read

Sura Ya Sitini Na Tatu: Al- Munafiqun

Imeshuka Madina. Ina Aya 11

بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ

Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema Mwenye kure­hemu.

إِذَا جَاءَكَ الْمُنَافِقُونَ قَالُوا نَشْهَدُ إِنَّكَ لَرَسُولُ اللَّهِ ۗ وَاللَّهُ يَعْلَمُ إِنَّكَ لَرَسُولُهُ وَاللَّهُ يَشْهَدُ إِنَّ الْمُنَافِقِينَ لَكَاذِبُونَ {1}

Wanapokujia wanafiki huse­ma: Tunashuhudia ya kuwa wewe ni Mtume wa Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu anajua kuwa hakika wewe ni Mtume wake. Na Mwenyezi Mungu anashuhudia ya kuwa hakika wanafiki ni waongo.

اتَّخَذُوا أَيْمَانَهُمْ جُنَّةً فَصَدُّوا عَنْ سَبِيلِ اللَّهِ ۚ إِنَّهُمْ سَاءَ مَا كَانُوا يَعْمَلُونَ {2}

Wamevifanya viapo vyao ni kinga, na wao wakajizuia kui­fuata Njia ya Mwenyezi Mungu. Hakika ni mabaya waliyokuwa wakiyafanya.

ذَٰلِكَ بِأَنَّهُمْ آمَنُوا ثُمَّ كَفَرُوا فَطُبِعَ عَلَىٰ قُلُوبِهِمْ فَهُمْ لَا يَفْقَهُونَ {3}

Hayo ni kwa sababu ya kuwa waliamini, kisha wakakufuru; kwa hivyo umepigwa muhuri juu ya nyoyo zao nao hawafa­hamu.

وَإِذَا رَأَيْتَهُمْ تُعْجِبُكَ أَجْسَامُهُمْ ۖ وَإِنْ يَقُولُوا تَسْمَعْ لِقَوْلِهِمْ ۖ كَأَنَّهُمْ خُشُبٌ مُسَنَّدَةٌ ۖ يَحْسَبُونَ كُلَّ صَيْحَةٍ عَلَيْهِمْ ۚ هُمُ الْعَدُوُّ فَاحْذَرْهُمْ ۚ قَاتَلَهُمُ اللَّهُ ۖ أَنَّىٰ يُؤْفَكُونَ {4}

Na unapowaona, miili yao inakupendeza, na wakisema, unasikiliza usemi wao. Kama kwamba wao ni magogo yaliy­oegemezwa. Wao hudhania kila ukelele ni kwa ajili yao. Hao ni maadui;
jihadhari nao.

وَإِذَا قِيلَ لَهُمْ تَعَالَوْا يَسْتَغْفِرْ لَكُمْ رَسُولُ اللَّهِ لَوَّوْا رُءُوسَهُمْ وَرَأَيْتَهُمْ يَصُدُّونَ وَهُمْ مُسْتَكْبِرُونَ {5}

Na wanapoambiwa: Njooni ili Mtume wa Mwenyezi Mungu awaombee maghufira, huvigeuza vichwa vyao, na unawaona wanageuka nao wamejaa kiburi.

سَوَاءٌ عَلَيْهِمْ أَسْتَغْفَرْتَ لَهُمْ أَمْ لَمْ تَسْتَغْفِرْ لَهُمْ لَنْ يَغْفِرَ اللَّهُ لَهُمْ ۚ إِنَّ اللَّهَ لَا يَهْدِي الْقَوْمَ الْفَاسِقِينَ {6}

Ni sawa kwao, ukiwatakia maghufira au usiwatakie maghufura, Mwenyezi Mungu hatawaghufiria. Hakika Mwenyezi Mungu hawaongoi watu mafasiki.

Aya 1-6: Hao Ni Maadui Jihadhari Nao

Maana

Qur’an imewasifia maswahaba na jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu na ikawasifia kwa nguvu daraja zao na vyeo vyao. Vile vile imezungumzia aina za wanafiki katika sura kadhaa na jinsi walivyong’ang’ania kuufanyia vitimbi Uislamu na manabii wake. Masimulizi kuhusiana na wanafiki hayana ukomo, kwa sababu uwongo wao na mbinu zao chafu hazina mpaka.

Kwa hiyo si ajabu kukaririka masimulizi yao, na Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kuwahusisha na sura kamili katika Kitabu chake na kuwasi­fia kwa sifa mbaya; miongoni mwazo ni hizi zifuatazo:-

Wanapokujia wanafiki husema: Tunashuhudia ya kuwa wewe ni Mtume wa Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu anajua kuwa hakika wewe ni Mtume wake.

Walidhamiria kumkufuru Mwenyezi Mungu na kumfanyia uadui Nabii wake mtukufu, wakadhihirisha mapenzi na imani kwake na kwa risala yake.

Na Mwenyezi Mungu anashuhudia ya kuwa hakika wanafiki ni waon­go.
Makusudio ya kushuhudia kwake Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ni kujua. Maana ni kuwa wanafiki wanasema kwa ndimi zao yale yasiyo nyoyoni mwao; na Mwenyezi Mungu anajua wanayoyaficha na wanayoyadhi­hirisha naye anawangojea tu.

Vile vile Nabii anajua hakika yao, lakini ameamrishwa kuwachukulia kwa dhahiri na sio kwa uhalisia; akasema: “Nimeamriwa kupigana na watu mpaka waseme: Lailahaillallah Muhammadur-rasurullah. (Hapana Mola isipokuwa Mwenyezi Mungu) wakishasema basi imehifadhika nami damu zao na mali zao, isipokuwa kwa haki yake, na hisabu yao iko kwa Mwenyezi Mungu.”

Ufasaha zaidi niliousoma kuhusiana na maudhui haya ni kauli ya Imam Ali (a.s.): “Ulimi wa mumin uko nyuma ya moyo wake na moyo wa mnafiki uko nyuma ya ulimi wake.” Yaani ulimi wa mumin unafuata moyo wake, hasemi isipokuwa analoliamini. Lakini mnafiki moyo wake unafuata ulimi wake na ulimi wake unazunguka na hawaa yake na malengo yake. Natija ya hayo ni kuwa mnafiki hana moyo isipokuwa hawa na matamanio.

Wamevifanya viapo vyao ni kinga, na wao wakajizuia kuifuata Njia ya Mwenyezi Mungu.

Mara nyingi njama za wanafiki zilikuwa zikifichuka, nao kila walipokuwa wakizungumza wanafanya kiapo ndio kinga yao kuzuia kughadhibikiwa na Mtume (s.a.w.) na kuficha njama zao dhidi ya Mtume na upinzani wao kwa risala yake.

Hakika ni mabaya waliyokuwa wakiyafanya ya vitimbi, hadaa na kuwa vigeugeu.

Hayo ni kwa sababu ya kuwa waliamini, kisha wakakufuru; kwa hivyo umepigwa muhuri juu ya nyoyo zao nao hawafahamu lolote.

Makusudio ya waliamini ni kuwa walijulikana na watu kwamba wameami­ni. Vinginevyo ni kuwa wao hawakuwahi kuamini hata chembe. Na makusudio ya wakakufuru ni kujulikana kuwa kumbe walidhihirisha imani na wakaficha ukafiri. Ama makusudio ya kupigwa muhuri juu ya nyoyo zao ni kuwa hawaongoki kwenye heri baada ya kupofushwa na hawaa na upotevu. Umetangulia mfano wake katika Juz. 5 (4:137).

Na unapowaona, miili yao inakupendeza, Wana mandhari mazuri na hisia mbaya. Kwa ibara ya Imam Ali (a.s.): “Nyoyo zao zina maradhi na nyuso zao ni safi.”

Na wakisema, unasikiliza usemi wao, kwa sababu wanazungumza maneno ya wenye ikhlasi na wanaizungumzia dunia kwa maneno ya wenye zuhudi.

Kama kwamba wao ni magogo yaliyoegemezwa. Ni mfano wa magogo, lakini wanakula na kunywa. Kila mwenye kupofu­ka na uongofu, basi ni maiti hai.

Wao hudhania kila ukelele ni kwa ajili yao. Hao ni maadui; jihadhari nao.

Wana roho za woga wa kufichuka siri zao, hawasikii sauti ila wanadhani ni sauti ya adhabu itakayowanyakuwa bila ya kujua. Woga huu ume­wazidishia lawama na uadui kwenu enyi wenye ikhlasi, basi jihadharini na njama zao na msiwape fursa kadiri mtakavyoweza.

Mwenyezi Mungu awaangamizilie mbali! Vipi wanageuzwa?

Hii ni shutuma kwa tamko la kuduia na kushangaa. Maana ni kuwa wao wamelaaniwa kwa vile wameiacha haki kwa inadi na jeuri.

Kila sifa walizosifiwa wanafiki wakati wa Mtume (s.a.w.) ni sura iliyoko kwa vibaraka wa leo wanaokula njama na maadui wa Mwenyezi Mungu na wa nchi kwa kuufanyia vitimbi uma wao.

Hakuna hatia kubwa kama kuu­fanyia hiyana uma, na hakuna fedheha kama mtu kumuuza mtu mwenza­ke.
Na wanapoambiwa: Njooni ili Mtume wa Mwenyezi Mungu awaombee maghufira, huvigeuza vichwa vyao, na unawaona wanageuka nao wamejaa kiburi.

Mtu akiwanasihi na kuwaambia tubieni mliyo nayo na Mwenyezi Mungu atawaghufiria, basi wao wanag’ang’ania batili na kuipinga haki, waki­inamisha vichwa vyao kwa dharau na kiburi. Kwa vile wao ni wakubwa kuliko wanayoyahitajia kwa Mtume; kama wanavyodai.

Ni sawa kwao, ukiwatakia maghufira au usiwatakie maghufira, Mwenyezi Mungu hatawaghufiria.

Hakuna faida ya kuwataka watengenee; kwa hiyo hakuna haja ya kuwatakia maghufira.

Ni kweli Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa maghufira mwenye kurehemu, hilo halina shaka, na rehema ya Mwenyezi Mungu ni yenye kuenea katika kila kitu, isipokuwa kwa mwenye kuikataa na akaifanyia kiburi. Kwa hiyo itakuwa si huruma kumfanyia yule anayeona kuwa haihitajii huruma yako.

Hakika Mwenyezi Mungu hawaongoi watu mafasiki, maadamu wanang’ang’ania ufuska.

Umetangulia mfano wake katika Juz. 10 (9: 80).

هُمُ الَّذِينَ يَقُولُونَ لَا تُنْفِقُوا عَلَىٰ مَنْ عِنْدَ رَسُولِ اللَّهِ حَتَّىٰ يَنْفَضُّوا ۗ وَلِلَّهِ خَزَائِنُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَلَٰكِنَّ الْمُنَافِقِينَ لَا يَفْقَهُونَ {7}

Hao ndio wanaosema: Msitoe kwa ajili ya walioko kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu, ili wawaondokee. Na hazina za mbingu na ardhi ni za Mwenyezi Mungu, lakini wanafiki hawafahamu.

يَقُولُونَ لَئِنْ رَجَعْنَا إِلَى الْمَدِينَةِ لَيُخْرِجَنَّ الْأَعَزُّ مِنْهَا الْأَذَلَّ ۚ وَلِلَّهِ الْعِزَّةُ وَلِرَسُولِهِ وَلِلْمُؤْمِنِينَ وَلَٰكِنَّ الْمُنَافِقِينَ لَا يَعْلَمُونَ {8}

Wanasema: Tukirejea Madina mwenye utukufu zaidi bila ya shaka atamfukuza aliye mny­onge. Na Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye utukufu - Yeye, na Mtume wake, na Waumini. Lakini wanafiki hawajui.

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تُلْهِكُمْ أَمْوَالُكُمْ وَلَا أَوْلَادُكُمْ عَنْ ذِكْرِ اللَّهِ ۚ وَمَنْ يَفْعَلْ ذَٰلِكَ فَأُولَٰئِكَ هُمُ الْخَاسِرُونَ {9}

Enyi mlioamini! Zisiwa­shughulishe mali zenu, wala watoto wenu, kumkumbuka Mwenyezi Mungu. Na wenye kufanya hayo ndio wenye hasara.

وَأَنْفِقُوا مِنْ مَا رَزَقْنَاكُمْ مِنْ قَبْلِ أَنْ يَأْتِيَ أَحَدَكُمُ الْمَوْتُ فَيَقُولَ رَبِّ لَوْلَا أَخَّرْتَنِي إِلَىٰ أَجَلٍ قَرِيبٍ فَأَصَّدَّقَ وَأَكُنْ مِنَ الصَّالِحِينَ {10}

Na toeni katika tulichowapa kabla hayajamfikia mmoja wenu mauti, kisha aseme: Mola wangu! Mbona hukuni­akhirishia muda kidogo nika­toa sadaka, na kuwa katika watu wema?

وَلَنْ يُؤَخِّرَ اللَّهُ نَفْسًا إِذَا جَاءَ أَجَلُهَا ۚ وَاللَّهُ خَبِيرٌ بِمَا تَعْمَلُونَ {11}

Wala Mwenyezi Mungu hata­iakhirisha nafsi yoyote inapofika ajali yake; na Mwenyezi Mungu ana habari za mnayoyatenda.

Aya 7 – 11: Mwenye Nguvu Atamfukuza Mnyonge

Maana

Hao ndio wanaosema: Msitoe kwa ajili ya walioko kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu, ili wawaondokee.

Wanaosema ni wanafiki na walioko kwa Mtume ni wahajiri walio mafukara. Matajiri wa Kianswar walikuwa wakiwasaidia hawa, ndio wanafiki wakawaambia matajiri msitoe mali zenu kwa muhajiri yoyote ili wapate kuona vibaya waweze kuondoka. Ndio Mwenyezi Mungu (s.w.t.) akawarudi kwa kuwaambia:

Na hazina za mbingu na ardhi ni za Mwenyezi Mungu, lakini wanafiki hawafahamu.

Mnawaamuru ubahili wale waliomwamini Mwenyezi Mungu na wakafanya juhudi katika njia yake, na hali Mwenyezi Mungu ndiye muum­ba wa viumbe na ndiye anayevimiliki pamoja na mali zao na ndiye mwenye kuviruzuku! Yeye anaweza kuwatajirisha waumini kwa fadhila yake, lakini nyinyi hamjui.

Wanasema: Tukirejea Madina mwenye utukufu zaidi bila ya shaka atamfukuza aliye mnyonge.

Wafasiri wamesimulia kisa cha Aya hii kinachohusiana na kiongozi wa wanafiki Abdallah bin Ubayya na vita vya Bani Mustaliq.

Hawa walikuwa ni sehemu ya Khuza’a na walikuwa wakiishi karibu na Makka. Waliona kuwa Uislamu utakuwa na nguvu katika Bara Arabu, hivyo wakajiandaa kupigana vita na Mtume (s.a.w.) wakiongozwa na kiongozi wao Harith bin Abu Dhirar. Mtume (s.a.w.) alipojua hilo akaharakisha kuwatokea na jeshi lake kabla ya wao kufika Madina.

Ibn Ubayya naye akatoka pamoja na jeshi la waislamu kwa tamaa ya ngawira. Basi Mwenyezi Mungu akampa ushindi Mtume wake dhidi ya maadui zake, wakapata mali nyingi ya ngawira. Mtume (s.a.w.)

akawaongezea mafukara wahajiri katika ngawira ili kupunguza pengo baina ya mafukara na matajiri. Ibn Ubayya akaona vibaya, akawa anawa­chochea Answar; miongoni mwa aliyoyasema ni: “Tukirejea Madina mwenye utukufu zaidi bila ya shaka atamfukuza aliye mnyonge.”

Mtukufu anajikusudia yeye mwenyewe na mnyonge anamkusudia Mtume (s.a.w.). Ndio ikashuka Aya hii na Ibn Ubayya akafedheka. Wafasiri wengi wamesema kuwa Ibn Ubayya alisema neno hili la kufuru kutokana na mzozo uliotokea baina ya mmoja wa wafuasi wake na mfanyakazi wa Umar bin Al-Khattab.

Abdallah bin Ubayya alikuwa na mtoto mwema aliyekuwa akiitwa Abdallah pia. Alipojua kuhusu baba yake, alimwendea Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) na kumwambia: “Umekwishajua alivyofanya baba yangu. Ukiwa unataka kumuua basi niamuru mimi nimuue, ili nisije nikashindwa kujizuia kumuona aliyemuua baba yangu, nikamuua mumin kwa sababu ya kafiri, nikaingia motoni.”

Mtume (s.a.w.) akamjibu: “Tutamuhurumia baba yako na tutaishi naye kwa wema muda ule atakaobakia nasi.”

Na Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye utukufu -Yeye, na Mtume wake, na Waumini.

Hii ni kumrudi Ibn Ubayya aliyejisifu kuwa mtukufu zaidi. Utukufu wa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ni kuwa yeye ndiye mtukufu zaidi kwa waja wake, utukufu wa Mtume ni dini yake kushinda dini nyingine zote na kuwashinda maadui zake, na utukufu wa waumini ni kushinda haki na watu wake.

Lakini wanafiki hawajui kwamba utukufu ni kwa imani na takua. Enyi mlioamini! Zisiwashghulishe mali zenu, wala watoto wenu, kumkumbuka Mwenyezi Mungu. Na wenye kufanya hayo ndio wenye hasara.

Mwenye kuitaamali Aya hii na ile iliyo kabla yake ataona kuwa makusu­dio ya kumkumbuka Mwenyezi Mungu hapa ni jihadi.
Kwa sababu Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kwanza ametaja utukufu wake, wa Mtume na wa waumini; kisha akawakataza na kuwahadharisha waumini, dunia isiwasahaulishe kumkumbuka Mwenyezi Mungu na akajaalia natija ya hayo ni hizaya na udhalili duniani na Akhera.

Hakuna mwenye shaka kwamba hizaya na udhalili ni natija ya kuipenda dunia na kuhofia jihadi na mauti. Hakuna linalosadikisha hakika hii kuliko maisha ya waislamu na waarabu hivi sasa jinsi yalivyo.

Na toeni katika tulichowapa kabla hayajamfikia mmoja wenu mauti, kisha aseme: Mola wangu! Mbona hukuniakhirishia muda kidogo nikatoa sadaka, na kuwa katika watu wema?

Makusudio ya kufikiwa na mauti ni kudhihiri alama zake na utangulizi wake. Maana ni kuwa chukueni fursa ya kutoa kile alichowapa Mwenyezi Mungu. Na mwenye kupuuza akangoja mpaka siku zake za mwisho mwisho atauma vidole kwa kujuta na kumnyenyekea Mwenyezi Mungu ampe muda kidogo, lakini wapi! Yaliyopita hayarudi.

Umetangulia mfano wake katika Juz. 13 (14:44).

Wala Mwenyezi Mungu hataiakhirisha nafsi yoyote inapofika ajali yake; na Mwenyezi Mungu ana habari za mnayoyatenda.

Ajali imekwishaamriwa haiwahi wala haichelewi. Mwenye kupoteza fursa hana jingine isipokuwa hasara na majuto. Umetangulia mfano wake katika Juz. 4 (3:145) kifungu cha ‘Ajali haina kinga.’ Na Juz. 8 (7:34).