Majlisi Ya 3: Kusomwa Habari Za Waliokwisha Pita Hapo Kale
Hapana shaka kuwa, upo mkazo na umuhimu mkubwa kusoma na kueleza habari na sifa za waumini waliokwisha fariki zamani, na pia kutaja matatizo na misiba iliyowafika katika maisha yao ya kueneza Uislamu. Kwani kuyataja mambo yao huwa sawa kama kuwataja wao katika hali ya uhai wao.
Ummah hunufaika kutokana na utukufu walioupata zinapotajwa sifa zao, pia tabia njema walizokuwa nazo na vitendo vyao vizuri hunufaisha Ummah wa Kiislamu.
Iwapo Ummah utatoa umuhimu wa kusimulia historia ya viongozi wao walio wema ndiyo nafasi bora ya kulinda Utukufu wake na huwa ni mwongozo mzuri kwa kizazi kitakachofuata.
Kwa hakika mwendo wa vizazi vya tangu hapo zamani na vile vilivyofuatia baadaye, upo katika mtiririko wa kutaja na kukumbuka ubora wa watu waliokufa na misiba iliyowafika kwa njia mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kuyakumbuka hayo kwa njia za uandishi, khutba na utunzi wa mashairi.
Maamuzi sahihi ya akili pamoja na mapokezi sahihi ni vitu ambavyo kimsingi vinatoa mwelekeo wa kuboresha hifadhi ya masimulizi ya watu waliopita.
Kadhalika misingi ya maendeleo na maarifa inalazimisha kuweko kumbukumbu za athari za zamani zenye manufaa kwa jamii.
Ukweli ulivyo ni kwamba uhifadhi wa athari hizo huzifanya roho za watu watukufu ziendelee kuwa hai, na kutokana na kumbukumbu zao hutokea mashindano kwa walio hai ili kujaribu kuzifikia sifa zao na wema wao.
“Hakika katika kutaja habari za watu waliopita kuna kumbukumbu yenye mazingatio kwa wenye akili.” (Qur'an 12:111)
Angalia kitabu cha Mwenyezi Mungu na Sunna ya Mtume wake (s.a.w.) vimeweka wazi sifa za Manabii na matatizo yaliowapata. Pia vimeonyesha bayana jinsi maadui wa Mwenyezi Mungu na Manabii wake walivyofedheheka.
Na lau kama si Qur'an na Sunna ya Mtume (s.a.w.), tusingefahamu Utukufu wa Manabii wa Mwenyezi Mungu, wala tusingejua uovu wa maadui wa Mwenyezi Mungu.
Basi ni vipi hatufahamu kwamba, lau si Qur'an na Sunna kusimamia maelezo ya mafunzo na miongozo ya Mwenyezi Mungu kwa Manabii na waja wa Mwenyezi Mungu, na pia mafunzo ya kuwausia subira kutokana na kero na usumbufu walioupata katika kupigania haki, tungejuaje vituko vya kina Namrud dhidi ya Nabii Ibrahim (a.s.), na Firaun dhidi ya Musa (a.s.) na wengineo?
Ifahamike wazi kwamba kauli zitolewazo kuharamisha kusomwa na kutajwa ubora wa watu watukufu, na kutaja matatizo yao na misiba iliyowafika ni lazima ziende sambamba na kuharamisha Qur'an na Sunna ya Mtume visisomwe.
Kadhalika ni lazima kauli hizo kama zitakubalika, basi hakutakuwa tena na haja ya somo la historia wala (Ilmur-rijal).
Na hakuna mwenye kuridhia upumbavu huu katika nafsi yake akachagua upofu wakati anatambua haki iko wapi.
(Tunajilinda kwa Mwenyezi Mungu kutokana na ujinga uliopita kiasi).
Ili kuthibitisha kwamba kuyataja mema ya waliopita ni tendo lililoanza tangu hapo kabla, tunasoma ndani ya vitabu vya historia juu ya matokeo ya mwaka wa arobaini Hijriya kama ifuatavyo:
Alipofariki Imam Ali (a.s.) alisimama mwanawe Imam Hasan (a.s.) akasema: "Hakika leo mmemuuwa mtu ambaye hajakuweko kabla yake wakumfananisha naye miongoni mwenu, na hatapatikana yeyote baadaye wa kufananishwa naye.
Taz. Tarekh Ibn Jarir na Ibn Athir
Taz. Juz. 2. Uk. 8 Al-Iqdul Farid