14. Kutoa Sadaka Usiku ni Sunnah
1. Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. daima alikuwa akitoka usiku katika kiza huku amejitwisha mafurushi ya mapesa na vyakula kwa ajili ya kwenda kugawa kwa masikini katika mji wa Madina, na kuwafikishia misaada wahitaji. Na siku ambayo Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. aliaga dunia, watu wakaona hawakufikiwa na misaada hiyo ndipo walipojua kuwa misaada hiyo ilikuwa ikiletwa na Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. ambaye daima alikuwa akificha uso wake ili watu wasijue kuwa ni yeye anayewafikishia misaada hiyo.
2. Mu’alla ibn Khunais anasema kuwa:
“Usiku mmoja kulikuwa kukinyesha manyunyu ya mvua, nikamwona Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. akielekea katika makazi ya Banu Sai’d, nami nikajaribu kumfuata nyuma kisirisiri na mara nikasikia katika giza kizito hicho kama kitu kimedondoka na nikamsikia Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. akisema:
‘Ya Allah swt! Ninaomba vitu hivi nivipate tena.’
Na hapo mimi nikatokezea karibu ya Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s., nikatoa salamu. Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. baada ya kuitikia salamu akaniambia, ‘Je! wewe ni Mua’alla?’
Nami nikamjibu :
‘Ndiyo ewe Imam! Niwe fidia juu yako’.
Hapo Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. akaniambia:
“Naomba uniokotee vitu hapo chini unisaidie.”
Mu’alla anasema mimi katika giza kizito hicho nikaanza kupapasa aridhini na nikakuta kumbe ni vipande vya mikate na wakati ninamkabidhi Imam a.s mikate nilivyo viokota katika giza kali nilihisi kifurushi alichokuwa nacho migongoni mwake kilikuwa kizito mno na hivyo nilimwomba Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. nimsaidie kubeba kifurushi hicho.”
Lakini Imam a.s alikataa akaniambia, “Ninapendelea kuubeba uzito huu mimi mwenyewe kwa sababu huu ndiyo utakao kuwa ufanisi wangu katika siku ya Qiyamah na bora kwangu na hivyo unaweza kuja nami katika safari hii.”
Tulipokaribia katika makazi ya Banu Sa’id, Imam a.s. alikwenda kwa kila mmoja ambaye ni mwenye shida, akamwekea mikate miwili na akarudi. Na wakati huo akaniambia kwa kutoa Sadaka usiku kunatuliza ghadhabu za Allah swt, na Allah swt husamehe madhambi makubwa, na kusahilisha hesabu katika siku ya Qiyamah.”
3. Zuhri anasema kuwa:
“Siku moja wakati wa baridi kali mno na ukungu ulikuwa umejaa mwingi mno mimi nilimwona Al Imam Zaynul 'Abediin ibn Hussein ibn 'Ali ibn Abi Talib a.s. akiwa amejitwisha kifurushi kikubwa cha chakula na mzigo mkubwa wa kuni.
Nami sikusita nikamwambia, ewe mwana wa Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w.! Je! nini haya?’
Imam a.s akanijibu nina [nia] mpango wa safari, na hivyo ndivyo ninavyojitayarisha kwa ajili ya mahitaji yangu.
Zuhri akasema:
‘Ewe mwana wa Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. ! Mimi nakupa mfanyakazi wangu ambaye atakusaidia kukubebea mizigo yako hiyo mizito.”
Al Imam Zaynul 'Aabediin a.s. alinikatalia, nami nikamwambia,
“Basi nipe mimi mwenyewe nikusaidie kukupunguzia huu mizigo. Kwa hayo Imam a.s. akajibu, “lakini kwa kufanya hivyo mimi sitakuwa nimetoka katika wajibu wa kufika mwisho wa safari yangu vile inipasavyo kufika!| kwa hiyo naomba uendelea na shughuli zako uniache peke yangu.”
Zuhri anasema:
“Baada ya kufika siku chache mimi nilipomwona Imam a.s nikamwambia,
“Ewe mwana wa Mtume wa Allah! Mimi sioni kama wewe ulikwenda safari yoyote ile.”
Imam a.s akamjibu:
“Naam ! Vile uchukuliavyo sivyo. Muradi wangu ulikuwa ni safari ya Aakhera. Mimi nilikuwa nikijitayarisha kwa ajili ya safari ya Mauti. Kumbuka kwamba kujikumbusha na kujitayarisha kwa mauti basi mambo mawili ni muhimu, kwanza kujiepusha na yaliyo haramishwa na pili ni kutoa muhanga wa mali katika njia ya Allah swt.”
4. Al Imam 'Ali ibn Abi Talib a.s. katika baadhi ya misemo yake anasema.:
“Toeni Sadaka kwa sababu kunatuliza ghadhabu za Allah swt.”
Toeni Sadaka katika njia ya Allah swt mnajaribiwa kwa sababu ya riziki mliyojaaliwa na Allah swt; kwa kufanya hivyo nyinyi mtahesabiwa katika wale wanaopigana katika njia ya Allah swt.
Yeyote yule ambaye ana imani kamili kuwa Allah swt hulipiza kile kinachopendwa itolewe [katika njia ya Allah swt] na Mu’min basi huyo mtu lazima ataitia nafsi yake katika shida na kwa kufanya mema.
Muwatibu wagonjwa wenu kwa Sadaka .
Muilinde na muihifadhi na kulinda mali yenu kwa kutao zaka1.
Urekebishe matumizi na mahitaji ya maisha yenu ili mweze kupima vyema.
Kuwa na mawazo ni nusu ya uzee unaoletwa nawe.
Mwenye matumizi yenye mahesabu yaani anayebana matumizi kamwe hawezi kuwa mwenye shida na dhiki.
Kumsaidia yule mtu ambaye anaheshima na ni mkuu na kumsaidia yule ambaye ana madeni, haya maneno mawili hayana kifani yoyote.
Kila jambo lina mazao yake, kwa hiyo mazao ya mema na kuwa na nia katika kutumia mali au chochote katika njia ya Allah na kwa ajili ya Allah swt, basi mazao yake ni kwamba kufanya haraka kutekeleza azma hiyo na kamwe usifanye kuchelewesha.
Muongezee na mupanue riziki yenu kwa kutoa Sadaka, kabla hamjaijiwa na balaa, mwombe dua na kwa hakika mtaweza kujiepusha nayo na kujiokoa nayo.
- 1. Ndugu msomaji kitabu hiki kinazungumzia mambo ya sadaqah na kuna kitabu kimoja nimekitarjumu katika lugha ya kiswahili kinachozungumzia dhambi kuu, kutokulipa zaka na sadaqah. Kwa hiyo ili kutaka kujua habari zaidi kuhusu zaka naomba usome kitabu hicho utapata kuelewa mambo marefu na mapana juu ya zaka.