Majlisi Ya 9: Imam Husein (a.s.) Aazimia Safari Ya Iraq
Imam Husein (a.s.) alipoazimia kwenda Iraq alisimama akatoa hotuba akasema: "Hamu yangu ya kukutana na wazazi na ndugu zangu waliotangulia (kufariki) ni kama shauku aliyokuwa nayo Yaaqub kwa mwanawe Yusuf (alipopotea) na kifo kitakchonifika kwangu ni jambo bora, kwani naona viungo vya mwili wangu vitakatwakatwa na maadui zangu hapo katika jangwa lililo baina ya Nawasiisi na Karbala.
Wakisha kuniua, lengo lao litakuwa limetimia na hamu yao dhidi yangu itakamilika. Hakuna njia ya kukwepa siku ambayo imekwisha kuandikwa. Alitakalo Mwenyezi Mungu liwe, kwetu sisi watu wa nyumba ya Mtume huwa tumeridhia pia liwe. Jamii ya Mtume wa Mwenyezi Mungu haitatenganishwa naye, bali itakusanywa iwe pamoja naye kesho Akhera mahali patukufu.
Mtume atawakaribisha jamii yake kwa wema na furaha na atawatimizia yote aliyowaahidi. Fahamuni enyi watu ya kwamba, ye yote atakayejitolea roho yake kwa ajili yetu, na akawa amejiandaa kukutana na Mwenyezi Mungu kwa wema, basi na asafiri pamoja nasi, kwani nitaondoka asubuhi pindi apendapo Mwenyezi Mungu Mtukufu."
Usiku wa kuamkia safari, alikuja Muhammad Al-Hanafiyyah ambaye ni mdogo wa Imam Husein (a.s.) (kwa mama mwingine) akamwambia Imam Husein (a.s.) "Ewe ndugu yangu bila shaka watu wa Al-Kufah ndiyo wao ambao wewe unafahamu khiyana waliyomfanyia baba yako na nduguyo (Hasan a.s.), nami nachelea kwamba yatakufika yaliyowafika waliokutangulia, basi iwapo utaona ni vema bora ubakie hapa Makkah, kwani wewe ni kiumbe bora mno katika Haram hii ya Makkah nawe ndiyo mlinzi wake."
Imam (a.s.) akajibu kwa kusema "Ewe ndugu yangu hakika nachelea Yazid asije ndani ya eneo hili takatifu, nami nikawa ndiyo kiumbe wa kwanza kuhusishwa na uvunjwaji wa heshima ya nyumba hii."
Muhammad AI-Hanafiyya akasema, "Basi ikiwa unachelea hilo, nenda Yemen au sehemu nyingine za nchi, kwani huko utapata hifadhi wala hakuna atakayeweza tena kukushambulia ukiwa huko."
Imam Husein akasema, "Nitaitafakari rai yako". Kulipokucha alfajiri mapema, Imam Husein (a.s.) alifungasha akaondoka.
Khabari zikamfikia Muhammad Al-Hanafiyya kwamba Imam Husein (a.s.) ameondoka, akamfuatia, na alipompata akazishika hatamu za ngamia aliyekuwa kapanda Imam Husein (a.s.) kisha akasema, "Ewe ndugu yangu hukuniahidi kwamba utalitafakari ombi langu?"
Imam akasema, "Bila shaka nilikuahidi."
Muhammad Al-Hanafiyyah akasema, "Basi jambo gani limekufanya utoke haraka namna hii?"
Imam akajibu, "Ulipoondoka Mtume wa Mwenyezi Mungu alinijia akaniambia, "Ewe Husein toka (wende Iraq) bila shaka Mwenyezi Mungu amekwisha taka kukuona wewe umeuawa."
Akasema Muhammad Al-Hanafiyya, "Hakika sisi ni milki ya Mwenyezi Mungu na bila shaka kwake tutarejea, lakini nini maana yako kuwachukuwa wanawake hawa pamoja nawe ikiwa hali yenyewe ndiyo hii uliyoniambia?"
Imam akajibu "Mtume ameniambia kwamba Mwenyezi Mungu amekwisha kutaka vile vile kuwaona wakiwa ni mateka."
Kadhalika kabla Imam (a.s.) hajatoka kuelekea Iraq, alikutana na Mabwana Abu Muhammad Ar-Raaqdiy na Zurarah bin Khalaj, na walimjulisha udhaifu wa watu wa Al-Kufah, na kwamba nyoyo zao ziko pamoja naye na wakati huo huo panga zao ziko juu ya shingo yake.
Imam Husein (a.s.) alinyoosha mkono wake juu mbinguni, ikafunguliwa milango ya mbingu na wakateremka malaika wengi mno, idadi yao aijuaye ni Mwenyezi Mungu kisha akasema, "Lau isingekuwa vitu viko karibu karibu na kama muda wa kifo changu ungekuwa bado Wallahi ningepigana na maadui zangu kwa jeshi na Malaika hawa, lakini nafahamu wazi kabisa kwamba huko niendako ndiko kwenye kifo changu na vifo vya wafuasi wangu, hataokoka yeyote isipokuwa Mwanangu".(Ali bin Husein Zainul Abidin (a.s.).
Imam Husein (a.s.) akawa ameondoka Makkah siku ya Jumanne tarehe nane mfungo tatu mwaka wa sitini A.H.
Amesema Bwana Maamar katika kitabu kiitwacho "Maqtalul- Husein" kwamba: Ilipokuwa siku ya nane mfungo tatu, Omar bin Saad bin Abi Waqas alifika Makkah akiwa na idadi kubwa ya askari ili kumshambulia Imam Husein (a.s.) hapo Makkah kutokana na amri ya Yazid, na ikiwezekana amuuwe kabisa.
Kumbe Imam naye akawa ametoka siku hiyo hiyo ya tarehe nane mfungo tatu, kwani hakuweza kukamilisha Hija yake kwa kuchelea kuuwa kwake hapo Makkah na itakuwa heshima ya nyumba Tukufu ya Mwenyezi Mungu imevunjwa, akafungua Ihram yake na akaifanya kuwa ni Umra "Mufradah".
Imepokewa kutoka kwa Imam Jaafar as-Sadiq (a.s.) katika mapokezi ya Sheikh Mufid amesema, "Alipoondoka Imam Husein (a.s.) Makkah kwenda Iraq, alikutana na makundi ya malaika waliokuwa na mikuki wamepanda ngamia wakamtolea salamu na wakasema, "Ewe uliye mwongozo wa Mwenyezi Mungu kwa viumbe wake baada ya Babu yako na Baba yako na nduguyo, bila shaka Mwenyezi Mungu alimsaidia Babu yako kwa kututumia sisi mahala pengi, na hapana shaka Mwenyezi Mungu amekupa msaada wewe kwa kupitia kwetu."
Imam (a.s.) akawaambia, "Makutano yawe katika uwanja wa kaburi langu, mahali ambapo nitapata shahada (nitauwa) napo ni Karbala, basi nikishafika hapo njooni."
Wale Malaika wakamjibu wakasema, "Ewe uliye mwongozo utokao kwa Mwenyezi Mungu, hakika Mwenyezi Mungu ametuamuru kukusikiliza na kukutii, je, unayo khofu kutokana na adui kwamba atakutana nawe (njiani) ili tuwe nawe pamoja (tukusaidie)?"
Imam Husein (a.s.) akasema, "Hawana uwezo kama huo juu yangu, na wala hawatanifanya lolote la ubaya mpaka nifike kwenye kiwanja changu."
Pia walimjia Imam (a.s.) makundi ya majini waumini wakamwambia, "Ewe kiongozi wetu sisi ni wafuasi wako na ni wasaidizi wako, tuamuru chochote ukitakacho (tutakufanyia), na lau utatuamuru kumuuwa adui yako nawe ukiwa hapo ulipo tutakutelezea jambo hilo."
Imam Husein (a.s.) akawajibu akasema, "Je, hamjasoma kitabu cha Mwenyezi Mungu kilichoteremshwa kwa Babu yangu Mtume wa Allah pale aliposema Mwenyezi Mungu, "Waambie hata kama mngelikuwa majumbani mwenu, wangelitoka wale ambao wameandikiwa kufa wakaenda mahali pao pakuangukia kifo." (Qur'an 3:154)
"Kwa hiyo ikiwa mimi nitabaki hapa basi kwa kitu gani atatahiniwa mja huyu muovu, na ni kwa jambo lipi watu hawa (waovu) watajaribiwa, basi ni nani pia atakayeingia katika kaburi langu, kaburi ambalo Mwenyezi Mungu alinichagulia siku aliyoumba ardhi na akapafanya kuwa ni mategemeo ya wafuasi wetu na wanaotupenda, mahala hapo hupokelewa matendo yao na sala zao, na hukubaliwa maombi yao, na wafuasi wetu watakuja ishi hapo, basi watapata amani duniani na akhera, lakini pamoja na yote niliyosema njooni siku ya "Ashura" ambayo nitauawa mwishoni mwa siku hiyo, hatabakia baada yangu mwenye kutafutwa katika watu wangu na ukoo wangu na ndugu zangu na watu wa nyumba yangu, na watatekwa wapelekwe pamoja na kichwa changu kwa Yazid bin Mu'awiyah."