Majlisi Ya 7: Yaliyotokea Al-Kufah Baada Ya Ibn Ziyad Kufika Hapo
Ibn Ziyad alipokwisha wasili katika mji wa AI-Kufah, alijiimarisha kwa kutawanya majasusi kufuatilia nyendo za Muslim bin Aqiil. Matokeo ya ujasusi huo yalimfanya yeye Ibn Ziyad afahamu kuwa Muslim bin Aqiil yuko katika nyumba ya Bwana Hani.
Kwa hiyo Ibn Ziyad aliwaita mabwana Muhammad bin al-Ashath na Hasan bin Asma bin Kharijah na Amru bin al-Hajaaj akawaambia, "Ni kitu gani kinamfanya Hani asije kwetu (kutusalimia)?"
Wao wakamjibu, "Hatujui lakini inasemekana ni mgonjwa." Ibn Ziyad akasema "Habari hizo nazifahamu, lakini pia nafahamu kwamba kesha pona na kwamba yeye mara kwa mara anaonekana mlangoni kwake amekaa, na lau ningefahamu kuwa bado anaumwa bila shaka ningelimtembelea kumjua hali."
Ibn Ziyad aliendelea kuwaambia, "Nendeni mkamwambie asiache kufanya wajibu wake juu ya haki yetu, (kutoa baia) hakika mimi sipendi kuuona ufisadi mbele yangu unaotokana na mtu mtukufu miongoni mwa Waarabu mfano wake yeye Hani."
Ilipokuwa jioni, mabwana hawa wakaenda nyumbani kwa Bwana Hani na wakasimama mbele ya mlango wa nyumba yake wakamwambia, "Ni kitu gani kinachokuzuia usikutane na Amiri (Ibn Ziyad) kwani yeye amekutaja na amesema lau ningefahamu kwamba (Hani) anaumwa ningelimtembelea kumjua hali."
Hani akasema, "Ni maradhi ndiyo yanayonizuia nisiende kukutana naye."
Wale mabwana wakasema kumwambia Hani, "Hakika zimeshamfikia habari kwamba wewe kila jioni unakaa mlangoni nyumbani kwako, naye anakuvumilia kwa hilo, na fahamu kuwa mtawala hawezi kuendelea kuwavumilia watu mfano wako, kwani wewe ni kiongozi wa watu wako, nasi tunakuapia ukweli ulivyo, twende pamoja mpaka kwa ibn Ziyad."
Waliendelea kujadiliana naye mpaka wakamshinda, kisha aliagiza mavazi yake akavaa na hatimaye akaomba aletewe nyumbu wake akapanda na wakaondoka. Walipolisogelea jumba la ibn Ziyad, Hani alihisi kutatokea mambo ambayo si mazuri kwake kama ambavyo tangu mwanzo alikuwa akihisi hivyo. Hani akamwambia Hasan bin Asma bin Kharijah, "Ewe mtoto wa ndugu yangu, kwa kweli mimi ninayohofu kubwa juu ya mtu huyu wewe unaonaje?"
Ibn Kharijah akasema, "Ewe ami yangu mimi siogopi chochote juu yako, usianze kutoa nafasi ya mashaka kwa nafsi yako."
Kwa bahati mbaya Hasan alikuwa hakufahamu dhamira na lengo la ibn Ziyad dhidi ya Bwana Hani. Basi Hani (Mwenyezi Mungu amrehemu) akaja pamoja na jamaa hao mpaka wote wakaingia kwa Ibn Ziyad. Ibn Ziyad alipomuona Hani akasema, "Muhaini kaletwa na miguu yake mwenyewe."
Hani akasema, "Unakusudia nini kusema hivyo ewe Amir."
Mjadala baina yao ulipokuwa mrefu, na Hani hakukubali madai dhidi yake, Ibn Ziyad alimwita Ma’aqal ambaye alipata kuwa mtumwa wake, akaja akasimama mbele yake.
Huyu Ma’aqal alikuwa jasusi wa ibn Ziyad na alikuwa akipeleleza nyendo zote za kina Hani na Muslim bin Aqiil hali ya kuwa wao hawana habari kwamba yule ni jasusi, kutokana kuwa akidhihirisha upendo na nia njema kwa kizazi cha Mtume (s.a.w), hivyo basi alifahamu mengi kuwahusu wao.
Hani alipomuona mtu huyo, ndipo alipotambua kwamba alikuwa ni jasusi wa ibn Ziyad na kuwa mambo yao yote amekwisha yafikisha hapo, na amefaulu kumtumbukiza mikononi mwa ibn Ziyad.
Hali ilivyokuwa hivyo, Hani akasema kumwambia ibn Ziyad, "Mwenyezi Mungu amfanye mwema Amir, naapa kwa jina la Mwenyezi Mungu kwamba, Muslim bin Aqiil sikumwita mimi lakini alinifikia bali ya kuwa anaomba ulinzi wangu nikamkubalia kumlinda, na niliona haya kumkatalia, na niliingiwa na utu ambao ulinilazimisha kumkaribisha, na sasa hebu nipe nafasi ili nirudi nikamuamuru atoke nyumbani mwangu aende apendako ili nijitoe kuwa mimi ni mdhamini wake, na kisha nitarudi nije nikupe kiapo changu cha utii."
Ibn Ziyad akasema, "Wallahi hutoki hapa isipokuwa uniletee huyo Muslim Bin Aqiil." Hani akasema, "Wallahi sitakuletea wataka nikuletee mgeni wangu kisha umuuwe?"
Ibn Ziyad akasema, "Wallahi naapa kuwa lazima utaniletea mtu huyo."
Hani naye akajibu, "Wallahi sikuletei hata kidogo."
Majibizano baina ya wawili hawa yalipozidi, bwana mmoja aitwaye Muslim bin Amri Al-Baahili akasema, "Mwenyezi Mungu na amfanye mwema Amir, hebu niachie nafasi mimi na yeye nizungumze naye." Akasimama yeye na Hani sehemu fulani humo ndani, kiasi kwamba ibn Ziyad anawaona na anasikia wanachokisema.
Wakati mazungumzo yao yanaendelea, mara sauti zao zikapanda juu zaidi, kisha Bwana al-Baahili akasema, "Nakuapia Mwenyezi Mungu ewe Hani usijiuwe mwenyewe, na wala usilete balaa kwa jamaa zako, Wallahi hakika mimi nakuona ni mtu muhimu sipendi kuona unauawa, mtoe huyu (Muslim bin Aqiil) uwape watawala, kwani jambo hilo la kumtoa siyo unyonge wala aibu bali unamtoa kwa mtawala (ataamua la kumfanya)."
Hani akajibu, "Wallahi kumtoa Muslim bin Aqiil kwangu mimi ni dalili za unyonge na aibu, nimtoe mgeni wangu na isitoshe ni Mjumbe wa mjukuu wa Mjumbe wa Mwenyezi Mungu hali nikiwa ni mzima mwenye nguvu na ninao wasaidizi wengi, Wallahi naapa japo hata ningekuwa peke yangu sina wakunisaidia nisingemtoa (Muslim bin Aqiil) mpaka nife kwa ajili yake."
Al-Baahili akawa anamsisitiza Hani amkabidhi Muslim kwa ibn Ziyad, lakini Hani hujibu, "Wallahi simtoi kamwe."
Ibn Ziyad akawa ameyasikia hayo akasema, "Msogezeni hapa karibu yangu", Hani akasogezwa kisha ibn Ziyad akasema kumwambia Hani, "Wallahi lazima uniletee huyo Muslim vinginevyo nitaikata shingo yako."
Hani akasema, "Kama utaniua fahamu wazi utakuwa umewasha moto wa fitna nyumbani kwako."
Akasema: "Ooo!!! Ole wako nakuonea huruma, unanitishia hiyo fitna?"
Kipindi hicho Hani alikuwa akidhani kwamba nduguze na jamaa zake watamsaidia.
Baada ya ibn Ziyad kutamka maneno yale akasema, "Msogezeni kwangu" akasogezwa, kisha ibn Ziyad akatoa fimbo ambayo alianza kumpiga Hani puani na usoni mpaka pua ya Hani ikakatika na nyama za usoni mwake zikachanika, damu zikawa zinamvuja na kutiririka kwenye nguo zake, na wala hakuacha kumpiga mpaka ile fimbo ikavunjika.
Naye Hani baada ya kutendewa haya, alinyoosha mkono akikusudia kuuchukua upanga wa askari moja aliyekuwa kasimama hapo, yule askari akauvuta upanga wake kuusalimisha.
Alipoona hivyo lbn Ziyad alipiga kelele akasema "Mshikeni mara moja". Basi Hani akakamatwa na kukokotwa hadi katika moja ya nyumba akafungiwa humo na kuwekewa mlinzi.
Hasan bin Asma bin Kharijah akasimama na kumwambia ibn Ziyad, "Hatujapata kuwa wajumbe wenye khiyana isipokuwa leo ewe Amir, umetuagiza kwa mtu huyu na ukatuamru tumlete kwako, na tulipokuwa tumekuletea umeuchanachana uso wake na umeimwaga damu yake na bado unadai kwamba utamuua."
Maneno haya yakamchukiza ibn Ziyad, akakasirika sana akasema kumwambia Hasan, "Na wewe uko hapa (kumtetea Hani)?"
Kisha akatoa amri Hasan apigwe, akapigwa na baadaye akafungwa kamba na akatupwa gerezani. Hapo Hasan akawa anaomboleza kwa kusema "Hakika sisi ni milki ya Mwenyezi Mungu na kwake tutarudi, ewe Hani kwa nafsi yangu ninakusikitikia."
Khabari za tukio hili zikamfikia Bwana Amri bin al-Hajaaj, na kwamba Hani amekwisha kuuawa.
Bwana Hani alikuwa ni mkwe wa huyu al-Hajaaj kwa binti yake aliyekuwa akiitwa "Ruwaihah". Hivyo basi Amri bin al-Hajaaj akafika hapo Al-Kufah akiwa na jamaa zake, wakalizunguka jumba la ibn Ziyad, kisha Amri alizungumza kwa sauti kubwa akasema, "Mimi ni Amri bin al-Hajaaj na hawa nilionao ndiyo viongozi wa jamii ya Madh-haj, nao hawajatoka katika utii wala kupinga umoja, lakini habari zimetufikia kwamba mwenzetu (Hani) kauawa."
Basi Qadhi Shuraih akaja kutoka ndani alimokuwa yeye na ibn Ziyad na anayaona yote yaliyomfika Hani akamwambia ya kwamba Hani yu katika amani. Basi wakaridhika na kuondoka kurejea kwao.