Kuteuliwa Kwa Wajumbe
Maimamu wa Ukoo wa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) wakati wote walifanya kazi zao wakiwa Maimamu katika hali zote. Imamu Hasan Askari (a.s.) alikuwa akiishi katika vizuizi vya namna nyingi sana kwamba ilikuwa vigumu kwa wenye kupenda kujifunza kutoka kwa Imamu kuweza kuonana naye. Hivyo Imamu aliwateua watu wenye kuaminika kutokana na uaminifu wao kuelewa kwao na elimu yao. Wajumbe hawa waliwaongoza watu kwa kadiri ya uwezo wao na kama palitokea tatizo lililokuwa zaidi ya uwezo wao basi walingojea mpaka wapate nafasi ya kumuona Imamu ili awape majibu na wao wawape watu. Mpango huu haukukataliwa sana na serikali kwa sababu ulihitaji mtu mmoja mmoja kwenda kumwona.
Wajumbe hawa walifanya kazi nyingine zaidi. Khums (moja ifananayo na Zaka) ilikuwa inatolewa na wale waliokiri kuwa Imamu alikuwa mwakilishi wa serikali ya Mwenyezi Mungu na kupewa hao wajumbe ambao waliitumia kama alivyoagiza Imamu. Watu hawa walipata jaribio gumu kweli, kwani wapelelezi wa serikali ya ukoo wa Bani Abbas walikuwa wakipeleleza shughuli zao. Hivyo Bwana Uthman bin Sa'id na mwanawe Abu Ja'afar Muhammad bin Uthman ambao walikuwa wajumbe mashuhuri wa Imamu walifungua duka kubwa la mafuta na manukato mjini Baghdad walikokuwa wakikaa ili kuepukana na kutiliwa wasiwasi na watu waliokwenda kumwona Imamu (a.s.). Kwa hiyo licha ya shari ya serikali, kazi ya Uislamu ilikuwa inaendelea.