read

21. Mwombaji Tusiyemjua Apewe Sadaka Japo Kidogo

Iwapo mwombaji haumjui mpe sadaka kidogo ili aweze kuwa na huruma na maadui wa Ahlul bayt a.s. wasipewe sadaka.

1. Al Imam Muhammad Sahibuz-Zamaan a.s. aliandikiwa barua na mtu mmoja akimwuliza kuwa:
“Je! inawezekana mimi nikatoa Zaka au Sadaka kutoka mali yangu nikampa mtu ambaye si jamaa wala ndugu yangu?”

Na kwa hayo Imam a.s. alimjibu:
“Usimpe Zaka au Sadaka mtu yeyote mwingine isipokuwa wenzako na majamaa zako.”

2. Al Imam Muhammad Sahibuz-Zamaan a.s. aliulizwa:
“Je! inawezekana kumpa Sadaka Nasibi (maadui wa Ahlul Bayt a.s.)?”
Imam a.s akamjibu kuwa:
“Musiwape Sadaka wala Zaka maadui wa Ahlul Bayt a.s. na ikiwezekana hata maji pia msiwape.”

3. Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. aliulizwa kuwa:
“Je! inaruhusiwa kumlisha mtu kama humwelewi kuwa ni Mwislamu au si Mwislamu?”

Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. akajibu kuwa :
“Mtu ambaye humwelewi na kama huelewi chochote kuhusu urafiki au adui, basi yeye unaweza kumpa. Kwa sababu Allah swt anasema tuwatendee watu mema. Lakini yule aliye mpingamizi wa haki au ambaye anaelekea kuhusu upotofu na madhambi au anayewachukua watu kuelekea upotovu na madhambi, huyo msimpe.”

4. Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. aliulizwa kuwa:
“Mara nyingi tunaona masikini wanaokuja kuomba, lakini sisi tunakuwa hatuwafahamu, Je! watu kama hawa tunaweza kuwapa?”

Kwa hayo Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. aliwajibu,
“Kama wewe moyoni mwako utaingiwa na huruma kwa ajili ya mtu huyo basi unaweza kumpa, ingawaje hata kama si kamili lakini hata kidogo itafaa.”

5. Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. amesema:
“Kidhahiri wapo waombaji wengi ambao (wengi wanatoka vijijini na maeneo karibu ya mji) hivyo nyie muwape Sadaka watoto, wanawake, wagonjwa, wadhaifu na wazee.”

6. Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. amesema:
“Mnapoijiwa na masikini kwa ajili ya kuomba ambao ni wazee kabisa na wanawake na watoto na wasichana wadogo basi muwasaidie Sadaka na vile vile muwasaidie Sadaka wale mnaoijiwa huruma mioyoni mwenu.”

7. Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. aliulizwa kuwa:
“Mijini mwetu wanakuja waombaji wengi sana kutoka vijiji na vitongoji ambavyo viko karibu na mji ambamo humo wamechanganyikana Mayahudi, Manasara, Wakristo na hata Majusi (Wanaoabudu moto) sasa katika sura hii, Je! tunaweza kuwasaidia Sadaka ?”

Kwa hayo Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. alijibu :
“Naam ! Mnaweza kuwapa.”

8. Al Imam 'Ali an-Naqi a.s. aliandikiwa barua na humo akaulizwa:
“Je! tunaweza kuwasaidia wale masikini waliopo mitaani ambao hatujui dini na wala Madhehebu zao?”

Kwa hayo Al Imam 'Ali an-Naqi a.s. aliwajibu:
“Kama mtaweza kuwatambua wale maadui na wenye chuki na Ahlul Bayt a.s. na mukiwasaidia basi Allah swt hatakulipeni chochote ama wale ambao nyie hamuelewi Madhehebu yao basi hakuna matatizo yoyote katika kuwapa Sadaka. Na muwasaidie masikini wale wowote wanaoomba kama mtaingiwa na huruma mioyoni mwenu. Hata kama hamtaweza kuwaelewa dini na madhehebu zao… Insha-Allah hakuna tatizo lolote katika kutoa Sadaka katika sura kama hizi.”

9. Al Imam Zaynul 'Abediin ibn Hussein ibn 'Ali ibn Abi Talib a.s. alimwambia mhudumu wake:
“Yeyote yule anayekuja kuomba nyumbani kwake basi asimruhusu akaondoka hadi pale ahakikishe kuwa amemlisha chakula, hususan siku ya Ijumaa.”

Mwandishi anasema kuwa mimi nilimwambia Imam:
“Ewe mjukuu wa Mtume wa Allah! Kila mwombaji huwa si mstahiki.”

Kwa hayo Al Imam Zaynul 'Abediin ibn Hussein ibn 'Ali ibn Abi Talib a.s. alinijibu:
“Ninaogopa kuwa inawezekana mwombaji akawa mstahiki lakini mimi nikamfukuza, isije tukapata matatizo na dhiki iliyo mpata Mtume Ya’aqub a.s na nyumba yake.”