read

47. Kulisha Chakula ni Sunnah

1. Al Imam Muhammad al-Baqir a.s. ameripoti riwaya kutoka kwa Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. kuwa amesema:
“Katika vitu vya kuleta uokovu mojawapo ni kuwalisha chakula wale wenye kuwa na shida na dhiki, na pili mtu awe ni mwanzilishi, awe ni mwanzo wa kutoa salamu na vile vile wakati watu wamelala usingizi mtu anaamka kwa ajili ya kusali na kufanya ‘ibada.”

2. Muhammad Yakub amenakili kutoka ‘Ali bin Ibrahim ambaye naye amenakili kutoka Muhammad bin ‘Isa bin ‘Ubaid ambaye naye amenakili kutoka Ahmad bin Muhammad naye amenakili kutoka ibn Fazzal Ma’aruf naye kutokea Tha’alaba bin Maymun ambaye naye pia amenakili riwaya hiyo kutoka kwa Zararah, kuwa Al Imam Muhammad al-Baqir a.s. amesema kuwa:
“Allah swt hupendezewa mno kulishwa chakula wale wenye dhiki na shida na njaa, na vile vile hupendezewa kutolewa kwa dhabihu (qurbani).”

3. Hisham bin Hakam amenakili riwaya kutoka kwa Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. kuwa:
“Tendo lililo bora na la kipenzi mbele ya Allah swt ni kule kumlisha muumin mwenye njaa mpaka akashiba, ama kummalizia shida aliyonayo au kumlipia deni lake.”

4. Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. amesema kuwa:
“Siku moja waliletwa wafungwa ambao walikwisha kutolewa hukumu ya kuuawa mbele ya Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. Basi ikatokea kwamba mmoja wa wafungwa hao alipoletwa mbele ya Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. Malaika Jibrail a.s. akaja akamwambia Mtume: ‘Ewe Mtume wa Allah swt ! Huyu mtu adhabu yake iahirishwe kwa leo. Na wengine waliendelea kuletwa na hukumu zikapitishwa na hatimaye wakauawa. Na mwisho yule mtu aliporudishwa mbele ya Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. na tena Malaika Jibrail a.s. akatokezea akamwambia:

“Ewe Mtume wa Allah swt ! Allah swt anakusalimia na huyu mtu huwa anawalisha wale wenye kuwa na shida, ni mkarimu kwa wageni, mwenye kusubiri wakati wa shida na dhiki, anaye chukulia majukumu na wajibu wa watu wengine kwa kuwasaidia.”

Basi Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. alimwambia huyo mtu kuwa Malaika Jibrail a.s. amekuja na kumwambia habari hizo, na hivyo yeye (Mtume s.a.w.w.) akamfanya yeye awe huru.

Kwa kujibu huyo mtu akasema:
“Je! Allah swt, mola wako amependezewa na matendo yangu hayo?”

Kwa hayo Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. akamwambia, “Naam! Na kwa hakika mtu huyo papo hapo aliisoma Kalimah ya Shahada na akaukubalia Uislam na akawa Mwislam papo hapo; na akasema:
“Kwa kiapo cha Allah swt ambaye amekutuma wewe katika haki, mimi kamwe sijamrudisha mtu yeyote akiwa amehuzunika yaani bila kusaidiwa kutoka mali na miliki yangu.”

5. Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. anamnakili baba yake Al Imam Muhammad al-Baqir a.s. kuwa amesema kuwa Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. amesema:
“Kisu kinapita haraka sana katika shingo ya mnyama lakini kwa kasi zaidi ya kisu ni kile chakula anacholishwa yule mwenye kuhitaji na dhiki.(hivyo malipo yake ni kasi zaidi kwa Allah swt ).”