read

Majlisi Ya 11: Imam Husein (a.s.) Awasili Karbala

Imam Husein (a.s.) aliendelea na safari yake mpaka ikabaki kiasi cha safari ya siku moja kutoka Al-Kufah hadi hapo alipokuwa.

Mara ghafla alitokea Bwana Hurr bin Yazid akiwa na Askari elfu moja wenye farasi na Imam (a.s.) akamwambia Hurr, "Je hapa nitasalimika au tutaangamia."

Hurr akajibu "Lililopo hapa ni kuangamia tu ewe Abu Abdullahi."

Imam akisema: La haula wala Quwwata illa billahil aliyyil-adhiim." Kisha wakawa wanazungumza baina yao (Imam (a.s.) na Hurr) hatimaye Imam Husein (a.s.) akasema "Basi iwapo ninyi mmekuwa na mawazo tofauti na zile barua zilizonifikia, pia vile ambavyo wajumbe wenu mlivyowatuma kwangu, basi niacheni nirudi nilikotoka. "

Hurr na jamaa zake wakamzuia Imam kurudi Makkah, bali Hurr akamwambia Imam (a.s.) "Ewe mjukuu wa Mtume, pita njia nyingine yoyote ambayo haitakufikisha Al-Kufah wala Madina, ili nami nipate kisingizio cha kumwambia Ibn Ziyad kwamba wewe umenikwepa njiani."

Imam Husein (a.s.) akaelekea upande wa kushoto, na alipofika mahali paitwapo Udhaibul-Hajanaat, Ubaidullah bin Ziyad (Mwenyezi Mungu amlaani) akatuma barua kwa Hurr akamlaumu kutokana na tendo lake la kumuachia Imam Husein (a.s.) ashike njia nyingine na akamuamuru kuanzia hapo amsonge Imam Husein (a.s.).

Hurr na wale askari wake wakamfuata Imam na kumzuia.

Imam Husein (a.s.) akamwambia Hurr, "Je, siyo wewe uliyetuamrisha tubadilishe njia?"

Hurr akamjibu Imam (a.s.) akasema, "Hakika ni mimi, lakini imenifikia barua ya Amiri (Ibn Ziyad) ananiamrisha nikusonge nisikupe nafasi, na ameniwekea mtu wa kunipeleleza iwapo ninatekeleza jambo hilo au hapana."

Imam Husein (a.s.) akasimama kuwahutubia watu wake, akamshukuru Mwenyezi Mungu na kumsifu, kisha akamtaja Babu yake (Mtume Muhammad s.a.w.) na akamswaIia kisha akasema, "Bila shaka yamekwisha kutufika mambo ambayo mnayaona wazi wazi, na kwamba duniya imebadilika na imeyakataa na kuyapa mgongo mema yake, na imeimarika kutenda yasiyokuwa na busara, na hakuna kilichobakia katika dunia isipokuwa ni kama maji kidogo ndani ya chombo, na maisha duni mfano wa malisho yasiyofaa, je, hamuoni kwamba ukweli sasa hivi hautumiki na kwamba uovu haukemewi? Basi aliye Mu'umini na atarajie kukutana na Mola wake kwa kuuawa (na madhalimu) kwani mimi naona kifo (katika njia ya haki) ni mafanikio na kuishi pamoja na watu dhalimu ni unyonge."

Baada ya hotuba ya Imam (a.s.) alisimama Bwana Zuhair bin Al-Qain akasema, "Tumesikia usemi wako ewe mwana wa Mtume wa Mwenyezi Mungu, lau dunia ingekuwa ni yenye kudumu kwa ajili yetu nasi tukawa ni wenye kuishi humo milele, Wallahi tungethamini mno kupambana na udhalimu tukiwa pamoja nawe ili kuitetea haki."

Kisha alisimama Hilal bin Nafii Al-Bajali akasema, "Wallahi hatuchukii kufa ili tukutane na Mola wetu, nasi katika nia zetu na tunavyofahamu ni kwamba tutamtawalisha anayekutawalisha wewe na tutampinga anayekupinga."

Naye Burair bin Khudhair alisimama akasema, "Wallahi Ewe Mwana wa Mtume wa Mwenyezi Mungu, bila shaka Mwenyezi Mungu ametuneemesha kwa kupitia kwako pale alipo tujaalia kuwa tutauawa mbele yako na viungo vyetu vitakatwakatwa kwa ajili yako, kisha siku ya Qiyama Babu yako (Muhammad s.a.w.) atakuwa ndiyo muombezi wetu."

Baada ya hapo Imam Husein (a.s.) aliondoka kuendelea na safari yake, lakini ikawa kila alipotaka kuelekea upande fulani Hurr na askari wake humzuia na wakati mwingine humsonga wakawa ubavuni mwa msafara wake.

Kutokana na hali hiyo ya kusongwa na majeshi hayo, wanawake waliokuwa pamoja na Imam (a.s.) wakaingiwa na woga na watoto nao wakawa na khofu isiyokuwa na kipimo.
Hurr na askari wake walimsonga Imam (a.s.) mpaka wakamfikisha Karbala ikiwa ni tarehe mbili mfungo nne (Muharram). Walipofika hapo Imam Husein (a.s.) akauliza Jina la Ardhi hiyo na akaambiwa, "hapa ni Karbala."

Imam (a.s.) akasema, "Ewe Mola najilinda kwako kutokana na huzuni na tabu." (Karb-balaa).

Kisha akasema tena, hapa ndipo mahali penye huzuni na taabu, basi teremkeni kwa kuwa ndicho kituo cha msafara wetu, na ndipo mahali ambapo damu zetu zitamwagika, na ni sehemu itakayokuwa na makaburi yetu, mahali hapa alinisimulia Babu yangu Mjumbe wa Mwenyezi Mungu kwa yote niliyoyaeleza."

Watu wote waliokuwa na Imam Husein (a.s.) wakashuka kando ya Imam Husein (a.s.).

Imam Husein (a.s.) aliketi akawa anauandaa upanga wake huku akisema mashairi yaliyokuwa yanabashiri kifo chake.

Dada yake Imam (a.s.) aliyekuwa akiitwa Zainab aliposikia maneno ya nduguye akasema, "Ewe kaka yangu maneno haya usemayo ni ya mtu ambaye tayari amekwisha thibitisha kwamba atauawa."

Imam akasema "Hivi ndivyo ilivyo kwangu ewe dada yangu."

Bibi Zainab akasema: "Aa!!! hasara iliyoje. Husein (a.s.) anaomboleza mbele yangu kifo chake mwenyewe!!!"

Kilio cha bi Zainab na maneno aliyoyasema yaliwafanya wanawake wote walie na wakawa wanapiga nyuso zao na kukata mikufu yao. Naye Ummu Kul-thuum akawa anaomboleza kwa kusema "Ewe Muhammad wangu (s.a.w), ewe Ali wangu (a.s.), Ewe Mama yangu (Fatma a.s), Ewe ndugu yangu, Ewe Hasani wangu (a.s.), tumeangamia baada yako ewe Abaa-Abdillah."

Imam Husein (a.s.) aliposikia maombolezo ya Ummu Kul-thuum akamtaka awe na subira akamwambia, "Ewe dada yangu vumilia ufarijike kwa Mwenyezi Mungu, kwani viumbe vya mbinguni vitakufa, na viumbe wa ardhini nao watakufa, kadhalika viumbe wote watakufa."

Imepokewa katika mapokezi mengine kwamba Bibi Ummu Kul-thuum alipofahamu madhumuni ya beti za mashairi aliyokuwa akiyasoma Imam (a.s.) alitoka kwa uchungu mkubwa huku akikokota nguo zake mpaka akaenda kusimama mbele ya Imam Husein (a.s.) akasema, "Ooo!!! Hasara iliyoje laiti mauti yangenichukua (leo), kwani leo ni sawa na kifo cha mama yangu Fatma, na Baba yangu Ali na ndugu yangu Hasan (a.s.). Ewe uliyebaki baada ya hao waliokutangulia, wewe ulikuwa ndiyo nguzo ya sisi tuliobakia."

Imam Husein (a.s.) alimtazama dada yake kisha akasema, "Ewe dada yangu angalia shetani asije akauchukua uvumilivu na subira yako katika machungu yako kwangu."

Imam Husein (a.s.) akashikwa na huzuni kubwa machozi yakawa yanamlengalenga kisha akasema, "Sina njia ya kufanya kuepuka mauti."