read

Utangulizi

Kila siku binadamu anatafuta mwongozo. Kutafuta huku humfanya binadamu huyu aonane na binadamu wengine wengi, hivyo kwamba tunaweza kukulinganisha huku kujaribu kwake zaidi au kidogo na kuhangaika kwa mtu mwenye kiu katika jangwa lisilo na maji, ambaye anadanganywa na mazigazi, (sarabi) mia moja na moja.

Tunahitaji mtu asiyefanya dhambi na asiyekosea; mtu ambaye kwamba hata tukichungua kiasi gani utu wake, hatuwezi kuona hata dalili ya hitilafu katika mpango wake, ambao wingi wa tabia zake za maisha hufanya picha tukufu kwa ajili ya macho yetu kutazama na roho zetu kujipatia mwongozo mwema.

Mtu huyo ni lazima awe katika hali ambayo kila binadamu duniani kote aweze kupata mfano wa kufuata. Tunapolinganisha na kuamua ni yupi kati ya watu mashuhuri duniani, tunaona kwamba uwezo wa uongozi wao unafikia kiwango fulani tu cha kazi zao na nguvu zao za uongozi. Tunaweza tukamtaja Vikramaditya kama mfano wa mfalme mwadilifu lakini mfano wake ni kwa wafalme tu; au tunaweza kumtaja Asoka kama bingwa wa amani, walakini anashindwa kutupa matumaini tunapojaribu kumfikiria kama kiongozi mashuhuri wa nchi; na wote hawa wawili waliotajwa hapo juu wanashindwa kutupa mfano kwa raia. Au tunaweza kumtaja Mtakatifu Petro kama roho cha mungu, lakini atawezaje kutuongoza kama tukikabiliwa na machafuko ya kitaifa? Tunaweza pia kuwataja wapiganaji na watekaji mashuhuri lakini majina yao hayatakuwa na maana kwetu tukihitaji mfano wa mtu mwenye uvumilivu na uwezo wa kuvumilia taabu na mateso.

Kwa kifupi, tunaweza kupata watu walio nyota zitumulikazo kwa nuru ya sifa za utu moja au zaidi, lakini historia itashindwa kutuonyesha jina linaloweza kuwaongoza watu wote waishio katika mazingira ya namna mbali mbali isipokuwa Hadhrat Ali bin Abi Talib (Amani ya Mwenyezi Mungu na iwe juu yake) tu.

Hapa tunatoa kwa ufupi tu maisha ya ajabu ya mtu huyu wa ajabu mwenye uwezo wa kufahamu mambo mengi ambaye walimwengu wanapasika kumjua na kumpendelea.