45. Kuwasaidia Wale Ambao Hawajitokezi Mbele ya Watu Kuomba
Kutoa sadaka ni sunnah lakini kusaidia, kutoa msaada kwa kutegemeana na wadhifa wa mtu ni faradhi.
1. Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. amesema kuwa Ayah ya Qur’an Surah Al-Hajj, 22 , Ayah 28:
’Ili washuhudie manufaa yao na walitaje jina la Mwenyezi Mungu katika siku maalumu juu ya nyama hao alio waruzuku. Basi kuleni katika hao na mlisheni mwenye shida aliye fakiri.’
“Allah swt katika ayah hii anamaanisha kuwalisha wale walio na shida na kuwasaidia, ambapo wao kwa heshima zao wenyewe hawajitokezi nje mbele ya watu kuomba.”
2. Isack bin Ammar amenakili riwaya kutoka Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. kuwa:
“Utafika wakati mmoja ambapo waombaji wanaorefusha mikono yao kwa watu watakuwa wakiishi kwa starehe na wale watakao kaa kimya kwa kutunza heshima zao watakuwa wakifa kwa shida zitakazo kuwa zikiwakabili.
Kwa hayo mimi nikamwuliza Imam a.s.,
“Ewe Maula! Je! yakitokea hayo katika zama za uhai wangu mimi nifanyeje?”
Kwa hayo Imam a.s akamjibu,
“Kwa hakika kile ulichonacho wewe uwasaidie hao watu kwa hali na mali na kwa hata cheo chako ulicho nacho na kwa wadhifa wako ulio nao uwasaidie ipasavyo.”