4. Kutoa Sadaka Kwa Niaba ya Wengine
Mtoe sadaka kwa niaba ya watoto wenu na watoto wenu watoe sadaka kwa mikono yao hata kama itakuwa kidogo kiasi gani.
1. Al Imam 'Ali ar-Ridha a.s. aliulizwa na Sahaba mmoja :
“Ewe mwana wa Mtume wa Allah! Mimi watoto wangu wawili wamefariki na amebakia mtoto wangu mdogo.”
Kwa hayo Al Imam 'Ali ar-Ridha a.s. kamwambia:
“Basi toa Sadaka kwa niaba ya mtoto wako huyo.”
Na siku moja Al Imam 'Ali ar-Ridha a.s. alipomtembelea huyo mtu akamwambia,
“Mwambie mtoto wako huyo atoe Sadaka kwa mkono wake walau kiasi kidogo chochote kile au hata kama kitakuwa ni kipande kidogo tu. Utambue wazi kuwa kiasi chochote kile hata kikiwa kiasi gani kama kitatolewa kwa roho safi basi mbele ya Allah huwa ni kipenzi, kwani Allah swt ameelezea katika Qur’an Tukufu, Surah Az-Zilzalah, 99, Ayah 7 – 8:
‘Basi anaye tenda chembe ya wema, atauona !
Na anaye tenda chembe ya uovu atauona !’
Vile viel Al Imam 'Ali ar-Ridha a.s. alimwelezea kuwa:
“Allah swt amesema katika Qur’an Tukufu, Surah Al-Balad, 90,
Ayah 11 – 16:
’Lakini hakujituma kwenye njia ya vikwazo vya milimani.
Na nini kitakujuvya ni nini njia ya vikwazo vya milimani ?
Kumkomboa mtumwa; Au kumlisha siku ya njaa,
Yatima aliye jamaa, Au masikini aliye vumbini.’
“Hivyo ewe Sahabi uelewe kuwa Allah swt anaelewa wazi wazi kuwa si watu wote wenye uwezo wa kuwanunua na wenye kufanya huru watumwa hivyo yeye ameweka thawabu hizo hizo kwa wale watakao toa Sadaka au watakao walisha yatima na masikini.”
2. Al Imam Musa al-Kadhim a.s. alijiwa mtu mmoja mbele yake na kuelezea habari za mtoto wake, na kwa hayo Al Imam akamjibu :
“ Toa Sadaka kwa niaba yake.”
Na mtu huyo akajibu kuwa, “Sasa mtoto wake amekuwa na umri yaani amekuwa kijana.”
Basi Al Imam Musa al-Kadhim a.s. alimwambia kuwa:
“Mtoto wako atoe Sadaka kwa mkono wake, hata kama itakuwa ni kipande cha mkate, na hapo ndipo Al Imam Musa al-Kadhim a.s. alisema riwayah ya Al Imam Muhammad al-Baqir a.s. kuwa:
“Katika Israil alikuwa mtu mmoja aliyekuwa akimpenda mno mtoto wake, na akaona katika ndoto yake ana ambiwa kuwa, mtoto wako huyo umpendaye mno atakufa usiku wa ndoa yake. Kulipowadia usiku wa harusi baba mzazi wa mtoto huyo, usiku kucha akawa katika wasiwasi na hakupata usingizi na kamwe hakupata raha usiku huo.
Na kulipo pambazuka asubuhi na mtoto alipotoka chumbani mwake akiwa hai basi baba yeke alimwuliza, ‘Ewe mwanangu! Je! katika usiku huu wako wa kuamukia leo umefanya mema yoyote?’
Kwa hayo mtoto akajibu:
“Ewe baba yangu! hakuna jambo la maana sana lililotendeka, bali alitokezea masikini mmoja akaja mlangoni kuomba chakula, alikuwa na njaa na kile chakula walichokuwa wameniwekea, mimi nikampa chakula chote huyo mtu aliyekuja kuomba.’
Kwa hayo baba yake akasema: “Kwa sababu hii tu ndiyo Allah swt amekuondoshea balaa kubwa iliyokuwa ikupate wewe usiku huo.”