Majlisi Ya 6: Yaliyotokea Makka Baada Ya Imam Husein (a.s.) Kufika Hapo
Ilipofahamika kwa wakazi wa Makkah kwamba, Imam Husein (a.s) yupo Mjini hapo, wakazi wa Mji huo walianza kumtembelea kwa wingi.
Miongoni mwa watu waliofika kwake ni pamoja na wageni kutoka sehemu mbalimbali waliokuja Makkah kufanya Umra.
Ikawa watu wanapishana, hawa wanatoka na wengine wanaingia. Pia Abdallah Bin Abbas na Talha Bin Zubair nao walifika kumuona Imam Husein (a.s).
Wawili hawa walimtaka Imam Husein (a.s.) akae hapo Makkah na anyamaze. (Asijihusishe na mambo ya Ukhalifa).
Imam aliwajibu akasema, "Hakika Mtume wa Mwenyezi Mungu aliniamuru jambo ambalo mimi nitalitekeleza."
Vile vile Abdallah bin Omar bin Khatab alifika kwa Imam Husein (a.s.) na kumtaka afanye mapatano na Yazid bin Mu'awiyah bin Abi Sufiyan.
Imam (a.s.) alijibu akasema, "Ewe Baba Abdur-Rahman, unafahamu kwamba Dunia hii kwa uovu uliyomo ni pamoja na kuvinyanyasa viumbe vitukufu vya Mwenyezi Mungu, na elewa pia kwamba kichwa cha Mtume Yahya bin Zakariya kilitolewa na kuwa kama zawadi kwa mtu muovu miongoni mwa watu waovu wa Kibani-Israil?" Akaendelea Imam (a.s) kusema, "Je, unafahamu kwamba, wana wa Israil walikuwa wakiwauwa manabii sabini katika kipindi cha kuchomoza Al-fajiri na kutoka jua, kisha baada ya kufanya tendo hili, huenda wakakaa sokoni na kufanya biashara zao za kununua na kuuza kama kwamba hawakutenda chochote cha uovu? Lakini Mwenyezi Mungu hakufanya haraka kuwa adhibu kutokana na maovu yao bali baadaye aliwaadhibu adhabu kali, basi muogope Mwenyezi Mungu ewe baba Abdur-Rahman na wala usiache kunisaidia."
Katika mji wa Al-Kufah, habari za kifo cha Mu'awiyah zilipowafikia, watu wa Mji huo pia kutawazwa kwa Yazid kuwa ndiyo Khalifa wao hawakupendezwa.
Na waIipofahamu kuwa Imam Husein (a.s.) amekataa kumpa baia Yazid na kwamba yuko Makkah, mashia walikusanyika katika nyumba ya bwana Suleiman bin Surd AI-Khuzai.
Walipokamilika Bwana Sulaiman alisimama akasema, "Kwa hakika Mu'awiyah amekufa na Husein (a.s.)amekataa kuwatii waliotwaa madaraka na ameondoka Madina, sasa yuko Makkah, nanyi ndiyo wafuasi wa baba yake basi ikiwa mnajua kwamba mnao wajibu wa kumsaidia na kumpiga adui yake na kuziangamiza nafsi zetu kwa ajili yake; muandikieni barua aje, na kama mtaogopa kushindwa basi msimuite mtu huyu."
Wakajibu kwa kusema; "Sisi tuko tayari kutoa nafsi zetu kwa ajili yake na tutampiga adui yake."
Sulaiman akasema, "Basi muandikieni". Wakamuandikia Imam Husein (a.s).
Bismillahi Rahman Rahim
Barua kwa Husein bin Ali (a.s.) kutoka kwa Sulaiman bin Surd na Musayib bin Najiya na Rifaat Shadad na Habib bin Mudhahir na mashia wake waumini Waislam katika watu wa Al-Kufah.
Amani iwe juu yake, hakika tunamtukuza Mwenyezi Mungu ambaye hapana Mola ila yeye.
Amma Ba'ad,
Sifa njema ni zake Mwenyezi Mungu ambaye amemuangamiza adui yako aliyekuwa jeuri na mpinzani wa haki huku anaijua.
Adui huyo aliukandamiza Ummah huu kwa nguvu, akapora mali za Ummah, akautawala Ummah hali yakuwa hautaki kutawaliwa naye, kisha akawa anauwa watu wema katika Ummah huu na kubakisha watu waovu; mali ya Mwenyezi Mungu akaifanya ni ya kutumiwa na matajiri na wakatili, basi na alaaniwe kama walivyolaaniwa watu wa Thamud.
Kwa hakika sisi hatuna kiongozi wa kutuongoza, basi njoo ili Mwenyezi Mungu apate kutuunganisha katika haki kwako wewe.
Na huyu Nu'uman (Gavana wa Mu'awiyah hapo al-Kufah) sisi hatushirikiani naye kwenye Ibaada ya Ijumaa wala hatutoki pamoja naye kwenye sala ya Idi.
Iwapo tutafahamu tu kwamba tayari umeshafika mjini hapa, basi tutamtoa tumrudishe Shamu Insha-allah.
Amani iwe juu yako ewe mwana wa Mtume wa Mwenyezi Mungu na pia amani imshukie Baba yako, wala hapana hila wala nguvu isipokuwa vitoke kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu."
Kisha barua hiyo wakapewa Mabwana Abdallah bin Masmaa Al-Hamadani na Abdallah bin Wail waipeleke Makkah na wakawaamuru kwenda mwendo wa haraka.
Baada ya siku mbili kupita tangu walipotuma barua yao, watu wa Mji wa Al-Kufah waliwatuma Mabwana wafuatao.
Qais bin Mas-har As-Saidawi
Abdalla na Abdur-Rahman watoto wa Shadad Al-arhabi
Ammarah bin Abdallah Al-Saluli
Waliwapatia barua zisizopungua mia tano kila mtu.
Baada ya siku mbili tena wakawatuma Mabwana Hani bin Haniy As-Subai na Said bin Abdallah Al-Hanafi waende kwa Imam Husein (a.s.) kumpelekea barua iliyokuwa na maneno yafuatayo.
Bismillahi Rahman Rahim
Kwa Husein bin Ali (a.s.) barua kutoka kwa wafuasi wake miongoni mwa waumini na Waislamu.
Ama baada salaam,
Njoo haraka, kwa hakika watu wanakusubiri, hawana rai nyingine ila kukusubiri wewe. Basi fanya haraka tena haraka sana."
Barua kwenda kwa Imam Husein (a.s.) zilifuatana mfululizo kiasi cha kufikia barua kumi na mbili elfu.
Pamoja na wingi wa barua na kuhimizwa kote alikohimizwa ndani ya barua hizo, Imam Husein (a.s.) alikuwa mzito kuwajibu watu hao.
Siku moja ilitokea zikamfikia barua mia sita, wajumbe waliotumwa wote wakakutana kwa Imam Husein (a.s.) katika kipindi hicho hicho.
Imam Husein (a.s.) akawauliza kuhusu hali ya watu ilivyo huko watokako, kisha akawaambia mabwana Hani na Said bin Abdallah al-Hanafi, "Hebu niambieni ni kina nani hasa waliojumuika kuniandikia barua hii? "
Mabwana hawa wakamfahamisha Imam Husein (a.s.) hali halisi ya watu wa Al-Kufah ilivyo na wakamtajia pia watu wenye msimamo na rai ya kumwita yeye Imam (a.s.).
Basi baada ya kutoshelezwa na maelezo ya mabwana hawa, Imam (a.s.) alisimama akaswali rakaa mbili halafu akaandika barua ifuatayo.
Bismillaah Rahman Rahim
Barua toka kwa Husein Bin Ali, kwenda kwa Watukufu Waumini na Waislamu.
Amma ba'ad, hakika Hani na Said wamenifikia wakiwa na barua zenu, nao ni watu waliofika mwisho miongoni mwa wajumbe wenu mliowatuma.
Kwa kweli nimeyafahamu yote mliyoyaeleza, na jambo muhimu mlilozungumza ni kwamba, "Hakika sisi hatuna kiongozi, basi njoo huenda Mwenyezi Mungu akatuimarisha kwenye haki na uongofu kupitia kwako."
Mimi ninamtuma ndugu yangu na ibn ammi yangu naye ni miongoni mwa watu wa nyumba yangu (Muslim bin Aqiil) aje huko. Basi iwapo ataniandikia kuniarifu kuwa rai za viongozi wenu na watu bora miongoni mwenu zimeafikiana kama ambavyo wajumbe wenu walivyonijulisha, na nilivyosoma barua zenu, basi mimi nitakuja huko haraka apendapo Mwenyezi Mungu Mtukufu.
Kwa yaqini naapa, "Hawi mtu ni Imam (kiongozi wa haki) ila yule anayehukumu kwa mujibu wa Qur'an, mwenye kusimamia haki, anayeishi kwa mujibu wa mafundisho ya dini ya haki (Uislamu) mwenye kuifunga nafsi yake katika dhati ya Mwenyezi Mungu."
Wasalaam.
Baada ya kuandika barua hiyo, Imam Husein (a.s.) alimwita nduguye Bwana Muslim bin Aqiil na akamtuma aende Al-Kufah, afuatane na mabwana Qais bin Mas-har as-Saidawi, Ammarah bin Abdallah na Abdallah na Abdur-Rahman watoto wa Shadad al-Arhabi.
Imam (a.s.) akamuusia nduguye kumcha Mwenyezi Mungu na awe mpole pia asizungumze sababu za yeye kwenda huko.
Mwisho alimtaka afanye haraka kwenda, kwani yaonesha watu wameshikamana pamoja juu ya kumtaka Imam Husein (a.s.) kwenda huko.
Muslim bin Aqiil aliondoka kuelekea Al-Kufah kupitia Madina, mahala ambapo alipofika, aliingia katika Msikiti wa Mtume (s.a.w.) akaswali kisha aliwaaga watu wa nyumbani kwake na wengine aliyopenda kuwaaga. Baada ya hapo aliondoka mpaka Al-Kufah na akafikia katika nyumba ya bwana Mukhtar bin Ubaid at-Thaqafi. Mashia wa Al-Kufah walipopata habari za kuwasili kwa Muslim bin Aqiil, wakawa wanapishana katika nyumba ya Mukhtar ili waonane naye, na kila wakikusanyika kikundi huwasomea barua ya Imam Husein (a.s.), kitu ambacho kilikuwa kikiwafanya walie.
Wakampa baia Muslim bin Aqiil watu wapatao elfu kumi na nane.
Muslim bin Aqiil alipoiona hali hiyo kutoka kwa watu wa Al-Kufah, alimuandikia Imam Husein (a.s.) kumjulisha na kumtaka aende huko.
Mashia waliendelea kumtembelea Muslim bin Aqiil, mpaka Nu'uman bin Bashir aliyekuwa Gavana wa Al-Kufah wakati wa Mu'awiyah na baadaye katika kipindi cha Yazid, akautambua mkusanyiko huo. Pamoja na kutambua hali hiyo, Nu'uman bin Bashir hakumfanyia lolote la ubaya Muslim bin Aqiil.
Lakini baada ya muda kupita, Abdallah bin Muslim bin Rabia al-Hadhrami ambaye alikuwa mfuasi mkubwa wa bani Ummaya, akamuendea Nu'uman bin Bashir akamwambia, "Hakika yote uyaonayo yanatendeka hapa hayana mafanikio kwako ila utapoteza madaraka, na msimamo unaouonyesha baina yako na adui yako ni msimamo wa watu wanyonge."
Kisha huyu Abdallah alimuandikia barua Yazid na akamuambia "Hakika Muslim bin Aqiil amefika hapa Al-Kufah, na watu wamempa baia kwa niyaba ya Husein, basi iwapo wewe unaitaka nchi hii ibaki mikononi mwako, mlete mtu imara atakayesimamia maslahi yako, na atafanya vile ambavyo wewe unamfanyia adui yako, kwani Nu'uman ni mtu dhaifu au pengine anajifanya dhaifu."
Nao kina Ammarah bin Uqba na Omar bin Saad, kila mmoja alimuandikia Yazid barua mfano wa ile aliyoandika Abdallah.
Barua hizi zilipomfikia Yazid, mara moja akamuandikia Ubaidullah bin Ziyad aliyekuwa Gavana wa Basra akamjulisha kwamba, kuanzia sasa yeye ni Gavana wa Al-Kufah na amemkabidhi nchi hiyo.
Kisha Yazid alimjulisha lbn Ziyad khabari za Muslim bin Aqiil na akamsisitiza kumkamata na hatimaye amuuwe.
Ubaidullah bin Ziyad aliyelaaniwa, aliondoka haraka kutoka Basra kuelekea Al-Kufah na akamkabidhi madaraka ya hapo Basra nduguye aliyekuwa akiitwa Athuman.
Ubaidullah aliingia Al-Kufah usiku, na watu wakadhani kuwa ni Imam (a.s.), wakafurahia na kumsogelea. Walipotambua kwamba kumbe ni Ibn Ziyad walitawanyika na kumuacha, naye akaenda hadi kwenye jumba la utawala wa bani Umayya akalala mpaka asubuhi.
Kulipokucha alitoka akaanza kutishia na kuonya kwa ukali wale wanaomuunga mkono Muslim bin Aqiil. Muslim bin Aqiil aliposikia habari za vitisho vya Ibn Ziyad akachelea usalama wake na akaenda nyumbani kwa Bwana Hani bin Urwah mahali ambapo alipewa hifadhi.
Baada ya vitisho na maonyo ya Ibn Ziyad hali iligeuka ikawa mbaya sana, kiasi cha kuwafanya watu waliokuwa wamempa baia Muslim bin Aqiil wahitilafiane na wakavunja baia yao, wala hawakuthubutu tena kujitokeza kumtetea Muslim bin Aqiil na ahadi yao ya kumsaidia wakashindwa kuitimiza.
Kwa hakika kilikuwa kipindi kigumu kwa Muslim bin Aqiil, kipindi chenye mateso na tishio la kuuawa. Ni wakati mgumu kwa kuwa waliokuwa wamemuahidi kumsaidia na kumhifadhi walimtelekeza. Kutelekezwa alikotelekezwa Muslim bin Aqiil kulitoa nafasi kwa adui yake kuzidisha uovu wake dhidi yake na ikafikia Muslim bin Aqiil kuwa anasakwa kila mahali na kuzingirwa barabara katika kila upande hali ya kuwa mpweke hana wakumsaidia.
Muslim bin Aqiil alipata mtihani unaowafika watu wema na alivumilia kungoja matokeo kutokana na vitisho vya panga za maadui zake.