read

Majlisi Ya 8: Maafa Yaliyompata Muslim Bin Aqiil

Muslim Bin Aqiil zilipomfikia habari za matendo aliyoyatenda Ibn Ziyad kumtendea Hani, alitoka yeye pamoja na watu waliokuwa wakimtii kwenda kumsaidia Hani na kumuokoa, pia kupigana na Ibn Ziyad.

Ibn Ziyad alipogundua jambo hilo alijificha katika jumba hilo la utawala wa Bani Umayya, ikawa wafuasi wake ndiyo wanapigana na watu wa Muslim bin Aqiil.

Wafuasi wa ibn Ziyad waliokuwa pamoja naye wakawa wanachungulia na kuwatahadharisha wafuasi wa Muslim bin Aqiil na wakawaonya kuwa litakuja Jeshi kutoka Sham kwa Yazid nalo litawashambulia.

Waliendelea kufanya hivyo mpaka usiku ukaingia, hapo ndipo wafuasi wa Muslim bin Aqiil walipoanza kutawanyika kumkimbia Muslim, na wakawa wanaambiana, "Ni kitendo gani tukifanyacho kwa kuikimbilia fitna, inatupasa kujificha majumbani wetu tuwaache hawa jamaa mpaka hapo Mwenyezi Mungu atakapoleta upatanishi baina yao."

Waliendelea kutawanyika mpaka ilipofika jioni, Muslim bin Aqiil aliswali Maghrib akiwa na watu thelathini tu ndani ya msikiti. Alipoiona hali hiyo alitoka kuelekea milango ya upande wa Kindah, na hakufika hapo ila alikuwa kabaki peke yake watu wote walikwisha kumtoroka.

Kisha Muslim alitoka kupitia mlangoni, lakini ghafla akajikuta hana mtu wa kumuongoza njia, kumbe alikuwa kabaki peke yake watu wote walikwisha kumtoroka.

Muslim bin Aqiil akaendelea mbele hali ya kuwa akipita katika vichochoro vya mji wa Al-Kufah, hajui la kufanya wala hafahamu aendako. Alitembea mpaka akafika kwenye mlango wa nyumba ya mama mmoja aliyekuwa akiitwa "Taua" ambaye alipata kuwa mjakazi wa Ash-Ath bin Qais, alipomuacha huru akaolewa na Usaid Al-Hadhrami akamzalia mtoto aliyeitwa "Bilal".

Huyu Bilal wakati Muslim bin Aqiil anafika kwenye nyumba ya mama yake, alikuwa katoka pamoja na watu fulani, hivyo basi mama yake alikuwa akimngojea pale mlangoni.

Muslim bin Aqiil akamtolea salamu mama yule "akaitikia", kisha akamuomba maji ya kunywa, "Akapewa". Yule mama aliporejesha ndani kile chombo cha maji, alitoka na kumkuta Muslim akiwa ameketi chini akamuuliza, "Je, hujanywa maji?" akajibu, "Nimekunywa."

Mama yule akaendelea kumsemesha Muslim, lakini akawa hakujibu, mwisho yule mama akasema "Sub-hanallah!!'. Ewa mja wa Mwenyezi Mungu simama uende kwenu, haifai wewe kuendelea kukaa mlangoni kwangu wala siwezi kukuruhusu ukae hapa."

Muslim bin Aqiil akasimama na akasema, "Ewe mtumwa wa Mwenyezi Mungu, katika mji huu sina makazi wala ndugu, je, wapenda kupata ujira mwema na malipo mazuri, ili nami hapo baadaye nikulipe kwa wema wako baada ya siku hii ya leo?"

Yule mama akasema "Nini makusudio yako ewe mtumwa wa Mwenyezi Mungu?"

Akajibu "Mimi ni Muslim bin Aqiil, watu wa Mji huu wamenidanganya na wamenihadaa, na sasa wamenifukuza."

Yule mama akasema, "Wewe ndiwe Muslim?"

Akasema, "Ndiyo."

Yule mama akasema, "Ingia ndani."

Muslim akaingia ndani ya nyumba miongoni mwa nyumba za mama yule isiyokuwa ile anayoishi mwenyewe, na yule mama akamtayarishia Muslim mahali pa kulala, na akamletea chakula ambacho Muslim hakukila.

Mtoto wa yule mama aliporudi na akawa amemtambua Muslim basi haraka alipeleka habari kwa ibn Ziyad kumjulisha mahali alipo Muslim bin Aqiil.

Ibn Ziyad akamleta Muhammad bin al-Ash-ath na akamtuma pamoja naye Ubaidullah bin Abbas As-Sulami wakiwa na watu sabini wa kabila la Qais mpaka kwenye nyumba aliyoko Muslim.

Basi Muslim aliposikia sauti ya kwato za farasi na sauti za watu, akafahamu kwamba amefuatwa yeye. Akawatokea akiwa na upanga wake, nao wakamvamia ndani ya nyumba kabla hajatoka, akawashambulia kwa upanga mpaka akawatoa nje. Kisha walimrudia tena naye akawashambulia vikali, na ikatokea mashambulizi yakawa baina ya Muslim na Bakru bin Hamran al-Ahmari, basi huyo Bakru "Mwenyezi Mungu amlaani" alimpiga Muslim dhoruba la Upanga akamkata mdomo wa juu, na akafanya haraka kumkata mdomo wa chini pia, meno ya chini ya Muslim yakabomoka.

Naye Muslim pamoja na hali hiyo alimpiga Bakru dhoruba kali ya kichwani, akamfuatisha nyingine katika sehemu iliyo kati ya shingo na bega, dhoruba ambayo ilikaribia kuingia ndani kabisa ya mwili wa Bakru.

Muslim pamoja na maumivu aliyokwisha yapata, aliendelea kuwashambulia watu wa ibn Ziyad mpaka akafaulu kuwauwa kikundi miongoni mwao.

Walipoona hali ya ushujaa wa Muslim, walianza kumshambulia wakiwa juu ya nyumba kwa kumtupia mawe, na wakawasha vijinga vya moto kisha wakawa wanamrushia kutoka katika paa la nyumba.

Muslim hakukata tamaa bali aliwatokea hali ya kuwa ameutoa upanga wake tayari kwa kupambana nao.

Muhammad bin al-Ash-ath akawa anamwambia Muslim "Jisalimishe usiiue nafsi yako."

Muslim alimjibu Muhammad al-Ash-ath hali ya kuwa akiwashambulia akasema: "Nimeapa, siuawi ila niwe katika hali ya uhuru, japokuwa mauti nayaona kuwa ni jambo gumu, nachukia kuhadaiwa au kudanganywa, nitakupigeni wala siogopi madhara."

Ibn al-Ash-ath akapiga ukelele aksema, "Hakika wewe hudanganywi wala kuhadaiwa."
Lakini kufikia kipindi hiki Muslim akawa ameshehenezwa kwa mawe na akashindwa kuendelea na mapambano, basi akauegemeza mgongo wake ukutani.

lbn al-Ash-ath akamwambia tena Muslim, "Jisalimishe."

Muslim akajibu, "Mimi nimekwisha salimika."

Akasema ibn Ash-ath, "Vema."

Kisha Muslim akawaambia jamaa waliokuwa wakimshambulia, "Je ninayo amani?"

Wakasema, "Ndiyo."

Akasema "Japo msinipe amani lakini siwezi kuweka mkono wangu mikononi mwenu" (Siwezi kuwatii).

Hapo wakamletea nyumbu, wakampandisha kisha wakamzunguka na wakamnyang'anya panga lake, ikawa kama kwamba Muslim katika kipindi hicho anaihuzunikia nafsi yake, basi ghafla akaanza kujawa machozi machoni mwake akasema: "Huu ndiyo mwanzo wa kuvunja ahadi, uko wapi basi uaminifu wenu?" Hapa Muslim akawa analia.

Ubaidullah As-Sulami akasema kumwambia Muslim bin Aqiil, "Hakika yeyote mwenye kutafuta mambo kama haya uyatafutayo, pindi anapofikwa na hali kama hii iliyokufika wewe hana haja ya kulia."

Muslim akajibu, "Hakika mimi Wallahi silii kwa ajili ya nafsi yangu, wala nafsi yangu siihuzunikii kutokana na kifo, japokuwa siipendelei nafsi yangu kuangamia, lakini (fahamu kwamba) nawalilia jamaa zangu wanaokuja kunifuata mimi, namlilia Husein na watu wa Husein (a.s.)."

Kisha Muslim akamuelekea Ibn al-Ash-ath akasema: "Hakika wewe utashindwa kunipa amani, basi je, kwako kuna wema wowote (unitendee)? Unaweza ukatuma mtu kutoka kwako kwa niyaba yangu akamfahamishe Husein (a.s.), kwani mimi simuoni Husein (a.s.) ila atakuwa leo ametoka au atatoka leo pamoja na watu wa nyumba yake basi akamwambie kwamba "Hakika mwana wa Aqiil amenituma kwako, hali ya kuwa yeye ni mateka mikononi mwa watu (wa Al-Kufah) haoni nafasi yoyote ila jioni atakuwa kisha uawa, naye anasema rudi, wewe na watu wa nyumba yako, baba yangu na mama yangu (nawatoa) iwe fidia kwako na wala wasikudanganye watu wa Al-Kufah, hakika wao ndiyo wale wale watu (waliojidai kushirikiana na) baba yako, ni wao ambao alikuwa akitamani (Baba yako) kutengana nao ima kwa mauti (ya kawaida) au kuuawa, hakika hawa watu wa Al-Kufah wamekudanganya na mwenye kudanganywa huwa hana rai."

lbn Ash-ath akamchukua Muslim mpaka kwenye mlango wa jumba la utawala, akaingia ndani na kumpa khabari zote ibn Ziyad.

Muslim kiu kali ikawa imemsonga, na hapo kwenye mlango wa jumba hilo kuna watu wengi wanasubiri kupewa ruhusa (kuingia). Mara ghafla likaletwa jagi la maji ya baridi, Muslim akasema "Ninywesheni maji haya."

Muslim bin Amri Al-Baahili akasema, "Wayaonaje, ubaridi ulioje wa maji haya!!!, Wallahi hutaonja japo tone moja kabisa, mpaka kwanza uonje joto kali lililomo katika moto wa Jahannam."

Muslim bin Aqiil akamjibu Muslim bin Amri akasema: "Mama yako kapata hasara (kuzaa mtoto kama wewe) una uovu kiasi gani na moyo mbaya kadiri gani (bali muovu mno) ewe mwana wa Baahilah, wewe ndiyo unastahiki mno kulipata joto hilo kali na pia kuishi milele ndani ya moto wa Jahannam."

Kisha Muslim bin Aqiil akaegemea ukutani.

Bwana Amri bin Huraith akaja na kile chombo kilichokuwa na maji, juu yake kuna kitambaa, pia alikuwa na jagi ambalo alilitia maji yale na akamwambia Muslim bin Aqiil "Kunywa maji", ikawa kila anapotaka kuyanywa maji, basi lile jagi hujaa damu yake inayobubujika kutoka mdomoni mwake.

Akajaribu mara mbili kuyanywa maji hayo bila mafanikio, na alipokusudia kwa mara ya tatu kunywa, meno yake mawili ya mbele yakabomoka na kutumbukia ndani ya jagi la maji.

Muslim bin Aqiil akasema, "Al-hamdulillah (Sifa njema ni zake Mwenyezi Mungu) lau ningekuwa nayo riziki iliyogawiwa kwangu (kwenye maji haya) ningeyanywa."

Baadaye akaingizwa ndani kwa ibn Ziyad, Muslim hakumtolea salam lbn Ziyad.

Mlinzi wa Ibn Ziyad akamwambia Muslim, "Mtolee salaam Amir (kiongozi)."

Muslim akasema, "Ole wako nyamaza, Wallahi kwangu mimi (huyu) siyo Amiri."

Ibn Ziyad akasema kumwambia Muslim, "Ewe mwana wa Aqiil uliwakuta watu (hapa Al-Kufah) wakiwa pamoja, ukawatenganisha na kuwatawanya (wasikubaliane), pia ukawafanya wagombane wao kwa wao."

Muslim akasema, "Sivyo kabisa, mimi sikuja hapa kwa ajili hiyo, lakini watu wa Mji huu walidai kwamba Baba yako (Muawiyah) amewauwa watu wema (miongoni mwa wenyeji wa hapa) na amemwaga damu zao, na akawatendea matendo ya (Wafalme Kisra na Kaisar, basi sisi tukawafikia (hapa) ili tuamrishe uadilifu na tuwaite (wote) kwenye hukumu ya kitabu (Qur'an)."

Ibn Ziyad akasema, "Tangu lini nawe (Muslim) ukafaa kuwa (kiongozi) wa hayo uliyoyasema? Kisha ibn Ziyad mwenye kulaaniwa akaendelea kusema kumwambia Muslim "Ewe muovu hakika nafsi yako inakutamanisha jambo ambalo Mwenyezi Mungu kisha kumpa mwingine, na haikukuonyesha mwenye kustahiki."

Muslim akasema, "Basi nani atastahiki jambo hilo (la uongozi wa Ummah) endapo sisi (tutaonekana) hatufai?"

Ibn Ziyad akajibu akasema, "Mwenye kustahiki jambo la (uongozi) ni Amirul Mu’uminina Yazid."

Muslim aksema, "Kwa kila hali Mwenyezi Mungu ashukuriwe, sisi tumeridhia na tunaridhia kwamba Mwenyezi Mungu ndiye atakayetoa uamuzi baina yetu na ninyi."

Ibn Ziyad akasema, "Mwenyezi Mungu anilaani iwapo sitakuuwa, tena kwa uwaji baya ambalo hajapata mtu kuuliwa katika Uislam."

Muslim akasema, "Ama ilivyo kweli na hakika wewe ni mtu uliyezusha katika Uislamu mambo ambayo hapo kabla hayakuwapo, na kwa tabia yako hutaacha kufanya mauaji ya kinyama, na hutoacha kuwa ni mfano mbaya, mwenye nia mbaya, na kijicho kwa yule mwenye kustahiki mno kwa jambo hili kuliko wewe."

lbn Ziyad akamuelekea Muslim kwa ulimi wa matusi kumtukana yeye na kamtukana Husein na Ali (a.s.) pia Aqiil (baba yake Muslim) akamtukana.

Muslim akanyamaza asimsemeshe kitu ibn Ziyad, bali aliwaangalia watu waliokuwa pamoja na lbn Ziyad, akamuona Omar bin Saad akiwa ni miongoni mwao, akasema kumwambia Omar bin Saad "Ewe Omar bila shaka baina yangu mimi na wewe kuna udugu, basi mimi ninayo haja fulani kwako, na itakupasa wewe ufanikishe haja yangu hiyo, lakini ni siri baina yangu na wewe."

Omar bin Saad (mwenye kulaaniwa) akakataa kumsikiliza Muslim, lakini Ubaidullahi bin Ziyad akamuamuru Omar asikilize ombi la Muslim.

Basi wakajitenga wawili hao upande fulani hali ya kuwa Ibn Ziyad anawaona, Muslim akasema, "Hakika kuna baadhi ya watu wa Al-Kufah wananidai Dirham mia saba, basi kauze upanga wangu na deraya yangu kisha ulipe deni hilo, na nitakapokuwa nimeuawa uchukue mwili wangu na uusitiri (uuzike) na pia mtume mtu aende kwa Husein amwambie arudi (asije hapa Al-Kufah) bila shaka mimi nilimuandikia kwamba watu wanamuunga mkono (kumbe wamegeuka) nami namuona kuwa anakuja."

Ibn Saad akasema kumwambia ibn Ziyad, "Je, wafahamu anasema nini (Muslim) ewe Amiri? hakika anasema kadha kadha". (Akasema yote aliyomwambia Muslim) "Ibn Ziyad akasema kumwambia Muslim bila shaka mtu mwaminifu hawezi kukufanyia khiyana lakini wewe umemuamini mtu mwenye khiyana."

Kisha huyu Ibn Ziyad "Mwenyezi Mungu amlaani" akaamuru Muslim apandishwe juu ya paa la jumba hilo na akatwe shingo yake huko juu, na itakapo anguka wakitupe kiwiliwili chini kuifuata shingo itakayokuwa imeporomoka chini pamoja na kichwa. Ibn Ziyad akamwita Bakru bin Hamran akamwambia "Panda juu ukamkate shingo yake." Akapanda.

Wakati Muslim akipandishwa juu ili akauawe, alikuwa akisoma Takbira na kuomba msamaha kwa Mwenyezi Mungu na akimsalia Bwana Mtume (s.a.w.) na pia akawa husema, "Ewe Mwenyezi Mungu, hukumu baina yetu na wale waliotudanganya na wametutweza, basi ghafla akainamishwa chini kisha shingo yake ikakatwa ikadondoka chini na mwili wake pia ukafuatishwa mpaka chini (Muslim bin Aqiil akawa ameuawa kishahidi, ewe Mola iteremshie amani na Rehema roho yake nasi tujaalie vifo vya kishahidi katika kukutumikia - Amin).

Baada ya kuuawa Muslim bin Aqiil, pale pale Ibn Ziyad akaamuru Hani atolewe (alikuwa bado kafungwa) akasema "Mtoeni mumpeleke sokoni kisha muikate shingo yake." Hani akatolewa ilhali mikono yake imefungwa na akawa anasema "Ee!!! jamaa zangu, leo sina jamaa yeyote, wako wapi jamaa zangu?"

Alipoona kwamba hakuna yeyote wa kumsaidia aliutoa kwa nguvu mkono wake katika kifungo alichofungiwa, kisha akasema, "Je, hakuna fimbo au kisu au jiwe ambalo mtu anaweza kujilinda nafsi yake?"

Askari wa ibn Ziyad wakamrukia na wakamfunga barabara na hapo hapo wakamwambia "Nyoosha shingo yako."

Hani akasema, "Sijawa mkarimu kiasi hicho kuwanyooshea shingo yangu, na pia siwezi kuwasaidieni katika kuiua nafsi yangu."

Mturuki ambaye alipata kuwa mtumwa wa ibn Ziyad akaachia dhoruba ya upanga kumkata Hani, lakini dhoruba hiyo haikumfanya kitu Hani.

Hapo Hani aksema, "Kwa Mwenyezi Mungu ndiko kwenye marejeo, Ewe Mola, narudi kwenye huruma zako na radhi zako."

Yule mturuki akarudia mara ya pili kumkata Hani akafaulu kumuuwa, hivyo Hani akafa akiwa shahidi kwa kutaraji rehema za Mola wake.