Sababu Halisi Ya Kuzuia Uandishi Wa Hadith
Uchambuzi wetu wa hapo mwanzoni unatuonyesha kuwa lawama zozote katika ucheleweshwaji wa uandishi wa Hadith hauwezi kamwe kutupiwa Mtume s.a.w.w. kwani riwaya zote zilizozuliwa juu yake haziwezi kamwe kukubaliwa kwa sababu mbali mbali. Katika jaribio hili, sisi tutakuwa tukitegemea mno juu ya riwaya zitegemewazo na Ahl al-Sunnah na penginepo tutatumia riwaya za Mashia. Ni mategemeo yetu kuwa msomaji ataweza kukadiria usahihi na ukweli wa uchambuzi huu kwa makini.
Aisha anaripotiwa kusema: "Baba yangu alikuwa amezikusanya Hadith mia tano za Mtume s.a.w.w. . Asubuhi moja, alinijia na kusema, 'Lete Hadith zote zilizopo, kwako.' Nami nilizileta mbele yake. Yeye aliziunguza zote kwa moto na kusema, 'Nisije mimi nikafa huku nimekuachia vyote hivi.'1
Imeripotiwa kwa mamlaka ya al-Zuhri kuwa: Umar alikuwa akitaka kuandika Sunan ya Mtume s.a.w.w. Yeye alikuwa akilifikiria kwa muda wa mwezi mmoja, alitarajia mwongozo kutokea kwa Allah swt katika swala hili. Siku moja asubuhi, alichukua uamuzi na kubainisha: "Mimi niliwakumbuka watu wote wale waliokwisha nitangulia, ambao waliandika na wakawa wamevutiwa mno katika yale waliyokuwa wameyaandika na ambao hatimaye walikiacha kitabu cha Allah (yaani Qur’an)." 2
Abd al-'Ala ansema: "Qasim ibn Muhammad ibn Bakr alizoea kutamka Hadith mbele yangu. alisema kuwa kulikuwapo na ongezeko katika Hadith katika zama za Umar. Naye Umar aliamrisha Ahadith zote zikusanywe, na zilipokusanywa, alizichoma moto zote kwa pamoja, akibainisha: 3 Kama muthnat ya Ahl al-Kitab. 'Mathnat' kama inavyoonekana kilikuwa ni kitabu ambacho Mayahudi walikiandika wao wenyewe na ambacho kilikuwa ni tofauti na Taurati. Hapa Umar alikilinganisha kitabu hicho pamoja na Hadith za Mtume s.a.w.w. , ambavyo alikuwa hataki ziwepo pamoja na Kitabu cha Allah (yaani Qur’an). Yahya ibn Ju'dah naye pia ameripoti kuwa 'Umar alidhamiriwa kuandika hadith na Sunan. Lakini alibadilisha dhamira yake na kutuma ujumbe wake katika miji yote, ikibainisha: "Yeyote yule aliyenacho chochote kutokana na hayo, ayateketeze yote." 4
Imeripotiwa kutoka 'Urwah ibn al-Zubayr kuwa, "Umar ibn al-Khattaab alikuwa akitaka kuandika Sunan ya Mtume s.a.w.w. Kuhusiana na swala hili, alishauriana na Sahaba wengineo. Sahaba wote waliafikiana kuwa Hadith zote ziandikwe. Lakini Umar alikuwa akizingatia swala hilo hadi ikafika asubuhi moja alipochukua uamuzi wake wa kughairi hivyo, na akasema, 'mimi nilitaka kuandika sunan. Lakini baadaye nilijikumbusha watu walionitangulia ambao waliandika vitabu na kukiacha kitabu cha Allah (yaani Qur’an). Kwa kiapo cha Allah swt mimi sitakifunika Kitabu cha Allah kwa kitu chochote kile." 5
Riwaya hii inatuonyesha kuwa Sahaba wote au angalau wale waliokuwa wameshauriwa walikubali juu ya uandishi wa Hadith. Lakini Khalifa, baada ya kufikiri kwa muda wa mwezi mmoja hivi, aliharamisha uandikaji wa Hadith katika misingi aliyoelezea yeye mwenyewe, jambo ambalo, bila shaka, halikuwepo pamoja na Sunnah za Mtume s.a.w.w.