Kitabu Kinginecho Mbali Na Qur’an
Kama itakavyoonekana kutokana na riwayah zinazotokana na wale wote waliokuwa wakizingatia kuharamishwa kwa Hadith kuandikwa, kwamba madai yao yote ya hasa kuficha ukweli yalikuwa ni khofu ya kutokezea kwa 'kitabu kinginecho mbali na Qur’an', na kwamba matokeo yake yatakuwa ni kutumika vitabu vingine na kuachwa kwa Qur’an. Hapa sisi tutajaribu kuchambua uhakika wa khofu kama hiyo na itaonekana wazi kuwa hayo yalikuwa ni hoja za kutaka kuuficha ukweli na wala hapakuwapo na makusudio mengineyo. Al-Qur’an na Sunnah vinakamilishana, na kama vile Waislamu wote wanavyoelewa kuwa kimoja hakikamiliki bila ya kingine - isipokuwa tu labda wale wenye kusema kuwa: "Kitabu cha Allah kinatutosha."
Jambo ambalo linahitaji kuzingatiwa hapa ni kuwa wale mabingwa wote wa kuharamisha uandishi wa Hadith iwapo wao walikuwa ni Makhalifa au wale waliofuata katika swala hili na waliweza kutumia hivyo kwa kuhalalisha tendo lao - walikuwa wakijua kauli ya Mtume s.a.w.w. kuhusu "Kitabu ubavuni mwa Kitabu cha Allah swt." Hata hivyo kimakosa au kimakusudi wao waliitumia visivyo hivyo kauli ya Mtume wa Mwenyezi Mungu.
Ni kweli kuwa katika zama za uhai wa Mtume s.a.w.w. baadhi ya Sahaba waliweza kujipatia vitabu vya Taurati na vitabu vinginevyo vya Mayahudi. Na Mtume s.a.w.w. alipokuja kupata habari kuhusu hayo, aliwaambia wasivilinganishe sambamba na Kitabu cha Allah, al-Qur’an. Katika uhusiano huu itatubidi kuzingatia riwaya ifuatayo iliyonakiliwa na Ja'bir. Ja'bir anaripoti kuwa Umar al-Khattab alileta nakala moja ya Tawrati mbele ya Mtume s.a.w.w. na kusema: "Hii ni nakala ya Tawrati ambayo mimi huwa ninaisoma." Mtume s.a.w.w. alikaa kimya lakini rangi ya uso wake ulibadilika. Abu Bakr aliiona hali hiyo, na alimwambia Umar, "Mama yako alie katika kilio chako, je, hauoni uso wa Mtume s.a.w.w.! Umar alipouona uso wa Mtume s.a.w.w. . akasema, "Mimi najikinga na Mungu kwa ghadhabu za Mtume s.a.w.w. Mimi namkubalia Allah kama mmiliki wa vyote, Islam kama Dini na Muhammad kama Mtume." Juu ya hayo Mtume s.a.w.w. alisema: "Kwa kiapo cha Mungu, iwapo Musa angalitokea hapa na wewe umfuate yeye kwa kuniacha mimi, basi ungalikuwa umepotoka njia ya haki. Iwapo Musa angalikuwa hai na kuniona mimi, angalikuwa akinifuata mimi."1
Mapokezi haya yanatuonyesha Mtume s.a.w.w. alivyokuwa amekasirishwa kwa sababu Umar alikuwa amekichukulia kitabu kingine sambamba na Qur’an. Katika mapokezi mengine kama haya, mtu kutoka Ansaar anachukua nafasi ya Abu Bakr. Inawezekana kuwa mapokezi hayo mawili yanatuelezea matukio mawili tofauti na kwamba tunaweza kuelewa kuwa matukio hayo mawili yametokea katika nyakati mbalimbali.
Imepokelewa kutoka Abu Qalabah kuwa mara moja Umar ibn al-Khattab alipita karibu na mtu aliyekuwa akisoma kitabu. Baada ya kumsikiliza kwa muda mfupi, Umar alipendezewa na kile alichokisikia. Basi alimwomba mtu yule amwandikie kutoka kitabu hicho. Mtu huyo alikubali kumwandikia hivyo. Hapo Umar alilinunua jani na kumletea huyo mtu, ambamo mtu yule aliandika kwa kujaza sehemu zote mbili. Baadaye Umar alifika mbele ya Mtume s.a.w.w. na kumsomea yaliyokuwa yameandikwa. Papo hapo rangi ya uso wa Mtume s.a.w.w. ilibadilika kwa ghadhabu. Basi hapo mtu aliyetokana na Ansaar alimwambia Umar: "Mama yako alilie kilio chako! Je, hauoni uso wa Mtume s.a.w.w. ?" Kwa hayo Mtume s.a.w.w. alisema: "Mimi nimetokezea kama Mtume, kama mfunguzi (fatih) na kama mfungaji (khatim), na mimi nimeleta kila kitu ambacho ilinibidi kujanacho (hivyo hakuna kilichobakia hadi nyinyi) kwenda kuvitafuta kutoka kwa watu wengineo." 2
Imeripotiwa kwa mamlaka ya al-Zuhri kuwa Hafsah binti yake Umar, alikileta kitabu chenye Hadith (masimulizi za Mtume Yusuf a.s. mbele ya Mtume s.a.w.w.. Yeye alianza kukisoma huku Mtume s.a.w.w. akiwa akisikiliza na uso wake kubadilika rangi kuwa mwekundu. Hapo ndipo Mtume s.a.w.w. aliposema, "kwa haki ya Mungu, iwapo Yusuf mwenyewe angalikuja hapa na iwapo wewe ungalimfuata yeye na kuniacha mimi basi wewe ungalikuwa umepotoka." 3
Riwaya hizi zote zinatuonyesha kile alichokuwa akikichukia Mtume s.a.w.w. kilikuwa ni maandishi mapotofu ambayo athari zake zilikuwa ni kueneza imani potofu za Mayahudi ambazo zilikuwa zikiitwa Israiliyyat - miongoni mwa Waislamu. Mtume s.a.w.w. alikuwa hataki vile vitabu vya Mayahudi viwe sambamba na Qur’an Tukufu, maneno yote ambayo yalikuwa ni maneno ya Allah swt; katika vitabu vya Mayahudi kulikuwamo na visa na Hadithi za uwongo na zenye imani za ushirikina na kuamini uchawi, vinaweza kumfanya mtu apotoke na njia iliyo na mafundisho halisi ya Qur’an ambayo yameelezwa mbele yao.
Riwaya zilizoelezwa hapo juu pia zinaonyesha kuwa Khalifa na binti yake walikuwa wakipendezewa mno na usomaji wa vitabu kama hivyo na mara nyingine ilitokea kuchunguzwa na Mtume s.a.w.w. Hata hivyo, kwa bahati mbaya, tunaona kuwa baadaye ambapo Ka'ab al-Ahbar, Myahudi aliyesilimu kidhahiri tu, alipomwijia Umar na kumwomba ruhusa ya kuisoma Tawrati, Umar alimwambia: "Iwapo wewe unajua kuwa hiyo ndiyo Tawrati aliyokuwa ameteremshiwa Musa a.s. huko katika Milima ya Sinai, basi uisome usiku na mchana."4 Na haya ndiyo yaliyokuwa majibu ya Umar baada ya Mtume s.a.w.w. kumkataza yeye mwenyewe kutoisoma Tawrati wala mambo yoyote kama hayo.
Zipo riwaya zingine ambazo zinathibitisha fikara zetu kuwa Mtume s.a.w.w. alichokuwa akiharamisha kuwapo kwa kitabu sambamba na Qur’an yalikuwa ni maandiko ya Mayahudi yaliyokuwa yakitumiwa na Waislamu. Ipo imeripotiwa kuwa Abdallah ibn Mas'ud aliposikia kuwa watu walikuwanacho kitabu ambacho walistaajabishwa na yale yaliyokuwemo,basi alikichukua na kuki teketeza, akisema: "Watu wa vitabu (Ahl al-Kitaab) waliangamia kwa sababu wao walikuwa wakitegemea mno maandiko ya Wanazuoni wao (ulamaa) na walikuwa wamepuuzia Kitabu cha Allah (yaani Tawrati)" 5 Neno ulamaa katika Waarabu wa zama hizo ilikuwa ikimaanisha Wanazuoni wa Kiyahudi na Kikiristo na vitabu vinavyozungumzwa katika riwaya hizi ni maandishi ya Kiyahudi.
Riwaya ifuatayo inaelezea vizuri zaidi swala hili. Murrah al-Hamdani anasema: Abu Murrah al-Kindi alikileta kitabu kutoka Syria (al-Shaam) na alimpatia Ibn Mas'ud alikipitia kitabu hicho, akaleta maji na kuyaosha yale maandishi yaliyokuwa yameandikwa katika kitabu hicho. Na hapo alisema, 'Watu walioishi kabla yenu waliangamia kwa sababu ya kuvifuata vitabu kama hivi na kukiacha cha Allah (yaani Qur’an)" Al-Husayn anasema, "Kwa hakika asingeteketeza maandishi hayo kama yangalikuwa ni Qur’an na Sunnah (yaani Hadith za Mtume s.a.w.w. Bali kilikuwa ni kitabu cha Ahl al-Kitaab."6
Imam Ali ibn Abi Talib a.s. ameripotiwa akisema: "Yeyote yule miongoni mwenu aliyenacho kitabu (mbali na Qur’an na Sunnah) akiteketeze.Watu waliowatangulia nyinyi waliangamizwa kwa sababu ya kufuata masimulizi ya Wanazuoni wao huku wakikiacha Kitabu cha Allah (yaani Qur’an)." 7
Al-Imam al-Sadiq a.s. ameripotiwa akisema: "Baadhi ya Wanazuoni wapo wanafuatilia riwaya za Mayahudi na Wakristo, huku wakitegemea kuongeza elimu yao. Watu kama hao, nafasi yao ipo chini mno ndani mwa Jahannam. 8 Imeripotiwa kwa mamlaka ya Amr ibn Yahya ibn Ju'dah kuwa kilipokuwa kimeletwa kitabu mbele ya Mtume s.a.w.w. alisema: "Inatosheleza kwa upumbavu na upotofu wa Ummah kwa kuyaacha yale yaliyokuwa yameletwa na Mtume wake na kuanza kuangalia yaliyokuwa yameletwa na Mitume mingine."9 Riwaya hii pia inatuonyesha aina ya kila kitabu kilichokuwa kimeletwa mbele ya Mtume s.a.w.w. na pia kutupia nuru juu ya maana ya: Kitabu sambamba na Kitabu cha Allah (yaani Qur’an).'
Vile vile Ibn Abbas anasema: "Je utawaulizaje swali Ahl al-Kitaab kuhusu matatizo wakati ambapo Al-Qur’an ipo miongoni mwetu ?" 10
Riwaya na masimulizi na mapokezi yote haya yanaonyesha kuwa Mtume s.a.w.w. aliharamisha kutayarishwa kwa kitabu sambamba na Qur’an huku akitahadharisha hatari ya uingiliaji wa Israiliyyat na kamwe, vyovyote vile, hakumaanisha Sunnah yake, ambayo ipo imeshikamana (wajib al-'ita'ah), kama vile wanavyokubalia Waislamu wote.
Mabishano yetu yanazidi kupata nguvu kwa uhakika kuwa Wanazuoni wa Hadith wa Islam walikuja baadaye wakaziandika na kuzikusanya Hadith. Ama kwa mfano wa wale kama 'Urwah walichoma moto Hadith walizokuwa wameziandika kwa kudai kuwa "sisi hatutaki kuwanacho kitabu sambamba na Kitabu cha Allah (al-Qur’an),'11 basi ni lazima tuseme kuwa wao walitenda kwa sababu ya kutoelewa vyema mafhumu ya kauli ya Mtume s.a.w.w.
Kama itakavyokuwa imeonekana hapo awali kuwa sisi hatuwezi kusema kuwa Mtume s.a.w.w. ndiye aliyehusika na uharamishwaji huo wa kuziandika Hadith; na msimamo kama huo unaweza kuchomoza maswali ambayo hayana majibu. Ilieleweka hapo awali kuwa baadhi ya Makhalifa walihusika moja kwa moja katika swala hili la kutoziandika Hadith na wao ndio walioharamisha uandishi wa Hadith. Hapa, baada ya kutaja sababu zilizotolewa nao kwa kuchukuwa hatua kama hiyo, sisi tutajaribu kutafuta maelezo yake. Baada ya kuthamini sababu chache zilizotolewa nao katika swala hili, sisi tutajaribu kuelezea kile tunachokiona kuwa ndiyo sababu maalum kuhusiana na uharamishwaji huo, pamoja na uthibitisho wa kutosheleza kuunga mkono maelezo yetu.
- 1. Tadhkirat al-huffadh , I, 461; rejea Jami’ bayan al -‘ilm, I, 89-79; Sunan al-Darimi, I 119, 120.
- 2. Sunan al-Darimi, I, 116; al-Musannaf , X, 313 ya ‘Abd al-Razzaq.
- 3. al-Musannaf , VI, 113, XI, 111 ya ‘Abd al-Razzaq ; Majma’ al-Zawa’id, I, 182.
- 4. al-Musannaf , XI, 110 ya ‘Abd al-Razzaq; Mizan al - ‘i’tidal, I, 666 ; Lisan al - Mizan, II, 408;
Bihar al-Anwaar , XI, 99 ; Gharib al - hadith, IV, 49, III , 28, 29; al - Fai’iq, IV, 114 ya al-
Zamakhshari - 5. Gharib al -hadith, IV, 262; al- Faiq, I 651.
- 6. Sunan al-Darimi, I, 122; Taqyid al-‘ilm, 53, 56.
- 7. Gharib al -hadith, IV, 48; Jami’ bayan al-ilm, II, 52, 53; ipo riwaya kama hiyo katika Taqyid al-'ilm kuwa aliletewa kitabu kutoka Yemen ambamo kulikuwamo hadith itokanayo na Ahl al Bayt a.s. na kuwa yeye aliiteketeza.
- 8. Jami’ bayan al - ‘ilm, I, 76.
- 9. Bihar al-Anwaar , II, 108
- 10. Jami’ bayan al - ‘ilm, II, 50.
- 11. al-Musannaf , X, 313 ya ‘Abd al-Razzaq