read

Majlisi Ya 12: Mapambano Dhidi Ya Askari Wa Ibn Ziyad

Baada ya Imam Husein (a.s.) kuamua kutua hapo Karbala miongoni mwa wafuasi wake waliokuwa bora na wanao ambatana naye mara kwa mara ni Bwana Nafii bin Hilal Al-Jamali.

Bwana huyu alikuwa hodari sana wa kupanga mbinu za mapambano ya vita hasa kwa kutokana na ujuzi mkubwa aliokuwa nao kuhusu mambo ya kisiasa.

Basi siku moja Imam (a.s.) akatoka nje ya mahema mpaka akawa mbali, Nafii akamuona Imam naye mara akachukua upanga wake na haraka akamfuata Imam (a.s.).

Nafii akamuona Imam akiwa katika harakati za kufanya uchunguzi kwenye mipaka ya maeneo ya mahema ya watu wake, mara Imam (a.s.) akageuka na akamuona Nafii akasema, "Nani wewe Nafii?"

Nafii naye akasema, "Ndiyo ewe mwana wa Mtume wa Mwenyezi Mungu, mimi ni fidia kwako".

Imam (a.s.) akasema kumwambia Nafii, "Ewe Nafii, ni jambo gani lililokutoa katika usiku huu?"

Nafii akasema "Ewe Bwana wangu kumeniogopesha kutoka kwako usiku kuelekea upande wa hawa maadui".

Imam (a.s.) akasema, "Ewe Nafii nimetoka ili kufanya uchunguzi wa maeneo yetu kwani nachelea hali ya usalama wetu siku tutapopambana na maadui hawa".

Nafii anasema, "Kisha Imam hali ya kuwa amenishika mkono wangu kushoto huko akisema "Wallahi hii ni ahadi isiyovunjwa".

Baadaye Imam Husein (a.s.) akasema kumwambia Bwana Nafii, "Ewe Nafii, pita baina ya milima hii miwili (Ukimbie) uokoe nafsi yako?"

Nafii bil Hilal aliporomoka chini akaibusu miguu ya Imam (a.s.) akalia na huko anasema, "Ewe Bwana wangu, bila shaka upanga wangu thamani yake ni Dirham elfu moja, kadhalika farasi wangu naye hivyo hivyo, namuapa Mwenyezi Mungu ambaye amenineemesha kwa kuwa pamoja nawe mahali hapa ya kwamba, sitakuacha mimi ni mtumwa wa Mungu naye atanilinda kwa hali yeyote itakayotokea." Nafii anasema: "Kisha Imam (a.s.) aliniacha na akaingia kwenye hema la dada yake Zainab bint Ali (a.s.), nami nikasimama namsubiri.

Bibi Zainab akamkaribisha Imam (a.s.) na akampa kiti akakaa na akawa anazungumza naye mazungumzo ambayo sikuwa nasikia kinachozungumzwa.

Basi mara ghafla bibi Zainab alilia na akawa anasema "Bila shaka nitashuhudia kifo chako, na huu ni mtihani mkubwa hasa utakapokuwa umeniacha kuwaangalia wanawake hawa waliojaa hofu na woga."

"Ewe ndugu yangu, kama unvyofahamu uadui walionao watu hawa toka hapo zamani, kwa hivyo jambo hili ni zito sana kwangu mimi, vifo vya vijana wa Kibani-Hashim ni msiba mkubwa sana kwangu."

Kisha Bibi Zainab akasema, "Ewe mtoto wa Mama yangu, hivi wazifahamu nia na dhamira za wafuasi wako? Bila shaka mimi nachelea kwamba watakutelekeza wakati wa mapambano." Imam Husein (a.s.) akalia kisha akasema, "Wallahi nimewajaribu ili nipate kuwafahamu Imani na nia zao, sikuona miongoni mwao isipokuwa ni watu mashujaa tena hodari wanafurahia kifo kwa ajili yangu na kuliwazika kama anavyoliwazika mtoto mdogo anyonyapo maziwa ya mama yake."

Nafii akasema, Nikalia kwa kumuonea huruma bibi Zainab, kisha nikamuendea Habib bin Mudhahir na nikamuona amekaa ndani ya hema lake, mkononi mwake ameushika upanga ulionolewa barabara huku anasema kama mtu anayesemesha upanga wake. "Ewe dhoruba ya upanga, jiandae kujibu mashambulizi pindi mapambano yatakapoanza."

Nafii anaendelea kueleza anasema, "Nikamsalimia Habib na akaniitikia kisha akasema, ewe ndugu yangu ni jambo gani lililokutoa nje usiku huu?"

Basi nikamsimulia mwanzo wa kisa cha mimi kutoka nje mpaka mahali ilipofikia Imam Husein (a.s.) kusema kwamba wafuasi wangu wanafurahia kifo kwa ajili yangu na wanaliwazika kama ambavyo mtoto anavyoliwazika pindi anyonyapo ziwa la mama yake."

Baada ya kuambiwa maneno haya Habib alisimama kisha akasema "Aa!!! Wallahi kama isingekuwa kusubiri amri ya Imam (a.s.) katika kuwashambulia adui zetu mimi ningewaanza kuwashambulia usiku huu kwa upanga wangu huu na wala asingemudu yeyote mapambano dhidi yangu."

Kisha Nafii akamwambia Habib "Ewe ndugu yangu nimemuacha Husein (a.s.) akiwa na dada yake Zainab wakiwa na hali ya khofu, nadhani wanawake wengine nao watakuwa tayari wameungana na Bibi Zainab katika hali ya huzuni na majonzi, je, waweza kuwakusanya wenzio ili muende mukawatulize nyoyo zao kuwaondolea woga walio nao, kwani nimeshuhudia hali ambayo siamini kama (Husein a.s) atabakia duniani hapa."

Habib akasema, "Mimi ninatii nakukubali utakavyo."

Pale pale Habib akaanza kuwaita jamaa zake akasema, "Wako wapi watu wakumnusuru Mwenyezi Mungu, wako wapi watakaomsaidia Mtume wa Mwenyezi Mdngu (s.a.w), wako wapi wasaidizi wa Amiril-Muuminina Ali (a.s.), wako wapi watakaomsaidia Fatma (a.s.) wako wapi watetezi wa Husein (a.s.), wako wapi watakaounusuru Uislam?"

Wakachomoza kutoka katika mahema yao mfano wa simba wakali wenye kushambulia hali wakiongozwa na Abul-Fadhli Abbas (a.s.) (mdogo wake Imam Husein). Walipokwisha kusanyika Habib akawaambia bani Hashim, "Rudini mahala penu (katika mahema yenu) hakuna haja ya kukesha."

Kisha akawaambia jamaa zake, "Enyi watukufu na enyi Simba mashujaa, huyu hapa Nafii bin Hilal amenijulisha kitambo kidogo kilichopita (akasimulia mambo yote aliyoambiwa na Nafii kuhusu hali ya Imam (a.s.) na Bibi Zainab) kisha akasema, niambieni nanyi niya zenu na dhamiri zenu juu ya haya."

Basi wote wakasema: "Ewe mwana wa Mudhahir, Wallahi lau jamaa hawa watatushambulia, tutavikata vichwa vyao na tutawakutanisha na wazee wao nasi tutamlinda Mtume wa Mwenyezi Mungu katika kizazi chake na ukoo wake."

Habib akawaambia, "Nifuateni, nifuateni." Akasimama akaondoka na kuikanyaga ardhi kwa kishindo, nao wakawa wanarukaruka nyuma yake huko wanamfuata mpaka aliposimama kwenye vigingi vya kamba za mahema ya Imam Husein (a.s.) na watu wa nyumba yake kisha akasema: "Amani ikushukieni enyi mabwana viongozi wetu, Amani ikushukieni enyi kikundi cha Utukufu wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w) hizi hapa panga za vijana wenu, wameapa kwamba hawatazichomeka panga zao ispokuwa ndani ya shingo ya yeyote anayetaka kuwatendeeni uovu."

Akaendelea kusema: "Hii hapa mikuki ya vijana wenu, wameapa kuwa wataitwika vifua vya wale wanaotaka kutawanyisha umoja wenu."

Basi hapo Imam Husein (a.s.) akawatokea na kusema "Enyi wafuasi wangu, Mwenyezi Mungu akulipeni malipo mema kutokana na (kuwalinda) watu wa Nyumba ya Mtume wenu."

Imepokewa kutoka kwa Imam Jaafar as-Saadiq (a.s.) kwamba yeye amesema, "Nilimsikia Baba yangu akisema, pindi walipokutana Imam Husein (a.s.) na Umar bin Saad na kisha vita vikaanza kupiganwa, Mwenyezi Mungu alimteremshia msaada Imam Husein (a.s.) na akampa hiyari baina ya kuwa mshindi dhidi ya maadui zake au auawe katika vita hivyo kisha aende kwa Mola wake, Imam (a.s.) alichagua kufa na kukutana na Mwenyezi Mungu."

Baadaye katika kipindi hicho cha kuanza mapambano Imam Husein (a.s.) aliita kwa sauti akasema, "Je, kuna mwenye kutusaidia (katika vita hivi) kwa ajili ya kupata radhi za Mwenyezi Mungu?"

Basi mara baada ya wito huu Bwana Hurr bin Yazid ar-Riyahi akamwendea Omar bin Saad akamwambia, "Je, wewe unataka kupigana na mtu huyu?"

Omar bin Saad akasema "Ndiyo niko tayari kupigana naye kwani naapa kwa Mwenyezi Mungu kuwa wepesi na uzuri wa mapambano ni pale vichwa vinaporuka (vikikatwa) na mikono nayo inapokatwa."

Hurr bin Yazid ar-Riyahi akawa anaondoka huku anatetemeka kwa uchungu mkubwa.

Muhajir bin Ausi akamwambia Hurr "Wallahi msimamo wako unatia mashaka, na lau ningeulizwa ni nani shujaa mno miongoni mwa watu wa Al-Kufah, nisingekutaja wewe kutokana na hali niionayo kwako."

Hurr akajibu akasema, "Namuapa Mwenyezi Mungu, hakika mimi ninahiyarisha nafsi yangu baina ya kuingia peponi au motoni, basi sitachagua chochote kinyume cha pepo japokuwa nitauawa na kukatwakatwa kisha nichomwe moto."

Kisha palepale alimpiga farasi wake akaondoka kumfuata Imam Husein (a.s.) huku ameweka mkono wake kichwani akiwa anasema, "Ewe Mwenyezi Mungu nimerejea kwako basi nisamehe kwani nimekuwa nikizihofisha nyoyo za mawalii wako na watoto wa binti ya Mtume wako."

Kisha Hurr akamwambia Imam Husein (a.s.) "Mimi ndiye yule niliyekuzuia usirudi ulikotoka na nikakusonga mpaka kukufikisha hapa, kwa hakika sikutarajia kabisa kwamba hawa jamaa watakufanyia haya ninayoyaona sasa hivi, nami kwa yote haya natubia kwa Mwenyezi Mungu, basi je, unaona kuwa ninaweza kusamehewa?"

Imam Husein akamwambia Hurr, "Ndiyo Mwenyezi Mungu atakusamehe."

Kisha Bwana Hurr akasema kumwambia Imam Husein (a.s.) "Mimi nilikuwa mtu wa mwanzo kutoka dhidi yako, basi nakuomba uniruhusu niwe wa mwanzo kuuawa mbele yako ili niwe miongoni mwa watu watakaopeana mkono na Babu yako Muhammad (s.a.w.) kesho siku ya Qiyama."

Imam Husein (a.s.) akamruhusu Bwana Hurr, na mapambano yalipoanza, Hurr alipigana kwa ushujaa na uhodari mpaka akawauwa wengi wa waliokuwa mashujaa upande wa maadui kisha baadaye aliuawa na kufa shahidi.

Alibebwa na kupelekwa kwa Imam Husein (a.s.) naye Imam (a.s.) akawa anampangusa udongo uliokuwa usoni kwake huku akisema "Wewe ni Hurr kama alivyokuita mama yako, basi umekuwa Hurr duniani na Akhera."

Imam Jaafar anaendelea kutusimulia, "Baada ya Hurr kuuawa alitoka Bwana Burair bin Khudhair, na Bwana huyu alikuwa mcha Mungu sana.

Nao upande wa maadui wa Imam Husein (a.s.) alitoka Yazidi bin al-Maghfal ili apambane na Burair.

Kabla ya kupambana watu wawili hawa waliafikiana kufanya "Mubahala" maapizano kwa Mwenyezi Mungu kwamba aliye katika haki na ukweli amuuwe aliye katika uongo na upotofu.

Walipokabiliana kupambana Burair alimuua Yazid, na akaendelea kupigana na wengineo kisha hatimaye aliuawa "Rehema za Mwenyezi Mungu zimshukie."

Baada ya kuuawa kwa Burair Bwana Wahhab bin Hibab al-Kalbi naye aliingia katika uwanja wa mapambano na akapigana vyema kwa upanga na kuonyesha ushupavu katika Jihadi.

Bwana huyu alikuwa kafuatana na Mkewe pamoja na Mama yake katika safari hii ya kumuunga mkono Imam Husein (a.s.)

Ikawa kipindi fulani alirudi kwenye mahema na kumuambia mama yake, "Je, mama uko radhi nami au hapana?"

Mama yake akasema "Siwezi kuwa radhi mpaka nione unauawa mbele ya Husein (a.s.) kwa kumtetea yeye."

Ama mkewe Bwana Wahhab, yeye alisema "Naapa kwa Mwenyezi, nakuonya usije niachia majonzi iwapo utauawa."

Mama yake akasema: "Mwanangu yapuuze maneno ya mkeo rejea ukapigane kwa ajili ya mtoto wa Binti ya Mtume utapata maombezi ya babu yake siku ya Qiyama."

Bwana Wahhab akarudi na akaendelea kupigana mpaka mikono yake yote miwili ikakatwa.

Mkewe Bwana Wahhab alichukua mkongojo akawa anamfuata mumewe huku akimwambia "Endelea kupigana kuwatetea watu wema upate kuilinda heshima ya Mtume wa Mwenyezi Mungu."

Bwana Wahhab akamfuata ili amrejeshe mahali waliko wanawake lakini mkewe huyo akaishika sehemu ya nguo zake kisha akasema. "Sirudi mpaka nihakikishe nakufa pamoja nawe."

Imam Husein (a.s.) alipoiona hali hiyo akasema "Hakika mumekwisha kulipwa mema kutokana na kujitoa kwenu muhanga kwa ajili ya watu wa Nyumba ya Mutme (s.a.w), Ewe mama rudi."

Anaendelea kusimulia anasema: "Kisha alitoka Bwana Muslim bin Usajah, (Mwenyezi Mungu amrehemu bwana huyu) yeye alipigana na maadui, na alikuwa mvumilivu kutokana na ukali wa mapambano na shida alizokabiliana nazo mpaka ikafika kipindi fulani alidondoka chini akawa karibu kukata roho. Na ndipo Imam Husein (a.s.) akiwa pamoja na Bwana Habib bin Mudhahir akaenda hapo alipoanguka."

Imam Husein (a.s.) akamwambia "Mwenyezi Mungu akurehemu ewe Muslim, katika waumini kuna ambao wamekwisha kufa wakitetea dini ya Mwenyezi Mungu, na wapo wengine wanakisubiri kifo kwa ajili hiyo, na kamwe hawakubadilisha misimamo yao."

Naye Bwana Habib (r.a.) akamsogelea na akasema "Kifo chako kwangu mimi sijaona mfano wake Ewe Ndugu yangu Muslim, basi jibashirie kupata pepo."

Muslim akajibu kwa sauti ya unyonge (kwani alikuwa karibu kukata roho) akamwambia Habib, "Mwenyezi Mungu nawe akubashirie Pepo."

Kisha Habib akamwambia Muslim "Lau ningalifahamu ya kwamba mimi nitakufuatia, basi ningependa uniusie kila jambo ambalo limekufanya usitulie ila uamue kuingia katika mapambano."

Muslim akamwambia Habib, "Nakuusia juu ya huyu (akamuashiria Imam Husein a.s.) pigana kwa yake mpaka ufe."

Habib akamwambia Muslim "Basi nitakufurahisha kwa kutimiza wasia wako".

Mara Bwana Muslim akakata roho (Mwenyezi Mungu amuwie Radhi). Imam Jaafar anaendelea kusimulia anasema; "Swala ya Adhuhuri ilipofika Imam Husein (a.s.) alimuamuru Zuhair bin al-Qain na Said bin Abdallah al-Hanafi wasimame mbele yake, kisha Imam (a.s.) akawasalisha swala ya khofu watu waliobakia.

Ghafla ulitupwa mshale kumlenga Imam Husein (a.s.), Bwana Said bin Abdallah al-Hanafi akajitokeza kuuzuiya kwa kukinga mwili wake.

Mshale ule ulimpiga Bwana huyu na hakuwahi wala kupiga hatua moja bali alidondoka chini huku akisema, "Ewe Mwenyezi Mungu, walaani watu hawa kwa laana uliyowalaani watu wa Aad na Thamud."

Akaendelea kusema Bwana Said, "Ewe Mola mfikishie salamu zangu Mtume wako na umjulishe yaliyonipata kutokana na maumivu ya majeraha, kwani mimi ninataka thawabu zako katika kukitetea kizazi cha Mtume wako."

Kisha Bwana huyu alifariki na mwili wake ulikutwa ukiwa na majeraha kumi na tatu ya mishale na mapigo ya panga pia mikuki iliyotokana na mashambulizi yaliyoelekezwa kwake.

Naye Bwana Suwaid bin Amri bin Abil-Mutai alijitokeza kupambana na madhalimu wa jeshi la Yazidi.

Bwana huyu alikuwa mcha mungu mwingi wa kuswali. Alipambana kwa uhodari mfano wa simba aliye shujaa, na alivumilia ukali wa mapigano mpaka alipokuwa kishaenezwa majeraha mengi alidondoka chini.

Alibakia hapo chini mpaka alipowasikia wakisema; "Husein (a.s.) kauawa", alijikakamua na kutoa kisu kilichokuwa ndani ya soksi zake akaanza kupambana nao mpaka akauliwa.

Hapo ndipo wafuasi wa Imam Husein (a.s.) walipoanza kupambana kwa ukali huku wakimkinga na kumlinda Imam Husein (a. s).

Hali ya vita ilipokuwa imezidi ukali, na maadui wakawa wanamuandama Imam Husein (a.s.) kutaka kumuuwa, Abbas bin Ali bin Abi Talib (mdogo wake Imam Husein (a.s.) kwa mama mwingine) aliwataka maadui hao waahirishe vita mpaka kesho yake.

Imam Husein (a.s.) alitumia fursa hiyo kuwaamuru wafuasi wake wayasogeze mahema yao yawe karibu na kamba zake wazipishanishe kati ya hema na hema jingine.

Pia aliwataka wasimame mbele ya mahema yao na wakamkabili adui kwa mwelekeo mmoja na mahema yawe nyuma yao na mengine yawe kulia kwao na mengine kushoto kwao.

Usiku ulipoingia Imam Husein (a.s.) na wafuasi wake walikesha wanaswali na kuomba msamaha kwa Mwenyezi Mungu, pia waliomba maombi mbali mbali kwa unyenyekevu.

Kifupi walikesha wakiomboleza kwa maombi na sauti zao zilichanganyika na kusikia kama mvumo wa nyuki wengi.

Miongoni mwao walionekana wenye kusimama wengine wamerukuu na wengine wamekaa na wengine wamesujudu, almuradi kila mmoja kwa namna ya ibada yake. Katika usiku huo, askari thelathini na mbili wa ibn Ziyad waliwavamia Imam (a.s.) na watu wake. Askari hao walimsonga Imam Husein (a.s.) yeye na watu wake kwa kipindi kirefu.

Ilifika wakati ambao Imam (a.s.) na watu walishikwa na kiu kali ya maji, ndipo Imam (a.s.) alisimama akaegemea mpini wa upanga wake, akasema kwa sauti kubwa "Nakuapieni Mwenyezi Mungu, Je, ninyi munanifahamu mimi?"

Imam akasema: "Je, mnafahamu kwamba Babu yangu ni Mjumbe wa Mwenyezi Mungu?"

Wakajibu: "Ndiyo tunafahamu."

Akawaambia tena "Je, mnafahamu kwamba Baba yangu ni Ali bin Abi Talib?"

Wakajibu: "Bila shaka tunafahamu."

Imam akasema: Je, munajua kwamba nyanya yangu Khadija Binti Khuwailid ndiye mwanamke wa kwanza kusilimu?"

Wakasema: "Ndiyo tunajua."

Akawaambia tena, "Je, mnafahamu ya kuwa Jaafar At-Tayaar aliyeko Peponi ni Ami yangu?"

Wakajibu: "Hilo pia tunalifahamu."

Imam (a.s.) akawaambia: "Je, mnafahamu kwamba upanga huu ni upanga wa Mjumbe wa Mwenyezi Mungu na kwamba mimi nimeurithi?"

Wakajibu: "Hilo tunalijua."

Akasema tena: "Je, mnajua kuwa kilemba hiki ni cha mjumbe wa Mwenyezi Mungu nami nimekivaa? "

Wakasema: "Ndiyo pia tunafahamu."

Akasema tena Imamu (a.s.) "Je, mnafahamu kwamba Ali bin Abi Talib ndiye Muislamu wa kwanza na ndiye mjuzi kuliko wengine (baada ya Mtume s.a.w.) naye alikuwa mpole kuliko wote, na kwamba yeye ndiye Walii wa kila Mu’umini mwanamume na mwanamke?"

Wakasema: "Pia tunafahamu."

Kisha Imam Husein (a.s.) akawaambia, "Basi ni kwa nini mnataka kumwaga damu yangu wakati Baba yangu ndiye mlinzi wa haudhi, na Bendera Tukufu ya Mtume itakuwa mikononi mwake siku ya Qiyama?"

Wakasema: "Na hilo nalo twalifahamu."

Kisha wakamwambia Imam (a.s.) "Yote hayo uliyoyasema sisi tunayajua vizuri, lakini hatutakuacha mpaka uyaonje mauti hali yakuwa una kiu."

Baada ya hotuba hii ya Imam Husein (a.s.) na ikawa imesikilizwa na mabinti zake pamoja na dada yake Bi Zainab bint Ali, wote hawa walianza kulia na kuomboleza kwa sauti kubwa.

Basi Imam (a.s.) alipoiona hali hiyo, akamtuma nduguye Bwana Abbas na Mwanawe Bwana Ali bin Husein akawaambia: "Nendeni mukawanyamazishe watazidi kulia."

Mapambano baina ya Imam Husein (a.s.) na askari hao wa ibn Ziyad yalikuwa makali kiasi ilifikia Imam (a.s.) akabaki yeye na watu wa nyumbani mwake.

Wafuasi wa Imam Husein (a.s.) waliuawa wote asibakie hata mmoja. Ilipokuwa Imam kabaki peke yake na watu wa nyumbani mwake, alitoka Ali bin Husein (a.s.) akamuomba ruhusa Baba yake ili akapigane na hao maadui.

Imam Husein (a.s.) akampa ruhusa mwanawe, kisha akamtazama kwa jicho Ia huzuni na mara macho yake yakaanza kububujika machozi na akasema "Ewe Mwenyezi Mungu shuhudia, hakika amewatokea kupambana nao kijana ambaye kwa umbo na tabia amefanana mno na Mjumbe wako (Muhammad s.a.w.) nasi tulikuwa kila tukimkumbuka Mtume wako basi humtazama kijana huyu na hamu hutuishia."

Imam Husein (a.s.) alipaza sauti akasema kumwambia Ibn Saad, "Ewe mwana wa Saad Mwenyezi Mungu na aukate ukoo wako kama wewe unavyoikata nasaba yangu.

Basi Ali bin Husein (a.s.) akawaelekea hao maadui ili kupambana nao na akapigana nao vikali sana, akawauwa wengi katika wao.

Ali bin Husein (a.s.) akarudi hadi kwa Imam Husein (a.s.) akamwambia "Ewe Baba hakika kiu ndiyo itakayoniuwa, je, naweza kupata maji ya kunywa japo kidogo ili nipate nguvu ya kupambana na maadui hawa?"

Imam Husein (a.s.) akasema "Ewe Mwanangu nitapata wapi maji ya kukupa, nenda kapigane si muda mrefu utakutana na Babu yako Muhammad (s.a.w) atakunywesha kikombe cha maji ambacho kitakutosheleza kiu yako na hutahisi tena kiu."

Ali bin Husein (a.s.) akarejea kwenye uwanja wa mapambano na akapigana kwa nguvu sana lakini Munqidh bin Murata al-Abadi akamtupia mshale ambao ulimpata na akadondoka chini pale pale akapaza sauti akasema kumwambia Baba yake (Imam Husein a.s) "Ewe Baba pokea salamu toka kwangu, pia huyu hapa Babu yangu (Mtume Muhammad s.a.w) naye anakutolea salamu na anasema fanya haraka uje huko tuliko," kisha alivuta pumzi ndefu akafariki.

Imam Husein (a.s.) alikuja mpaka mahali alipofia mwanawe, akaweka shavu lake juu ya shavu la mwanawe akasema: "Mwenyezi Mungu awalaani watu waliokuuwa ewe mwanangu. Akaendelea kusema watu hawa: ni majasiri kiasi gani kuweza kuvunja heshima ya Mtume (s.a.w.)."

Baada ya hapo Bibi Zainab bint Ali alitoka akawa anaomboleza kwa kusema: "Ewe kipenzi changu, Ewe mwana wa Ndugu yangu."

Bibi Zainab alikwenda mpaka akaukumbatia mwili wa Ali bin Husein (a.s.), Imam Husein akamuondoa na kumrudisha waliko wanawake.

Baada ya kuuawa kwa Ali bin Husein (a.s.) ikawa sasa anatoka mtu baada ya mtu katika watu wa Nyumba ya Imam Husein (a.s.) mpaka idadi yao kubwa wakauawa.

Hali hiyo ilimfanya Imam Husein (a.s.) aseme kwa sauti ya juu "Fanyeni subira Enyi wana wa Ami zangu, vumilieni enyi watu wa Nyumba yangu, Wallahi hamtaona unyonge mwingine baada ya leo."

Baada ya hali hiyo yuko kijana mwingine katika watu wa Nyumba ya Imam (a.s.) alitoka ili akapigane na maadui hao.

Kijana huyu alikuwa na uso wenye kung'ara kama mwezi, na alipoingia katika mapigano alipigwa upanga wa kichani na mtu mmoja aliyekuwa akiitwa Ibn Fudhail al-Azdi upanga ule ukampasua na akadondoka chini na akaita "Ewe Ami yangu" (kumuita Imam Husein (a.s.).

Imam Husein (a.s.) alipoona kijana huyu naye ameuawa, alijiweka tayari kujibu shambulio hilo, na ndipo akampiga ibn Fudhail kwa dhoruba kali ya upanga. Bwana huyo alijaribu kuzuia kwa mkono wake lakini Imam (a.s.) akamkata katika fundo la mkono. Bwana huyu alipiga makelele kwa nguvu zote mpaka askari wa Yazid wote wakasikia na ikawafanya washituke ili kumuokoa, lakini kuja kwao kwa wingi na kwa hofu kulisababisha wakamkanyagakanyaga kwa miguu ya farasi mpaka akafa.

Kisha Imam Husein (a.s.) alisimama kichwani kwa yule kijana wake ambaye alikuwa karibu kukata roho, akasema "Walaaniwe watu waliokuuwa."

Kisha akasema tena kumwambia kijana wake, "Wallahi limekuwa ni jambo zito kwa ammi yako kumwita asikuitike au akuitike lakini asikusaidie kitu, Wallahi maadui zake ni wengi na ni wachache mno watu wa kumsaidia."

Imam Husein (a.s.) alimbeba kijana huyo (baada ya kufariki) akamuweka mahali walipokuwa maiti wengine katika watu wa nyumba yake.

Hali ya mauaji ya watu wa Imam Husein (a.s.) ilipofikia kuwa ya kutisha na kuhuzunisha aliazimia kupambana na maadui zake yeye mwenyewe binafsi.

Imam alianza kwa kutoa mwito akasema: "Je, kuna mtetezi atakayeitetea heshima ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w)?"

"Je, kuna mchamungu amuogopaye Mwenyezi Mungu kwa ajili yetu sisi? (Kizazi cha Mtume)."

"Je, yupo mwenye kutoa msaada hali ya kuwa anatarajia mema kwa Mwenyezi Mungu katika kutusaidia sisi?"

"Je, kuna mwenye kutunusuru ambaye anatarajia radhi ya Mwenyezi Mungu kwa kutunusuru sisi?"

Mwito huu wa Imam Husein (a.s.) uliwafanya wanawake waliokuwepo hapo walie kwa sauti na makelele mengi yakasikika.

Imam Husein (a.s.) akaenda mpaka kwenye mahema walikokuwa wanawake akamwambia Bibi Zainab binti Ali. "Hebu nipe huyo mwanangu mdogo nipate kumuaga."

Imam Husein (a.s.) akamchukua mtoto huyo akawa anataka kumbusu, lakini Hurmalah bin Kahil akamtupia mshale mtoto yule, ukampata shingoni akamuua.

Kuona hivi Imam Husein (a.s.) akamwambia Bibi Zainab mchukue mtoto huyu kisha yeye Imam akakinga viganja vyake, damu ya mwanaye ikawa inatiririka katika viganja.

Pindi viganja vyake vilipojaa damu, Imam aliirusha damu ile juu mbinguni kisha akasema "Si mazito kwangu mimi yaliyonipata kwa kuwa yote yanatendeka mbele ya macho ya Mwenyezi Mungu mtukufu."

Imam Al-Baqir (a.s.) amesema "Hakuna hata tone moja la damu lililodondoka chini pale Imam Husein (a.s.) alipoirusha mbinguni damu ya mwanawe."

Mpokezi wa habari hizi anasema, "Hali ilizidi kuwa ngumu kwa Imam Husein (a.s.) kiu kali ilimshika akapanda katika tuta la ukingo wa mto Furat kwa nia ya kwenda kuchota maji yeye pamoja na nduguye Bwana Abbas bin Ali (a.s.).

Lakini wanajeshi wa ibn Saad wakamzuia na mtu mmoja katika Bani Daarama akamtupia Imam Husein mshale ukamchoma Imam (a.s.) katika midomo yake mitukufu.

Imam (a.s.) akauchomoa mshale huo na akakinga viganja vyake chini ya midomo yake, damu ikiwa inatairirka ndani ya viganja, vilipojaa akairusha damu hiyo juu kisha akasema "Ewe Mwenyezi Mungu nakushitakia mambo anayofanyiwa mtoto wa Binti ya Mtume wako". Kisha maadui hao wakamzuia Abbas bin Ali (a.s.) na wakamzingira kila upande mpaka wakamuuwa.

"Imam Husein (a.s.) alilia sana kwa kuuawa Abbas (a.s.)."

Baada ya kuuwawa Abbas (a.s.) Imam Husein (a.s.) aliwaita watu hao wapambane naye mmoja mmoja.
Alipigana nao kwa njia hii ikawa kila aliyejitokeza Imam (a.s.) alimuuwa mtu huyo.

Imam Husein (a.s.) aliendelea kupambana nao mpaka walipomzunguka yeye pamoja na farasi wake akasema kwa sauti kubwa "Ole wenu enyi wafuasi wa kizazi cha Abu Sufiyan, ikiwa ninyi hamna Dini na hamuogopi (adhabu) mtakaporudi (kwa Mwenyezi Mungu) basi kuweni watu Huru katika dunia yenu hii, na tazameni utu wenu iwapo ni Waarabu kama mnavyodai."

Shimri alijibu kwa kusema: "Wasemaje Ewe mwana wa Fatima?"

Imam (a.s.) akasema: "Nasema kwamba, hakika mimi nakupigeni nyinyi nanyi mwanipiga mimi, lakini wanawake hawa hawana kosa lolote, basi hebu wazuiyeni watu wenu hawa waovu na wajinga, wasinivunjie heshima yangu muda wote nitapokuwa ni mzima."

Shimri akasema "Hilo ni jukumu lako Ewe Mwana wa Fatima". Basi wakamuelekea ili wamshambulie, ikawa huwashambulia nao humshambulia huku akitafuta maji azime kiu aliyokuwa nayo lakini hakupata.

Mashambulizi dhidi ya Imam Husein (a.s.) yalizidi mpaka akapatwa na majeraha sabini na mbili yaliyotokana na mishale.

Imam (a.s.) alichoka na ikambidi asimame ili apumzike hali ya kuwa mnyonge kutokana na mapambano.

Wakati akiwa amesimama lilitupwa jiwe ambalo lilimpiga usoni mwake.

Imam (a.s.) alichukua nguo yake akawa anapangusa damu inayotiririka usoni kutokana na jiwe lililompiga.

Basi ghafla ulimjia mshale wenye ncha tatu uliopakwa sumu ukamchoma moyoni, hapo Imam Husein (a.s.) akasema "Nakufa kwa Jina la Mwenyezi Mungu na kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na katika mila ya Mjumbe wa Mwenyezi Mungu."

Kisha alinyanyua kichwa chake juu akasema: "Ewe Mola wangu, wewe unafahamu kwamba, watu hawa wanamuuwa mtu ambaye ni mtoto wa Mtume hali ya kuwa hapana katika Dunia hii mtoto wa Mtume isipokuwa yeye."

Imam Husein (a.s.) akauchomoa ule mshale kupitia mgongoni, basi damu nyingi sana ikamtiririka mfano wa bomba linavyotoa maji. Hali hii ikamfanya Imam (a.s.) asiwe na nguvu kabisa ya kupigana bali akabaki amesimama.

Maadui wale wakawa kila ajaye kutaka kumshambulia Imam (a.s.) hukimbia na kurudi kwa kuchelea kwamba jukumu la kumuua Imam Husein (a.s.) lisijekuwa juu yake pindi atapokutana na Mwenyezi Mungu (s.w.t).

Baadaye mtu mmoja aitwaye Malik bin Nasir akamfuata Imam (a.s.) akamtukana na hatimaye akampiga upanga wa kichwani ukapasua kilemba alichokuwa kavaa nakumjeruhi kichwani.

Kilemba hicho kikajaa damu iliyokuwa inavuja.

Mpokezi wa habari hizi anaendelea kusema:

Imam (a.s.) aliomba kitambaa ili afunge kichwa chake, kisha akaomba tena apewe kofia, akapewa na akavaa halafu juu yake akafunga kilemba chake.

Jamaa hao walikaa muda fulani kisha wakamrudia tena Imam (a.s.) wakamzunguka kila upande.

Mambo yalipofikia katika hali hii, Abdallah bin Hasan bin Ali (a.s.) kijana ambaye alikuwa hata bado hajafikia umri wa miaka kumi na mitano alitoka mahali walikokuwa wanawake akaenda kusimama karibu na Imam Husein (a.s.).

Bibi Zainab binti Ali (a.s.) akamfuata kijana yule ili amzuie asiende alipo Imam kumuepusha asiuawe, lakini kijana huyo akakataa sana sana kurudi na akasema "Wallahi sitamuacha Ami Yangu" (peke yake).

Mara Bahri bin Kaab wanahistoria wengine wanasema Hurmalah bin Kahil akarusha upanga kumpiga Imam Husein (a.s.) yule kijana akasema "Ole wako Ewe mtoto wa Mwanamke muovu unataka kumuuwa ami Yangu?"

Kijana huyu alikinga mkono wake ili upanga ule usimpate Imam Husein (a.s.), lakini ukampata na kumkata mkono ukabakia unaning'inia kwa kushikiliwa na kipande cha ngozi kilichobaki.

Basi kijana huyu akapiga ukelele kutokana na maumivu akasema "Ewe Ami Yangu!!!" Imam Husein (a.s.) akamshika na kumkumbatia kisha akamwambia "Ewe mwana wa Ndugu yangu vumilia kutokana na yaliyokupata na ujihesabu kwamba umo katika wema, kwani Mwenyezi Mungu atakukutanisha na wazazi wako wema."

Mara ghafla, Hurmalah bin Kahil akamtupia mshale kijana huyu hali akiwa miguuni mwa Imam Husein (a.s.) akamuuwa.

Watu hawa waliendelea kumshambulia Imam (a.s.), kwa mishale toka kila upande akawa kama nungunungu majeraha mwili mzima, Salehe bin Wahab al-Mariy alimchoma Imam kwa mkuki kiunoni.

Basi Imam alidondoka kutoka juu ya farasi wake mpaka chini hali ya katanguliza upande wa kulia wa uso wake na akasema "(Nakufa) kwa Jina la Mwenyezi Mungu na kwa Ajili ya Mwenyezi Mungu na katika Mila ya Mjumbe wa Mwenyezi Mungu."

Bibi Zainab binti Ali alitoka kwenye hema huku analia na kusema, "Ooo!!! Masikini ndugu yangu, Ee!!! Kiongozi wangu, Ee!!! Wana hali gani watu wa Nyumba yako, laiti mbingu ingeliifunika ardhi na laiti milima nayo ingeporomoka"(yote haya ilikuwa ni maneno ya kuonyesha uchungu na huzuni kwa yaliyomfika nduguye).

Na hapa ndipo yalipotokea yaliyotokea ambayo siwezi kuyataja.