Sura Ya Sabini Na Nne: Al- Muddathir
Imeshuka Makka Ina Aya 56.
بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ
يَا أَيُّهَا الْمُدَّثِّرُ {1}
قُمْ فَأَنْذِرْ {2}
وَرَبَّكَ فَكَبِّرْ {3}
وَثِيَابَكَ فَطَهِّرْ {4}
وَالرُّجْزَ فَاهْجُرْ {5}
وَلَا تَمْنُنْ تَسْتَكْثِرُ {6}
وَلِرَبِّكَ فَاصْبِرْ {7}
فَإِذَا نُقِرَ فِي النَّاقُورِ {8}
فَذَٰلِكَ يَوْمَئِذٍ يَوْمٌ عَسِيرٌ {9}
عَلَى الْكَافِرِينَ غَيْرُ يَسِيرٍ {10}
Aya 1 - 10: Ewe Uliyejigubika
Maana
Aya hizi zinaashiria wadhifa wa Muhammad (s.a.w.) kama mjumbe wa haki kwa viumbe. Pia kuna ishara kuwa watu wote mbele ya Mwenyezi Mungu wako sawa; ufafanuzi ni kama ufufatavyo:
Ewe uliyejigubika!
Huyo ni Mtume mtukufu (s.a.w.). Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amemwita kwa sifa hii kwa sababu wakati huo alikuwa katika hali hiyo kutokana na sababu fulani; kama tulivyosema mwanzo wa Sura iliyopita.
Simama uonye!
Neno linaweza kuwa na maana moja ya kilugha, lakini maana hayo, mara nyingi, yanatofautiana kulingana na msemaji na anayeambiwa. Mfano neno ‘onya,’ maana yake katika kamusi za lugha lina maana ya kuhofisha na kuhadharisha.
Kwa mfano ukimuona mtu anachimba shimo njiani na kumwambia toa onyo, utakuwa unamaanisha atangaze na kuwaonya wapita njia wasiingie shimoni. Ukimwambia mwana fakihi katika kijiji: ‘onya.’ Utakuwa unamaanisha awafundishe watu wa hapo hukumu za dini na kuwahofisha kuzihalifu.
Ama kauli ya Mtukufu kwa Nabii wake; ‘simama uonye,’ Maana yake ni pambana na waasi wenye nguvu na kiburi kwa neno la haki na uwambie: nyinyi ni wapotevu wafisadi na mtajua kesho hizaya na udhalili utakaowapata, kama hamtarudi kuuacha upotevu wenu. Ukiwambia hivi uvumilie yatakayokupata kutoka kwao na umsabihi Mola wako na kumshukuru.
Tukiona jinsi Muhammad (s.a.w.) alivyopambana na makuraishi wakiwa na nguvu na kauli na yeye hana chochote zaidi ya ikhlasi na imani, hapo ndio tunabainikiwa na yaliyomsibu kutoka kwao: walimpa sifa ya uchawi, uwongo, ushairi na hata wendawazimu. Walimshakizia watoto wamfanyie masikhara na kumtupia mawe; wakawaambia wanawake waweke miba kwenye njia atakayopita na wasafihi wamwekee uchafu na najisi njiani; hata kuna mmoja wao aliyewahi kumvua kilemba Mtume na kukifunga shingoni mwake. Fauka ya yote hayo makuraishi waliweka azimio la kumwekea vikwazo Mtume na watu wake na kumzuia asiwe na mahusiano na jamii.
Pamoja na yote hayo Nabii (s.a.w.) alivumilia na kuendelea na mwito wake bila ya kujali hali ngumu waliyompa makuraishi, wakaunda vikosi na majeshi. Akavumilia, akawa imara na subira na kuitikia kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: “Ewe uliyejigubika! Simama uonye.”
Haya yanatuwekea wazi kuwa wadhifa wa Mtume ni kuonya pamoja na uvumilivu wa tabu na mashaka. Hili ndilo jambo la kwanza. Ama la pili, ni usawa baina ya watu, linalofahamika kutokana na kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:
Na Mola wako mfanyie takbira!
Ukimwambia mtu wa kawaida: Mfanyie takbira Mwenyezi Mungu, tutafahamu kuwa unataka asema Allahf akbar; kama vile ukisema: mswalie Mtume.
Lakini kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu kumwambia Nabii wake: ‘Na Mola wako mfanyie takbira, ina maana kubwa na nzito zaidi, ambayo ni: Ewe Muhammad (s.a.w.) waambie usoni mwao wale wanojifanya majabari wenye kiburi kuwa enzi ni ya Mwenyezi Mungu na Yeye pekee ndiye mkubwa aliye juu, na kwamba nguvu, utukufu na utawala ni wa mmoja aliye pekee asiyekuwa na mshirika kutoka kwenye miungu wenu au nyinyi wenyewe au kutoka kwa wengine; na kwamba watu wote wako sawa katika kumwabudu Mwenyezi Mungu; hakuna tofauti baina ya mweusi na mweupe wala baina ya tajiri na fukara.
Muhammad aliitikia mwito wa Mola na kuwaambia mataghuti mengi tu; miongoni mwayo ni: “Hakika nyinyi na hayo mnayoyaabudu badala ya Mwenyezi Mungu ni kuni za Jahannam, mtaifikia.” Juz. 17 (21:98).
Na nguo zako zitwaharishe.
Vile vile hii inafungamana na kulingania na kuonya. Hakuna anayetia shaka kuwa usafi wa mwili na nguo ni katika imani, lakini makusudio hapa ni zaidi ya hivyo; kwamba Mtume (s.a.w.) atoe mwito wa usafi wa nje, kama vile uchafu, na usafi wa ndani, kama vile udanganyifu na hiyana, ria na unafiki, ujinga na kuhadaika na madhambi mengineyo.
Mwenyezi Mungu (s.w.t.) hayo ameyatolea ibara ya usafi wa nguo, kwa kutumia desturi ya waarabu; wanaposema: Fulani ni msafi wa mapindo ya nguo yake, wakimaanisha kuwa ni msafi wa moyo na dhati.
Na mabaya yaambae!
Hii inakuwa ni tafsiri na ufafanuzi wa kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: ‘Na nguo zako zitwaharishe,’ kama ilivyosemekana. Pia imesemekana makusudio ni ushirikina na kuabudu masanamu.
Wala usitoe kwa kutaka kingi.
Makusudio ya kutaka kingi hapa ni kujiona umefanya mengi. Maana ni kuwa Ewe Muhammad! umewafanyia watu mema mengi na fadhila nyingi, lakini usimsimbulie yeyote kwa hilo ukajiona kuwa umefanya mengi, ukasema mimi nimefanya hili ni kawafadhili lile. Kwani kila ulilojitolea ni fadhila yako kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Kuna fadhila gani na tukufu zaidi kuliko kuafikiwa kufanya kheri?
Mara nyingi huko nyuma tumeeleza kuwa makatazo yanafaa hata ikiwa anayeambiwa hana azma ya kufanya hilo linalokatazwa, mbali ya kuwa amri za Mwenyezi Mungu na makatazo yake yanawahusu waja wake wote, hata wale wenye takua.
Imesemwa katika Nahjul-balagha: “Kutekeleza haja hakuwezi kuendelea ila kwa mambo matatu: Kwa kuifanya ndogo itakuwa kubwa, kwa kuificha itajitokeza na kwa kuiharakisha itasifika.”
Na kwa ajili ya Mola wako, fanya subira!
Mwenyezi Mungu hakumwamrisha Nabii wake mtukufu jambo lolote la taklifa ya kufikisha na utume ila analikutanisha na subira, kama ilivyosemekana, kwa sababu ya kujua kwake Mwenyezi Mungu Mtukufu maudhi atakayopambana nayo kutoka kwa wenye inadi.
Basi litapopulizwa barugumu; siku hiyo, basi, itakuwa siku ngumu; kwa makafiri haitakuwa nyepesi.
Ni kama mfano wa kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:
فَإِذَا نُفِخَ فِي الصُّورِ {101}
Baada ya Mwenyezi Mungu kumwamuru Mtume wake kuwa na uvumilivu kutokana na adha ya wakadhibishaji, sasa anawahadharisha na Siku ya Kiyama ambayo itakuwa ngumu na kali sana kwao; itakuwa nzito isiyofuatiwa na wepesi. Yametangulia makumi ya Aya kuhusiana na aliyoyaandaa Mwenyezi Mungu kwa wakosefu; yakiwemo chakula, kinywaji na adhabu kali.
ذَرْنِي وَمَنْ خَلَقْتُ وَحِيدًا {11}
وَجَعَلْتُ لَهُ مَالًا مَمْدُودًا {12}
وَبَنِينَ شُهُودًا {13}
وَمَهَّدْتُ لَهُ تَمْهِيدًا {14}
ثُمَّ يَطْمَعُ أَنْ أَزِيدَ {15}
كَلَّا ۖ إِنَّهُ كَانَ لِآيَاتِنَا عَنِيدًا {16}
سَأُرْهِقُهُ صَعُودًا {17}
إِنَّهُ فَكَّرَ وَقَدَّرَ {18}
فَقُتِلَ كَيْفَ قَدَّرَ {19}
ثُمَّ قُتِلَ كَيْفَ قَدَّرَ {20}
ثُمَّ نَظَرَ {21}
ثُمَّ عَبَسَ وَبَسَرَ {22}
ثُمَّ أَدْبَرَ وَاسْتَكْبَرَ {23}
فَقَالَ إِنْ هَٰذَا إِلَّا سِحْرٌ يُؤْثَرُ {24}
إِنْ هَٰذَا إِلَّا قَوْلُ الْبَشَرِ {25}
سَأُصْلِيهِ سَقَرَ {26}
وَمَا أَدْرَاكَ مَا سَقَرُ {27}
لَا تُبْقِي وَلَا تَذَرُ {28}
لَوَّاحَةٌ لِلْبَشَرِ {29}
عَلَيْهَا تِسْعَةَ عَشَرَ {30}
وَمَا جَعَلْنَا أَصْحَابَ النَّارِ إِلَّا مَلَائِكَةً ۙ وَمَا جَعَلْنَا عِدَّتَهُمْ إِلَّا فِتْنَةً لِلَّذِينَ كَفَرُوا لِيَسْتَيْقِنَ الَّذِينَ أُوتُوا الْكِتَابَ وَيَزْدَادَ الَّذِينَ آمَنُوا إِيمَانًا ۙ وَلَا يَرْتَابَ الَّذِينَ أُوتُوا الْكِتَابَ وَالْمُؤْمِنُونَ ۙ وَلِيَقُولَ الَّذِينَ فِي قُلُوبِهِمْ مَرَضٌ وَالْكَافِرُونَ مَاذَا أَرَادَ اللَّهُ بِهَٰذَا مَثَلًا ۚ كَذَٰلِكَ يُضِلُّ اللَّهُ مَنْ يَشَاءُ وَيَهْدِي مَنْ يَشَاءُ ۚ وَمَا يَعْلَمُ جُنُودَ رَبِّكَ إِلَّا هُوَ ۚ وَمَا هِيَ إِلَّا ذِكْرَىٰ لِلْبَشَرِ {31}
Aya 11 - 31: Niache Peke Yangu Na Niliyemuumba
Kisa Kwa Ufupi
Walid bin Al-Mughira Al-Makhzumi, alikuwa ni miongoni mwa vigogo wa kikuraishi, akiwa na mali nyingi na watoto. Siku moja akamsikia Mtume akisoma Aya mojawapo ya Qur’an, akasema: “Hii sio maneno ya binadamu wala jinni. Wallah, hakika kauli yake ‧ yaani Qur’an ‧ ina utamu na ina mvuto na kwamba juu yake kuna matunda na chini yake kumejaa. Hakika iko juu na haishindwi.”
Basi makuraishi waliposikia hivi wakahofia maneno ya Walid kama yakienea kwa watu, watamwamini Muhammad (s.a.w.). Wakamtaka Walid ampinge Mtume. Akasema nisemeje sasa? Niseme ni mwendawazimu, nani ataamini? Au niseme ni kuhani, naye hakuwahi kuwa kuhani kabisa.
Nikisema ni mshairi, yeye hajawahi kutamka shairi na nikisema ni mwongo, hakuna yeyote aliyewahi kusikia uwongo kwake. Kisha akafiria akaona ampe sifa ya uchawi na kwamba yeye ameichukua Qur’an kutoka kwa wachawi.
Maana
Niache peke yangu na niliyemuumba.
Maneno yanaelekezwa kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.). Makusudio yake ni kumkemea na kumhadharisha Walid bin Mughira kwa maafikiano ya wafasiri. Maana ni kuwa niachie mimi huyo ewe Muhammad, usijishughulishe naye, wala na yale anayokuzulia. Mimi peke yangu ndiye nitakayempiga vita na kumpa adhabu.
Mwenyezi Mungu alifikia ghadhabu hii kwa Walid, kwa sababu yeye alipituka mipaka na uovu; akakufuru neema ya Mwenyezi Mungu na akaipinga haki na kuifanyia kiburi haki na watu wake. Kila mwenye kuipinga haki basi ni mlengwa wa ghadhabu hii na makemeo haya; kama vile Walid Bin Mughira, kwa vile sababu ya kushuka Aya haihusiki na aliyeteremshiwa tu, bali inaenea, kama tulivyosema mara nyingi.
Kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: Na nikamjaalia kuwa na mali mengi, inaashiria kuwa linasobabisha na kuleta msukumo wa kufanya uovu ni utajiri na wingi wa mali. Aya kadhaa zianaashria hakika hii, ikiwemo Aya 11 ya sura iliyopita na pia kauli yake Mwenyezi Mungu akimsimulia muasi aliyojifaharisha kwa mtu mwema:
أَنَا أَكْثَرُ مِنْكَ مَالًا {34}
Inatosha kuwa ni ushahidi wa hayo kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:
إِنَّ الْإِنْسَانَ لَيَطْغَىٰ {6}
أَنْ رَآهُ اسْتَغْنَىٰ {7}
Kwa kutegemea Aya hizi na nyingine zilizo mfano wake, inawezekana kusema, ijapokuwa ni kwa kubuni, kwamba asili ni kuwa kila tajiri ni muasi, mpaka ithibitike kinyume. Imelezwa kwenye Nahjul-balagha: “Ni uzuri ulioje wa matajiri kuwanyenyekea mafukara kwa kutaka yaliyoko kwa Mwenyezi Mungu! Na uzuri zaidi kuliko huo ni maringo ya mafukara kwa matajiri kwa kumtegemea Mwenyezi Mungu.”
Kuna Hadith isemayo: “Heri zote ni za aliyesilimu na ikawa maisha yake ni kutosheka.. ewe Mwenyezi Mungu mruzuku Muhammad na kizazi cha Muhammad kujichunga na kutosheka.”
Na wana wanaoonekana, wakiwa pamoja naye wakishindana kumhudumia. Na nikamtengenezea mipango. Nimemsahilishia njia ya jaha na mali akiogelea kwenye neema atakavyo.
Kwa mnasaba huu tunaashiria kwamba neema za dunia hazifahamishi kuridhiwa na Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu (s.w.t.) anasema: “Hakika maisha ya dunia ni mchezo na upuzi tu.” Juz. 26 (47:36). Kwenye Hadith amesema: “ Lau dunia mbele ya Mwenyezi Mungu italinganishwa na kheri kwa ubawa wa mbu, basi kafiri asingekunywa hata tama moja la maji.”
Ilijitokeza dunia kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu, mbora wa viumbe wa Mwenyezi Mungu, akaikataa, lakini Walid, muovu wa viumbe wa Mwenyezi Mungu, ilikithiri mali yake, kisha anatumai nimzidishie! Yaani ana tamaa ya kuzidishiwa mali yake ili azidi uovu na uadui.
Haiwezekani kuchanganyika wema na tamaa katika moyo mmoja. Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) anasema: “Tamaa ni ufunguo wa kila maasi na ni msingi wa kila hatia na ni sababu ya kuanguka mambo mema.”
Sivyo! Kwani hakika yeye alikuwa akizifanyia inadi Aya zetu!
Tokomea mbali ewe mpinzani mwenye hiyana! Hivi una tamaa kwa Mungu na wewe unaifanyia inadi haki na kuizuia kwa kutangaza vita kwa watu wa haki? Wapokezi wanasema kuwa iliposhuka tu Aya hii Walid alibadilika kutoka kwenye enzi na kuwa dhalili, utajiri kuwa fukara, na akafa na hali mbaya.
Amesema kweli aliyoesema: “Hawakusema watu kwa jambo lolote kuwa lina heri ila kuna shari iliyofichwa na nyakati.” Hii ni duniani, ama malipo yake huko Akhera yanaelezwa na Aya hii:
Nitamtesa kwa mateso ya hali ya juu.
Hali ya juu inaweza kuwa ni ukali na mashaka na inaweza kuwa ni zaidi. Mfumo wa maneno unajulisha maana zote mbili na kwamba adhabu siku hiyo itazidi kiwango na kiaina, muda baada ya muda.
Hakika yeye alifikiri na akapima.
alifikiria kuhusu Qur’an na akaandaa kauli ya uzushi kwamba Qur’an ni uchawi ulionukuliwa, kama itakavyokuja mbele.
Basi amelaaniwa! Vipi alivyopima! Tena amelaaniwa! Vipi alivyopima!
Amelaaaniwa kisha akalaaniwa katika kufikiria kwake na kupanga kwake kauli, vitendo na makusudio yake yote. Hakuna kitu kinachofahamisha ufasaha zaidi kuliko kukaririka laana kwa waovu.
Kisha akatazama. Baadaa ya kufikiria aliinua jicho lake kwa vigogo wa kikuraishi, kisha akakunja uso, kwa kukunja nyusi zake na akanuna; uso ukamuiva.
Kisha akageuka, na akatakabari.
Alihakikisha alipofikiria kuwa Qur’an ni haki isiyokuwa na shaka, lakini pamoja na hayo aliipinga na akaitukukia akasema: “Haya si chochote ila ni uchawi ulionukuliwa. Haya si chochote ila kauli ya binaadamu,” aliyoichukua Muhammad kutoka kwa makuhani wa kichawi.
Picha hii ya Walid iliyopigwa na Qur’an, ya kufikiri, kupima, kukunja uso na kununa, inatujulisha kuwa yeye alikuwa hana la kufanya katika kupanga uwongo kwenye jambo analoliamini kuwa ni haki na kweli.
Nitamtia kwenye Moto wa Saqar. Atakayetiwa ni huyo huyo Walid. Saqar ni miongoni mwa majina ya Jahannam. Na nini kitakujuulisha ni nini huo Moto wa Saqar? Kwani umefika kikomo cha kutisha; miongoni mwayo ni kwamba huo haubakishi yeyote katika wakosefu wala hauachi aina yoyote ya adhabu ila inawashushia na unababua ngozi.
Makusudio ya kubabua hapa ni kuiva, kama alivyosema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
كُلَّمَا نَضِجَتْ جُلُودُهُمْ بَدَّلْنَاهُمْ جُلُودًا غَيْرَهَا {56}
Juu yake wapo kumi na tisa.
Yaani juu ya hiyo Saqar. Kumi na tisa ni walinzi wa Jahannam. Je, kumi na tisa ni idadi, au aina au ni viongozi? Mwenyezi Mungu ndiye ajuaye zaidi.
Kuna riwaya isemayo kuwa Abu Jahl, aliwaambia makuraishi: ‘’Hamna maana ninyi! Hivi watu kumi katika nyinyi wanashindwa kumshika mmoja katika hao 19?”
Mmoja alieyitwa Abul-Mushid alisema: “Mimi peke yangu nitawatoshea na 17, nyinyi shikeni wawili tu.” Huyu alisema kwa madharau kama alivyosema Abu Jahl.
Na hatukuwafanya walinzi wa Moto ila Malaika.
Walinzi wa moto si katika aina ya binadamu; bali ni malaika wakali wenye nguvu; hakuna anayewazidi nguvu isipokuwa aliye pekee, Mwenye nguvu ambaye ameumba kila kitu.
Kama kwamba muulizaji ameuliza: Nini makusudio ya kutajwa idadi, jambo ambalo linafungua mlango wa madharau kwa wapinzani? Ndio akajibu Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kwamba kutaja kwake kuna faida tatu:
1. Wala hatukufanya idadi yao ila kuwa jaribio kwa wale waliokufuru.
Ndio! Mwenyezi Mungu anajua kwamba washirikina watakaposikia idadi watacheka na kufanya stihizai, lakini pamoja na hayo ametaja, kwa sababu haki inapaswa itangazwe, hata kama natija yake ni madharau ya wanaodharau. Kwa maneno mengine ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) anawajaribu waja, naye ni mjuzi zaidi kuliko nafsi zao. Anawajaribu kwa raha na dhiki. Vile vile anasema haki ili vijitokeze vitendo vyao vinavyostahiki thawabu na adhabu.
Kutajwa idadi kumedhihirisha hakika ya washirikina ya kudharau ghaibu, hivyo wakastahiki ghadhabu na adhabu ya Mwenyezi Mungu; kama kulivyodhihirisha hakika ya waumini wakastahiki radhi za Mwenyezi Mungu na thawabu zake, kama yatakavyokuja maelezo. Zaidi ya hayo ni kuwa kutangaza Mtume neno la haki bila ya kuangalia yatakayompata kwa ajili yake, ni dalili mkataa kwamba hana jingine analolitaka isipokuwa kuihakikisha haki na kuibatilisha batili.
2. Ili wawe na yakini waliopewa Kitabu.
Ulama wa kiyahudi na wa kinaswara wakati huo walishuhudia kwa imani na yakini kwamba walinzi idadi yao ni 19, kwa sababu hilo linaafikiana na waliyoyasoma katika Tawrat na Injil.
3. Na wazidi imani wale walioamini.
Wahyi wa mambo ya ghaibu unawazidisha makafiri upinzani na jeuri na waumini wanazidi imani. Imesemekana kuwa waumini huzidi yakini wakiambiwa na watu wa Kitabu kuwa idadi imo kwenye vitabu vyao. Usawa ni kuwa kila Aya katika Aya zake Mwenyezi Mungu Mtukufu inawazidisha waumini yakini kwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake; ni sawa watu wa Kitabu wakubali au wapinge. Ni kweli kwamba kukubali kwao ni hoja kwa wapinzani.
Wala wasiwe na shaka wale waliopewa Kitabu na waumini.
Huu ni ufafanuzi na msisitizo wa yaliyokuwa kabla yake, kwa sababu kutokuweko shaka ni kuwa na yakini na kuzidi imani.
Na wapate kusema walio na maradhi katika nyoyo zao na makafiri: Mwenyezi Mungu amekusudia nini kwa mfano huu?
Vile vile huu ni ufafanuzi na msisitizo wa kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: “Wala hatukufanya idadi yao ila kuwa jaribio kwa wale waliokufuru,” pamoja na kufafanua aina ya makafiri ambao ni wanafiki walio na maradhi katika nyoyo zao. Umetangulia mfano wake katika Juz. 1 (2:26).
Ndio kama hivyo Mwenyezi Mungu humpoteza amtakaye na humwongoza amtakaye.
Mwenye kufuata njia ya upotevu Mwenyezi Mungu humpoteza:
فَلَمَّا زَاغُوا أَزَاغَ اللَّهُ قُلُوبَهُمْ ۚ {5}
فِي قُلُوبِهِمْ مَرَضٌ فَزَادَهُمُ اللَّهُ مَرَضًا ۖ {10}
Na mwenye kufuata njia ya uongofu Mwenyezi Mungu humuongoza: “Na ambao wameongoka anawazidishia uongofu.” Juz. 26: (47:17).
Umetangulia mfano wake katika Juz. 22 (35:8).
Na hapana ajuae majeshi ya Mola wako ila Yeye.
Askari wa Mwenyezi Mungu sio wale 19 tu, viumbe wote wanatii matakwa hata wanyama, wadudu, ndege, upepo, matetemeko, matufani na mengineyo ambayo hakuna anayejua isipokuwa mwanzishaji wa viumbe na mrudishaji.
Na huo si chochote ila ni ukumbusho kwa watu.
Huo ni huo moto wa Saqar. aliyoumba Mwenyezi Mungu (s.w.t.) na kuwahadharisha nao ili wayaogope maasi kwa ndani na nje.
كَلَّا وَالْقَمَرِ {32}
وَاللَّيْلِ إِذْ أَدْبَرَ {33}
وَالصُّبْحِ إِذَا أَسْفَرَ {34}
إِنَّهَا لَإِحْدَى الْكُبَرِ {35}
نَذِيرًا لِلْبَشَرِ {36}
لِمَنْ شَاءَ مِنْكُمْ أَنْ يَتَقَدَّمَ أَوْ يَتَأَخَّرَ {37}
كُلُّ نَفْسٍ بِمَا كَسَبَتْ رَهِينَةٌ {38}
إِلَّا أَصْحَابَ الْيَمِينِ {39}
فِي جَنَّاتٍ يَتَسَاءَلُونَ {40}
عَنِ الْمُجْرِمِينَ {41}
مَا سَلَكَكُمْ فِي سَقَرَ {42}
قَالُوا لَمْ نَكُ مِنَ الْمُصَلِّينَ {43}
وَلَمْ نَكُ نُطْعِمُ الْمِسْكِينَ {44}
وَكُنَّا نَخُوضُ مَعَ الْخَائِضِينَ {45}
وَكُنَّا نُكَذِّبُ بِيَوْمِ الدِّينِ {46}
حَتَّىٰ أَتَانَا الْيَقِينُ {47}
فَمَا تَنْفَعُهُمْ شَفَاعَةُ الشَّافِعِينَ {48}
فَمَا لَهُمْ عَنِ التَّذْكِرَةِ مُعْرِضِينَ {49}
كَأَنَّهُمْ حُمُرٌ مُسْتَنْفِرَةٌ {50}
فَرَّتْ مِنْ قَسْوَرَةٍ {51}
بَلْ يُرِيدُ كُلُّ امْرِئٍ مِنْهُمْ أَنْ يُؤْتَىٰ صُحُفًا مُنَشَّرَةً {52}
كَلَّا ۖ بَلْ لَا يَخَافُونَ الْآخِرَةَ {53}
كَلَّا إِنَّهُ تَذْكِرَةٌ {54}
فَمَنْ شَاءَ ذَكَرَهُ {55}
وَمَا يَذْكُرُونَ إِلَّا أَنْ يَشَاءَ اللَّهُ ۚ هُوَ أَهْلُ التَّقْوَىٰ وَأَهْلُ الْمَغْفِرَةِ {56}
Aya 32 – 56: Tukijiingiza Pamoja Na Wanaojiingiza
Na hawatakumbuka isipokuwa atake Mwenyezi Mungu.
Maana
Sivyo! Komeni enyi washirikina kucheza na moto na kuwadharau walinzi wake.
Naapa kwa mwezi na kwa usiku unapokucha na kwa asubuhi inapopambazuka. Hakika huo ni mojawapo ya mambo makubwa.
Baada ya Mwenyezi Mungu kuwakemea wapinzani, sasa anaapa kwa mwezi, usiku na mchana kwamba Moto ni kweli isiyokuwa na shaka na ni adhabu ambayo haina mfano na hakuna adhabu nyingine inayoishinda hiyo. Kuapa kwa maumbile haya ni kuashiria kuwa wenye busara wanapata dalili ya mtengenezaji kutokana na ubunifu wa utengenezaji, na kwamba mwenye kufanya kitu bila ya chochote, anaweza kuipa uhai mifupa iliyochakaa.
Ni onyo kwa watu, kwa anayetaka miongoni mwenu kwenda mbele au kurudi nyuma.
Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amewahadharisha waja na moto na akawafahamisha njia yake na kuwambia jichagulieni wenyewe kuundea au kuwa mbali nao. amejitoa lawamani Mwenye kuonya .
Kila nafsi iko kwenye rahani kwa iliyoyachuma.
Hii ni sababu ya kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: Kwa anayetaka kwenda mbele au kurudi nyuma. Maana ni kuwa jichagulieni wenyewe, nyinyi mmefungika kwenye rahani ya mliyoyafanya na mna deni la mliyoyatanguliza; ikiwa ni heri basi mtalipwa heri na ikiwa ni shari basi ni shari. Umetangulia mfano wake katika Juz. 21 (30:44).
Isipokuwa watu wa kuliani.
Qur’an inawaita watu wa upande wa kulia wale wanaomcha Mungu na wakosefu inawaita watu wa upande wa kushoto, Tazama Juz. 27 (56: 8-9, 38-41).
Maana ni kuwa hakuna mtu yeyote ila nafsi yake inakuwa ni mateka wa matendo yake; isipokuwa wenye takua, wao wamelipa madeni yao na wamezifungua nafasi zao kwa matendo yao mema, na malipo yao ni Bustani za milele zinazopitiwa na mito.
Watakua katika mabustani wakiulizana kuhusiana na wakosefu: Ni kipi kilichowapeleka Motoni.
Baada ya kutulia watu wa Peponi wataulizana wenyewe kwa wenyewe: Wako wapi wakosefu waliokuwa wakitupa tabu?
Mwenyezi Mungu (s.w.t.) atawaonyesha walipo katika Jahannam, ili wazidi furaha, kama yalivyoeleza baadhi ya mapokezi.
Atawauliza kwa kuwatahayariza: ni jambo gani lililowapeleka kwenye makazi haya? Watasema kwa lugha ya hali au ya maneno: Hatukuwa miongoni mwa waliokuwa wakiswali. Yaani hatukuacha machafu na maovu duniani. Tafsiri hii tumeichukua katika kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:
إِنَّ الصَّلَاةَ تَنْهَىٰ عَنِ الْفَحْشَاءِ وَالْمُنْكَرِ ۗ {45}
Wala hatukuwa tukiwalisha masikini, bali tulilimbikiza mali bila ya kuyatoa katika njia ya Mwenyezi Mungu. Na tulikuwa tukijiingiza pamoja na wanaojiingiza.
Makusudio ya kujiingiza hapa ni kupiga porojo. Maana ni kuwa tukidharau kila jambo isipokuwa upuzi na mchezo na tukijiingiza kila mahali isipokuwa kwenye haki na kheri.
Na tulikuwa tukikadhibisha siku ya hukumu, mpaka ikatujia yakini, yaani mauti.
Neno hukumu tumelifasiri kutokana neno Din. Sheikh Abdul-Qadir Al-Maghribi anasema: “Siku ya Kiyama imeitwa hivyo kwa sababu ndani yake mna malipo, hisabu na hukumu. Yote haya ni katika maana ya neno din. Vile vile inaitwa siku ya ufufuo, kuhukumiwa watu, mlipaji na hakimu.
]
Wamesema Ali bin Abi Twalib ni hakimu wa umma huu baada ya Nabii; yaani baada ya Nabii (s.a.w.) yeye alikuwa na aina ya pekee ya kuhukumu baina ya mahasimu. ( kwa kutumia neno din kwa maana ya hukumu)”
Basi hautawafaa uombezi wa waombezi
Hakuna muombezi atakayefaa wala udhuru utakaokubalika, isipokuwa toba na matendo mema.
Basi wana nini wanapuuza ukumbusho huu; kama kwamba wao ni punda waliotimuliwa, wanaomkimbia simba.
Wanaambiwa washirikina, makusudio ya ukumbusho ni Qur’an na punda ni wa mwituni. Maana ni kuwa wananini hawa wanakimbia uongofu na haki kama wanaokimbia mauti?
Bali kila mmoja katika wao anataka apewe nyaraka zilizofunuliwa.
Kuna riwaya isemayo kuwa washirikina walimwambia Mtume wa Mwenyezi Mungu: “Hatutakuamini mpaka umteremshie kila mmoja wetu waraka usemao fulani bin fulani mfuate Muhammad (s.a.w.).”
Iwe sawa riwaya hii au la, lakini inafasiri dhahiri ya Aya. Hilo linatiliwa nguvu na Aya isemayo:
وَلَنْ نُؤْمِنَ لِرُقِيِّكَ حَتَّىٰ تُنَزِّلَ عَلَيْنَا كِتَابًا نَقْرَؤُهُ ۗ {93}
Lakini wao hawawezi kuamini hata kama wangeliitikiwa matakwa yao, kama ilivyoliweka wazi hilo kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:
وَلَوْ نَزَّلْنَا عَلَيْكَ كِتَابًا فِي قِرْطَاسٍ فَلَمَسُوهُ بِأَيْدِيهِمْ لَقَالَ الَّذِينَ كَفَرُوا إِنْ هَٰذَا إِلَّا سِحْرٌ مُبِينٌ {7}
Siri katika hilo ni kupupia kwao masilahi yao na mambo yao na wala sio hasadi, kama walivyosema baadhi ya wafasiri. Dalili ya hayo tuliyoyasema ni kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu iliyokuja moja kwa moja: Sivyo! Bali hawaiogopi Akhera. kwa sababu wao hawajui isipokuwa maisha ya dunia wala hawategemei isipokuwa anasa zake na starehe. Ama ubinadamu, haki na heri kwao ni maneno yasiyokuwa na maana.
Sivyo! Kwa hakika hiyo ni ukumbusho.
Mara nyingine tena Mwenyezi Mungu (s.w.t.) anawakemea wakadhibishaji na kuwabainishia kuwa hii Qur’an ni mawaidha kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwenda kwa waja wake na wala sio kauli ya mchawi wala mshairi.
Basi atakaye ataukumbuka.
Yaani atanufaika na hukumu zake na mawaidha yake.
Na hawatakumbuka isipokuwa atake Mwenyezi Mungu.
Unaweza kuuliza: Kauli yake Mwenyezi Mungu: ‘atakaye ataukumbuka,’ inaonyesha kuwa mtu ana hiyari ya uhuru wake na utashi wake. Na kauli hii ‘Hawatakumbuka isipokuwa atake Mwenyezi Mungu,’ inaonyesha kuwa mtu hana hiyari, anaendeshwa na hana uhuru wala utashi; sasa ni vipi mgongano huu?
Jibu: Makusudio ya matakwa ya kwanza, ni kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amemwachia mtu hiyari ya kujichagulia imani au ukafiri. Na makusudio ya ya matakwa ya pili ni kuwa mpinzani anayekana hawezi kuamini mpaka Mwenyezi Mungu amlazimishe kwa nguvu. Kwa hiyo maana ya kauli mbili ni kuwa Mwenyezi Mungu amemwamchia mtu hiyari ya kuamini au kukufuru; kama isemwavyo kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:
وَقُلِ الْحَقُّ مِنْ رَبِّكُمْ ۖ فَمَنْ شَاءَ فَلْيُؤْمِنْ وَمَنْ شَاءَ فَلْيَكْفُرْ ۚ {29}
Juz. 15 (18:29).
Lakini mpinzani mwenye inadi hawezi, kwa hali yoyote ile, ila akifanyishwa kwa nguvu na Mwenyezi Mungu; na hili haliwezi kuwa kabisa, kwa vile linapingana na uadilifu wa Mwenyezi Mungu na hikima yake. Kwa sababu uadilifu wake Mwenyezi Mungu Mtukufu na desturi yake kwa waja wake, ni kuwabainishia njia ya heri na kuwahimiza na kuwabinishia njia ya shari na kuwahadharisha nayo.
Kwa hiyo kila mmoja anakuwa na hiyari yeye mwenyewe ya mwishilio wake; vinginevyo thawabu na adhabu zitakua hazina maana yoyote.
Hili linaungwa mkono na kauli yake Mwenyezi Mungu iliyokuja moja kwa moja:
Takua ni kwake na maghufira ni yake.
Yaani yeye Mwenyezi Mungu ambaye imetukuka hikima yake, ndiye anayestahiki kutiiwa katika maamrisho yake na makatazo yake, na kuogopewa kwa ghadhabu yake na adhabu yake. Vile vile yeye ndiye mwenye kuwahurumia waja na kuwasamehe wanaotubia na kurejea.
Kwa mnaeno machache na ya uwazi zaidi ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amemuumba mtu akiwa na hiyari, mwenye akili na utashi, akamtofautisha na mnyama kwa hilo; kwa hiyo akamkalifisha utiifu na msimamo. Kama angelitaka Mwenyezi Mungu angelimuondolea utashi wa akili na kumfanya kama mnyama au chini yake zaidi.