read

Shi’ah na Hadith

Kwa hakika Mashi’ah wana mchango mkubwa sana katika uandishi wa Hadith na katika hali ambayo ni sahihi. Na wa kwanza kabisa ni mchango wa Al Imam 'Ali ibn Abi Talib a.s. ambao hauna kifani wala usioelezeka, Je! litakuwa ni kosa gani iwapo wafuasi wake watamfuata yeye katika kuzidumisha na kuzihifadhi Sirah na sunnah za Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w.? Katika historia vile vile tunapata mambo yaliyowazi kabisa kuwa kulikuwa na baadhi ya Ma-Sahaba wa Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. ambao walikuwa wakikataa kabisa kusiandikwe Hadith kwa sababu ya visingizio kuwa vilikuwa vikigongana na ayah za Qur'an Tukufu. Na wapo Ma-Sahaba wengine pia wameadhibiwa vifungo na adhabu mbalimbali kwa ajili ya kunakili na kusambaza Hadith za Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. Kwa hakika Ibn Hajar ana andika katika utangulizi wa Futuh al-Bari, jambo moja la kustaajabisha, kuwa yeye anasema:
“Mwanzoni mwa Waislam kulikuwa na utata katika uandishi wa Hadith, kwa sababu baadhi yao walikuwa wanasema kuwa ni karaha kuziandika. Na katika wale waliokuwa wakisema kuwa ni makruh alikuwepo ‘Umar bin Al Khattab, Ibn Masoud na Abu Sai’d Al Khudhri. Na katika upande wa pili ambao walikuwa wakieneza Hadith kwa usahihi walikuwa ni Al Imam 'Ali ibn Abi Talib a.s., mwana wake Al Imam Hasan ibn 'Ali ibn Abi Talib a.s. na vile vile Anas alikuwapo. Na kwa hakika Mashi’ah wamekuwa mbele katika kueneza Hadith zilizokuwa sahihi na miongoni mwao nawaletea majina yao:

1. Mtumwa wa Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. aliyekuwa akiitwa Abu Rafi’, na ambaye alikuwa miongoni mwa wale Waislam wa mwanzoni kabisa.
Bwana ‘Abbas, mjomba wake Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. ndiye aliyekuwa amempa zawadi huyo, na wakati huyo mtumwa alipo mpa habari Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. kuwa mjomba wake huyo Bwana ‘Abbas ameukubalia Uislam, basi Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. kwa kusikia hiyo habari nJe!ma alimfanya huru huyo mtumwa kwa sababu ya kuleta habari hizo njema. Katika fadhila zake tunaona kuwa yeye alifanya Hijra mara mbili, na amesali katika Qibla zote mbili na amefanya Bay’a ya Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. mara mbili.

Na vile vile ameshiriki katika vita vya Jihad vingi sana pamoja na Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w., na baada ya kifo cha Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. yeye hakumwacha Al Imam 'Ali ibn Abi Talib a.s. na daima alikuwa naye pamoja. Alikwenda na Al Imam 'Ali ibn Abi Talib a.s. hadi Kufa, nchini Iraq na alishiriki naye katika vita vitukufu vyote vilivyotokea na alikuwa ni mtu mmoja aliyekuwa akiaminiwa sana na Al Imam 'Ali ibn Abi Talib a.s. kiasi kwamba yeye alikuwa akitunza Baitul Maal pia.
Yeye alifariki akiwa na umri wa miaka themanini na tano. Na yeye ni miongoni mwa Rawi wa Kishi’ah1 wanaoaminiwa na kusadikiwa, naye ameandika kitabu kimoja ambamo ameandika riwaya za Al Imam 'Ali ibn Abi Talib a.s. kinachoitwa Kitabu Sunan Wal-ahkam Wal-Qadhaya. Katika vitabu vya ‘Ilmul Rijal kitabu hiki ni muhimu sana na chenye faida kubwa sana.

2. Bwana Salman Muhammad (Al Farsi) ambaye baada ya kifo cha Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. aliandika habari za Jasliq (au ‘Al-Jathalique’- kitabu cha ahadith) kwa niaba ya Mfalme wa Roma.

3. Asbagh bin Nabata, aliandika usia wa Al Imam 'Ali ibn Abi Talib a.s. alioumfanyia Bwana Malik Ashtar, vile vile aliandika Nasiha alizomfanyia mtoto wake Muhammad. Asbagh bin Nabata alikuwa ni mmoja wa Ma-Sahaba wa karibu sana wa Al Imam 'Ali ibn Abi Talib a.s.

4. Suleim bin Kais Al Hilali, yeye ameandika kitabu chenye Ahadith ambacho kinatumika mpaka sasa hivi na kwa mara ya mwisho kilikuwa kimechapwa huko Najaf Al Ashraf, nchini Iraq. Hadith zake zimetokana na Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. mwenyewe na vile vile Al Imam 'Ali ibn Abi Talib a.s., Miqdad, Salman, Abudhar na wapenzi wa Ahlul Bayt a.s.

5. Mitham al-Tammaar yeye alikuwa mmoja wa Ma-Sahaba mashuhuri na mshupavu wa Al Imam 'Ali ibn Abi Talib a.s. yeye naye ameandika kitabu ambacho Sheikh Saduq amekitumia katika ‘Aamali na vile vile Tabari ametumia katika Basharatul Mustafa.

6. Zaid bin Wahab Aljahni ambaye ametunga kitabu kimoja ambamo ameandika hotuba zote za Al Imam 'Ali ibn Abi Talib a.s. alizokuwa akizitoa siku za Ijumaa na Idi, kwa hakika ameufanyia ‘umma huu ihsani kubwa sana. Ibn Hajar na Ma’ulamaa wengine wanasema kuwa huyu bwana Zaid bin Wahab Thiqqah na wanampa Ukuu, yeye amefariki katika mwaka takribani 96 Hijriyyah.

7. Mkusanyiko mkubwa kabisa wa Semi na Dua za Ma’sumiin a.s. yanayojulikana kama Sahifa al-Kamila na vile vile inajulikana kama Zaburi Ali-Muhammad. Kitabu hicho kimekuwa tangia uhai wa
al-Imam Zaynul 'Abediin ibn Hussein ibn 'Ali ibn Abi Talib a.s. na humo kumeandikwa semi zao n.k. ambayo yalikuwa yamesimamiwa kikamilifu na al-Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. ndiye aliyefanya mpango huo.

8. Jabir bin Yazid bin Al Harith Al Jaufi, yeye ameziandika yaani yeye katika nuru ya ahadith za Ma’sumin a.s. ameandika Tafsiri, vita vya Jamal, Siffin, na Naherwaan, na vile vile ameandika kuuawa kwa al- Imam 'Ali ibn Abi Talib a.s. na al-Imam Hussein ibn 'Ali ibn Abi Talib a.s. Yeye amefariki katika mwaka 128 Hijriyyah.

9. Bwana Abu Hamza Thumali (aliyefariki mwaka 150 Hijriyyah) alikuwa mmoja Sahabi mashuhuri mwaminifu kabisa wa Al Imam Zaynul 'Abediin ibn Hussein ibn 'Ali ibn Abi Talib a.s. na Al Imam Muhammad al-Baqir a.s. na ameweza kutunga kitabu kiitwacho Annawadir Wa-Dhuhud. Vile vile amefanya tafsiri ya Qur'an Tukufu pia.

10. Vile vile miongoni ma Ma-Sahaba wa Al Imam Zaynul 'Abediin ibn Hussein ibn 'Ali ibn Abi Talib a.s. na Al Imam Muhammad al-Baqir a.s. alikuwa akiitwa Muhammad bin Keis Al Bijalli ambaye ameandika kitabu kiitwacho Qadhaya Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s.

11. Aban bin Taghlib (aliyefariki mwaka 141 Hijriyyah) ni kwamba wote wanaafikiana kuwa yeye ameishi katika zama za Al Imam Zaynul 'Abediin ibn Hussein ibn 'Ali ibn Abi Talib a.s., Al Imam Muhammad al-Baqir a.s. na Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s., na Hadith zao alizozileta huyu Aban bin Taghlib zinasemwa kuwa ni Asili. Yaani inamaanisha kuwa Hadith zake hizo yeye alizoziandika zimetoka moja kwa moja kutoka kwa Maimamu a.s. na si kwa kupitia watu wengine walizozisikia inamaanisha kuwa ni yeye mwenye amezisikia hizo.

12. Takriban waliosomea ilimu ya Hadith ilifikia elfu nne au na zaidi kuanzia katika zama za Al Imam Muhammad al-Baqir a.s. na Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. Siku moja Hasan bin Ali Alwashakhi yeye alikutana na wale watu waliokuwa wakizoea kuzisema Hadith si chini ya mia tisa katika Masjid Al-Kufa, na wengi wa wale waliokuwa wakizisema hizo Hadith walikuwa wakisema tumeambiwa Hadith hii na Ja’afer bin Muhammad yaani zilikuwa ni Hadith asili ambazo huyo mtu amezisikia moja kwa moja kutoka kwa Maimamu a.s.

13. Ibn Nadhiim katika kitabu chake Fahrist amemwandikia yule Yunusu bin ‘Abdul Rahman na habari zake kuwa ni mtu mmoja mwaminifu na mwenye kutegemewa kabisa ambaye miongoni mwa Ma-Sahaba wa Al Imam Musa al-Kadhim a.s. na Al Imam 'Ali ar-Ridha a.s. Kwa hakika kitabu hiki ni chenye manufaa sana kiitwacho Jawamiul Aasar.

14. Ibn Nadiim katika kitabu chake Fahrist amewaandika watoto wawili wa Sa’id bin Himad ambao ni Hussein na Hasan na vile vile ameandika habari zao pia, kuwa hawa watu walikuwa ni hodari kabisa katika ‘ilimu ya Hadith, Fiqh na Manaqib. Hao wote walikuwa wana kitabu walichokitunga juu ya Hadith na walikuwa ni miongoni mwa Ma-Sahabawa Al Imam Muhammad Taqi Al Jawad a.s. na Al Imam 'Ali ar-Ridha a.s.

15. Fadhl Bin Shaazan Nishapouri (aliyefariki 260 Hijriyyah) yeye amewahi kuwa Sahaba wa Maimamu watatu a.s. ambao ni, Al Imam Muhammad at-Taqi a.s., Al Imam 'Ali an-Naqi a.s. na Al Imam Hasan al-'Askari a.s. Naye ameandika vitabu vitatu:
• cha kwanza Kitabul Faraidh Al Akbar,

• cha pili Kitabul Faraidh Al Awsat,

• cha tatu Kitabul Faraidh Al-Asghar ambacho ni mashuhuri.

16. Na baada ya hapo, hii kazi ya ukusanyaji na uandishi wa Hadith ulikuwa umeendelezwa na Ma-Sahaba na wazee na wameweza kuleta kazi nne zilizo kubwa kabisa. Kazi hizo nne ambazo mpaka leo zinajulikana kwa jina la mashuhuri Kutub Al-‘Arbi’a yaani inajulikana kwa jina la vitabu vinne. Kitabu Cha kwanza kabisa ni Al Kafi, ambacho kimetayarishwa na kuandikwa na Thiqatul Islam Al Kulayni a.r. (amefariki mwaka 329 Hijriyyah); katika kitabu hiki zipo Hadith takriban elfu kumi na sita. Vile vile kuna kitabu kingine kinachoitwa Man la yahdhurul faqih ambacho kimeandikwa na Bwana Abu Ja’afer As-Saduq; humo takriban Hadith elfu sita zinapatikana. Vile vile kulikuwa na kitabu chake kingine kijulikanacho kwa jina Madinatul ‘Ilm ambacho Shahid a.r. amekizungumzia.

Na kwa kutokana na fitina za zama hizi kitabu hiki hakipo yaani hakipatikani; na Sheikh Saduq a.r. alifariki katika mwaka 381 Hijriyyah.

Vile vile tunapata vitabu viwili mashuhuri na vyenye faida sana ambavyo vinavyoitwa Tahdhibul Ahkam na kingine Al-Istibsaar vyote vikiwa vya Sheikh al-Ta'ifa Bwana Ja’afer Muhammad bin Hasan Tusi (aliyefariki mwaka 460 Hijriyyah). Kwa kuunganisha vitabu vyote viwili zipo Ahadith elfu kumi na nane zilizo andikwa.

Kwa hakika katika zama zote hizi ilimu hii ya Hadith na katika nuru ya Ayah za Qur'an Tukufu na Sunnah ya Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. ‘ummah umeweza kuwatambua na kuwafuata Ahlul Bayt a.s. na kuweza kujipatia ma’arifa yao na Ma-Sahaba. Katika kila zama kazi zilikuwa zikifanyika kwa kiwango fulani katika kuendeleza jitihada hizi za Hadith.

Lakini katika mwaka wa 11 Hijriyyah kulifanywa kazi moja kwa kiasi kikubwa sana cha kutungwa kwa kitabu kiitwacho Bihar Al Anwar ambacho kilitungwa na Muhaqqiq ‘Allama Majlisi a.r. (aliyefariki 1111 Hijriyyah), kitabu hicho ambacho kilikusanya Hadith kwa wingi. Kwa hakika kitabu hiki kimoja yaani Bihar Al Anwar sisi hatujakipa heshima kiasi inavyotakiwa na wala sisi hatujafaidika na kitabu hiki kiasi tunachotakiwa kufaidika nacho.

Bihar Al Anwar ni kitabu ambamo Hadith ambazo hazikuandikwa katika Kutub Al-‘Arbi’a basi hizo Hadith zinapatikana katika kitabu hiki cha Bihar Al Anwar. Kwa hakika kitabu hiki kina Juzuu ishirini na sita lakini katika Jamhuri ya Kiislam ya Iran na Beirut wamejaribu kukipanga katika vitabu vidogo zaidi ambavyo vimefikia Juzuu mia moja na kumi, ambavyo hata mimi ninavyo. Katika zama hizi vitabu hivyo na vingine vingi vinapatikana kwa urahisi katika CD za compyuta ambavyo mtu hana haja ya kujitwisha vitabu hivyo na inakuwa rahisi kutafuta masuala atakayo.

Kwa hakika Ma’ulamaa wamefaidika sana na Hadith zilizo andikwa katika Bihar Al Anwar na vile vile inadhihirisha vile wanavyo onyesha kuisifu na kuiheshimu kazi hiyo na hapa nimejaribu kuwaletea baadhi ya majina yao ambao wamekuwa katika zama hizo na mmoja miongoni mwao kama Marhum ‘Allamah Majilisi alipewa ruhusa yaani ‘ijaza’ ya ya kunakili riwaya.

1. Muhammad bin Hasan Hurri ‘Aamili aliyefariki mwaka 1104 na mwandishi wa kitabu kinachoitwa Wasa’il as-Shi’ah, nacho kimechapwa si chini ya Juzuu ishirini.

2. Mullah Muhsin Faiz Khashani aliyefariki 1091 na ambaye ni mwandishi wa Al-wafi. Kitabu hiki kina Juzuu kumi na nne kinazungumzia juu ya Usul, Furu’, Sunan, na Ahkam.

3. Mawla Abdullah bin Nurullah Bahrani mwandishi wa kitabu kiitwacho Al Awalim kitabu hiki kiko katika Juzuu mia moja.

4. Sheikh Muhammad Ridha bin Abdul Latif Tabrizi, aliyefariki mwaka 1158 na ni mwandishi wa kitabu kiitwacho Ash-Shifa’.

  • 1. Nimetarjumu orodha ya Rawi 100 wa Kishi’ah wanaojuikana na walio ma’arufu katika vitabu vya Ahl as-Sunnah. Kwani wengi wa Masunni wanadai kuwa Mashi’ah ni Rafidhi (walio asi ) na wengine majaheli kuthubutu kusema kuwa Mashi’ah ni Makafiri. Hivyo itakuwa vyema iwapo utapata makala hayo ukayasoma.