read

39. Ni Sunna Kusaidia Kisiri

Kumsaidia mtu kabla hajaomba na kumsaidia katika hali ya kutokujulikana ni nani anayesaidia ni sunnah.

1. Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. amesema:
“Kwa hakika uwema ni ule ambao mtu anamsaidia mtu kabla hajaombwa, na kumpa baada ya kujua hali yake inamaanisha umempa baada ya kujua hivyo. Inawezekana maskini huyo mtu usiku kucha akawa anatapatapa iwapo atafanikiwa au hatafanikiwa, huku akiwa amejawa mawazo, niende kwa nani nisiende kwa nani, na hatimaye moyo ukiwa unadunda, mwili ukiwa unatetemeka na akiwa amejawa na aibu kubwa anatokezea mbele yako.”

2. Yas’ab bin Hamza anasema kuwa:
“Mimi siku moja nilikuwa pamoja na Al Imam Musa al-Kadhim a.s., watu walikuwa wamekaa huku wamemzunguka, yaani watu wengi walikuwapo. Watu walikuwa wakiulizia masuala ya halali na haramu, na mara tukaona akaingia mtu mmoja mrefu na akaanza kusema, “Iwe salamu juu yako ewe mwana wa Mtume wa Allah ! Mimi ni mpenzi na mfuasi wako wewe na baba na mababu zako, na hivi nimerudi kutoka Hijja Tukufu. Mimi nimeibiwa mali yangu yote na hivyo sitaweza kufika nchini kwangu (yaani nyumbani). Mimi naomba nisaidiwe sadaka kiasi kwamba niweze kufika nyumbani kwangu, na mimi nitakapo rudi katika mji wangu kiasi hicho cha fedha nitakitoa nigawe katika kuwasaidia wengine kama sadaka.

Imam a.s. akamwambia:
“Naomba ukae kidogo upumzike, Allah swt akurehemu. Na Imam a.s. aliendelea na mazungumzo yake pamoja na umati uliokuwa pale katika kuulizana na kueleweshana kuhusu maswala mbalimbali. Hatimaye mimi Khaysama na Suleiman Al-Ja’afari ndio tuliokuwa tumebakia na hapo Imam a.s. kwa kuniangalia mimi akasema:
“Je! unaniruhusu mimi niende chumbani kwangu?”

Suleiman akasema: “Allah swt aiendeleze amri yako”.

Hapo Imam a.s. aliinuka na kuelekea katika chumba chake na baada ya muda si muda akatoka nje, akafunga mlango na mwenyewe akasimama nyuma ya mlango na akatoa mkono tu nje huku akisema, Je! huyo msafiri kutoka Khurasan yuko wapi?”

Hapo mimi nikamjibu: “Ya Imam a.s.! Mimi niko hapa.”
Na kwa hayo Imam a.s. akamwambia,
“Nimekupa hizi Dinar mia mbili ambazo zitakusaidia wewe katika gharama na matumizi ya safari yako na vile vile napenda nikujulishe kuwa hakuna haja tena ya hizi pesa kuzitolea sadaka ufikapo nyumbani kwako, asante na unaweza kuendelea na safari yako na itakuwa vyema tusitazamane nyuso. Msafiri huyo akachukua hizo pesa na kuondoka zake.”

Suleiman Al-Ja’afer akauliza:
“Niwe fidia juu yako ewe Mwana wa Mtume s.a.w.w.! Kwa hakika wewe umefanya wema na ihsani mkubwa sana wenye huruma, lakini pamoja na hayo kwa nini umejificha?”

Kwa hayo Imam a.s. akamjibu:
“Hakuna sababu nyingine ila sikutaka kuona uso wa mwombaji ukiwa umeingiwa na aibu na unyonge sababu ya kuomba. Je! wewe hujaisikia hadith ya Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. ambamo amesema, kwa yeyote yule anayeficha wema hulipwa thawabu za Hijja sabini na yeyote yule baada ya kutenda maasi na madhambi anatangaza basi daima hubakia dhalili. Na yeyote yule anayeficha madhambi na maovu basi Allah swt humsamehe.”