read

Kutokubalika Kwa Hadith Za Abu Hurayrah

Kuhusiana na hayo, kuna Hadith kutoka kwa Abu Hurayrah ambayo pia imehusika. Abu Hurayrah asema:
"Mtume s.a.w.w. alitufikia wakati tulipokuwa tunaziandika Hadith. "Je, mwaandika nini?" Aliuliza Mtume s.a.w.w. mimi nilijibu: "Haya ni mambo ambayo sisi tumeyasikia kutoka kwako."

Mtume s.a.w.w. alisema: "Je, munataka kuandika kitabu mbali na Kitabu cha Allah swt? Hakuna kilichopotosha mataifa isipokuwa tu pale wameandika kitabu mbali na Kitabu cha Allah (Qur’an)." 1

Hadith hii pia haikubaliki kwa sababu zifuatazo:

Kwa sababu ya wengi waliokwisha kutoa sababu zao katika masomo yao na ambazo sisi pia tumeziona kuwa zinaweza kukubalika baada ya kuchunguzwa, hivyo usadikifu ('adalah) wa Abu Hurayrah hauwezi kukubaliwa. Vile vile inawezekana kuwa Hadith hii imezuliwa na wengine halafu wakaja kumtaja Abu Hurayrah kuwa ndiye aliyeiripoti.

Pili, mazungumzo yaliyomo ni sawa kabisa, kama vile yalivyokuwa yametolewa na Khalifa Umar wakati alipokuwa ameamua kuziandika Hadith na baadaye kughairi. Lakini Khalifa mwenyewe kamwe hakumsingizia Mtume s.a.w.w. Wakati ambapo Abu Hurayrah, au wale wote wengineo wakimsingizia Mtume s.a.w.w., hawakutupatia mwanya wa kubishana nao kwa madai yao (kwani madai yao ni kuwa Mtume s.a.w.w. tu ndiye aliyeyasema, hivyo hakuna ubishi juu ya kauli ya Mtume): Khalifa Umar kama vile tutakavyoona hapo mbeleni, alifikia maamuzi hayo baada ya kuzingatia mambo fulani fulani.

Tatu, mazungumzo yaliyomo na yanayonekana katika Hadith hii ingawaje inaonekana kuwa inayo mizizi katika kauli ya Mtume s.a.w.w. ambayo itazungumzwa hapo mbeleni, inazungumzia juu ya Mtume s.a.w.w.. kuharamisha vitabu vya Mayahudi na Wakristo, na wala si kuharamishwa Hadith za Mtume s.a.w.w. ambazo ni kitu kilicho kamili baada ya Qur’an.

Nne, je, inawezekana kwa Mtume s.a.w.w. kuharamisha kuandikwa kwa Sunnah, ambayo ndiyo inayofuatia baada ya Qur’an? Au aliharamisha kuwa hivyo isibakie sambamba na Qur’an? Je, ni nafasi ipi iliyo ya Sunnah ya Mtume s.a.w.w. isiokuwa ubavuni mwa Qur’an? Je, ni ukweli unaoweza kupingwa kuwa Qur’an na Sunnah ndivyo kwa pamoja vinafanya Shariah za Kiislam?

Ipo Hadith nyingine ivutiayo, ambayo inadhihirisha tabia ya udanganyifu wa Hadith kama hizo, nayo ni ile iliyonakiliwa na Abu Hurayrah. Baada ya kuelekezea kama taarifa tuliyonayo ipo, inaendelea kuongezea mambo mengi ambayo yanatudhihirishia upotofu katika upande wa Abu Hurayrah, au mzushi aliyezusha juu yake. Kwa mujibu wa Hadith hii, Mtume s.a.w.w. aliwasikia watu wameziandika Hadith zake. Papo hapo, alikwenda juu ya Mimbar na baada ya kumsifu Allah swt alisema:
"Ni aina gani ya vitabu hivi ambavyo nimesikia mmeviandika? Kwa hakika mimi ni mwanadamu tu. Yeyote aliyeandika chochote kile, basi ni lazima aniletee mimi." 2

Hadith hiyo kwa wazi wazi inakanusha Sunnah ya Mtume s.a.w.w. kwani Mtume s.a.w.w. yupo anakana uwezekano na uhalali wake wa Utume kwa kusema kuwa yeye alikuwa ni mtu kama watu wengine wa kawaida. Hili ni jambo ambalo mtu yeyote hawezi kulikubali kwani ni uzushi mtupu.

Jambo la kuvutia zaidi ni kuhusu kusema kwa Mtume s.a.w.w. hapa ('mimi ni mwanadamu') ipo imeelezwa katika Hadith nyingine kuwa hayo yalisemwa na kikundi cha watu wa Quraysh kuhusu Abdallah ibn Amr ibn al-Aas, ambaye alikuwa ameandika Hadith za Mtume s.a.w.w. Hapo Mtume s.a.w.w. hatilii maanani maoni yao kwa hakika yupo anayakanusha. Anasema:"Mimi hakuna nilisemalo isipokuwa ni haki tupu." 3

Tano, ipo imeripotiwa kutoka Abu Hurayrah mwenyewe kuwa hakuna mtu yoyote yule anayemzidi katika kunakili Hadith, isipokuwa Abdallah ibn Amr ibn al-Aas, kwa sababu huyu alikuwa akiziandika wakati ambapo Abu Hurayrah hakuwa akifanya hivyo. 4 Taarifa hii inaonyesha kutokuwapo kwa uharamisho. Abdallah aliziandika Hadith zote, ambapo zipo sababu za kibinafsi zilizomfanya Abu Hurayrah asiziandike. Hivyo, inatuonyesha wazi wazi kuwa hapakuwepo na amri yoyote yenye kuharamisha kuandikwa kwa Hadith za Mtume s.a.w.w.; wote waliotaka kuziandika waliziandika, na yeyote asiyetaka kuziandika hakuziandika lakini kwa sababu zao binafsi bila ya kuzuiwa.

Sita, katika ripoti nyingineyo Abu Nuhayk/Nahyak, mwanafunzi wa Abu Hurayrah, asema:

"Mimi nilikuwa nikiviazima vitabu kutoka kwa Abu Hurayrah, nilinakili, na kumchukulia (makala zangu) Abu Hurayrah na kumsomea. Kwa kila Hadith nilikuwa nikimwuliza iwapo amewahi kumsikia Mtume Mtukufu s.a.w.w. akiisema, naye alikuwa akiitikia." 5

Hadith hii pia inaonyesha uongo wa Hadith isemayo kuharamishwa uandishi wa Hadith, ambayo amesingiziwa Abu Hurayrah.

Imeripotiwa na Hamman ibn Munabbih, mwanafunzi wa Abu Hurayrah kuwa alikusanya Mus-haf iliyokuwa na Hadith zote zilizokuwa zimenakiliwa na mwalimu wao katika uhai wake. 6

Hayo pia yanatuonyesha kupingana na Hadith hiyo, kwani isingewezekana kwa Abu Hurayrah kunakili Hadith inayoharamisha uandishi wa Hadith wakati ambapo wanafunzi wake wameziandika Hadith mbele yake na katika uhai wake, au tuseme labda kuwa Abu Hurayrah hakutekeleza Hadith ipigayo marufuku uandishi wa Hadith kwa kunakili Hadith na kuzifundisha.

Vile vile ipo Hadith nyingineyo iliyoripotiwa na Zayd ibn Thabit kwamba siku moja alimwendea Muawiya, ambaye alimwuliza kuhusu Hadith fulani. Hapo Muawiya alimwambia mtu fulani kuiandika. Hapo Zayd alisema: "Mtume Mtukufu s.a.w.w. ametuambia tusiandike Hadith ya aina yoyote ile." 7

Sisi twaamini kwa uhakika uliowazi kuwa Hadith zilikuwa zimeandikwa na Tab'iun/Tabi'in na baadhi ya wanazuoni wa Sunni, wanathibitisha kutotegemewa kwa Hadith kama hizo. Hapo mbeleni katika kulichambua swala hili, sisi tutaona uthibitisho utakao onyesha sababu za kweli katika kuharamisha uandishi wa Hadith za Mtume Mtukufu s.a.w.w. Uhakika na uthibitisho huu unaonyesha kuwa sahihi kwa kumsingizia Mtume s.a.w.w. kwa taarifa kama hizo.

Pia imeripotiwa kuwa Ibn Mas'ud alielezea katika usia wake kuwa mkusanyo (sahifa) wa Hadith zilizofanywa naye, ziteketezwe. 8 Katika sura hii, haionyeshi wazi iwapo tendo hili lilikuwa limejibu amri ya Mtume Mtukufu s.a.w.w. Labda inawezekana, alikuwa akifuata amri ya Makhalifa. Pili, kama vile tutakavyo zungumza hapo mbeleni, tendo hilo linaelezea kuhusu kuteketeza riwaya na mapokezi ya Mayahudi (Israiliyyat) na wala si Hadith za Mtume s.a.w.w.

Vile vile imeripotiwa kuwa Abu Musa al-Ash'ari aliziteketeza Hadith zilizokuwa zimeandikwa na mtoto wake. Tukichukulia utiifu wa Abu Musa kwa Khalifa wa Pili, labda inaweza kusemwa kuwa tendo lake hili lilikuwa bila shaka chini ya ushahidi kuonyesha kuwa Abu Musa alitenda kwa kuvutiwa na uharamisho huo wa Mtume s.a.w.w. kuhusu Hadith.

Moja ya kitu kinacho onyesha kutokuwa halisi kwa mapokezi hayo yaliyozuliwa juu ya Mtume s.a.w.w. kuharamisha uandishi wa Hadith, ni kauli aliyoitoa Umar kuhusiana nalo kwa nia yake ya kutaka kukusanywa kwa Hadith za Mtume s.a.w.w. Umar anaripotiwa akiwa amesema: "Mimi nilinuia kuziandika Sunnah za Mtume s.a.w.w. Lakini lilikuja wazo akilini mwangu kuwa watu waliopita walikuwa wameandika baadhi ya vitabu na walikuwa wakivitegemea mno, hatimaye wao waliacha kukitegemea Kitabu cha Allah swt. Kwa kiapo cha Mungu, mimi sitakubaliana na chochote kile kitakachoweza kukifunika (kuachwa) Kitabu cha Allah (Qur’an)." 9

Katika riwaya ya hapo juu, inaonyesha kuwa Khalifa wa Pili alinuia kuandika Hadith hapo awali. Katika baadhi ya tafsiri ya riwaya hii inaelezea kuwa aliwashauri Sahaba wengine kuhusu swala hili nao pia walilikubalia (kuandika Sunnah za Mtume s.a.w.w.); lakini hapo baadaye yeye alilibadilisha shauri lake hilo kwa sababu zake alizozitaja, na wala si kwamba Mtume s.a.w.w. ndiye anayehusika katika kuharamisha.

Jambo lingine ambalo linaloweza kuonekana kama uthibitisho wa kukanusha uhalisi wa Hadith isemayo juu ya uharamisho wa kuandika Hadith, ni maneno aliyoyasema Mtume s.a.w.w. siku ya Alhamisi ya mwisho katika maisha yake (yaani kabla ya kufariki). Siku hiyo, walikusanyika Sahaba wote katika kitanda chake Mtume s.a.w.w. na hapo Mtume s.a.w.w. aliwaambia: "Nileteeni wino na karatasi ili niweze kuwa andikieni mambo fulani fulani ambayo hapo baadaye nyie mnapashwa kujitahadharisha msitumbukie katika makosa." Hapo baadhi ya watu wakiongozwa na Umar walipinga hayo wakisema "Kitabu cha Allah kinatosheleza kwetu sisi." 10

Riwaya hii inatuonyesha kuwa uandishi wowote mbali na Qur’an haukupigwa marufuku tu, bali hata ulichukuliwa na Mtume s.a.w.w. kuwa ni lazima ili kuokoa Ummah kuangukia makosa na upotofu. Wakati Mtume s.a.w.w. alipokuwa akiulizia vifaa vya kuandikia na kikundi cha Sahaba - kikiongozwa na Khalifa wa Pili kwa mujibu wa al-Shahristani katika al-Milal wa al-Nihal - walimpinga Mtume s.a.w.w., kwani Mtume s.a.w.w. alikuwa akielewa wazi maafa yatakayotokea hapo baadaye kutokea tukio au kisa hiki. Hapo mbeleni sisi tutachambua kwa undani zaidi yaliyokusanywa na kusemwa na wanazuoni wa Sunni kuhusu athari mbaya zilizotokana na kutoandikwa kwa Hadith lakini ni lazima tujiulize, "Je, ni sahihi kwa kumdhania Mtume s.a.w.w. katika kuharamisha kuziandika Hadith zake, jambo ambalo limeleta maovu makubwa katika utamaduni wa Kiislamu na kusababisha Sunnah za Mtume s.a.w.w. kuchezewa na Hadith hizo za kuzuliwa? Je, ni kweli kuwa Mtume s.a.w.w. ndiye anayehusika moja kwa moja katika upotofu huu na madhara yote yaliyotokea?"

  • 1. Taqyid al-ilm,uk.34.
  • 2. Taqyid al-iml,uk.34
  • 3. Taqyid al-ilm,uk.80
  • 4. Al-Kifayah fi`ilm al-riwayah,uk.82.
  • 5. Sharh Ma’anil athar,vol. 4, uk.320.
  • 6. `Ulum al-Hadith, uk.21,22.
  • 7. Taqyid al’ilm, uk.35; Umdat al-Qari, vol. 1,uk. 572; Musnad Ahmad, vol. 5,uk. 182.
  • 8. Taqyid al’ilm, uk.39; Sunan al-Darimi, vol. 1,uk. 124,125.
  • 9. Jami’bayan al’ilm, vol.1 uk.57,anaielezea riwaya hii kwa kupitia mfululizo wa wasimulizi (turuq);
    vile vile tazama Talkqyid al-’ilm, uk. 49,50,51.
  • 10. Musnad Ahmad ibn Hanbal, VI,451; All-Musannaf ya Abd al-Razzaq, V,438,439.