Majlis Ya 5: Kumtolea Sadaka Maiti
Hapana shaka kwamba, ni jambo zuri kuwatolea sadaka maiti wa Waumini kwani jambo hilo alilifanya Mtume (s.a.w.) na akaamuru lifanywe.
Ndani ya sahihi mbili (Bukhari na Muslim) imepokewa toka kwa Bibi Aisha amesema: "Sikupata kumuonea wivu mwanamke yeyote miongoni mwa wakeze Mtume kuliko nilivyomuonea wivu Bibi Khadija ambaye hata sikuwahi kumuona, lakini Mtume alikuwa akimtaja sana (Khadija) na wakati mwingine alikuwa akichinja kondoo na kumkatakata vipande vipande kisha huvipeleka kwa jamaa za Khadija kuwa ni sadaka, basi wakati mwingine nilimuambia Mtume (s.a.w), "Kama kwamba katika dunia hii hakupata kuweko mwanamke isipokuwa Khadija, basi Mtume husema hakika alikuwa ni mwanamke wa pekee bora (katika wake nilioowa) na wala hajakuwepo wa mfano wake na kwake yeye Khadija nilipata watoto."
Hadithi hii inatuonyesha kwamba ni jambo zuri kutowa sadaka kwa marafiki au jamaa wa maiti.
Taz. Sahihi Bukhari Juz. 2 Uk. 207.
Naye Imam Muslim ameandika kwamba, mtu mmoja alifika kwa Mtume (s.a.w.) akasema: "Ewe Mjumbe wa Mwenyezi Mungu, hakika mama yangu amefariki na wala hakuacha usia, je, atapata malipo iwapo nitamtolea sadaka? Mtume akasema: "Ndiyo".
Taz. Sahihi Muslim Juz. 1 Uk. 372.
Kuzaliwa Kwa Al-Imam Husein Bin Ali (a.s.)
Al-Imam Husein (a.s.) amezaliwa tarehe tano Mwezi wa Shaaban Mwaka wa nne Hijiriyah. Baada ya kuzaliwa kwake alishuka Jibril (a.s.) akiwa na kundi la Malaika wapatao elfu moja, wakampongeza Mtume (s.a.w.).
Mtume (s.a.w.) alifurahi sana kwa kuzaliwa kijana huyu, na akawa amempa jina la Husein.
Imepokewa kutoka kwa Ummul-Fadhli mkewe Bwana Abbas Bin Abdil-Mutalib amesema; "Niliota ndoto kabla Husein (a.s.) hajazaliwa, nikaona kama kwamba kipande cha nyama ya mwili wa Mtume kimewekwa mapajani mwangu basi nikamsimulia jambo hilo Mtume wa Mwenyezi Mungu. Mtume (s.a.w.) akasema: "Naona kuna kheri iwapo ndoto yako itakuwa ya kweli, kwani Fatma (a.s.) atazaa mtoto wa kiume nami nitakupa wewe umlee."
Anaendelea kusimulia Ummul-Fadhli anasema: "Basi mambo yakawa kama alivyosema Mtume (s.a.w.) na akanipa Husein (a.s.) nimlee."
Siku moja nikaja naye kwa Mtume (s.a.w.), wakati Mtume (s.a.w.) akiwa anambusu Husein (a.s.), alikojoa na likaruka tone la mkojo kwenye nguo ya Mtume (s.a.w); nikamshika Husein (a.s.) ili kuepusha asizikojolee nguo za Mtume (s.a.w.). Husein (a.s.) akalia; Mtume akasema katika hali ya kama mwenye kukemea, "Tulia ewe Ummul-Fadhli, nguo yangu itafuliwa lakini umemuumiza mwanangu."
Ummul-Fadhli anasema: "Nikamuacha Husein (a.s.) mapajani kwa Mtume na nikasimama kwenda kumletea Mtume (s.a.w.) maji aisafishe nguo yake.
Basi nikaleta maji na nikamkuta Mtume (s.a.w) analia, nikamwambia unalia nini ewe Mjumbe wa Mwenyezi Mungu?
Mtume (s.a.w.) akasema: "Hakika Jibril amenijia na kuniambia kwamba Ummati wangu watamuuwa mwanangu huyu basi ole wao, Mwenyezi Mungu asiwafikishie shufaa (maombezi) yangu siku ya Qiyama watu watakaomuuwa."
Al-Imam Husein (a.s.) alipotimiza mwaka mmoja tangu kuzaliwa kwake, walimshukia Mtume (s.a.w.) Malaika kumi na wawili, nyuso zao nyekundu huku wanalia na wakawa wanamuambia Mtume (s.a.w.) kwamba: "Hakika mwanao yatampata masaibu yaIiyompata Habil kutoka kwa Qabil, na kwa ajili hiyo atapewa malipo mema kama alivyopewa Habil, na atakayemuuwa atakuwa na dhambi sawa na dhambi za Qabil.
Hapakubakia Malaika huko Mbinguni ila wote walikuwa wakishuka na kuja kumpa pole na kumuomba awe mvumilivu na pia walikuwa wanamfahamisha malipo atakayolipwa Imam Husein (a.s.), si hivyo tu, bali walikuwa wanamuonyesha udongo wa mahali atakapouawa, na Mtume (s.a.w.) akawa husema: "Ewe Mwenyezi Mungu mpinge atakayempinga na umlaani atakaye muuwa..."
Alipotimia Imam Husein (a.s.) umri wa miaka miwili Mtume alitoka kufanya safari na katika safari yake hiyo alisimama mahali fulani, basi aliamua kutoendelea na safari yake na mara macho yake yakawa yanabubujika machozi, akaulizwa sababu gani iliyomfanya alie. Mtume (s.a.w.) akasema: "Jibril ananieleza kuhusu ardhi iliyoko kando ya mto Furat iitwayo "Karbala" mahala ambapo atauawa mwanangu Husein (a.s.), sasa hivi ni kama nauona uwanja wa mapambano baina yake na adui zake, pia kama kwamba napaona mahala atapozikwa.
Kisha baadaye Bwana Mtume (s.a.w.) aliamua kurudi hali ya kuwa mwenye huzuni na majonzi, akapanda katika Mimbari na akatoa khutba huku Hasan na Husein (a.s.) wakiwa mikononi mwake.
Alipoteremka kwenye Mimbari akaweka mkono wake wa kulia juu ya kichwa cha Imam Hasan (a.s.) na mkono wa kushoto akauweka kichwani kwa Imam Husein (a.s.) akanyanyua kichwa chake mbinguni akasema: "Ewe Mwenyezi Mungu hakika mimi Muhammad, mja wako na ni Nabii wako na hawa wawili (Hasan na Husein) ni watu bora katika familia yangu na ni wabora katika kizazi changu na atakuwa mbora mtu atakayewafuata hawa katika Ummati wangu, na hakika Jibril ameniambia kwamba mwanangu huyu atapingwa na atauawa. Ewe Mola, mpe baraka nyingi atakapouawa na umfanye awe miongoni mwa Mabwana wa Mashahidi. Ewe Mwenyezi Mungu, usimbariki atakayemuuwa na atakayempinga."
Basi baada ya maneno hayo watu wakaangua kilio Msikitini, kisha Mtume (s.a.w.) akatoa tena khutba nyingine fupi hali yakuwa rangi imembadilika na macho yake yanatoka machozi akasema, "Enyi watu hakika mimi ninawaachia vizito viwili, Kitabu cha Mwenyezi Mungu Mtukufu na Kizazi changu watu wa Nyumba yangu, na hakika viwili hivyo havitatengana mpaka vinifikie katika Haudh, fahamuni kwamba hakika mimi ninavisubiri viwili hivyo, na kwa hakika siwatakeni jambo lolote isipokuwa ni lile aliloniamuru Mola wangu. "Muwapende jamaa zangu". (Kizazi changu).
Mtume (s.a.w.) akaendelea kusema: "Fahamuni ya kwamba (siku ya Qiyama) yatanijia makundi matatu katika Ummah huu.
Kundi la kwanza litakuwa la watu weusi sana, wamezingirwa na Malaika, kisha watasimama mbele yangu nami nitasema: "Ni kina nani nyie"?
"Watashindwa kunitambua, nao watasema: "Sisi ni watu wa Tauhidi miongoni mwa Waarabu.
Basi mimi nitawaambia, "Mimi ndiye Ahmad, Nabii wa Waarabu na wasio Waarabu."
Kisha wao watasema: "Sisi ni katika ummati wako."
Nami nitawaambia: "Basi ni vipi mulinifuata katika kizazi changu na katika Kitabu cha Mola Wangu."
Watanijibu: "Ama kitabu tulikipuuza na kizazi chako tulikiangamiza kwa kuwauwa."
Basi nitageuza uso wangu, nao watarudi wakiwa na kiu kali hali ya kuwa nyuso zao ni nyeusi.
Kisha litanijia kundi jingine jeusi mno kuliko lile la mwanzo nami nitawaambia: "Vipi mulinifuata katika vizito viwili, kile kikubwa na kile kidogo, yaani Kitabu cha Mwenyezi Mungu na Kizazi changu?"
Basi hao watasema: "Ama kile kikubwa (Qur'an) tulikipinga, na ama kile kidogo tulikinyanyasa na kukitawanya ovyo ovyo."
Basi nitawaambia niondokeeni mbele yangu hapo, wataondoka hali wakiwa na kiu kali, makoo yamewakauka na nyuso zao nyeusi.
Baadaye litanijia kundi jingine la watu ambao nyuso zao zinangara kwa nuru.
Basi nami nitawauliza, "Ni kina nani ninyi?"
Watasema: "Sisi ndiyo watu wa neno la Tauhidi na Uchamungu, sisi ni Ummati wa Muhammad Mteule, nasi ndiyo bora katika watu wa haki, tulikilinda vema Kitabu cha Mola wetu, tukaihalalisha halali iliyohalalishwa na Kitabu na tukaiharamisha haramu iliyoharamishwa na Kitabu, na tuliwapenda kizazi cha Nabii wetu."
Basi nitawaambia: "Furahini hakika mimi ndiye Nabii wenu Muhammad (s.a.w) na hakika ninyi duniani mliishi kama hivyo mlivyonitajia."
Basi hapo nitawanywesha maji kutoka ndani ya Haudhi langu (alilonipa Mwenyezi Mungu) nao watarejea hali ya kuwa kiu imewakatika tena watakuwa na furaha, na baadaye wataingia peponi waishi humo milele na milele.
Kuthibiti Uimamu Kwa Husein (a.s.)
Ulithibiti Uimamu kwa Imam Husein (a.s.) baada ya kufariki kwa nduguye Al-Imam Hasan bin Ali bin Abi Talib (a.s.) na hapo ikawa ni faradhi kwa viumbe wote kumtii Imam Husein (a.s.).
Na Uimamu wake ulikuwa ni kwa mujibu wa kauli ya baba yake na babu yake (a.s.) na pia usia wa nduguye Imam Hasan (a.s).
Imam Hasan na Imam Husein (a.s.) wao ni Mabwana wa vijana wa peponi kwa mujibu wa Mwenyewe Mtume wa Mwenyezi Mungu ambaye ni babu yao.
Miongoni mwa ubora waliokuwa nao Imam Hasan na Imam Husein (a.s.), baada ya kuwa ni wajukuu wa Mtume (s.a.w.) na vipenzi vyake katika watu wa nyumba yake, pia ni miongoni mwa watu aliyotoka nao kwenda kuapizana na wakristo wa Najran pale iliposhuka aya ya 61 Sura ya Tatu:
"Basi watakaokuhoji kuhusu Nabii Isa, baada ya kukufikia ujuzi (wa jambo hili) basi waambie njooni tuwaite watoto wetu na watoto wenu na wanawake wetu na wanawake wenu na sisi wenyewe na ninyi, kisha tuapizane tuombe laana ya Mwenyezi Mungu iwashukie waongo."
Aya hii inaitwa aya ya Mubahala, na sababu ya kushuka kwake, ni pale viongozi wa Kikristo kutoka Najran walipokuja Madina katika mwaka wa tisa Hijiriya kumjadili Bwana Mtume (s.a.w.) kuhusu Nabii Isa (a.s.) Mtume akawajibu kwamba; "Hakika mfano wa Isa mbele ya Mwenyezi Mungu ni kama mfano wa Adam…"(Qur'an 3:59)
Wakristo hao waliendelea kumjadili Mtume (s.a.w) hata baada ya jibu hili, ndipo Mwenyezi Mungu aliposhusha aya hii ya 61 Sura ya Tatu, Mtume akaambiwa kama wataendelea kumhoji, basi awaambie waje waapizane kama ilivyoashiria aya hiyo.
Kutokana na uzito wa suala la kuapizana baina ya Mtume (s.a.w.) na Wakristo hao, ilibidi Bwana Mtume (s.a.w) kwa upande wa Waislamu atoke na watu ambao pia watakuwa na uzito wa kukabili maapizano hayo.
Ndipo alipowachukua Hasan na Husein (a.s.) kama wawakilishi wa watoto wa Kiislamu, na Bi Fatma (a.s.) kama mwakilishi upande wa wanawake wa Kiislamu na yeye Mtume (s.a.w.) na Imam Ali (a.s.) wakawa ndiyo nafsi za Waislamu.
Kwa mujibu wa uwakilishi wa Imam Hasan na Imam Husein (a.s.) katika tukio hili unadhihiri ubora na utukufu wa vijana hawa wawili ndani ya Uislamu, na inamuwajibikia kila Mwislamu kuitambua heshima yao na daraja waliyopewa na Mwenyezi Mungu, kama ambavyo Kiongozi Mkuu wa Wakristo hao kutoka Najran alivyokiri ubora na utukufu uliyomo ndani ya nyumba ya Mtume (s.a.w.), siku hiyo ya maapizano akasema: Hakika mimi naziona nyuso za watu ambao lau watamuomba Mwenyezi Mungu auondoe mlima mahala ulipo atauondoa, hivyo basi musiapizane nao mtaangmia na hatabakia Mkristo yeyote ulimwenguni baada ya leo."
Pia miongoni mwa hoja zilizowazi kuhusiana na utukufu walio kuwa nao Imam Hasan na Imam Husein (a.s.) ni kuteremka aya zinazothibitisha kuwa wao ni katika watu watakaoingia Peponi hali ya kuwa bado wakiwa ni vijana wadogo, na jambo hili linapatikana katika Surat Ad-Dahr kuanzia aya ya saba mpaka aya ya kumi na mbili.
Kabla ya kuzitaja aya hizo ni bora kukisimulia kisa cha kushuka aya hizo japo kwa mukhtasar.
Imepokewa kwa Ibn Abbas kwamba, Hasan na Husein (a.s.) waliugua. Basi Mtume (s.a.w.) na baadhi ya watu wakenda kuwaona, watu hao wakamwambia Imam Ali (a.s.) "Lau utaweka nadhiri itakuwa bora."
Imam Ali, Bi Fatma (a.s.) na Mjakazi wao aliyekuwa akiitwa Fiza, wakaweka nadhiri ya kufunga siku tatu ikiwa Hasan na Husein (a.s.) watapona.
Vijana hawa wawili walipona na ikawa kipindi cha kutekeleza ile nadhiri kimefika, lakini ndani ya nyumba hamkuwa na kitu.
Hivyo Imam Ali (a.s.) alikwenda kwa Myahudi mmoja aliyekuwa akiitwa Sham-u’un na akakopa vibaba vitatu vya shayiri.
Bi Fatma (a.s.) akaisaga shayiri hiyo na akaoka mikate mitano kwa ajili ya kufuturu kulingana na idadi yao katika nyumba yao.
Chakula hicho kilipowekwa ili waanze kula, alibisha hodi mgeni na akawatolea salam akasema:
"Asalaam alaikum enyi watu wa Nyumba ya Mtume, mimi ni masikini wa Kiislamu naomba mnipe chakula, nanyi Mwenyezi Mungu atakulisheni chakula cha Peponi."
Basi wakamuonea huruma, wakampa chakula chote, nao wakanywa maji kisha wakalala.
Asubuhi wakaamka na saumu na jioni mwana Fatma aliandaa tena mikate na ilipowekwa tayari kufuturu alibisha hodi yatima na kuomba chakula, wakampa na wao wakanywa maji kisha wakalala.
Asubuhi waliamka na saumu, kisha jioni Bi Fatma (a.s.) alioka tena mikate mitano kwa ajili ya kufuturu.
Walipoketi kufuturu alibisha hodi mtu aliyekuwa mateka akaomba chakula wakampa mikate yote kisha wakanywa maji wakalala.
Kwa ajili ya wao kujinyima kwa muda huo wa siku tatu mfululizo ndipo ziliposhuka aya zifuatazo katika Sura Ad-Dahr:
"Wanaotekeleza nadhiri (zao) wanaiogopa siku ambayo shari yake itaenea na wanawalisha chakula masikini na yatima na mateka hali wao pia wanakitaka chakula hicho. (nao husema watoapo chakula hicho) tunakulisheni kwa ajili ya kutaka radhi ya Mwenyezi Mungu, hatutaki kwenu malipo wala shukurani.
Hakika tunaogopa kwa Mola wetu siku hiyo yenye taabu na shida. Basi Mwenyezi Mungu atawalinda na shari ya siku hiyo na kuwakutanisha na neema na furaha. Na atawalipa kwa kuwapa Bustani (Pepo) na (Mavazi) ya hariri kutokana na kusubiri kwao.”(Qur'an 76:7-12)
Taz. Tafsiri Al- Kashaaf
Zaidi ya hayo ni kwamba Bwana Mtume (s.a.w.) alidhihirisha wazi Uimamu wao kwa Ummah wake pale aliposema: "Wanangu hawa (Hasan na Husein) ni Maimamu wawe wima au wawe wamekaa."
Mlolongo wa uimamu wa Maimamu wetu umekuja kwa kila mmoja kumbainisha atakayechukua nafasi ya Imam anayeondoka.
Na jambo hili la kubainisha Imamu anayefuata lilianzia kwa mwenyewe Bwana Mtume (s.a.w.) kumbainisha Imam Ali (a.s.) katika bonde la Khum pale alipokuwa akitoka katika Hija ya mwisho. (Mwenye kutaka ziada kuhusu jambo la Uimamu wa Ali bin Abi Talib (a.s.) atizame vitabu vya hadithi za Mtume na vitabu vya Historia vinavyotegemewa usahihi wake atalikuta liko wazi). Naye Imam Ali (a.s) alimbainisha Imam Hasan (a.s.) kuwa ndiye atakaye chukua nafasi yake, naye Imam Hasan (a.s.) alimbainisha nduguye Husein (a.s.) kuwa ndiyo Imam wa haki baada yake.
Lakini kwa bahati mbaya sana siyo Imam Ali wala Imam Hasan na Husein (a.s.) aliyepata fursa ya kuongoza Ummah kama ilivyotarajiwa.
Na hii ilitokana na hali iliyowasibu watukufu hawa baada ya Mtume kuondoka.
Tukimuangalia Imam Husein (a.s.) unakuta matatizo yaliyomkuta ni kama yale yaliyomkuta baba yake hata akasema lmamu Ali (a.s.) kama ifuatavyo: "Nikawa nafikiri baina ya kuwa niupate (Ukhalifa) kwa kuuvuta kwa nguvu au nivumilie uvumilivu wa vipofu wasiojua kitu." Mpaka alifikia kusema, "Basi nikaamua kuvumilia hali ya kuwa jichoni mwangu mna mchanga, na katika koo langu mna dukuduku, nauona urithi wangu umechukuliwa kwa nguvu."
Kwa mwendo kama huu, ndivyo alivyofanya Imam Hasan (a.s.) katika siku za uhasama wa Bani Umayya, pindi Mu'awiyah bin Abi Sufiyan alipotwaa madaraka ya Ukhalifa kwa nguvu.
Lakini ifahamike wazi sera ya Maimamu wetu kuwa ni sera ya Mtume (s.a.w.) kwani taabu ilimpata Mtume mwanzo wa kubashiria Uislamu, hakupata utulivu kila alipokuwa akiwaita watu kwenye Uislamu.
Kwa hiyo hali ya Mawasii wake baada yake ni kama ilivyokuwa kwake Mtume (s.a.w.) hasa itakapokumbukwa kwamba, Maquraishi walipata kumtenga Bwana Mtume (s.a.w.) na baadaye akalazimika kujificha pangoni wakati akihama Makkah kwenda Madina.
Hali ya matatizo na usumbufu, kama ilivyowapata Manabii ndivyo ilivyokuwa kwa Maimamu.
Mu'awiyah bin Abi Sufiyan alipofariki na hali ya vita ikawa imemalizika, hali ambayo ilikuwa ikimzuia Imam Husein (a.s.) kujitangaza Uimamu wake wazi wazi, kipindi hiki walitokea watu wa kumsaidia Imam Husein (a.s.) katika kufikisha Ujumbe wa Mwenyezi Mungu. Imam Husein (a.s.) alisimama na kujiandaa kufikisha na kusimamia Dini ya Mwenyezi Mungu (s.w.t.).
Ili kuanza utekelezaji wa kazi hii, ilimbidi Imam Husein (a.s.) asafiri kutoka Madina kwenda Makkah na hatimaye aelekee Iraq kutokana na wito wa watu wa Al-Kufa waliomtaka aende huko ili akawasaidie na kuwaokoa dhidi ya watawala dhalimu.
Kabla yeye Imam Husein (a.s.) kuelekea huko, alimtanguliza Ibn ammi yake Bwana Muslim Bin Aqiil ili akaanze kuwalingania Dini ya Mwenyezi Mungu na kuchukua kwao baia (kiapo cha utii) kwa niaba ya Imamu Husein (a.s.) kwamba watakuwa naye katika Jihadi ya kutetea neno la Mwenyezi Mungu, na kuiokoa Dini na Waislamu kutokana na wanafiki waliokuwa wamewakalia Waislamu kwa mabavu.
Muslim Bin Aqiil alipofika huko, watu hao walimpokea na kumuahidi kumsaidia. Lakini haukupita muda mrefu watu hao wakatangua kiapo chao kwa Muslim Bin Aqiil na wakamuacha akauawa mbele yao kifo cha dhulma akiwa ugenini, lakini pia alikufa akiwa ni shahidi.
Na wao hao hao waliomuita Imam Husein (a.s.) wakatoka hapo Al-Kufa kumfuata Imam Husein (a.s.) kwenda kumpiga vita, na wakamtendea mambo ambayo hawakuyatenda Khawarij (Kundi lililomuasi Imamu Ali (a.s.).
Walimsonga Imam Husein (a.s.), wakamzuia asirudi Makkah wala Madina, wakaweka vizuizi baina yake na maji ya mto Furat mpaka wakamuua hali akiwa na kiu, na wakamdhulumu hali akiwa katika Jihadi, mwenye subira akitaraji radhi za Mola wake.
Hakika ilitenguliwa baia yake na heshima yake ilivunjwa na wala ahadi alizoahidiwa hazikutekelezwa na wakapora mali zake, wakawashika mateka familia yake, wakakidhulumu kizazi cha Mtume (s.a.w.) hali ya kuwa kimekosa ni mahali gani kitakwenda, njia zote zimefungua.
Kizazi cha Mtume (s.a.w.) kikawa na huzuni isiyo kifani.
Safari Ya Imam Husein (a.s) Toka Madina Hadi Makka
Baada ya Imam Hasan (a.s.) kufariki, mashia waliokuwa Iraq walimuandikia Imam Husein (a.s.) kumjulisha kwamba wao wanampa baia na wako tayari kumnusuru.
Imam (a.s.) aliwajibu kwa kusema: "Baina yetu na Mu'awiyah upo mkataba kuhusu jambo hili, hivyo haifai kuuvunja mkataba huo."
Katikati ya mwezi wa Rajab mwaka wa Sitini Hijiriyah Mu'awiyah Bin Abi Sufiyan alikufa na Yazid mwanawe Mu'awiyah akachukua mahali pa baba yake, na ile ahadi na makubaliano aliyoyafanya Imam Hasan (a.s.) na Mu'awiyah yakavunjwa, kwani usia wa Mu'awiyah ulitaka Yazid ndiyo awe Khalifa kinyume na makubaliano kwamba atakapokufa Mu'awiyah ukhalifa urudishwe katika nyumba ya Mtume (s.a.w.).
Basi ilikuwaje alipochukua Ukhalifa Yazid, yule mlevi asiyejali utu wake, mcheza na mbwa, hana akijuacho katika dini kama alivyokiri yeye mwenyewe ndani ya ibara zifuatazo baada ya kukalia Ukhalifa akasema: "... na kwa hakika nimetawazwa baada yake (Mu'awiyah) na wala sitowi udhuru (wa kuacha jambo hili) kutokana na ujinga (nilionao) na wala sijisumbui kutafuta elimu."
Taz. Kitabu cha Qawaid AI-Lughatil-Arabiya Juz.3 Uk.48 chapa ya pili mwaka 1973-1393.
Kitabu hiki kinatolewa na Wizara ya Elimu ya Saud Arabia kwa ajili ya shule za kati kwa wasichana ndani ya sahi ya tatu."[1][1]
Jambo aliloona kwamba ndiyo maslahi kwake yeye Yazid, ni kuandika barua kumpelekea lbn ami yake Walid bin Utba ambaye alikuwa ndiyo Gavana wa Madina siku hizo, akamuamuru achukue baia kutoka kwa watu wote na kutoka kwa Imam Husein (a.s.) kwa niaba yake yeye Yazid, akasema katika barua hiyo "Iwapo Husein (a.s.) atakataa kutoa baia basi muuwe na uniletee kichwa chake."
Walid bin Utba alipoipata barua hiyo alitaka ushauri wa Marwan.
Marwan akamwambia Walid "Hakika Husein (a.s.) hawezi kumbai Yazid, lakini lau mimi ningekuwa na cheo kama chako ningemuua."
Baadaye Walid alimwita Imam Husein (a.s), naye akaja kwa Walid akiwa na watu thelathini miongoni mwao wakiwa ni watu wa nyumba yake na wafuasi wake.
Imam Husein (a.s.) alipofika mbele ya Walid, yeye Walid akamjulisha Imam (a.s.) juu ya kifo cha Mu'awiyah na pia akawa anamlazimisha ampe baia Yazid.
Imam Husein (a.s.) akamwambia "Hakika kiapo cha utii (baia) siyo jambo la siri, basi kesho waite watu nasi pia tuite (tutafanya hiyo baia).
Marwan akasema kumwambia Walid, "Ewe Amir usikubali udhuru wake, kama ni baia atoe sasa hivi au sivyo muuwe." Imam Husein (a.s.) akakasirishwa na maneno ya Marwan akamwambia, "Ewe mwana wa Zarqaa unaniuwa wewe au yeye? Hakika wewe ni muongo tena umefanya jambo la uovu (kutamka hivyo)". Kisha Imam (a.s.) akamgeukia Walid akasema: "Kwa yakini sisi ndiyo watu wa Nyumba ya Mtume (s.a.w.), na kwetu ndiyo kwenye kituo cha Ujumbe (wa Mwenyezi Mungu) na Mwenyezi Mungu alileta nusra kupitia kwetu sisi na akaukamilisha Ujumbe wake kwa Ulimwengu kwetu sisi, na huyu Yazid ni mtu mlevi, muuwaji wa nafsi bila sababu, anafanya maovu wazi wazi, kwa hiyo basi watu kama mimi hawawezi kumpa baia mtu kama yeye." Kisha Imam Husein (a.s.) alitoka mahala hapo akaenda zake.
Marwan akamwambia Walid: "Unaona ulipinga ushauri wangu." (Sasa Husein amekukatalia wazi wazi) Walid akamkemea Marwan akasema: "Kefule!!! Ulilokuwa umenishauri ni jambo la kuniharibia Dunia yangu na Akhera yangu, Wallahi sipendi kuona Dunia yote inakuwa yangu wakati nitakuwa nimemuuwa Husein eti kwa sababu amesema hatombai Yazid, walasidhani kama yeyote atakayemuuwa Husein kwamba atakutana na Mwenyezi Mungu akasalimika, bali mtu huyo atajikuta siku ya Qiyama mizani yake ni nyepesi (hana chochote) na Mwenyezi Mungu hatomtazama mtu huyo wala hatamtakasa na atapata adhabu kali". (kwa kumuuwa Husein).
Basi Imam Husein (a.s.) alikaa nyumbani kwake usiku huo ambao ulikuwa ni usiku wa kuamkia Jumamosi tarehe 27 Rajab mwaka wa Sitini.
Kulipokucha akatoka ili apate kujua habari zilizoko mjini, mara akakutana na Marwan, kisha Marwan akasema: "Ewe Abu Abdillah (Imam Husein) mimi ninayo nasaha kwa ajili yako tafadhali nitii kwa nitakayokuambia utafanikiwa."
Imam Husein (a.s) akasema: "Ni nasaha gani hiyo sema niisikie?"
Marwan akasema: "Hakika mimi nakuamuru umtii Yazid kwani jambo hilo ni bora kwako na ni bora katika Dini yako na Dunia yako."
Imam Husein (a.s.) akasema: "Hakika sisi ni milki ya Mwenyezi Mungu na hakika sisi kwake tutarejea, Eti mimi kumtii Yazid ndiyo itakuwa ni amani kwa Uislamu? Hakika Ummah umepata mtihani mkubwa kwa kuwa na kiongozi mfano wa Yazid."
Mazungumzo baina yao yalikuwa mengi kiasi ambacho Marwan aliondoka ilhali kachukia.
Jioni ya Jumamosi Walid alituma watu waende kwa Imam Husein (a.s.) ili aje afanye baia.
Imam Husein akawaambia: "Ngojeni kutapokucha kesho kisha mtaona ni lipi la kufanya, nasi pia tutaona la kuamua." Wakanyamaza wala hawakuendelea kumlazimisha afanye baia.
Basi Imam Husein (a.s.) alitoka usiku wa kuamkia Jumapili tarehe 28 Rajab kuelekea Makkah, pamoja na wanawe na ndugu zake na kikundi cha watu wa nyumba yake, akaondoka Madina hali anasoma aya ya Qur'an (Al-Qasas Aya 21) isemayo: "Akatoka katika mji huo hali anakhofu, anangoja (lipi litamfika) akasema: "Mola wangu niokowe kutokana na watu madhalimu." (Qur'an 28:21).
Alipita njia kuu iliyo mashuhuri, akaombwa abadili njia kukwepa kufuatwa na adui kama alivyofanya Ibnuz-Zubair, akakataa kufanya hivyo na akasema: "Sitaiacha njia hii mpaka Mwenyezi Mungu aamuwe chochote atakachoniamulia".
Imam Husein (a.s) alifika Makkah usiku wa kuamkia Ijumaa tarehe tatu Shaaban, na aliingia Makkah huku akisoma aya (Sura Al-Qasas Aya 22) ifuatayo:
"Na alipoelekea upande wa Madiyan alisema: Huenda Mola wangu ataniongoza njia iliyo sawa." (Qur'an 28:22)
Alikaa hapo Makkah kuanzia Mwezi huo wa Shaaban mpaka mfungo pili na siku nane za Mwezi wa mfungo tatu, kisha aliona usalama wake pale Makkah ni mdogo.
Kwa hiyo Imam Husein (a.s.) hakuwa na utulivu tena wa kumwezesha kukamilisha Ibada yake ya Hija kwa kuhofia kukamatwa na majasusi ambao wangemkamata hapo Makkah na kumpeleka kwa Yazid Bin Mu'awiyah.
Hivyo basi akafungua Ihram yake na akaifanya kuwa ni Umrah.
Imam Husein (a.s.) akautoka Mji wa Makkah ambao ni Mji wa Mwenyezi Mungu uliotukuka, katika Mji huo ndege na wanyama wanapewa amani waingiapo, basi vipi kwa mjukuu wa Mtume (s.a.w.) kutishiwa amani yake?
Alitoka Makkah kama alivyo uacha mji Mtukufu wa Madina mji wa babu yake ambaye in Mtume wa Mwenyezi Mungu, hali anakhofu mwenye kungojea lipi litamtokea.
[1] Ibara hii haiko ndani ya Kitabu cha asili bali tumeiongeza tu ili kuonesha udhaifu wa Yazid.