read

46. Sadaka itolewe Kutoka Mali iliyo Halali

Sadaka kutolewa kutoka mali iliyo halali na hairuhusiwi kutoa sadaka kutoka mali iliyo haramu.

1. Abu Basir anasema kuwa Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. aliitolea maelezo Ayah ya Qur’an Tukufu Surah Al Baqara, 2, ayah 267 isemayo:
Enyi mlio amini! Toeni katika vile vizuri mlivyo vichuma, na katika vile tulivyo kutoleeni katika ardhi. Wala msikusudie kutoa vilivyo vibaya, hali nyinyi wenyewe msinge vipokea ila ingekuwa mmefumba macho. Na jueni kwamba Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujitosha na Msifiwa.’

Amesema kuwa:
“Zama kabla ya Islam watu walikuwa wamejilimbikiza (kusanya) mali iliyopatikana kwa njia zisizo halali (kwa njia zilizo haramu) na baada ya wao kusilimu, walikuwa wakidhani kuwa kwa kutoa mali (kuwasaidia wenye shida) iliyo patikana kwa njia haramu, watakuwa wametakasisha mali yao kuwa halali, kwa hivyo Allah swt alitoa amri kuwa sadaka itolewe kutoka mali iliyo halali tu.”

2. Shahab, kwa kuzungumzia ayah hiyo ya juu amenakili riwaya kutoka Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. kuwa:
“Ambamo amesema kulikuwa na kaumu moja ambayo walikuwa na mali nyingi iliyo chafu (iliyopatikana kwa njia za haramu). Wakati wao walipoukubalia Islam walianza kuchukizwa na malimbikizo yao hayo machafu na wakataka kutoa kwa njia za sadaka. Allah swt aliwaonya kwa kuwaambia kuwa sadaka hutolewa kutokea mali iliyo halali tu.”

3. Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. amesema:
“Iwapo watu watachuma au watajipatia mali kwa mujibu wa hukumu za Allah swt na wakaitumia kinyume na hukumu za Allah swt au iwapo watachuma kwa njia zilizo kinyume na hukumu za Allah swt na wakazitumia kwa mujibu wa hukumu za Allah swt; katika hali zote mbili Allah swt hazikubalii.

Katika kutaka kukubaliwa sharti ni kwamba mapato hayo yawe yamepatikana kwa njia zilizo halali na zitumiwe katika njia zilizo halali vile vile.”

4. Halabi anasema kuwa mtu mmoja alimwuliza Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. kuhusiana na ayah hii katika Qur'an Tukufu Surah Al Baqarah, 2, ayah 267:
‘Enyi mlio amini! Toeni katika vile vizuri mlivyo vichuma, na katika vile tulivyo kutoleeni katika ardhi. Wala msikusudie kutoa vilivyo vibaya, hali nyinyi wenyewe msinge vipokea ila ingekuwa mmefumba macho. Na jueni kwamba Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujitosha na Msifiwa.’

Na hapo Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. akasema:
“Wapo baadhi ya watu ambao baada ya kuingia katika Uislam bado wameendelea kubakia na mali iliyopatikana kwa njia zisizo halali. Na humo kulikuwa na mmoja ambaye kwa makusudi alianza kutoa sadaka kutoa mali hiyo isiyo halali. Na Allah swt alimzuia kufanya hivyo yaani sadaka haiwezi kutolewa isipokuwa kutokea mali iliyotokana kwa njia halali.”

5. Al Imam Hasan al-'Askari a.s. katika Ma’anil Akhbar kwa kupitia sanad amenakili riwaya moja kutoka Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. kuwa amesema:
“Wale ambao wanajiona utukufu na wakubwa na ambao wanatenda matendo kwa mujibu wa nafsi zao, mfano wake ni wa yule mtu ambaye mimi nilisikia watu wakimsifu sana na kumheshimu sana, na hivyo mimi nikawa na shauku ya kutaka kuonana na mtu huyo lakini katika hali ambayo yeye hataweza kunitambua. Siku moja mimi nilimwona alikuwa amezingirwa na watu. Baada ya muda mchache kupita mimi nikamwona yeye ametoka humo na akawa anaondoka, basi mimi nilimfuata nyuma yake.

Tulipita katika duka la muuza mikate, huyo mtu kwa kuficha macho yake na kificho ficho akaiba mikate miwili. Kwa hakika mimi nilistaajabishwa mno, na nikadhani kuwa labda wao wana maelewano fulani kabla ya tukio hilo.

Tukaendelea mbele yeye akamghafilisha mfanya biashara huyo na akaiba makomamanga mawili humo. Na hapa pia nikafikiria kwa labda wao watakuwa na maelewano kama hayo kabla ya kutokea tukio hili, nikiwa hapo nikaingiwa na wazo kuwa Je! iwapo watakuwa na maelewano kama hayo basi kwa nini achomoe vitu kimafichoficho?

Basi mimi niliendelea kumfuata nyuma yake, tukafika njiani akamwona mtu mmoja mgonjwa basi huyo akasimama kwa mgonjwa huyo na akatoa ile mikate miwili na hayo makomamanga mawili, akampa huyo mgonjwa.

Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. akamwuliza huyo mtu kulikuwa na dharura gani kwa kufanya hivyo. Mtu huyo kwa kuniona mimi akasema Je! wewe ni Ja’afar bin Muhammad ? Nami nikamjibu naam, basi yeye hapo akaanza kusema nasikitika sana kwa kutokujitambulisha kwako hapakuja kukufikishia faida (kwa sababu Imam a.s. alikuwa hakujionyesha kuwa yeye ni Imam bali alikuwa amejiweka kama yeye ni mtu wa kawaida).
Imam a.s. akamwambia kwa hakika matendo yako hayo yana aibisha.

Basi yeye akasema kuwa Allah swt anasema katika Qur'an Tukufu Surah An A’am, 6, Ayah 160:
‘Afanyae wema atalipwa mfano wake mara kumi. Na afanyae ubaya hatalipwa ila sawa nao tu. Na wao hawatadhulumiwa.’

Ama kwa mujibu wa ayah ya Qur'an Tukufu mimi nimeiba mikate miwili hivyo nimetenda madhambi mawili na nimeiba makomamanga mawili hivyo nimetenda madhambi mawili na kwa ujumla nimetenda madhambi manne.

Na pale mimi nilipompa mgonjwa sadaka mimi kwa kila wema nimepata malipo kumi ya thawabu hivyo jumla nimepata malipo ya thawabu arobaini. Na kutoka arobaini ukitoa nne ninayo mema thelathini na sita bado.”

Kwa hayo Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. akamjibu:
“Mama yako akae kwenye kilio chako! Wewe kwa hakika umeitoa maana isivyo ya Ayah za Qur'an Tukufu. Je! wewe huelewi ayah ya Qur'an Tukufu isemayo Surah Al Maida, 5, Ayah ya 30:
‘Basi nafsi yake ikampelekea kumuuwa nduguye, akamuuwa na akawa miongoni mwa wenye kukhasirika.’

Kwa mujibu wa ayah hiyo wewe umeiba mikate miwili umetenda madhambi mawili na kwa kuiba makomamanga mawili umetenda madhambi mawili mengine na hivyo jumla umetenda madhambi manne, na pale ulipotoa hiyo mali yaani mikate na makomamanga, kama sadaka bila idhini ya mwenye mali basi umetenda madhambi mengine manne. Kwa hivyo umetenda madhambi nane kwa pamoja. Sasa wewe unafikiria mema hayo arobaini yametoka wapi?”

Kwa hakika mtu huyo aliduwaa, akimwangalia Imam a.s. na akajiondokea zake.

Baada ya hapo Imam a.s. akasema kwa kujitolea maana potofu ya ayah za Qur'an Tukufu vile isivyo sahihi ndio matokeo yake haya na vile vile kuwapotosha watu wengine pia.”

6. Al Imam Muhammad al-Baqir a.s. katika tafsiri Ayyashi amenakiliwa akitoa tafsiri ya ayah Surah Al Baqarah, 2, ayah ya 267:
‘Enyi mlio amini! Toeni katika vile vizuri mlivyo vichuma, na katika vile tulivyo kutoleeni katika ardhi. Wala msikusudie kutoa vilivyo vibaya, hali nyinyi wenyewe msinge vipokea ila ingekuwa mmefumba macho. Na jueni kwamba Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujitosha na Msifiwa.’

Imam a.s. akaelezea:
“Miongoni mwa watu kulikuwa kumelimbikwa mali iliyopatikana kwa riba na njia zingine zisizo za halali, basi wao walinuia kutoa sadaka humo, na ndipo Allah swt alipowakataza kufanya hivyo (kutoa sadaka kutoka mali iliyopatikana kwa njia za haramu hairuhusiwa).”