9. Sadaka Huondoa Balaa ya Kila Aina
Kama kuna hofu ya kuja kwa balaa ama kwa kutokezea ubaya wowote au kwa sababu ya ugonjwa na hofu yoyote basi toeni sadaka.
1. Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. ameripoti riwayah kutoka kwa Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. ambaye amesema:
“kwa baraka za Sadaka Allah swt humwondolea mwenye kutoa Sadaka balaa sabini, ambamo kuna magonjwa, madhara yatokanayo na moto, kuzama maji, kufunikwa na majumba mpaka kufa na atamwepusha ili asiwehuke au asiwe mwehu.”
2. Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. ameripoti riwayah kutoka Al Imam 'Ali ibn Abi Talib a.s. kuwa:
“Ili kutaka kuepukana na shari za madhalimu basi toeni Sadaka.”
3. Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. anaelezea kuwa: Siku moja Myahudi mmoja alikuwa akienda kukata miti porini na Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. alimwangalia na kuwaambia Ma-Sahaba wake :
“Myahudi huyu leo ataumwa na nyoka na kifo chake kitasababishwa na sumu ya nyoka. Myahudi huyo kama kawaida yake alikata kuni na alijitwisha kichwani mwake na akarudi akiwa salama.
Na tena Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. alipomwona Myahudi huyo akamwambia ateremshe mzigo wa kuni huo na auweke chini. Na Myahudi akafanya hivyo alivyoambiwa, na katika mzigo huo wa kuni wakaona kuna nyoka mweusi mwenye sumu kali sana huku akiuma kuni.
Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. alimwuliza Myahudi yule,’Je! wewe leo umefanya jambo gani?’
Myaudi huyo akasema: Mimi nimekata kuni na kuzifunga tu, lakini wakati nilivyokuwa nikirudi, nilibakiwa na vipande viwili vya mkate na kipande kimoja mimi nikala na kipande kimoja nikampa masikini Sadaka.
Hapo ndipo Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. akasema kwa kiapo cha Allah swt ni kwa sababu ya Sadaka ndiko balaa hii imekuondokea, kwa hakika Sadaka humwepusha mtu na ajali mbaya.”
4. Al Imam 'Ali ibn Abi Talib a.s. siku moja alikuwa pamoja na Ma-Sahaba wake katika Masjid Nabawi, na upande mmoja wa ukuta ukaanguka chini. Kulikuwa na mtu mmoja hapo ambaye aliponea chupu chupu tu, kulianguka kizingiti kizito karibu na mguu wake. Lakini yeye bahati nzuri hakupata udhuru wowote.
Hapo Al Imam 'Ali ibn Abi Talib a.s. aliwaambia Ma-Sahaba wake, hebu mwulizeni huyu mtu leo amefanya matendo gani? Na wakati alipoulizwa huyo mtu akasema:
“Mimi nilipotoka nyumbani mwangu leo nilikuwa na kokwa chache za tende. Na kukatokezea masikini mmoja akaniomba basi mimi nikampa kama Sadaka .
Al Imam 'Ali ibn Abi Talib a.s. akajibu,
“Basi kwa sababu hiyo tu leo, Allah swt amekuepusha na balaa hii ambayo ingekumaliza.”
5. Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. siku mmoja alimwambia Sahaba wake Mayassari kuwa:
“Ewe Mayassari Je! wajua kuwa wewe umeisha fikiwa na mauti mara nyingi, lakini Allah swt amekuongezea umri wako zaidi kwa sababu ya wewe kuwa mkarimu na kuwajali jamaa na ndugu zako umewawia wema ndio maanake umri wako umezidi.”