Maoni Ya Baadhi Ya Sahaba Kuhusiana Na Uandikaji Wa Hadith
Mbali na imani ya baadhi ya Sahaba kuwa Hadith zisiandikwe, kikundi miongoni mwao kiliendelea kufanya hivyo. Ukweli huu ni dalili yenyewe inayoelezea kuwa kuharamishwa kwa uandishi wa Hadith ulitokana na Makhalifa na wala si Mtume s.a.w.w. kama inavyodaiwa. Miongoni mwa Sahaba waliokuwa wakiamini ruhusa ya uandishi wa Hadith walikuwa Amir al-Mu'miniin Ali ibn Abi Talib a.s. na mwana wake al-Hasan a.s. ambao si tu kwamba waliziandika Hadith, bali walitilia mkazo juu ya uandikaji wake pia. 1
Abdallah ibn al-Abbas, imeripotiwa kuwa alizoea kusema, "Ikamateni (kuitia mahabusi) 'ilim kwa njia ya kuiandika." 2 Harun ibn Antarah anaripoti kutoka kwa baba yake kuwa Abdallah ibn al-Abbas baada ya kuitamka hiyo Hadith aliyomwomba aiandike. 3
Salami anaripoti kuwa yeye aliona vipande vya maandishi kwa Ibn Abbas ambamo alikuwa ameandika matendo ya Mtume s.a.w.w. kama vile ilivyokuwa imesimuliwa na Abu Rafi'.4 Imeripoti kuwa Anas ibn Malik alizoea kumwambia mwanae:
“Ikamateni ilim kwa kuiandika." 5 Al-Kattani anaripoti kuwa Ayadh alizoea kusimulia ruhusa ya kuziandika Hadith kutokea Sahaba na Tabi'un.6 Hata hivyo, wengi wa Sahaba, inavyoonekana, ama walikuwa hawana uhakika katika yale waliyoyaandika kuhusu kuruhusiwa kwa kuziandika Hadith au hawakuwa na ari ya kuyazingatia na kuyasisitiza hayo kimatendo; uthibitisho huo ni kule kujiepusha kwao katika ukusanyaji wa Hadith.
Zaazan anaripoti: "Mimi nilichukua baadhi ya maandishi (tasbih) kutoka Umm Ya'fur na kumwendea Imam Ali ibn Abi Talib a.s. Naye alinifundisha hayo na baadaye aliniambia nikayarudishe kwa Umm Ya'fur." 7
Imenakiliwa pia kwamba Ibn Abbas alizoea kuziandika Sunan za Mtume s.a.w.w. juu ya vibao vya kuandikia, ambazo alizichukua mwenyewe hadi pale palipokuwapo na mkusanyiko wa Wanazuoni. Pia imenakiliwa kwa wingi (mutawatir) kuwa alipofariki aliacha vitabu vingi mno vinavyoweza kupakiwa juu ya ngamia mmoja. 8
Kwa mujibu wa ripoti kuwa Abu Bakr aliandika baadhi ya Hadith baada ya Mtume s.a.w.w. na baadaye alizichoma moto,9 nayo pia inadalilisha kuwa uandishi wa Hadith ulikuwa ni desturi iliyokuwa inakubaliwa miongoni mwa Sahaba.
Riwaya iliyonakiliwa kutoka Imam Ali ibn Abi Talib a.s. ambamo alisema kuwa yeyote aandikaye Hadith basi aandike pamoja na sanad 10 yake navyo pia inaungana na mawazo hayo. Vyanzo vyote vyote ni dhahiri kuwa Sahaba wengi walikubaliana kuwa uandishi wa Hadith ulikuwa umeruhusiwa.11 Ripoti kuhusu Sahifah ya Ja'bir ibn Abdallah ambayo ilikuwanayo Hadith za Mtume s.a.w.w.12 pia inaunga mkono juu ya tabia na mazoea ya Sahaba katika uandishi wa Hadith zilikuwapo miongoni mwa Sahaba. Katika misingi hiyo, tunaweza kumalizia kuwa uandishi wa Hadith ulikuwa umekubaliwa na vikundi vya Sahaba na upinzani wa Makhalifa juu ya uandishi wa Hadith haukutokana na kukatazwa na Mtume s.a.w.w. kama inavyodaiwa, bali ulitokana na uamuzi wao wenyewe.
- 1. Abu Zuhra, Tarikh al-madhahib al - fiqhiyyah ,24; Al- ‘Imla’ wa al- ‘istimla’ , 146
- 2. Vianzio vya habarri hizi zinapatikana hapa chini.
- 3. Taqyid al-'ilm ,92.
- 4. Sharh Ma’ani al- ‘athar, IV,319; Sunan al-Darimi ,I, 128
- 5. Al- Taratib al-idariyyah ,II, 246; Taqyid al-'ilm , 92
- 6. Tabaqat al-Kubra , VII,21; Sunan al-Darimi,, I, 127; Taqyid al-'ilm ,96, 97.
- 7. Al- Taratib al-idariyyah , II, 247
- 8. Katika kitabu cha Ibn Abi Shaybah al-Musannaf, II, 390.
- 9. Tabaqat al-Kubra , II, 123; Sayr al - hadith, 9; Taqyid al-'ilm , 136; ‘Ulum al - hadith, 20
- 10. Tadhkirat al-huffadh , I, 5.
- 11. Tadrib al-rawi, II, 67.
- 12. Sunan al-Darimi, I, 127,128, al-Ma’rifah wa al-tarikh, II, 279; Jami’ bayan al - ‘ilm, I, 84; al- Tabaqat al - kubra, II, 371; Taqyid al-'ilm , 113 - 199.