36. Heshima ya Mu’min ni Kule Kutokuwa Mwombaji wa Watu
Kuishi na watu kwa wema ni sunnah na kutokuwa na tabia ya kuwaomba omba wala kuwa na tamaa kwa yale waliyo nayo.
• Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. amesema:
“Heshima ya muumin ni kule kuamka kwa ajili ya sala za usiku, na vile vile heshima yake ni kule kutokuwa mwombaji wa watu.”
• Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. amenakili riwaya kutoka kwa Al Imam 'Ali bin Abi Talib a.s. kuwa amesema:
“Wewe lazima uwe na moyo wa kuishi vyema na watu na kuwaheshimu na kutosheka nao. Na kuishi nao vyema ni kule kuongea nao kwa upole na utamu na uwe na uso wenye tabasamu na uishi nao vile kwamba kila wakuonapo uwe ukionyesha furaha usoni mwako na hivyo utakuwa umejiwekea heshima katika jamii.”
• Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. anasema:
“Iwapo kutatokezea miongoni mwenu anayemtegemea Allah swt azikubalie kila dua zake anazoziomba basi awe akiishi na watu wote kwa wema na kamwe asimtegemee mtu yeyote isipokuwa Allah swt peke yake na atakapo jiona kuwa yeye kwa hakika anao moyo kama huo basi atambue wazi kuwa chochote kile atakachomwomba Allah swt atampatia na kumjaalia.”
• Al Imam Zaynul 'Abediin bin Hussein bin 'Ali ibn Abi Talib a.s. anasema kuwa:
“Iwapo mtu atataka wema wote kwa ajili yake ni kwamba yeye ajiepushe mbali na tamaa za kila aina ya kutamani yale waliyonayo watu, na kama yeye ana matamanio yoyote au maombi yoyote basi asiwategemee hawa watu bali zote azielekeze kwa moyo mkunjufu na halisi kwa Allah swt na lazima Allah swt atazikubalia dua na maombi yake na atamtimizia.”
• Abul A’ala bin A’ayan anasema kuwa mimi nimemsikia Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. akisema:
“Enyi watu nyie mtajidhuru pale mtakapo peleka maombi yenu na mahitaji yenu kwa watu, na kwa hakika itakupunguzia heshima na adabu. Mkae na watu katika hali ya kuridhika na kutokuonyesha mahitaji kwa watu ndio usalama wa Imani ya mumiin na ndio heshima yake. Kwa hakika tamaa yenu ndiyo dalili ya ufakiri wenu.”
• Ahmad bin Muhammad bin Abi Nassr anasema kuwa yeye siku moja alimwambia Al Imam 'Ali ar-Ridha a.s. :
“Ewe mwana wa Mtume wa Allah! Ninaomba uniandikie barua moja kwa Ismail bin Daud, ili kwamba niweze kupata chochote kutoka kwake. Kwa hayo Al Imam 'Ali ar-Ridha a.s. akamwambia iwapo mimi kitu unachokitaka au cha kukutosheleza wewe ningekuwa nimekukataa, ndipo ningekuandikia, ama sivyo uchukue kile nilicho nacho mimi kwangu na ukitegemee hicho.”
• Al Imam Muhammad al-Baqir a.s. amesema:
“Kwa hakika yale waliyonayo watu katika uwezo wao na kuridhika nayo ndimo humo kuna heshima ya muumin ya imani yake, Je! nyie hamjaisikia kauli ya Hatim? Hatim alisema kuwa pale mtakapoona nafsi zenu zimevutiwa kwa mali za watu wengine basi muelewe kuwa shida na taabu ziko zinawakaribia, na kwa hakika tamaa ni ufakiri ulio dhahiri.”
• Abdullah Bin Sinan anasema kuwa yeye amemsikia Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. akisema:
“Kwa ajili ya muumin mapendezi ya dunia na akhera yako katika mambo matatu.
• Kwanza ni sala katika sehemu ya mwisho wa usiku,
• kutokuvutiwa na kutokuwa na husuda na mali na miliki wanayomiliki watu wengine na
• kuwa mwaminifu na mtiifu kwa ukamilifu wa Ahlul Bayt a.s. na mapenzi yao.”
• Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. amesema kuwa:
“Alikuwapo mtu mmoja mbele ya Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. na akamwuliza, ‘Ewe Mtume wa Allah! naomba unionyeshe na unieleze jambo moja nilifanye jambo ambalo Allah swt atakuwa radhi pamoja nami. Kwa hayo Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. alimjibu:
Udumishe amani na upendo katika utamaduni wa dunia, jambo ambalo kimatokeo utapata mapenzi ya Allah swt na usiwe na kijicho na wivu wala tamaa kwa mali na miliki za watu, jambo ambalo litahifadhi heshima yako machoni na mioyoni mwao.”
• Ja’bir bin Yazid ananakili riwaya kutoka kwa Al Imam Muhammad al-Baqir a.s. kuwa amesema:
“Usiwe na wivu, choyo wala tamaa kwa mali za watu kwa hakika ni jambo jema kabisa kwa kuitakasisha nafsi yako kuliko hata kutoa mhanga wa mali. Vile vile wakati wa shida na dhiki fanya subira. Kuhifadhi heshima yako na utakatifu wako, mambo haya ni afadhali hata kuliko kugawa mali kwa watu. Kwa hakika kuwa na imani kamili juu ya Allah swt na kutotaka, kutovutiwa, kutokuwa na wivu au kijicho au tamaa kwa mali waliyonayo watu wengine ndio hayo mambo yaliyo bora kabisa katika maisha ya mwanadamu.”