1. Isisitizwe Kutoa Sadaka kwa wenye Shida, Masikini na wenye Madeni
1. Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. amesema kuwa :
“Sadaka inalipia madeni na inaongezea katika barakah.”
2. Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. amenakili riwayah kutoka Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. kuwa:
“ Sadaka inamepusha mtu na ajali mbaya.”
3. Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. anasema kuwa:
“Mtu yeyote yule aliye mja wa Allah swt akiwa Mu’min na akatoa Sadaka, basi Allah swt baada ya kifo chake huyo mtu huwaweka vyema na kuwasaidia wananyumba yake katika hali njema.”
Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. akaendelea kusema :
“Faida ya kutoa Sadaka ni kwamba inamsaidia kulipia madeni na vile vile kuongezea katika baraka.”
4. Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. amesema kuwa:
“Kusaidia na kutoa sadaka vyote hivyo vinaondoa umasikini na hurefusha umri wa mtu. Na yule anayetoa huweza kuepukana na aina sabini za ajali mbaya.
5. Al Imam Muhammad al-Baqir a.s. katika kuelezea tafsiri ya aya, ya Qur'an Tukufu, Sura Al-Layl, 92, Ayah ya 5 na 6 :
’Ama mwenye kutoa na akamcha Mungu, Na akaliwafiki lililo jema.’
ndipo amesema kuwa;
Allah swt ndivyo anavyo walipa wale watendao mema, kwa mema yao ma ra kumi, au hata mara laki moja na hata zaidi ya hapo.
Na vile vile amesema kuwa: anayetoa katika njia ya Allah swt basi Allah swt humjaalia kila aina ya tawfiqi katika kazi hiyo ya kheri.”
6. Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. amemnakili Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. kuwa
“Mtu yeyote yule ambaye anamwamini Allah swt kuwa atamlipa na atamwongezea zaidi ya kile anacho kitoa basi huyo mtu kwa moyo mkunjufu na bila aina ya ubakhili wowote atatoa sadaka na misaada kwa wingi kabisa.”
7. Amesema Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. amemnakili Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. kuwa
“Siku ya Qiyama ardhi itakuwa imepata moto kupita kiasi na waumini watakuwa katika kivuli na kivuli hicho itakuwa ni kile alicho kuwa akitoa Sadaka.”
8. Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. amenakili riwayah moja kutoka Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. akisema kuwa:
“Enyi watu! Toeni sadaka; bila shaka sadaka inaongezea katika mali yenu, na hivyo mtoe sadaka na Allah swt atawarehemu.”
9. Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. ameripotiwa katika Kitab ‘Uddatud-Da’i’ kuwa alimwuliza mtoto wake :
“Je! nyumbani kuna kiasi gani kwa ajili ya matumizi ?”
Naye alimjibu : “Zipo Dinar arobaini tu.”
Imam a.s. alimwambia: “Dinar zote hizo zigawe Sadaka.”
Kwa hayo mtoto wake alimwambia Imam a.s.:“Ewe Baba! Mbali na Dinar hizi arobaini, hatutabakia na akiba yoyote.”
Imam a.s. alimwambia: “Nakuambia kuwa zitoe Dinar zote Sadaka kwani ni Allah swt tu ndiye atakayetuongezea kwa hayo. Je! wewe huelewi kuwa kila kitu kina ufunguo wake ? Na ufunguo wa riziki ni Sadaka ( kutolea mema).”
Kwa hayo, mtoto wake aliyekuwa akiitwa Muhammad, alizitoa Sadaka Dinar hizo na hazikupita siku kumi, Imam a.s. alitumiwa Dinar elfu nne. Hapo Imam a.s. alimwambia mwanae:
“Ewe Mwanangu! Sisi tulitoa Dinar arobaini tu na Allah swt ametupa Dinar elfu nne badala yake.”
10. Al Imam Musa al-Kadhim a.s. amesema kuwa:
“ Toeni sadaka mjipatie riziki.”
11. Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. amesema kuwa:
“ Toeni sadaka mjiongezee riziki yenu. Bila shaka anayeamini kuwa Allah swt hulipa mambo yote. Basi yeye huwapa sadaka masikini kwa kupita kiasi. Allah swt humjaalia riziki kwa njia mbalimbali kwa kile huyu mtu akitoacho katika mali yake.”
12. Al Imam Muhammad al-Baqir a.s. amesema kuwa Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s. siku moja alitoa Dinar moja kama Sadaka na hapo Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. alimwambia :
“Ya ‘Ali! Je! unaelewa kuwa pale mtu anapotoa Sadaka kwa mkono wake mwenyewe basi hujiepusha na mitego ya mashetani sabini, na kila shetani husema, ‘Ewe fulani, usitoe sadaka kamwe.’”
Akaendelea kusema Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w.
Ya ‘Ali! Kile utoacho Sadaka kabla hakijaingia katika mkono wa yule anayeomba, kwanza hupitia katika mkono wa Allah swt.
Na baada ya hapo Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. alisoma aya hii ifuatayo ambayo iko katika Qur'an, Surah Tawbah, 9, Ayah 104:
‘Je! hawajui ya kwamba Mwenyezi Mungu anapokea toba ya waja wake, na anazikubali sadaqah , na kwamba Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa kupokea toba na Mwenye kurehemu?’
13. Al Imam 'Ali ar-Ridha a.s. amenakili riwayah kutoka Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. akisema:
“Kuwa na aqida ya Tawhid ni nusu ya sehemu ya dini, enyi watu! Toeni Sadaka ili mpate riziki zaidi”.
14. Al Imam 'Ali ar-Ridha a.s. ametoa riwayah kutoka Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w.:
“Kuwa mali halisi ya mtu ni ile ambayo yeye ametolea sadaka.”
15. Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. amesema kuwa:
“Toeni Sadaka asubuhi na mapema ili balaa zisiwafikieni katika siku nzima.”
16. Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. amenakili riwayah kutoka Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s. kuwa:
“Sadaka ni kinga dhidi ya moto wa Jahannam .”
17. Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. amesema kuwa Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. alikuwa akisema:
“ Enyi watu muwatibu wagonjwa wenu kwa kutoa Sadaka.”
18. Al Imam 'Ali ibn Abi Talib a.s. katika Nahjul Balagha amesema kuwa:
“Mnapoona riziki yenu inapungua na kuwa finyu basi muwe mkitoa sadaka ndivyo mtakuwa mkifanya biashara na Allah swt.”
19. Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. amesema kuwa:
“ Imani ya mu’umini inakuwa na sifa nne za lazima,
Awe na tabia njema
Awe mkarimu na mwepesi wa kutoa
Asizungumze zaidi ya yale yanayo takikana (hazungumzi mambo ovyo ovyo)
Hutumia kile kiasi kinacho takiwa, siyo mfujaji ( anaotoa katika njia ya Allah swt ).