read

Majlisi Ya 2: Ruhusa Ya Kuomboleza

Hapana shaka kwamba ipo ruhusa ya kuomboleza vifo vya Waumini, na kwamba jambo hilo ni halali, na hapana dalili iliyo kinyume cha hivi.

Kwa hakika baba yetu Nabii Adam (a.s.) aliomboleza kifo cha mwanawe Habil, na maombolezo yakawa yanaendelea mpaka leo kila inapotokea jambo la kifo katika kizazi cha wanaadamu bila upinzani.

Ama Mtume Muhammad (s.a.w.) aliwaruhusu Masahaba wake kufanya maombolezo kwa wingi kutokana na huzuni, na pia aliruhusu kutaja mema ya waliofariki na kutoa sifa zao katika tabia nzuri na matendo mazuri.

Na wakati Mtume (s.a.w) alipofariki, Masahaba walishindana katika kutaja sifa zake walipokuwa wakiomboleza kifo chake.

Katika kifo hicho cha Mtume (s.a.w.) Bibi Fatma binti wa Mtume (s.a.w.) pia aliomboleza wazi wazi na kuonyesha huzuni yake kwa kusoma beti za Kishairi.

Taz. Ir-Shad As-Saari cha Al-Qas-Talan Uk.318 Juz. 3.

Kadhalika kifo cha Bwana Mtume kiliombolezwa na shangazi yake Mtume (s.a.w.) Bibi Safia kama inavyoonesha katika Istiiab cha Ibnu Abdil-Bari. Pia lbnu ami yake Mtume Bwana Abu Sufian bin Harith Bin Abdil-Mutalib na Bwana Abu-Dhuarib al-Hadh-li, Bwana Abul-Haithami at-Taihani, Ummu Ra-Ala alQushairiyya na Bwana Amir bin at-Tufail na wengineo wote waliomboleza.

Taz. AI-Istiiab na Al-Isaba

Pamoja na maelezo haya, ili kumkinaisha mtu kuhusu suala la maombolezo yafaa sana kukiangalia na kukisoma kitabu kiitwacho Al-Istiiab na pia At-Tabaqat cha Ibn Saad na Usudul Ghaaba na Al-Isaba, kwani humo atakuta mambo mengi yanayohusu maombolezo yaliyofanywa na Masahaba.

Katika Masahaba walioomboleza sana sana kutokana na vifo ni Sahaba wa Kike Bibi Al-Khinsaa, ambaye aliomboleza vifo vya nduguze wawili, Mabwana Sakhr na Muawiyah ambao walikuwa makafiri.

Bibi huyu alikuwa miongoni mwa watu wachamungu kiasi kwamba alitoa wanawe kwa ajili ya kutumikia Uislamu, na wote waliuawa katika njia ya kutumikia Uislamu, kitu ambacho Bibi huyu alikifurahia.

Lakini pamoja na yote hayo hakuacha kuomboleza mauti ya nduguze mpaka alipofariki na wala hakutokea mtu wa kumkemea kwa tendo hilo.

Kwa kifupi suala la kuomboleza ni mashuhuri katika kila zama na kila mahali baina ya Waislamu na wala hawapingani katika hilo.

Sisi tunatosheka na dalili ya kuhalalisha maombolezo yetu tuyafanyayo kama walivyopokea wapokezi wetu kutoka kwa Bwana Zaidi bin as-Shuhaam amesema: "Tulikuwa mbele ya Abu Abdullahi as-Sadiq (a.s.) huku tukiwa na kundi la watu kutoka Al-Kufah, mara akaingia Jaafar bin Affan basi Imam al-Sadiq (a.s.) akamkaribisha na akamsogeza karibu yake kisha akasema: "Ewe Jaafar nimepata habari kwamba wewe unasoma mashairi juu ya Imam Husein (a.s.) na unayasema vizuri, Jaafar bin Affan akasema: "Ndiyo", Imam Jaafar (a.s.) akasema: "Hebu soma mashairi hayo, nikasoma."

Baada ya Mashairi hayo kusomwa katika hali ya kuomboleza mauaji ya Imam Husein (a.s), Imam Jaafar as-Sadiq (a.s.) alilia na wakalia watu waliokuwa wamemzunguka kiasi ambacho machozi yalimtiririka usoni mwake hadi kwenye ndevu, kisha Imam akasema: "Ewe Jaafar, Wallah wamekushuhudia Malaika Watukufu na wao wanasikiliza maneno yako unapo omboleza kwa ajili ya Imam Husein (a.s.), na kwa hakika wamelia kama tulivyolia sisi na zaidi ya hapo, na Mwenyezi Mungu Mtukufu amefaradhisha kwako Pepo katika muda huu na amekusamehe."

Kisha Imam Jaafar as-Sadiq (a.s.) akasema kumwambia Jaafar bin Affan, "Je, nikuongezee ubora kwa wenye kuomboleza mauaji ya Imam Husein (a.s.)", akasema Jaafar bin Affan, "Ndiyo Ewe Bwana wangu."

Akasema Imam Jaafar (a.s.): "Hapana yeyote yule atakayesoma Shairi la maombolezo ya Imam Husein (a.s.), na kwa maombolezo hayo akalia na akawaliza wengine isipokuwa Mwenyezi Mungu atamsamehe na kumwajibishia kupata Pepo."

Imam Muhammad bin Idris ash-Shafii (Imam Shafii) ni miongoni mwa watu waliomboleza mauaji ya Imam Husein (a.s.) aliposoma mashairi ambayo tafsiri yake ni kama ifuatavyo:

Ulimwengu ulitingishika kwa ajili ya kuuawa kizazi cha Mtume Muhammad (s.a.w.), Milima migumu ilikuwa karibu kuyeyuka kwa ajili ya kuuawa kizazi cha Mtume Muhammad (s.a.w.), Milima migumu ilikuwa karibu kuyeyuka kwa ajili ya kuwahuzunikia wao (kizazi cha Mtume), Basi nani atanifikishia barua ya huzuni kwa Husein (a.s.)? Nitaomboleza kifo cha Husein (a.s.) japo nafsi za watu na nyoyo zitachukia.

Taz. Maarij al-Usul.