imamia wameongeza sharti la uadilifu wa huyo kion­gozi; vinginevyo itakuwa kupatikana kwake na kukosekana kwake itakuwa ni sawa. Hanafi wametosheka na kuweko tu huyo kiongozi hata kama si mwadilifu.

Shafii, Malik na Hambali wamesema ni wajibu kwa hali yoyote ile. Imamia wamesema kama hakupatikana kiongozi na akawako fakihi mwadilifu kutakuwa na hiyari baina ya Ijumaa na Adhuhuri. Ufafanuzi uko kwenye Kitabu chetu Fiqh Imam Ja’afar As-swadiq Juz. 1.

Na wacheni biashara.

Makusudio ya biashara hapa ni matumizi yoyote yatakayozuia swala ya Ijumaa, iwe biashara au la. Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ametaja biashara, kwa vile mara nyingi huwa inategemea wakati au kwa vile watu wanapen­dela sana biashara kuliko viwanda na kilimo. Mafakihi wametofautiana kuhusiana na biashara inayofanywa wakati wa kunadiwa Ijumaa, je itaswihi au itaharibika na kutokuwa na athari yoyote, lakini ina dhambi kwa muuzaji na mnunuzi?

Biashra hii - kwetu - ni sahihi. Kwa sababu kukatazwa muamala hakufa­hamishi kuharibika, lakini hilo amelipinga mwenye Mjamaul-bayan.
Hayo ni bora kwenu, kama mnajua mambo ya kheri na shari na yanay­owadhuru na kuwanufaisha.

Na itakapokwisha Swala, tawanyikeni katika ardhi mtafute fadhila za Mwenyezi Mungu, na mkumbukeni Mwenyezi Mungu kwa wingi ili mpate kufaulu.

Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kuamuru swala ameamrisha kuhangai­ka kutafuta riziki na maisha kwa biashara na mengineyo, pamoja na kumtegemea Mwenyezi Mungu, katika hali zote. Kwa kipimo hiki ndio kutahakikika kufaulu duniani na Akhera; mfano wake ni kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:

وَابْتَغِ فِيمَا آتَاكَ اللَّهُ الدَّارَ الْآخِرَةَ ۖ وَلَا تَنْسَ نَصِيبَكَ مِنَ الدُّنْيَا ۖ {77}

“Na utafute kwa aliyokupa Mwenyezi Mungu makazi ya akhera; wala usisahau fungu lako la dunia.” Juz. 20 (28:77).

Kwa maneno mengine ni kuwa hakuna tofauti mbele ya Mwenyezi Mungu baina ya anayeacha kuifanyia kazi Akhera yake na anayeacha kuifanyia kazi dunia yake.

Na wanapoiona biashara au pumbao wanayakimbilia hayo na wakakuacha umesimama.

Katika vitabu vya tafsir na Hadith kuna maelezo kuwa siku moja Mtume (s.a.w.) alipokuwa amesima akihutubia swala ya Ijumaa, uliingia msafara wa ngamia uliobeba chakula, basi maswahaba wakautokea, na hawakubakia na Mtume isipokuwa watu 12, ndio ikashuka Aya hii.

Riwaya hii imepokewa kwa njia mbalimbali na kuandikwa kwenye vitaba vya sahih, kwa sababu mmojawapo wa wapokezi wake ni Jabir bin Abdillah Al-answari, ambaye ni katika watu wakweli na mwadilifu. Kwa hiyo riwaya inakuwa ni tafsiri na ubainifu wa Aya.

Kwa mnasaba huu tunaashiria kwamba masilahi ya kimada yana athari kubwa katika maisha ya watu. Kwa sababu uchumi ni mhimili wa maisha. Hilo halina shaka. Ndio maana Mwenyezi Mungu (s.w.t.) akasema mki­maliza swala tawanyikeni katika ardhi mtafute.

Hata hivyo si sahihi kuse­ma kuwa uchumi ndio msukumo pekee wa kila harakati na msimamo wa mtu. Hapana! Kuna upande mwingine unamsukuma mtu kwenye harakati na kufanya kazi. Maswahaba wengi walimwacha Mtume akiwa amesima­ma na kwenda kwenye biashara, kama ilivyonukuu Aya, lakini wako waliobakia na Mtume, kama ilivyonukuu riwaya.

Sema: Yaliyoko kwa Mwenyezi Mungu ni bora kuliko pumbao na biashara. Na Mwenyezi Mungu ni Mbora wa watoa riziki.

Kwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kuna riziki ya dunia na ya Akhera, na baina yake hakuna kizuizi. Si amali ya Akhera inayopunguza riziki ya dunia wala sio amali ya dunia inayopunguza riziki ya Akhera; bali kila amali inay­otekeleza haja ya maisha basi hiyo ni amali ya Akhera vile vile.

Sitakua nimekwenda mbali kama nikisema kuwa kila amali aliyoyahalal­isha Mwenyezi Mungu, katika maisha haya, basi ni ngazi ya Akhera. Na aliyoyahalalisha Mwenyezi Mungu kwa waja wake ni mengi mno. Imam Ali (a.s.) anasema: “aliyowahalalishia Mwenyezi Mungu ni mengi zaidi ya aliyowaharamishia. Basi acheni yaliyo machache mchukue mengi, na muwache yaliyofinyu mchukue yaliyo na nafasi.”