read

Upinzani Wa Baadhi Ya Sahaba Na Tabi'un Katika Uandishi Wa Hadith

Baada ya Khalifa kukataza uandishi wa Hadith, kwani mienendo yao ilichukuliwa na watu kama ni Sunnah, basi kikundi cha Sahaba na Tabi'un pia walijiepusha na uandishi wa Hadith na walikuwa wakitegemea mno juu ya kile kimehifadhiwa akilini mwao.Wao walieneza Hadith kwa midomo tu na walichukia wazo la kuziandika. Kwao ilikuwa sivyo sahihi katika kuziandika Hadith za Mtume s.a.w.w. 1 ambapo Qur’an na Mtume s.a.w.w. vyote vimeweka msisitizo mkubwa juu ya uandishi kwa ujumla.

Abu Burdah anaripotiwa akisema kuwa baba yake alimwambia Abu Musa al-Ash’ari amletee chochote kile alichokuwa amekiandika kutokana na riwaya za baba yake.Na yote yalipoletwa, aliyaangamiza yote na alisema, "Wewe nae pia, kama sisi, lazima ukariri tu bila ya kuandika chochote." 2

Abd al-Rahman ibn Salamah al-Jamhi anaripoti: "Mimi nilisikia Hadith ya Mtume s.a.w.w. kutoka kwa Abdallah ibn Amr na niliiandika. Na baada ya kuhifadhi (kuikariri) akilini mwangu, nilikiteketeza kile nilichokiandika."3

Asim alisema: "Mimi nilitaka kumwachia Ibn Sirin kitabu, lakini yeye alikataa kukiweka, akisema kuwa yeye hakutaka kuwa na kitabu chochote karibu yake." 4

Abu Nadhrah asema: "Mimi nilimwambia Abu Sa'id awe akituandikia sisi, yeye alijibu, 'mimi sitawaandikieni na mimi siwezi kuwafanyieni chochote kama Qur’an kwa ajili yenu. Wewe uichukue (Hadith) kutoka sisi vile tulivyopokea kutoka Mtume s.a.w.w.' Abu Sa'id alizoea kusema, Simulieni Hadith miongoni mwenu, kwani mmoja wenu anamkumbusha mwingine vile kujali." 5

Imeripotiwa kutoka kwa Ibn Abi Tamin kuwa Ibn Sirin na wenzake wasingeliziandika/ hawakuziandika Hadith.6

Al-Harawi anaandika kuwa Sahaba na Tabi'un walikuwa hawaziandiki Hadith na walikuwa wakizihifadhi akilini mwao, isipokuwa kitabu cha Sadaqa. 7

Al-Nuwawi anaandika: "Mwelekeo wote wa Sahabah ulikuwa juu ya jihad, harakati dhidi ya matamanio ya mwili, na vile vile juu ya ibadah. Kwa hivyo wao hawakuwa na muda wa kunakili na kuandika (!). Kwa sababu kama hizo, Tabi'un pia hawakuweza kuleta chochote kile kilichoandikwa (tasnif)." 8

Abu Kathir al-Ghubri anamnakili Abu Hurayrah akiwa amesema:"Ahadith zisifichwe wala zisiandikwe." 9

Abdallah ibn Muslim anaripoti kuwa Sa'id ibn Jubayr alikuwa anachukizwa na uandishi.10 Vivyo hivyo, Ibrahim al-Nakhai alibainisha kuwa yeye kamwe alikuwa hajawahi kuandika chochote. 11 Wakati alipoulizwa sababu ya kutoandika, yeye alijibu, "Wakati mtu anapoandika kitu chochote, basi huja kutegemea juu ya yale aliyoyaandika." 12

Habib ibn Abi Thabit anaripotiwa kusema: "Mimi sina kitabu chochote ulimwenguni kote, isipokuwa kwa ajili ya Hadith ambayo ni kwa ajili ya sanda yangu." 13

Al-Hasan ibn Abi al-Hasan wakati wa kifo chake alimwamrisha mfanyakazi wake aliwashe tanuru na kuvitupa vitabu vyote alivyokuwa navyo isipokuwa kimoja tu. 14 Ibn Sirin alikuwa akisema: "Iwapo mimi nitahitaji kuandika kitabu basi nitaandika kitabu juu ya barua za Mtume s.a.w.w." 15 Yahya ibn Sa'id anasema: "Mimi niliwaona Wanazuoni ni katika hali ambayo wanapingana juu ya kunakili na kuandika."16 Suleyman ibn Harb anaripoti: "Yahya ibn Sa'id alitujia na alikuwa akisema Hadith. Mwanzoni mwenzi wetu walikuwa hawaziandiki Hadith alizokuwa akizisimulia, lakini baada ya muda kupita, wao walianza kuziandika." 17

Qasim ibn Muhammad ibn Abi Bakr alikuwa akimwambia Abdallah ibn 'Ala asiwe akiandika Hadith. 18 Sufyan ameripoti kuwa, pale alipoambiwa Amr ibn Dinar kuwa yeye alikuwa akiziandika Hadith za Amr, 'Amr alisimama na kusema, "Yeyote yule anayeziandika Hadith basi atoke hapa kwangu." Sufyan anasema kuwa kuanzia hapo hakuandika chochote kile alichokisikia kutoka Amr isipokuwa alikuwa akihifadhi tu.19

Imeripotiwa kutoka Ibn Tawus kuwa baba yake alisema: "mtu mmoja alimwuliza Abdallah ibn Abbas, swali ambalo lilimfurahisha mno. Huyo mtu alimwomba Ibn Abbas amwandikie jibu lake. Lakini Ibn Abbas alisema kuwa wao kamwe hawaandiki chochote kile kilicho cha 'ilim' 20 Riwaya hii ipo katika mzozano pamoja na riwaya zinginezo zilizotangulia za Ibn Abbas.

Malik ibn Anas anaripoti kuwa Ibn Musayyab alipofariki, hakuacha hata kitabu kimoja. Vivyo hivyo ndivyo ulivyokuwa ukweli wa Qasim ibn Muhammad, Urwah ibn al-Zubayr na Ibn Shihab al-Zuhri.21 Mansur ibn Mu'tamir ameripotiwa akiwa amesema: "Mimi sijaandika chochote hadi leo."22 Na taarifa kama hiyo hiyo ipo imeripotiwa kutokaYunus ibn Ubayd.23 Imeripotiwa kuhusu Ibn Abi Dhu'ayb kuwa yeye alikuwa akikariri tu Hadith. Yeye alitokana na tabaka la tano na aliishi katikati ya karne ya 2 A.H./8 A.D. 24 Imesemwa kuhusu Sa'id ibn Abd al-Aziz alikuwa haandiki chochote. 25

Ismail ibn Ayyash, aliyetokana na tabaka la sita alikuwa amehifadhi akilini mwake kiasi cha Hadith elfu kumi lakini hakuandika hata moja.26 Abu Hatim anaripoti kuwa yeye kamwe hakuona chochote kilichoandikwa mikononi mwa Abd al-Walid al-Tayalisi.27 Wote hao walikuwamo katika tabaka la saba na walichukia mno uandishi wa Hadith. Pia imesemwa kuwa al-Nufayli kamwe hakuonekana pamoja na kitabu chochote. 28 Vile vile Sahib al-Basri inasemekana alichukia mno uandikaji.29

  • 1. Tadrib al- rawi , II, 68.
  • 2. Tadrib al- rawi , II, 65.
  • 3. Kashf al - ‘astar, I, 109.
  • 4. Al-Ma’arifah wa al -ta’rikh, II, 523.
  • 5. Al-Kifayah, 353; Al-Ma’arifah wa al -ta’rikh, II, 59.
  • 6. Hayat al -Sahabah, I, 243, 244.
  • 7. Al- Taratib al-idariyyah , I, 62; al -Turuq al- hukmiyyah, 256.
  • 8. Al- Taratib al-idariyyah , II, 249.
  • 9. Al- Taratib al-idariyyah , II, 249.
  • 10. Tabaqat al-Kubra , II, 364.
  • 11. Tabaqat al-Kubra, VI, 258; katika uk. 257 ameiandika ahadith ya Ibn ‘Abbas.
  • 12. Tabaqat al-Kubra, VI, 258.
  • 13. Tabaqat al-Kubra, VI 271, wakati ambapo mwanafunzi wake alisikitika mno kwa kutoandika hadith na riwaya, tazama uk. 270.
  • 14. Tabaqat al-Kubra, VI 320.
  • 15. Tabaqat al-Kubra, VII, 157.
  • 16. Tabaqat al-Kubra,VII, 157; Sunan al-Darimi, I, 120.
  • 17. Tabaqat al-Kubra , VII, 141; Jami’ bayan al - ilm, I, 81.
  • 18. Taqyid al-'ilm , III, Tadhkirat al-huffadh , I, 113
  • 19. Tabaqat al-Kubra , V, 188.
  • 20. Tabaqat al-Kubra , V, 480; Tadhkirat al-huffadh , I, 113.
  • 21. Al- Musannaf, XI, 258 ya ‘Abd al-Razzaq ; Taqyid al-'ilm , 42.
  • 22. Tadhkirat al-huffadh , I, 111.
  • 23. Tadhkirat al-huffadh , I, 142.
  • 24. Tadhkirat al-huffadh , I, 145.
  • 25. Tadhkirat al-huffadh , I, 192.
  • 26. Tadhkirat al-huffadh , I, 219.
  • 27. Tadhkirat al-huffadh , I, 254.
  • 28. Tadhkirat al-huffadh , I, 382.
  • 29. Tadhkirat al-huffadh , I, 441.