read

Utangulizi

Uislamu haukuwa mkusanyo wa mafundisho ya kanuni tu. Uliletwa ili uwe kitu cha kutumika kutatulia matatizo ambayo yanawatokea watu katika maisha yao ya kila siku. Uislamu hauweki mawazo ya kielimu tu ambayo hayana kiini cha maisha halisi, bali hutoa mifano bora ya maisha ya Uchamungu na maisha maizuri.

Ni kweli kwamba maisha ya Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) hayangeweza kuchukua hali zote zitokanazo na maisha ya binadamu. Kwa hilo baada ya yeye, walifuata makhalifa wake kumi na wawili ambao walikuwa mfano mzuri wa maisha ya Uchamungu, na kwa vile iliwabidi waishi katika hali za namna mbalimbali, walionyesha namna ya mtu awezavyo kuishi katika nyakati za amani au vita. Hapa tunaona kwa kifupi maelezo ya maisha ya Imamu Hasan Askari (a.s.), Khalifa wa kumi na moja wa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.).

Jina La Ukoo

Jina lake ni Hasan, 'Kunyat' (Jina la heshima) ni Abu Muhammad na kwa kuwa aliishi katika sehemu ya jiji la Samarrah iliyoitwa Askari, jina lake lililojulikana zaidi ni lile la Askari. Baba yake alikuwa Imamu Ali Naqi (a.s.) na mama yake ni Bibi Salil Khatun ambaye alikuwa mfano wa utawa wa hali ya juu, Uchamungu, Utakatifu na Ukarimu.

Kuzaliwa Kwake

Alizaliwa tarehe 10 ya Rabi-ul-Thani (Mfunguo Saba) mnamo mwaka 232 Hijiriya huko Madina.

Kulelewa Kwake

Alikaa na baba yake kwa muda usio pungua miaka kumi na moja katika sehemu ya kwao. Muda huu unaweza kuitwa muda wa amani. Baada ya hapo ilimbidi Imamu Ali Naqi (a.s.) aende Iraq na Imamu Hasan Askari (a.s.) alifika Samarrah na baba yake baada ya taabu zote za safari ndefu. Huko aliishi na baba yake jela chini ya uchunguzi na wakati mwingine aliishi katika uhuru kidogo. Lakini kila wakati aliishi na baba yake akijifunza kwa makini tabia yake katika hali za kila aina ambayo, pamoja na Mwanga alioupewa na Mwenyezi Mungu, alikuwa kamili kabisa kwa kazi ambazo alitazamiwa kuzishika.

Uimamu Wake

Mnamo mwaka wa 254 Hijiriya, Imamu Ali Naqi (a.s.) alifariki wakati Imamu Hasan (a.s.) akiwa na umri wa miaka 22. Miezi minne kabla hajafa, Imamu Ali Naqi (a.s.) aliutangaza Uimamu wa mwanawe na aliwaita wafuasi wake waje kushuhudia.