read

Utangulizi

Umuhimu wa Hadith katika maadili ya mafunzo ya Kiislamu – ikiwemo Tafsir, Fiqh (Sharia), na maadili, n.k.- unakubalika katika madhehebu yote ya Kiislamu. Leo itakuwa ni vigumu kumpata mtu yeyote yule atakayekuwa akidai kuwa Qur’an Tukufu inajitosheleza kwa Shariah ya mafunzo ya Kiislamu pamoja na maelezo bila ya msaada wa Sunnah na Hadith.1 Zaidi ya hayo, yapo matamko mengi ya Mtume s.a.w.w., na baadhi ya taarifa katika Qur’an yenyewe, ambazo zinaelekeza katika umuhimu wa amri na matendo ya Mtume s.a.w.w.2 Kwa hivyo ni dhahiri umuhimu uliopo juu ya Hadith na Sunnah za Mtume s.a.w.w., hivyo hapana shaka wala haja ya ushahidi kwa swala hili.

Madhumuni ya makala yafuatayo ni kuchambua na kutazama vile mfumo wa Hadith ulivyokuja kuandikwa na kutazama muda uliotumika kukusanya matamko (kauli), matendo (fi’l) na kukubaliwa kwa ukimya (taqrir) wa Mtume s.a.w.w. hadi kufikia katika sura ya ukusanyaji na uandishi. Ni dhahiri, swala hili linaweza kuwa na umuhimu wa kuchambua ushahidi wa mfumo wa Hadith.
Ama kuhusu swala la Qur’an, sisi twajua kuwa hapakuwapo na pengo la muda baina ya kufunuliwa Ayah za Qur’an na kuandikwa kwao.3 Vivyo hivyo, hapana shaka juu ya usahihi wa Qur’an, kwani Mtume s.a.w.w. alikwishawachagua waandishi kuanzia mwanzoni mwa ufunuo na hapo walipatiwa kazi za kuzikusanya na kuziandika. Hata hivyo, utaratibu huu haukutumika katika swala la Hadith, ambavyo imekuja kupokelewa vinginevyo.

Umuhimu wa hadith na daraja lake katika maswala ya kijamii na kisiasa vimesababisha baadhi ya makundi kuonyesha hali ya kiasi fulani cha kutovumilia kuelekea hayo. Kutovumilia huku ndiko kuliko sababisha Hadith kucheleweshwa kusimuliwa na kuandikwa na kuenezwa. Na kwa masikitiko makubwa, kucheleweshwa huku kumeleta hali ya mtatanisho kwa ajili ya uthamini wake kwa vizazi vya baadaye.

Hata hivyo, ni lazima kutambulisha kuwa hali ya Hadith katika Shiah ilikuwa ni tofauti na ile hali ya Hadith katika Ahl al-Sunnah. Tofauti hii inatokana na imani ya Mashiah kuhusu Uimamu wa Shia wa Ahl al-Bayt a.s. ambapo kuwapo kwao ulikuwa ukiendelea hadi katikati ya karne ya 3 A.H. / 9 A.D. Kwa hivyo, Hadith zilizonakiliwa na Mashiah hazikukumbwa na matatizo ya kucheleweshwa kwa kuandikwa.

Hapa sisi tutatazama kwa kimukhtasari sana uthibitishaji kuhusu swala hili, lakini sehemu kubwa ya uchambuzi huu utakuwa ukihusiana na historia ya uandikaji wa Hadith miongoni mwa zile za Ahl as-Sunna.

Historia hii inaonyesha kuwa Hadith zilikuwa hazikuandikwa kwa kipindi fulani. Siyo hayo tu, hata kuzieneza kwao pia kulipigiwa marufuku kwa muda fulani, kwa kipindi cha miaka mia moja. Ahadith (wingi wa Hadith) zilienezwa kwa desturi ya matamshi tu. Ingawaje sehemu ya Hadith ilianza kuandikwa katika karne ya 2 A.H. / 9 A.D., sehemu yake kubwa iliandikwa tu baada ya muda wa kutosha kupita.

Hapa sisi tutatazama kwanza Maimamu a.s. wa Kishia wakisisitiza uandikaji wa Hadith. Na baadaye tutachukua historia ya uandikaji wa Hadith miongoni mwa Ahl al-Sunnah. Uchunguzi wa aina hii utatusaidia kama mwongozo kwa ajili ya kuthamini misingi halali ya Hadith ya Madhehebu zote za Islam na kutudhihirishia ipi iliyo na ufululizo wa uandikaji wa Hadith (bila ya kuvunjika kwa mfululizo huo) Umuhimu mkubwa wa uchunguzi huu ni uthamini kwa undani wa sanad na mutun (kiini) cha Hadith, jambo ambalo linalohitaji utafiti maalum ingawaje baadhi ya kazi kama hizi zimeshaandikwa juu ya somo hili, lakini bado kunahitajika juhudi zaidi katika uchunguzi kama huu.

Kwa kifupi, kitabu hiki ni mkusanyiko wa makala yaliyokuwa yakichapishwa katika jarida la Al-Tawhid J. V, II uk. 39-55; j. V, III & IV uk. 71-84 na VI, I uk. 19-35 – Sazmaan Tablighaat, Teheran Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Niliona kuwa itakuwa ni kazi yenye manufaa iwapo nitayakusanya hayo na kuyatarjumu katika lugha ya Kiswahili katika sura ya kitabu.

Amiraly M.H.Datoo
P.O.Box 838
Bukoba - Tanzania
7 Agosti 2000

  • 1. Ingawaje imeonekana kuwa baadhi ya wanazuoni wa Misri kwa mara nyingine wamesema kuwa kauli yao iwe ni sisi twategemea juu ya Kitabu cha Allah swt tu
  • 2. *Kwa mfano wa Ayah zifuatazo: (33:21); (33:26); (59:7).
  • 3. *Rejea kitabu kiitwacho Ukdhubat tahrif al-Qur’an bayna al-Shiah wa al-Sunnah, iliyoandikwa na Rasul Ja’aferiyan