read

16. Je! Sadaka Itolewe Wakati Gani?

1. Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. alikuwa ameulizwa na mmoja wa Ma-Sahaba wake,
“Ewe Mtume wa Allah swt! Ni Sadaka ipi iliyo bora kabisa kuliko zote!”
Kwa hayo Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. alijibu:
“Sadaka iliyo bora ni ile ya wakati ule ambapo mtoa Sadaka yuko salama u salimini, mwenye afya kamili na anayeishi maisha mema bila wasiwasi, na ambaye anauogopa umasikini.

Na wala msicheleweshe kiasi kwamba mpaka kwamba mwisho wa maisha yenu yamesha wafikia shingoni, na hapo ndiyo mnaanza kutoa usia kuwa kiasi fulani mpe masikini fulani na fulani mpe kiasi fulani na kadhalika. Kama tunaelewa kuwa mtu fulani kweli ni mstahiki wa msaada au Sadaka, sasa kwa nini tusubiri mpaka sisi tunataka kufa ndiyo basi tuseme msaidieni wakati shida alikuwa nayo tangu hapo zamani?”

2. Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. aliombwa na mtu mmoja kuwa ampatie nasiha, na hivyo Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. akamwambia:
“Tayarisha matayarisho yako ya safari, na matayarisho yako hayo yatume kabla wewe hujaenda safari. Jifanyie matendo yako mwenyewe yaani kama unataka kufanya mema uyatende mema kabisa katika uhai wako na mambo yoyote yale ambayo unayoona yanafaida kwako uyatende wewe mwenyewe na wala usiwatupie wengine kama unaweza kujitimizia wewe mwenyewe.1

3. Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. (kwa kuzungumzia swala tulilozungumzia Namba 2 hapo juu) siku moja alikuwa amekwenda katika ghala la mtu mmoja ambaye alikuwa amefanya usia kuwa baada ya kifo chake maghala yake yote yaliyokuwa yamejaa tende yagawiwe Sadaka kwa masikini. Na baada ya kifo chake ikatekelezwa usia wake na Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w.; alipokwenda kule baada ya kufagia akakuta kokwa moja ya tende imebakia mguuni mwake basi Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. akainama akalichukua kokwa hilo la tende moja akasema:
“Kama mtu huyu katika uhai wake angelikuwa amegawa kokwa hii moja ya tende basi angepata thawabu zaidi kuliko hata mlima mkubwa kabisa wa Uhud.”

  • 1. Mara nyingi sisi hatufanyi mambo mema, hatutoi Sadaka, hatusali, hatufungi saumu na tunafanya usia wakati wa kufa; tunategemea tuache usia kwamba kazi fulani nilikuwa nataka kuifanya mtoto wangu aifanye, Sadaka fulani nilikuwa nataka kuitoa mtoto wangu aitoe, siku fulani sikusali mtoto wangu anisalie, saumu sikufunga mtoto wangu anifungie saumu zangu n.k. Kwa hakika mambo kama hayo hayana dhamana kuwa yatatimizwa hivyo unaweza kukosa wewe vyote na ukawa mstahiki wa ghadhabu na adhabu za Allah swt siku ya Qiyamah.