Majlisi Ya 10: Imam Husein (a.s.) Safarini Kwenda Iraq
Siku aliyotoka Imam Husein (a.s.) kuelekea Al-Kufah ndiyo siku ambayo Muslim bin Aqiil alikuwa yumo katika mapambano na askari wa ibn Ziyad, nayo ilikuwa ndiyo siku ya tarehe nane Dhil-Hija, na Muslim aliuawa siku ya nane tangu Imam Husein (a.s.) atoke Makkah, na siku hiyo ilikuwa ni siku ya "Arafah".
Kwa hiyo, siku ya kuondoka kwake Imam hapo Makkah, walikusanyika watu mbali mbali kutoka Hijaz na Basra wakaungana na watu wa nyumba ya Imam (a.s.) na wafuasi wake.
Wakati akitaka kwenda Iraq Imam Husein (a.s.) alitufu na kufanya Sa'ayi, kisha alifungua Ihram yake na akaifanya kuwa Umra Mufradah, ndipo alipoondoka na watu wake na wanawe pia watu ambao walioungana naye miongoni mwa wafuasi wake.
Imepokewa kutoka kwa Farzadaq amesema kwamba, "Nilikwenda Hija pamoja na Mama yangu mwaka wa sitini Hijriya, wakati nilipokuwa namuongoza ngamia wa mama kuingia Al-Haram nilikutana na Husein (a.s.) anatoka Makkah akiwa na panga na ngao zake nikasema, msafara huu ni wa nani? Pakasemwa kuwa ni wa Husein bin Ali (a.s.), basi nikamuendea na nikamsalimia kisha nikasema, "Mwenyezi Munga akupe maombi na matarajio yako katika mambo uyapendayo ewe mjukuu wa Mtume wa Mwenyezi Mungu, ni jambo gani likufanyalo uache Hija kwa haraka namna hiyo?"
Imam Husein (a.s.) akasema. "Lau sitafanya haraka nitakamatwa nikiwa hapa hapa, kwani wewe uniulizaye ni nani?"
Nikasema "Mimi ni mtu miongoni mwa Waarabu, basi Wallahi Husein (a.s.) hakunidadisi zaidi ya hivyo nilivyomwambia."
Kisha Imam Husein akasema kuniuliza "Hebu nifahamishe hali ya watu huko utokako?"
Nikasema "Hakika umemuuliza mtu anayefahamu hali halisi nayo ni kuwa, nyoyo za watu ziko nawe, panga zao ziko juu ya shingo yako na maamuzi yote yanashuka kutoka mbinguni."
Imam Husein akasema "Usemavyo ni kweli kabisa, mambo yote ataamua Mwenyezi Mungu, iwapo uamuzi wake utashuka kwa yale tuyapendayo basi tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa neema zake, naye ndiye mwenye kuombwa msaada ili kuitekeleza shukurani tunayo mshukuru, na ikiwa uamuzi wake utakuwa kinyume cha matarajio hatajitenga yeyote ambaye niya yake ilikuwa kutafuta haki, na ucha Mungu ndilo lengo lake."
Basi nikamwambia Imam Husein (a.s.), "Basi vema, namuomba Mwenyezi Mungu akutimizie yale uyapendayo na atakulinda kutokana na yale unayoyachelea, kisha nilimuuliza baadhi ya mambo ikiwa ni pamoja na nadhiri na ibada mbali mbali nikataka aniambie, Imam (a.s.) alimtikisa mnyama aliyekuwa kapanda (Ishara ya kuondoka) na akaniambia amani iwe juu yako na hapo tukaachana."
Wakati Imam Husein (a.s.) anaondoka, Yahya bin Said na kikundi cha watu waliokuwa wametumwa na Amri bin Said bin Al-aas (Gavana wa Yazid) walijaribu kumzuia Imam Husein (a.s.).
Imam alikataa katakata yeye na wafuasi wake, jambo ambalo lilipelekea kuzuka mashambulizi ya fimbo baina ya pande mbili hizi.
Basi Imam (a.s.) aliendelea na safari yake mpaka akafika mahali paitwapo Tan'im, hapa alikutana na msafara fulani unatoka Yemen akanunua kwa watu wa msafara huo ngamia kwa ajili ya matumizi ya safari yake na wafuasi wake. Naye Bwana Abdallah bin Jaafar aliwatuma wanawe wawili Aun na Muhammad wamfuate Imam Husein (a.s.), kisha akawapa na barua ambayo ndani yake alisema kama ifuatavyo:
Amma ba'ad, bila shaka mimi nakuomba kwa Jina la Mwenyezi Mungu (Basi kubali maombi yangu) utapoiona barua yangu usiende rudi, kwa hakika nakuhurumia kutokana na upande unaoelekea, kwani huenda huko kukawa kuna kifo chako na watu wa Nyumba yako kutawanyika ovyo. Na iwapo wewe utauawa leo hii, basi Nuru ya ulimwengu itakuwa imezimika kwani wewe ndiyo bendera ya wenye kuongoka na ndiyo matumaini ya Waumini.
Basi tafadhali usifanye haraka kwenda katika safari yako, bila shaka mimi nitakuja kukufuatia baada ya barua yangu hii.
Wasalaam.
Huyu Bwana Abdallah aliondoka mpaka kwa Amri bin Said (Gavana wa Makkah) akamuomba kwamba amuandikie Imam Husein (a.s.) maandishi ya kumpa hifadhi na amani ili arudi asiendelee na safari yake aliyokusudia.
Amri akamuandikia Imam Husein (a.s.) kama alivyoombwa, na akaituma barua hiyo kwa Imam Husein (a.s.), na ikapelekwa na Yahya ambaye ni ndugu wa Amri akiwa pamoja na Abdallah bin Jaafar, nao wakampa barua hiyo Imam Husein na wakajitahidi kumfanya arudi lakini akasema:
"Hakika mimi nimemuona Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) usingizini na ameniamuru kama hivi ambavyo ninafanya."
Abdallah alipokwisha kila namna kumrai Imam (a.s.) abadili msimamo, alikata tamaa na pale pale akawaamuru wanawe wafuatane na Imam Husein (a.s.) katika safari hiyo na wapigane upande wake itapobidi mapambano, naye Bwana Abdallah na Yahya wakarudi Makkah.
Imam Husein (a.s.) akaendelea na safari yake kwenda Iraq bila kupinda kushoto wala kulia mpaka akafika mahali paitwapo "Dhat-Irqi". Hapo alikutana na Bwana Bishri bin Ghalib akitokea Iraq, Imam akamuuliza hali ya watu ilivyo huko Bwana Bishri akasema "Huko nimeacha nyoyo za watu zikiwa pamoja nawe, na panga zao ziko pamoja na bani Umayya."
Imam (a.s.) akasema: "Amesema kweli ndugu wa Bani Asad, bila shaka Mwenyezi Mungu anafanya ayatakayo na anaamua mambo ayapendayo yawe."
Habari zilipomfikia Ibn Ziyad kwamba Husein anakuja (huko al-Kufah) kutoka Makkah, alimtuma kamanda wake aliyekuwa akiitwa Al-Hasin bin Numair akaja mpaka Qadisiyya na akalipanga jeshi lake kuanzia Qadisiyya mpaka Khifaan na pia kuanzia Qadisiyya hadi Al-Qatqataniyya.
Imam Husein (a.s.) alipofika katika kijia cha Batnu-Rumah, alimtuma Bwana Qais bin Mas-har As-Saidawiy, baadhi ya wanahistoria wanasema alimtuma ndugu wa kunyonya Abdallah bin Yaqtar, kwenda al-Kufah.
Wakati Imam anatuma ujumbe huo alikuwa bado hajafahamu yaliyompata Muslim bin Aqiil.
Katika ujumbe huo aliandika barua ifuatayo:
Bismillahi Rahman Rahim
Barua toka kwa Husein bin Ali, kwenda kwa nduguze Waumini wa Waislamu:
Amani ya Mwenyezi Mungu ikushukieni, bila shaka mimi ninaowajibu kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwenu nyinyi, Mwenyezi Mungu ambaye hapana Mola apasaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa yeye tu.
Amma ba'ad,
Hakika barua ya Muslim bin Aqiil imenifikia ikiwa na maelezo yanayoonyesha uzuri wa rai yenu, na kukubaliana kwenu juu ya kutusaidia na pia kuitetea haki yetu.
Basi mimi nimemuomba Mwenyezi Mungu ayafanye mema mambo yenu na akulipeni kwa yote ya wema mnayokusudia kututendea, wema ulio mkubwa kabisa. Kwa hakika mimi nimeondoka Makkah kuja huko siku ya Jumanne tarehe nane mfungo tatu.
Basi atapokufikieni mjumbe wangu mujizatiti katika maamuzi yenu bila shaka mimi nitafika hivi karibuni.
Wasalaam.
Kabla Muslim hajauawa kwa siku ishirini na saba, alikuwa kamuandikia barua Imam (a.s.).
Watu wa Al-Kufah nao walimuandikia Imam Husein (a.s.) katika kipindi hicho wakimjulisha kwamba, "Wapo wapiganaji laki moja hapa kwa ajili ya kukusaidia usichelewe kuja."
Qais bin Mas-har alielekea Al-Kufah akiwa na barua ya Imam Husein (a.s.) mpaka alipofika Al-Qadisiyya akakumbana na Al- Hasin bin Numeir (Askari wa Ibn Ziyad) akampokonya barua hiyo na akampeleka yeye pamoja na barua mpaka kwa Ibn Ziyad.
Alipofikishwa hapo, ibn Ziyad akamuamrisha Qais apande kwenye mimbar amtukane Husein na baba yake na nduguye. Qais akapanda juu ya mimbar kisha akamshukuru Mwenyezi Mungu na akamtukuza halafu akasema, "Enyi watu bila shaka huyu Husein bin Ali (a.s.) ni miongoni mwa viumbe vya Mwenyezi Mungu vilivyo bora mno, naye ni mwana wa Fatma binti ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.), nami ni Mjumbe wake amenituma kwenu, basi muitikieni, muungeni mkono."
Kisha Qais akamlaani Ibn Ziyad na Baba yake na akamuombea msamaha Ali bin Abi talib na akamtakia Rehma na Amani.
Kuona hivyo, ibn ziyad akaamuru Qais atupwe kutoka juu ya jumba la Ibn Ziyad, akakamatwa kisha akatupwa kama ilivyoamuriwa mpaka chini akakatika vipande vipande.
Baadhi ya wanahistoria wanasema alifungwa mikono kisha akarushwa kutoka juu na alipoanguka chini akawa bado hajafa, lakini mtu moja aitwaye Abdul-Malik bin Umair Al-Lakhmi akaja akammalizia kwa kumchinja.
Imam Husein (a.s.) aliendelea na safari yake kutoka hapo Batnu-Rumah kuelekea Al-Kufah mpaka alifika sehemu fulani iliyokuwa na maji, hapo akakutana na Bwana Abdallah bin Mutii al-Adawi.
Bwana huyu alipomuona Imam (a.s.) alisimama kisha akamwambia "Ewe mwana wa Mjumbe wa Mwenyezi Mungu ni jambo gani lililokuleta huku?" Imam Husein (a.s.) akasema, "Bila shaka habari za kifo cha Mu'awiyah zimekwisha kukufikia, basi kwa kifo hicho cha Mu'awiyah watu wa Iraq waliniandikia barua wakiniita niende kwao."
Ibn Mutii akasema "Nakukumbusha Mwenyezi Mungu Ewe mjukuu wa Mtume wa Mwenyezi Mungu, pia ikumbuke heshima ya Uislamu (uliyonayo) nachelea itavunjika (kwa safari yako hii)."
Aliendelea Ibn Mutii kumwambia Imam Husein (a.s.) "Wallahi iwapo utakitaka kilichomo mikononi mwa bani Umayya watakuua, na wakisha kukuuwa wewe hawatamuogopa yeyote baada yako, (kumfanyia uovu) Wallahi heshima ya Uislamu itaporomoka na heshima ya Maquraish na Waarabu kwa jumla, basi usiende huko Al-Kufah na wala usiitoe nafsi yako kuwapa Bani Umayya."
Imam Husein (a.s.) alikataa rai ya Bwana Mutii na akaamua kutimiza lengo lake tukufu katika kuunusuru Uislam.
Kwa upande wake ibn Ziyad alikuwa ameweka askari wake kuanzia Waqisa hadi kwenye njia iendayo Shamu na ile iendayo Basra, na akawamuru wasimruhusu yeyote kuingia wala kutoka.
Imam (a.s.) akaendelea na safari yake, njiani akakutana na mabedui akawauliza khabari za huko Iraq, wakamjibu, "Sisi hatuna tukijuacho lakini uwezekano wa mtu kuingia huko au kutoka hakuna."
Hata baada ya kufahamu hilo Imam (a.s.) hakukata tamaa bali aliendelea na safari kama alivyokusudia.
Kuna kikundi cha watu kutoka Fizarah na Bajiila walisimulia wakasema, "Wakati tulipokuwa tunatoka Makkah, msafara wetu ulikuwa jirani na msafara wa Husein (a.s.) na Zuhair bin al- Qain alikuwa nasi, lakini tulikuwa tunachukizwa mno kuweka kambi mahali alipoweka Husein (a.s.), cha ajabu ni kwamba kila Imam Husein alipoweka kituo kupumzika nasi tulijikuta tunalazimika kuweka kituo chetu tupumzike, ingawaje tulikuwa tukipumzika upande usiokuwa ule aliyoko Imam Husein (a.s.).
Jamaa wanaendelea kusimulia, "Basi kipindi fulani tulipokuwa tumepumzika tunakula chakula chetu ghafla alitufikia Mjumbe wa Imam Husein (a.s.) akatusalimia kisha akasema, "Ewe Zuhair hakika Abu Abdillah Husein (a.s.) amenituma kwako anakuita."
Baada ya maneno ya Mjumbe huyu kusemwa kila mmoja wetu alidondosha chakula alichokuwa nacho mkononi hata tukajikuta kama kwamba vichwani mwetu kumetuwa ndege (aliyesababisha mshituko)."
Mkewe Zuhair akamwambia Zuhair (akiitwa Dailam bint Omar) "Sub-hanallah. Mjukuu wa Mtume anakutumia ujumbe nawe hutaki kumuitika basi afadhali uende ukamsikilize maneno yake." (atakayo kukuambia)
Basi Zuhair akaondoka kwenda kwa Husein (a.s.), na wala hakukaa sana akarudi hali ya kuwa mwenye furaha na uso wake unapendeza, pale pale akaamuru hema lake likunjwe na mizigo yake akafunga akahamia kwa Imam Husein (a.s.).
Wakati akiondoka alimwambia mkewe 'Wewe sasa hivi umeachika hivyo basi rejea kwenu, hakika sipendi upate taabu kwa sababu yangu bali nakutakia kheri, na sasa nimeazimia kufuatana na Husein (a.s.) na roho yangu nitaitoa iwe ni fidia kwake na nitamlinda kwa nafsi yangu."
Kisha Zuhair akampa mkewe mali zake na akamkabidhi kwa baadhi ya watoto wa Ammi zake wamrejeshe kwao.
Yule mama alisimama kisha akalia na kumuaga mumewe akasema. "Mwenyezi Mungu amekugeuzia (mwelekeo) basi nakuomba unikumbuke mbele ya Babu yake Husein (a.s.) siku ya Qiyama."
Kisha Zuhair akawaambia jamaa zake, "Mwenye kupenda kunifuata miongoni mwenu anifuate, vinginevyo hapa ndiyo mwisho wa mahusiano kwangu mimi, lakini sina budi kuwasimulieni hadithi: Hakika tulipata kupigana vita iitwayo Al-Bahr, na Mwenyezi Mungu akatupa ushindi pia tulipata ngawira, Salman Al-Farisi akatuambia, je mmefurahi kwa ushindi aliokupeni Mwenyezi Mungu na ngawira mlizopata? Tukasema, "Ndiyo."
Salman akasema "Iwapo mtakutana na Bwana wa vijana wa kizazi cha Muhammad (s.a.w.), furahini mno kupigana mkiwa pamoja naye kutokana na haya mliyoyapata leo". Kisha Zuhair akaondoka na akafaulu kuwa miongoni mwa waliomsaidia Imam Husein (a.s.).
Wamesema Abdallah bin Suleiman na Mundhir bin Mash-al (Mabwana katika kabila la Asadi) "Tulipomaliza Hija yetu hatukuwa na jambo lolote la muhimu ila tulikusudia tumpate Imam Husein (a.s.) njiani ili tuone ni jambo gani litamtokea, basi tukaelekea aliko kwa haraka mpaka tukamkuta amefika Zuruud, na tulipomsogelea mara tukamuona mtu katika watu wanaotoka Al-Kufah amegeuza njia baada ya kumuona Husein (a.s.), naye Imam (a.s.) akasimama kama kwamba anataka kumfuata mtu yule, lakini akabadili nia na akamuacha aende zake naye akaendelea na safari yake."
Wale mabwana wanaendelea kusimulia wanasema, "Sisi tulipoona hivyo tukamfuata mtu yule mpaka tukampata tukamsalimia "Asalamu Alaika" akaitika "Wa-alaikumus-Salaam" tukamwambia: "Wewe ni nani?"
Akasema: "Mimi ni katika kabila la Asad."
Tukasema: "Nasi pia ni katika Asadi, basi jina lako nani?"
Akasema: "Mimi naitwa Bakri Bin fulan, kisha nasi tukamtajia nasaba zetu, kisha tukamwambia, "Hebu tupe khabari za watu walivyo huko utokako?"
Akasema: "Bila shaka sikutoka Al-Kufah mpaka alipokuwa Muslim bin Aqiil ameuawa yeye na Hani bin Ur-wah na nimewaona wawili hawa baada ya kuuawa wanakokotwa kwa miguu yao kuzungushwa sokoni" (waonekane kwa kila mtu).
Wale mabwana wanaendelea kueleza kisa chao wanasema, "(Tukamuacha mtu yule) na tukauelekea msafara wa Imam Husein (a.s.), tukaenda naye mpaka alipotua mahala paitwapo Tha-alabiya ikiwa ni jioni. Sisi tukamwendea hapo alipokuwa tukamsalimia naye akaitikia."
Tukamwambia "Tunamuomba Mwenyezi Mungu akupe Rehma, bila shaka sisi tunayo mazungumzo, iwapo utapenda tukuzungumzie wazi au kwa siri."
Imam (a.s.) akatutazama sisi kisha akawatazama watu wake akasema, "Hakuna siri kwa hawa waliopo hapa."
Basi tukamwambia "Je, ulimuona yule msafiri uliyepishana naye jana jioni?"
Akasema, "Ndiyo, na nilitaka kumuuliza khabari fulani."
Sisi tukamwambia Husein (a.s.) "Bila shaka Wallahi sisi tutakutosheleza habari zake, na tumemuuliza mambo yake kwa niyaba yako, na mtu huyo ni katika watu wa kabila letu kisha ni mwenye mawazo mazuri tena mkweli mwenye akili timamu."
Wakaendelea kusema, Na yeye amezungumza kwamba ametoka Al-Kufah baada ya kuuawa Muslim na Hani, na amewaona wakikokotwa kwa miguu yao wakipitishwa sokoni."
Imam Husein (a.s.) akasema, Inna lillahi wainna ilaihi Raajiu'n - bila shaka sisi ni milki ya Mwenyezi Mungu na hakika kwake tutarudi, Rehma za Mwenyezi Mungu ziwashukie Muslim na Hani, akarudia kusema hivyo mara nyingine."
Baada ya Imam (a.s.) kupata habari hizo alikaa akasubiri mpaka kulipokucha, akawaambia vijana wake ongezeni akiba ya maji nanyi mnywe vya kutosha munyanyuke tuendelee na safari.
Imam akaondoka kuendelea na safari, akaenda mpaka akafika mahali paitwapo "Zubalah", hapo zikamfikia habari za Abdallah bin Yaqtar na yote yaliyomfika, na ndipo alipotoa barua mbele za watu aliokuwa nao na akawasomea kama ifuatavyo:- "Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehma Mwenye Kurehemu, amma ba'ad, kwa yakini zimetufikia khabari za kusikitisha, kwamba Muslim bin Aqiil na Hani bin Urwah na Abdallah bin Yaqtar wameuawa, na wafuasi wetu huko Iraq wamtutupa mkono, hakuna watakalo tusaidia, basi yeyote miongoni mwenu apendaye kuondoka (kuachana nasi) basi na aondoke bila ya taabu na wala hatakuwa na lawama."
Basi baada ya tangazo hili, watu wengi wakamkimbia Imam Husein (a.s.) wakawa wanakimbia kuelekea kila upande, wengine kulia na wengine kushoto.
Ikawa hapakubaki ila watu wale wale aliondoka nao Madina na wachache katika watu waliomfuata baadae.
Imam alifanya hivyo kwa sababu alifahamu kwamba, Mabedui waliokuwa wamemfuata walifanya hivyo kwa kutaraji kwamba Nchi anayoelekea Imam ataikuta ikiwa na watu wanaomtii yeye Imam Husein (a.s.) ndiyo maana Imam (a.s.) akaona vibaya kwenda nao hivi bila kuwajulisha hali halisi bali akawatangazia bayana wafahamu ni kitu gani watakachokutana nacho.
Baada ya hapo Imam akasafiri hadi akapita sehemu iitwayo ‘Batnul-Uqbah’ na akatua hapo.
Mahali hapa alikutana na mzee mmoja katika Bani Ikrimah aitwaye Omar bin Luwadhan, na huyu mzee akamuuliza Imam: "Unakusudia kwenda wapi?"
Imam akasema: "Al-Kufah."
Yule mzee akasema "Nakunasihi tafadhali usiende, Wallahi huko hutakutana isipokuwa na mikuki na mapanga, na hawa waliokuita lau wangekuwa ni wenye kukusaidia kwa vita na wakakuandalia mapokezi mazuri, hapo ilikuwa na busara kwako wewe kwenda kwao, lakini kutokana na hali hii unayozungumza mimi naona si vema kwako kuenda."
Imam (a.s.) akamwambia yule mzee, "Ewe mtumwa wa Mwenyezi Mungu, kwangu mimi halijifichi lipi la kufanya na lipi la kuacha, lakini fahamu kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu anapoamua jambo hakuna wa kupinga."
Kisha Imam (a.s.) akasema, "Wallahi naapa kwamba, maadui zangu hawataniacha mpaka wahakikishe wanautoa uhai wangu, na wakisha fanya hivyo Mwenyezi Mungu atawapambanisha na watu watakaowanyanyasa mpaka wawe wao ndiyo viumbe dhalili mno katika makundi ya Umma" (Duniyani).