read

Majlisi Ya 4: Vikao Kwa Ajili Ya Kuhuzunikia Wafu

Hapana shaka kwamba Mtume (s.a.w.) alihuzunika huzuni nyingi kwa ajili ya kufiwa na Ami yake Bwana Abu Talib na Bibi Khadija Ummul-Mu'uminin (a.s.), kwani wawili hawa walifariki ndani ya mwaka mmoja, na Mtume akauita mwaka huo kuwa ni mwaka wa "huzuni."

Kipindi hiki cha msiba huu mkubwa, Bwana Mtume (s.a.w.) alipunguza kutoka, ikawa muda mrefu hukaa nyumbani, na ikawa Maquraishi wanapomhujumu huomboleza kwa kusema: "Ewe Ammi yangu imekuwa mapema mno kukukosa."

Taz. Siratul-Halabiya Uk.462 Juz.1.

Na zimethibiti habari kwamba Mtume (s.a.w.) alifanya kikao ndani ya Msikiti kwa ajili ya kuwahuzunikia ibni ammi yake Jaafar na Zaid pamoja na ibn Ruwaha waliouawa katika vita ya Muuta.

Vile vile imethibiti kuwa yeye Bwana Mtume (s.a.w.) alihuzunika sana na haikuonekana huzuni namna hiyo kwa Mtume (s.a.w.) baada ya kuuawa wasomaji wake wa Qur'an, na alifanya Qunut kuwaombea msamaha kwa muda wa mwezi mmoja, na pia akawa huwaapiza katika Qunut hiyo waliowauwa.

Kwa hiyo basi kutokana na dalili hizi utakuta zinatoa maamuzi ya kutia nguvu kuwekwa vikao kwa ajili ya kuonesha huzuni kwa kuwakosa watu wema na wenye kumbukumbu nzuri na ukarimu.

Kwani katika kuwapambanua na makundi mengine, huwa na sababu ya kuwahamasisha watu ili waweze kutokea miongoni mwao wenye mfano kama huo. Pia jambo hilo dhahiri yake ni kuwapa haki yao wanayostahiki baada ya kufa kwao, na hupelekea kuwapata watu wengi watakaoiga mienendo yao.

Ama tukija upande wa kufanya vikao kwa ajili ya kumbukumbu ya Masaibu yaliyowapata Maimamu katika njia ya kuleta amani na sulhu kwa Ummah, jambo hili hufanya nafsi kuwa na imani na uongofu na kuzifanya nyoyo kuwafuata Maimamu, japo zimekwisha kupita siku nyingi na matukio hayo yalitokea sehemu za mbali.

Na maneno ya wanaolaumu mambo haya, wakasema kwamba haifai kufanya vikao kwa ajili ya kuhuzunikia maiti hasa unapokuwa umepita muda mrefu, hayana maana tunapoizingatia misiba iliyotupata kutokana na mambo waliyofanyiwa watu wa nyumba ya Mtume (s.a.w.), kiasi ambacho ukweli maneno yao hayaturudishi nyuma katika kuwahuzunikia watu wa nyumba ya Mtume (s.a.w.) japo ni muda mrefu umepita, na wala hayaondoi huzuni iliyotokana na misiba hiyo, na wala hayazimi joto la huzuni muda wote.

Je! hawaioni hadithi iliyoandikwa na Imam Ahmad bin Hambal katika Musnad yake kwamba, Imam Ali (a.s.) alipokuwa akienda Siffin, alipofika Nainawa akawa anasema: "Kuwa na subira Ee Abu Abdillah, kuwa na subira Ee Abu Abdillah katika kingo za mto Furat."

Akaulizwa Imam Ali (a.s.) maana ya kusema hivyo, naye akajibu kwa kusema: "Siku moja niliingia kwa Mtume (s.a.w) nikamkuta analia, basi nikamuuliza sababu ya kulia kwake akasema: "Hivi punde Jibril alisimama mbele yangu akaniambia kwamba hakika Husein (a.s.) atauawa katika kingo za mto wa Furat, akasema Jibril: Je, nikunusishe udongo wa sehemu hiyo? Nikamwambia ndiyo, basi akanyoosha mkono wake akachota gao moja la udongo akanipa."

Taz. Musnad Imam Ahmad Juz. 1 uk. 85

Na imepokewa kutoka kwa Bibi Aisha UmmuI-Mu'uminin kwamba siku moja Husein bin Ali (a.s.) aliingia nyumbani kwa Mtume (s.a.w) hali ya kuwa Mtume anapokea Wahyi, basi Jibril akasema: "Hakika Ummah wako wataingia katika fitna baada yako na watamuuwa mwanao huyu (Husein a.s.), na (Jibril a.s) akanyoosha mkono wake akachukua udongo mweupe na akasema katika ardhi ya udongo huu atauawa mwanao."
Basi Jibril alipoondoka Mtume wa Mwenyezi Mungu alitoka nje hadi kwa Sahaba zake wakiwemo Abubakar, Umar na Ali na Hudhaifa, Ammar na Abudhar, hali ya kuwa analia, basi wote wakamwambia: "Kitu gani kinakuliza ewe Mjumbe wa Mwenyezi Mungu?"

Mtume akasema: "JibriI ameniambia kwamba mwanangu Husein (a.s.) atauawa katika ardhi ya At-Taf na ameniletea udongo huu akasema kuwa, katika udongo huu ndipo yatakapokuwa malazi yake."

Basi mtu wa kwanza kumlilia Imam Husein (a.s.) katika Ummah huu na wa kwanza kupewa udongo wa malazi ya Imam Husein (a.s.) na wa kwanza kuunusa na wa kwanza kuwasomea watu mauaji ya Imam Husein (a.s.) katika ardhi ya At-Taf ni Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.).

Na ni yeye Mtume (s.a.w.) ndiye wa kwanza aliyewasikilizisha masahaba zake hadith ya mauaji ya Imam Husein (a.s.).

Basi hapana shaka kwamba Masahaba walimliwaza Mtume (s.a.w.) kutokana na huzuni hiyo na kilio chake.
“Hakika mnacho kiigizo chema kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu kwa yule anayemtaraji Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho, na yeyote mwenye kupinga basi hakika Mwenyezi Mungu ni mkwasi Mtukufu.” (Qur'an 33:21)