read

Hadith Za Mtume s.a.w.w. Katika Kuruhusu Uandishi Wa Hadith

Hadith zimepokelewa kutoka Mtume s.a.w.w. ambamo yeye ameruhusu uandishi wa Hadith kiujumla au kuruhusu kikundi fulani. Hadith hizi, zenyewe, zinatosheleza kukanusha Hadith zilizotangulia zinazozungumzia kuhusu kuharamishwa kwa uandishi wa Hadith, au tuseme haikosi, kuleta vurugu la riwayaat (wingi wa riwaya) katika hali yoyote, zinashindwa kubakia na uhai wao (hujjiyyah); kwani idadi ya Hadith hizi ni kubwa mno, na kwa kutilia maanani ya makanusho yaliyonayo dhidi ya Hadith zinazozua juu ya kutoandika Hadith, basi uhalisi wa Hadith kama hizi ni zenye kusadikiwa kabisa. Hadith hizi si kwamba zinazoruhusu kuandika Hadith bali pia zinatuamrisha kuziandika Hadith za Mtume s.a.w.w.

Hadith ifuatayo imenakiliwa kupitia mfululizo wa upokezi kuwa kulikuwapo na mtu aliyemlalamikia Mtume s.a.w.w. juu ya udhaifu wake wa kuhifadhi mambo katika akili yake. Mtume s.a.w.w. alimwambia: "Chukua msaada wa mkono wa kulia (i.e. kuandika) dhidi ya udhaifu wa hifadhi ya akili yako." 1
Mtume s.a.w.w. yupo anaripotiwa akisema:
"Ikamateni (hifadheni, iandikeni) elimu kwa njia ya kuandika." 2

Imeripotiwa kutoka Rafi' ibn Khadija kuwa yeye alisema: "Sisi tulimwuliza Mtume s.a.w.w. 'Je tunaweza kuandika baadhi ya mambo ambayo twayasikia kwako?' Mtume s.a.w.w. alijibu, 'Andika hayo na wala hakuna madhara ndani yake.' 3
Imeripotiwa kwa mamlaka ya Amr ibn Shu'ayb kuwa baba yake alimwuliza Mtume s.a.w.w.: "Sisi tukisikia mambo kutoka kwako ambayo hatuwezi kuhifadhi akilini mwetu kwa kipindi kirefu, je, tunaruhusiwa kuyaandika?" Hapa Mtume s.a.w.w. alijibu: Naam, muyaandike." 4

Imeripotiwa kupitia mifululizo ya wanaonakili, kutoka Abdallah ibn Amr ibn Al-Aas kwa kusema: "Mimi nilimwuliza Mtume s.a.w.w.: 'Je, tunaweza kuandika kile tukisikiacho kutoka kwako? Mtume s.a.w.w. alijibu, 'Naam.' Mimi niliulizia. 'Bila ya kujali wewe ukiwa umeghadhabika au mpole? Mtume s.a.w.w. alijibu, "Naam, mimi sizungumzi chochote kile isipokuwa haki tupu, hata kama nikiwa nimeghadhabika au nikiwa nimefurahishwa." 5

Katika Hadith nyingine, msimulizi anaripotiwa kwa kumwuliza Mtume s.a.w.w. "Je, twaweza 'kuikamata' elimu?" Mtume s.a.w.w. alijibu: "Naam." 6

Huyo huyo Abd Allah ibn Amr anaripotiwa kuwa,"Nilikuwa nimezoea kuandika chochote kile nilichokisikia kutoka kwa Mtume s.a.w.w. kwa ajili ya kurekodi. Baadaye Ma- Qureyshi walinizuia kufanya hivyo, na mimi pia niliachilia kuandika. Baadaye, mimi nilimwelezea Mtume s.a.w.w. swala hilo. Naye alisema, "kwa kiapo cha Mungu ambaye anayamiliki maisha yangu, mimi kamwe sitamki chochote kile isipokuwa haki tupu." 7

Imeripotiwa na Amir al-Mu’miniin Ali ibn Abi Talib a.s. kuwa Mtume s.a.w.w. alisema: "Andikeni elimu (ilim) kwani mutafaidi nacho humu duniani na akhera vile vile. Eleweni kuwa elimu haikubali mmiliki wake ateketee."8

Hadith nyingine mashuhuri ya Ma-Imam wa Ahl al-Bayt a.s. ambayo imesimuliwa na chanzo cha Sunni na Shia, inaelezea maandiko (sahifah) juu ya upanga wa Mtume s.a.w.w. Al-Imam al-Sadiq a.s. anaripotiwa akiwa amesema:

"Kulikuwapo na Sahifah katika mpini wa upanga wa Mtume s.a.w.w. yakisomwa: "Amelaaniwa yule anayeiba mipaka ya ardhi. Amelaaniwa yule ajifanyiaye marafiki mbali na mawali wake." Au alisema, "amelaaniwa yule ambaye anakana neema za Mola wake aliyempatia." 9

Abu Hurayrah anaripotiwa akisema: "Hakuna yoyote yule anayeweza kuelewa zaidi yangu kuhusu Hadith za Mtume s.a.w.w. isipokuwa Abdallah ibn Amr, kwa sababu yeye alikuwa akiyaandika kwa mkono wake, na kuhifadhi akilini mwake, ambapo mimi nilikuwa nikiyahifadhi tu bila ya kuyaandika. Naye huyo alikuwa amepatiwa idhini na Mtume s.a.w.w. kwa ajili ya kuziandika Hadith zake."10 Abdallah ibn Amr anaripotiwa kwa kusema: "Mimi nataka kusimulia Hadith zako na iwapo wewe utaniruhusu mimi nitaweza kuutumikisha mkono wangu (i.e. katika kuandika) ili kuusaidia moyo wangu (i.e. kuhifadhi). Na Mtume s.a.w.w. alisema, 'iwapo ni Hadith zangu, basi lazima uchukue msaada wa mkono wako.'''11 Yeye pia anaripotiwa kuwa na sahifah ambayo ilijulikana vyema kama al-Sahifat al-Sadiqah,12 ingawaje wengine wanakana kama ilikuwa na Hadith za Mtume s.a.w.w.13 Al-Mughirah ibn Shu'bah anaripotiwa kwa kuthibitisha kuwa Abdallah ibn Amr alikuwa na Sahifah iliyoitwa al-Sahifah al-Sadiqah.

Katika Hadith nyingine, Mtume s.a.w.w. anaripotiwa akisema: "Wakati mu’min anapokufa, karatasi alimoandika elimu (ilim) itabakia daima na itakuwa ni pazia baina yake na moto wa Jahannam Siku ya Qiyama." 14

Al-Tirmidhi ameripoti kuwa Sa'id ibn Ubadah alikuwa na sahifah ambamo alikusanya idadi kubwa ya Hadith za Mtume s.a.w.w.15 Mtoto wake pia alikuwa anayo mazoea ya kunukuu Hadith kutoka sahifah hiyo. Kwa mujibu wa riwayah za al-Bukhari, ilikuwa ni nakili ya sahifah ya Abdallah ibn Awfi ambaye alizoea kuandika Hadith ndani mwake kwa mikono yake mwenyewe. 16

Samurah ibn Jundab pia alikusanya Hadith nyingi katika kitabu chake kikubwa na mtoto wake, Sulayman, aliyerithi, alizoea kunakili Hadith kutokea humo. Bila shaka yalikuwa ni maandiko haya ambayo Ibn Sirin anayasemea: "Katika risalah aliyoiacha Samurah kwa mtoto wake, humo kuna kiwango kikubwa mno cha ilimu. 17

Imeripotiwa na Anas akisema huku amenyooshea mkono kwa Mus-haf: "Hizi ni Hadith ambazo mimi nimezisikia kutoka kwa Mtume Mtukufu s.a.w.w. Mimi niliziandika na nilimpatia Mtume s.a.w.w. (kwa ajili ya uthibitisho wake)." 18

Al-Imam Ja’far al-Sadiq a.s. anasimulia kutokea Mababu zake a.s. kwamba Mtume s.a.w.w. alisema: "Wakati unapoandika Hadith, andika pamoja na sanad yake (ufululizo wa upokezi wake). Iwapo itakuwa ni kweli, basi utagawana thawabu zake; na iwapo zitatokezea kuwa ni za uongo, basi madhambi yake yatamwia aliyesema." 19

Mtume s.a.w.w. pia anaripotiwa kwa kusema: "Ikamateni elimu." Na alipoulizwa ni nini alichokuwa akimaanisha, alielezea kuwa yeye alikuwa akimaanisha uandishi. 20

Umm Salma r.a. ameripotiwa akiwa amesema: "Mtume s.a.w.w. aliulizia adim ya kondoo iliyotiwa dawa ili isioze iletwe mbele yake. Imam Ali ibn Abi Talib a.s. alikuwa pamoja naye. Baadaye aliyazungumza mambo mengi mno kwa Imam Ali ibn Abi Talib a.s. hadi kukaandikwa sehemu zote mbili za ngozi hiyo na vile vile kingo zake pia zilijaa maandishi."21

Hadith zote hizi zinathibitisha wazi kuwa Mtume s.a.w.w. aliruhusu uandishi wa Hadith. Wapo Wanazuoni wengi ambao wanashikilia kwamba Mtume s.a.w.w. alikuwa ameharamisha hapo mwanzoni na kuruhusu hapo baadaye. 22 Iwapo ndiyo hali ilivyo, je, ilikuwa ni kwa misingi gani ambapo baadhi ya Makhalifa waliharamisha uandishi wake na baada ya Hadith nyingi mno kuandikwa, tukamsingizia ati kuwa ni Mtume s.a.w.w. ndiye aliyeharamisha uandishi wa Hadith?

Rashid Ridha amezichambua Hadith zinazoharamisha na zenye kuruhusu kuandika Hadith.Yeye anajaribu kuthibitisha kuwa Hadith zinazopiga marufuku zinashinda zile zenye kuruhusu, hivyo Hadith zinazoelezea kuharamishwa kwa kuandika Hadith ni lazima zichukuliwe kuwa ni halisi na kweli. Yeye anaandika:

"Iwapo tutachukulia kuwapo kwa mgogoro baina ya Hadith zenye kupiga marufuku na zile zenye kuruhusu, basi mtu anaweza kusema kuwa mojawapo baina yao imetengua (batilisha) nyengine kwa kuthibitisha kuwa Hadith zinazoharamisha zinashinda zile zenye kuruhusu, kwa sababu mbili: Kwanza, Sahaba walisimulia Hadith zinazoharamisha hata baada ya Mtume s.a.w.w. Pili, Sahaba hawakuziandika Hadith; kwani iwapo wao wangalikuwa wameziandika, basi zingalikuwa zimetufikia sisi." 23

Sisi hatuwezi kukubaliana na maelezo hayo kwa sababu zifuatazo:
Kwanza, Sahaba ndio waliosimulia Hadith zenye kuruhusu uandikaji wa Hadith pamoja na zile zinazoharamisha, na kama vile tulivyokwisha ona hapo juu, baadhi ya Sahaba waliendelea na kuziandika hizo Hadith.

Pili, sababu ya Sahaba kutojishughulisha na ukusanyaji wa Hadith kulitokana na kutolewa kwa amri ya kuharamishwa na Makhalifa wa kwanza na pili, na wala si kuwa ni Mtume s.a.w.w. aliyeharamisha.

Tatu, kwa kuwa haiwezekani sisi tukadai kuwa aina moja ya Hadith hizi zinashinda aina ya pili yake, sisi twaweza kusema kuwa ugomvi wao unazifanya zote ziwe zimebatilika na wala si kwamba mojawapo inaishinda ya pili yake.

Kuhusiana na kukubali kwa Abu Hurayrah kuwa Abdallah ibn Amr alizoea kuandika Hadith, Rashid Ridha anasema: "Hakuna sababu ya kwamba sisi tuchukulie hivyo kama uthibitisho wa ruhusa ya kuandika Hadith, kwa sababu haijaelezwa katika Hadith kuwa Abdallah aliandika Hadith kwa kuruhusiwa na Mtume s.a.w.w. 24

Sisi tulikwishawaonyesha hapo juu riwaya zinazoonyesha kuwa Abdallah ibn Amr kwa hakika alikuwa amepatiwa ruhusa kama hiyo. Zipo riwayat nyingi ambazo zimeshuhudia hayo, na mojawapo hapo juu Abu Hurayrah kwa kusisitiza anasema kuwa Abdallah ibn Amr alikuwa amepatiwa ruhusa na Mtume s.a.w.w. kama hiyo.

Ama kwa upande wa upinzani, wengineo, kama Abu Zuhrah, wenye mawazo ya kusema kuwa Mtume s.a.w.w. aliruhusu uandishi wa Hadith kufikia mwishoni mwa Utume wake ambapo hapakuwapo na hatari ya kuzichanganya Hadith pamoja na Aya za Qur’an. 25 Iwapo sisi tutachukulia kusema kuwa matendo ya baadhi ya Sahaba, hasa yale ya Makhalifa, sisi hatuwezi kuikubalia hivyo, ama kwa upande wa pili, iwapo tutakubalia, basi itatubidi kuwalaumu baadhi ya Makhalifa kwa mienendo yao. Sisi hatujui iwapo Bwana Abu Zuhrah ataupendelea uelekeo upi.

  • 1. Bihar al-Anwar,II: 152;Taqyid al-ilm,68; Mizan al-’i’tidal, 1,653; Lisan al-Mizan,II,298,IV,21.
  • 2. Musnad Ahmad, 1,238; JamI’bayan al-’ilm, 1,84; Fath al-Bari, i,84;Taqyid al-’i’ilm,86.
  • 3. Al’Idq al-farid,II,419; al-Bayan wa al-tabyin, II,38;Taqyid al-’ilm 68-70; Sunan al-Darimi, I,127; Husn al-tanbih,194; Jami’bayan al-’ilm,172; Kanz al--’ummal, V.224; Abu Nu’aym aliyeandika Akhbar Isfahan. II.228.
  • 4. Majma’ al-Zwayid, I,151; Kana ala-Ummal, V.225; Taqyid al’ilm 72-74; al-Manar,1,763; al-Taratib al-’idariyyah,II,245.
  • 5. Taqyid al-Ilm,74,79;Musnad Ahmad,215;Bihar al-anwar,II,147; Jamia’bayan al-ilm 1,85.
  • 6. Taqyid al-’ilm,1, 85.
  • 7. Taqyid al-’ilm, 1,74,75, 85; Fath al-Bari, 1,184; Tadhrib al-rawi, II, 66
  • 8. Musnad Ahmad,II,162,192; Jami’bayan al-’ilm, 1,85.
  • 9. Kanz al - ‘ummal, X, 157
  • 10. Jami ‘bayan al- ‘ilm 1, 85 vile vile tazama Fath al-1,182,199, 203, 246,247; Taqyid al-
    ‘ilm,88,89;al-Bukhari’s al-mufrad,129; Musnad Ahmad, 1,100.
  • 11. Al-Taratib al- ‘idariyyah, II ,24, akinakili kutoka al-Tabaqat al-kubra, Musnad Ahmad and Sunan al-Tirmidhi; tazama al-Musannaf, XI, 254; Sahih al-Bukhari, I, 148; Jami’ bayan al-‘ilm, I, 84;
    Sharh Ma’nil a‘thar, IV, 318-320; Tadhkirat al-huffadh,I, 42; Tadrib al-rawi, II, 66.
  • 12. Sunan al Darimi,I, 126; Tadrib al-rawi, II, 66.
  • 13. Al- Taratib al-idariyyah , II, 245; Tabaqat al-Kubra ,VII, 494, IV, 262; Taqyid al-'ilm , 84; Ta’wil mukhtalif al-hadith, 93; al-Ma’arif ya Ibn Qutaybah, 200.
  • 14. Hashim Ma’ruf al-Hasani, Dirasat fi al-hadith wa al-muhaddithin.
  • 15. Bihar al-Anwaar , II, 144
  • 16. Sunan al-Tirmidhi , kitab al-ahkam, bab al-yamin ma’a al-shahid.
  • 17. Al-Sayr al hadith fi tarikh tadhwin al-hadith,uk 9; ‘Úlum al-hadith, 13.
  • 18. Tahdhib al-Tahdhib , IV, 235; Ulum al-hadith, 14
  • 19. Taqyid al-'ilm ,96
  • 20. Al- ‘Imla’ wa al-‘istimla’, 12
  • 21. Bihar al-Anwaar , II, 152; Jami’ bayan al- ‘ilm,II, 34
  • 22. Al- ‘Imla’ wa al- ‘istimla’ , 12
  • 23. ‘Ulum al-hadith wa mustalahuh,8,9; Tarikh al-madhahib al - fiqhiyyah , 24; Al- ‘Imla’ wa al- ‘istimla’,46
  • 24. Adwa ‘ala al-Sunnat al- Muhammadiyyah,48.
  • 25. Adwa ‘ala al-Sunnat al- Muhammadiyyah,50, akinakiliwa al-Manar