read

7. Katika Kutoa Sadaka Hata Kiasi Kidogo Chochote Kile ni Sunnah

1. Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. anasema kuwa kuna riwayah kutoka kwa Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. kuwa
“Toeni Sadaka, angalau hata kwa sa’ ya tende, na kama sa’ moja hiyo hamnayo basi mtoe tende kwa kiganja kimoja na hata kama hivyo haitawezekana basi mtoe tende kiasi chochote kile na kama hivyo haitawezekana basi mtoe angalau kokwa moja ya tende, na kama hivyo pia haitawezekana basi yule masikini aliyekuja kuwaomba, mumwambie maneno mazuri na matamu na maneno matakatifu katika kumwelezea kuwa hakuna chochote, na hayo pia ni sadaka.

Kwa sababu isitokee Siku ya Qiyama kwamba Allah swt atakapo kuuliza hesabu ya neema alizokujaalia akakuambia
‘Ewe mja! Mimi nilikupa mambo chungu nzima, sasa hebu angalia nafsini mwako, Je! kwa kutumia neema hizo wewe umejiandalia nini?’

Na hapo wewe utaangalia sehemu zote nne za dunia na utajawa na masikitiko, na utakuta hakuna jambo lolote lile litakalo kuokoa dhidi ya adhabu za Allah swt.”

2. Al Imam Muhammad al-Baqir a.s. amesema kuwa:
“Mtoe tende kiasi fulani kwani itawaokoa na moto wa Jahannam , mpanue riziki zenu na mteremshiwe riziki nyingi kwa kutoa Sadaka na kupitia dua mziondoe balaa na shida zenu.”

Mkumbuke kuwa kwa kutoa Sadaka hamtapungukiwa katika mali yenu. Na miongoni mwa jamaa zenu wanapokuwa na shida muwasaidiapo, hiyo siyo Sadaka bali hiyo ni wajibu wenu.”

3. Al Imam Muhammad al-Baqir a.s. amesema kuwa:
“Kulikuwa na mja mmoja aliyekuwa akifanya ibada ya Allah swt kwa umri wake wa miaka themanini.

Siku moja alimwona mwanamuke mmoja mzuri aliyekuwa akipendeza naye akawa ameingia katika mtego wake. Yeye alitimiza matamanio yake visivyo halali na mara akatokezea Malakul mauti (malaika anayetoa roho). Ulimi wake ulifunga kuongea na jasho lilianza kumtoka na kutokwa kwa roho na mara hapo alipita masikini akiomba.

Basi mtu huyu ambaye alikuwa katika hali ya kukata roho alimwambia yule masikini kwa ishara kuwa mahala fulani kuna mkate hivyo auchukue hivyo aweze kula huyo masikini, na masikini huyo alivyoelekezwa akauchukua mkate akaondoka zake.

Kwa hiyo ikatokea kwamba Allah swt aliibatilisha ibada zake za miaka themanini kwa sababu ya kuzini na ikatokea kwamba Allah swt akamsamehe madhambi yake yote kwa sababu ya kutoa Sadaka kwa moyo mkunjufu.”

4. Al Imam 'Ali ar-Ridha a.s. amesema kuwa:
“ Katika zama za Bani Israil kuliwahi kutokea baa la njaa (ukame) ambao uliendelea kwa muda wa miaka mingi.
Katika wakati huo ikatokezea kwamba bibi kizee mmoja akiwa amekabwa na njaa hali ya juu, alikuwa ameketi akiwa na kipande kidogo cha mkate huku akitaka kukila kipande hicho, mara akasikia mlangoni sauti ikisema ya masikini aliyekuwa amekuja kuomba:
‘Ewe mja wa Allah swt! Mimi nakufa kwa njaa naomba unisaidie”, bibi kizee huyo akajiambia kwa hakika Sadaka ndiyo wakati huu muafaka wa kutoa, na kile alichokuwa akila akakitoa haraka akampa huyo aliyekuwa akiomba.
Bibi kizee huyo alikuwa na mtoto mmoja aliyekuwa amekwenda porini na ghafla kule alishambuliwa na mnyama. Kwa kusikia sauti ya mtoto wake huyo bibi kizee ikimwita, alikimbia kumfukuza mnyama huyo na kwa muujiza wa Allah swt yaani Allah swt alimtuma Malaika Jibrail a.s kwenda kumwokoa mtoto huyo katika mdomo na mabano ya mnyama aliyemshambulia, na Malaika Jibrail a.s. akamwambia ‘Ewe bibi kizee! Je! umefurahi sasa? Kwa kile ulichokitoa sadaka basi Allah swt naye amekulipa mema yake.”

5. Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. amesema kuwa:
“ Mfanye mema katika hali ya shida na ufakiri, na wema huo ni Sadaka.
Toeni Sadaka kama itakuwa ni kiasi gani kwa udogo wake. Mnaweza kutoa kiasi cha tende mkajiokoa na Jahannam. Kwa hakika udogo huo siyo hoja na Allah swt ataulea udogo huo kama kwamba nyie mnavyo walea watoto wadogo wanaonyonya maziwa, na siku ya Qiyama wakati mema yenu hayo (mliyokuwa mkisema ni madogo) yatakapoletwa mbele yenu mtaona kuwa ni sawasawa na ukubwa wa milima mikubwa sana.”

6. Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. amesema kuwa Allah swt anasema kuwa :
“Hakuna kitu kingine mbali na Sadaka ambacho mtu anaweza kumpatia mtu mwingine kidhahiri, na kwa hakika mimi ndiye wakili wake mstahiki, na mimi ninayepokea kwa mikono Sadaka hiyo halafu hata ikiwa kama ni tende kidogo, haidhuru mimi ndiye ninaitunza, kama vile mwanadamu anavyowatunza watoto wake.

Siku ya Qiyama huyo mtoa Sadaka atastaajabishwa mno kwa Sadaka zake ndogo alizokuwa akitoa zimekuwa kubwa kama milima ya Uhud, milima mikubwa sana.”