Sababu Zilizotolewa Kwa Kuharamisha Uandishi Wa Hadith Za Mtume s.a.w.w.
1. Sababu ya kwanza iliyotolewa ni khofu ya watu kushindwa kutofautisha baina ya Qur’an na Hadith za Mtume s.a.w.w. ambazo zingalisababisha uharibifu (tahrif) wa maandiko ya Qur’an, madhambi yasiyo samehewa. 1
Mazungumzo haya, ambayo hayawezi kukubalika, yamekanushwa na Ustadh Abu Riyyah katika maneno yafuatayo:
"Mtu kama huyo anaweza kuwashawishi watu wa kawaida, lakini haiwezi kukubalika kiutafiti. Kwa sababu itakuwa ikimaanisha kuwa ufasaha wa Qur’an unasimama sawasawa na ufasaha wa Hadith za Mtume s.a.w.w.
Kile anachokimaanisha hapa ni muujiza wa ufasaha wa Qur’an unavyo tambulikana miongoni mwa watu, hatuwezi kudai kuwa wao wangalikuwa chini ya upotofu kwa kuzichanganya aya za Qur’an kwa Hadith za Mtume s.a.w.w., ambazo zipo chini kwa kulinganishwa na ufasaha wa Qur’an. Msimamo kama huu, kwa hakika unamfanya mtu akipingana na muujiza wa Qur’an.
Zaidi ya hayo, kuamini katika uwezekano wa kuchanganyika kwa Aya za Qur’an na Hadith ni sawa na kuamini katika uwezekano wa kuja kupotea kwa maandiko ya Qur’an. Imani kama hiyo inakanushwa kwa sababu uhalisi wa Qur’an upo unathibitishwa na Allah swt katika Qur’an: Sura Hijr, 15:9.
Tunaweza kusema zaidi ya hayo kuwa kikundi cha Sahaba walikuwa wamehifadhi moyoni mwao Qur’an nzima na kwa uangalifu mkubwa na upendo wao mkubwa juu ya Qur’an. Hatuwezi kamwe kuwafikiria kuwa wao walikuwa na hatari ya kuchanganyikiwa baina ya Qur’an na Hadith. Sisi twaweza kusema kuwa labda kulikuwapo na hatari ya uwezekano tu, na uwezekano huo hauwezi kupewa uzito sawa na madhara na hatari za kutoziandika Hadith.
Madhara yaliyokuwa yameshajulikana kuanzia awali kabisa Sahaba hawakukubaliana miongoni mwao katika siku za awali kuhusu baadhi ya Shariah za Kiislamu na ilikuwa ni dhahiri kuwa athari za ufarakano huo ungelikuwa na hatari kubwa iwapo Hadith za Mtume s.a.w.w. zingalikuwa hazikuandikwa. Lakini hatari hiyo ilitokea tu. Baina ya tishio la mbali na hatari fulani (ya kupanua tofauti), iliwabidi wao walitilie mkazo swala la uandishi wa Hadith, ingawaje, kimsingi swala la kutoruhusu uandishi wa Hadith halikuwa na uzito wowote.
2. Maelezo ya pili yatolewayo na Abu Riyyah yanasema, tuchukulie kwamba uharamisho wa kuandika Hadith ulitokana na Mtume s.a.w.w. kwamba Mtume s.a.w.w. alitaka maamrisho ya Shariah yawe katika mipaka iliyodhibitiwa na alipinga kueneza zaidi kwa maamrisho ya Shariah (adillah). Haya, kwa mujibu wake, ni sababu ambayo pia inatokana na nyakati zinginezo ambapo Mtume s.a.w.w. alichukia kuulizwa maswali. Sababu hiyo hiyo ipo inatumika katika hali ambapo Hadith ambazo zilikuwa sahihi katika kipindi fulani na ambapo haikuruhusiwa kufuata hapo baadaye. 2
Sisi tunachukulia maelezo hayo kuwa ni dhaifu mno, kwani haiwezekani kamwe kudai kuwa Mtume s.a.w.w. alipinga kwa kuenea Hadith halali kisheria zikitumika kama misingi ya kanuni halali za shariah. Je, itawezekanaje kwetu sisi kukubaliana nayo wakati Qur’an na Hadith kwa pamoja zinawajibika kujibu mahitaji katika sura mbalimbali ya Shariah kwa ajili ya siku ya Kiyama na siku zote kutoa maongozi kwa mwanadamu? Pamoja na hayo, sisi tutaelezea tena kwa mara ya pili kuwa sisi hatuamini ya kwamba Mtume s.a.w.w. alitoa amri ya kuharamisha uandishi wa Hadith.
3. Al-Awzai anatoa maelezo mengineyo, anaandika: "Sayansi ya Hadith ni tukufu pale inapoenezwa kwa mdomo tu, inawafanya watu wakumbushana daima Hadith. Lakini, pale inapoandikwa, nuru yake inafifia na pia huweza kufikia mikono ya watu wasiostahili kupatiwa." 3
Sisi tunaweza kuonyesha kuwa ingawaje kuenezwa kwa Hadith kwa mdomo kuna faida ya kukumbusha watu yaliyomo ndani mwa Hadith, utumiaji wake kama halisi, na pekee, njia za kuzirekodi hizo zipo mashakani. Kwa hakika, faida kama hizo ziliambatana na madhara makubwa mno. Hata hivyo, hii ndiyo sababu mojawapo ambayo al-Awzai ameibuni, na ipo inashukiwa iwapo ikizingatiwa na wale waliokuwa wameharamisha uandishi wa Hadith.
4. Ibn Abd al-Birr, anaandika wakati wa kutoa maelezo kama hayo:
Uandishi wa Hadith uliharamishwa ili watu wasitegemee mno yale yaliyoandikwa na wao, wakiepukana na huzihifadhi. Katika hali kama hiyo, desturi ya kuhifadhi moyoni Hadith ingalikuwa imepotea. 4
Wazo kama hilo pia haliwezi kukubalika, kwa sababu madhara yaliyotokana na kushindwa kuziandika Hadith yalikuwa ni makubwa mno kwa kulinganishwa na faida iliyotokana na kupigwa marufuku kwa uandishi wa Hadith. Ustaarabu na utamaduni wa mwanadamu umekuwa ukilindwa kwa kupitia maandishi na wala si kwa kusema tu, ingawaje kuhifadhi Hadith kwenyewe ni tabia nzuri na yenye maana.
5. Sababu nyingine imetolewa pamoja na haya ni kwamba iwapo Hadith zingalikuwa zimeandikwa basi watu wangalikuwa wameiacha Qur’an huku wakizipatia Hadith umuhimu wote. 5
Mazungumzo hayo pia hayawezi kuchukuliwa kuwa ni kinga, kwani jambo kama hilo linaweza kusemwa iwapo Hadith itakayomaanishwa itakuwa ni zile zisemwazo kwa mdomo tu, na Qur’an kwa upande wa pili. Ni kweli kabisa kuwa kupitia umuhimu wote Hadith ni upotofu ambao wale wafanyao hivyo waonywe na wachukue umuhimu kama huo katika Qur’an. Lakini uharamisho wa uandishi wa Hadith, umeleta uharibifu usioweza kutegemewa katika utamaduni wa Islam, kwa njia hiyo si ya kupatikana kwa matokeo sahihi.
6. Abjad al-'ulum anaandika:
"Sahaba na Tabi'un, kwa sababu ya uhalisi wa imani yao na kuwapo kwao karibu na kipindi cha Mtume s.a.w.w., na kutokuwapo kwa mabishano na uwezekano wa kuwaelekea watu waliotegemewa, hawakuwa na hitajio la kuziandika Hadith na shariah. Lakini vile Islam ilipoanza kuenea penginepo, wao walianza kuzikusanya na kuziandika Hadith, Fiqh na tafsiri ya Qur’an.' 6
Kile anachokitaka kukisema huyu mwandishi siyo sababu ya kupinga kwa baadhi ya Sahaba kwa ajili ya uandishi wa Hadith, bali ni maelezo tu- nayo pia siyo sahihi- ni kwa nini Hadith hazikuandikwa; sababu yake halisi ilikuwa ni kupingwa kwa uandishi wa Hadith, na wala si kutohitajika kama vile anavyodai mwandishi huyo. Zaidi ya hayo, ueneaji wa Islam ulitokea katika miaka ya ishirini au zaidi ya miaka hamsini baada ya kifo cha Mtume s.a.w.w. Uandishi na ukusanyaji wa Hadith ulicheleweshwa hadi kufikia nusu ya karne ya 2 A.H./8 A.D. mbali na nukta hizo mbili inaeleweka kuwa sifa hii ya kumzulia Mtume s.a.w.w. ilianza katika maisha yake, na hatimaye iliweza kuongezeka kwa sababu ya kutokuwepo kwa Hadith zilizoandikwa. Pia ilikuwa ni wajibu wa Sahaba, ambao walitofautiana miongoni mwao katika mambo ya Shariah, kuzuia kukua kwa upotoshi na tofauti kwa kuanza kuziandika Hadith.
Sababu hasa ambayo ipo nyuma ya kuharamishwa kwa uandishi wa Hadith, ambayo mimi ninaamini, imeelezwa na mwanachuo mashuhuri aitwaye Sayyid Ja'far Murtadha na imethibitishwa kwa ushahidi uliopo:-
Kulikuwapo na madhehebu mawili miongoni mwa Mayahudi. Dhehebu moja waliamini katika uandishi wa Hadith, ambapo dhehebu la pili halikuafiki hivyo, waliamini katika kutoandika chochote kile isipokuwa Taurati peke yake. Kundi hili la pili liliitwa Qurra (wasomaji). Haya yapo yamedokezwa na Dhadha katika kitabu chake cha fikara za Dini ya Kiyahudi. Ka'ab al-Ahbar, Myahudi aliyesilimu (katika zama za Umar) alitokana na kundi hilo la pili. Mara moja Umar alimwuliza swali kuhusu mashairi ya vitu avisemavyo kuhusu Waarabu, kuwa kikundi cha kizazi cha Ismail, walikuwa wamehimili Biblia katika nyoyo zao na walizungumza kwa busara.....Labda inawezekana kuwa Khalifa alilichukua wazo hilo (la kutoandika chochote kile isipokuwa Qur’an tu) kutoka kwa Ka'ab al- Ahbar; ambaye pia vile vile alikuwa akiheshimiwa (na Khalifah)kwa ushauri wake.
Zaidi ya hayo, uharamisho juu ya uandishi wa Hadith ulikuwa ukienda vyema pamoja na Siasa za tawala, kwani waliweza kuyazima malalamiko dhidi yao na kuendelea kuimarisha utawala wao. Kwa hakika hatua kama hiyo inawezekana kuwa na matokeo ya upotezi wa sehemu ya Hadith izungumziayo juu ya haki za wapinzani na ustahiki na ambayo ilifaa kuletea nguvu sehemu walizokuwa wamezidhibiti. 7
Mtunzi huyo, kama vile taarifa yake ionyeshavyo, anadhani zipo sababu mbalimbali zilizosababisha kuharamishwa kwa Hadith, moja na muhimu kabisa ni kushawishiwa kwa mawazo ya Ahl al-Kitab juu ya Khalifa wa pili, ambaye, inavyoonekana, alipenda kusoma vitabu vyao kuanzia wakati aliposilimu.
Uthibisho unaothibitisha ushawishi huu ni riwaya ya Urwah ibn al-Zubayr, isemayo kuwa Khalifa alikuwa amenuia kukusanya 'sunan' na hata pia aliwasiliana na Sahaba wengineo juu ya mpango wake huo. Wao walikubaliana nalo, lakini alibadilisha mpango wake huo kwa kusema kuwa watu wa Ahl al- Kitaab waliviacha vitabu vitukufu na kuanza kuvifuata vile walivyokuwa wameviandika na hivyo yeye hakutaka kufuata kitakachotokea juu ya Qur’an kama hivyo ilivyokuwa imetokea. 8
Ni jambo la kuweza kutokea kuwa maelezo hayo ya Khalifa yaliletwa na Ka'ab al-Ahbar, aliyetokana na kikundi cha Qurra, ambaye alijiepusha na kuandika chochote kile mbali na Tawrati. Ka'ab alikuwa na njama mbaya dhidi ya Islam; ingawaje Khalifa alikuwa hana nia kama hizo, naye, kwa bahati mbaya, alishindwa kuona kwa kupitia ulaghai wa Ka'ab.
Mabishano ya Umar dhidi ya uandishi wa Hadith yalirudiwa na wengineo. Abu Burdah anaripoti kutoka kwa baba yake aliyesema: "Banu Israil waliandika vitabu na kukiacha Kitabu cha Allah." 9 Hakam ibn Atiyyah anaripoti kutokea Muhammad (bila shaka, Muhammad ibn Sirin) kuwa alizoea kusema: "Imenukuliwa kuwa Banu Israil walipotoshwa kwa sababu ya vitabu walivyovirithi kutokea mababu zao." 10
Mwanachuoni mwingine anaandika:
"Moja ya ushawishi mkubwa wa Mayahudi juu ya Waislamu ulikuwa ni kuepukana na desturi ya kuandika Hadith.
Imeandikwa katika Talmud, "Nyinyi hamna haki ya kuandika mambo ambayo munayazungumzia tu. "Huwezi kupinga kuwa Waislamu hawakushawishiwa na Ka'ab al-Ahbar katika swala hili, ingawaje wao waliileta mbele katika sura ya Hadith ya Mtume s.a.w.w. Ushahidi wake ni amri iliyotolewa na Khalifa baada ya kuzichoma Hadith alizokuwa amezikusanya:
"Mathnat (au Mishnah) kama Mathnat ya Ahl al-Kitab." 11 Maneno haya pia yanatuonyesha vile alivyokuwa ameshikamana pamoja na desturi za Mayahudi.
Abu Ubayd katika Gharib al-Hadith, anaandika:
"Mimi nilimwuliza mwanachuo wa Taurati na Injili kuhusu neno 'Mathnat.' Yeye alinijibu: "Mapadre wa Kiyahudi na waalimu wa Kiyahudi waliviandika baadhi ya vitabu baada ya Musa, mbali na vitabu vitukufu, na ambavyo wao waliviita kwa jina la 'Mathnat.'
Ni dhahiri kuwa Khalifa alikuwa akiufuata mfano wa Mayahudi ambao wao walikuwa katika kambi mbali na iliyoelezwa hapa. Abu Ubayd anaendelea kusema:
Baada ya kupata maelezo hayo, mimi nimeelewa maana ya riwaya hii. Na hii ndiyo iliyokuwa sababu Abdallah ibn Amr ibn al-Aas alikuwa akichukia kukichukua chochote kile kutokea kwa Ahl al-Kitaab, ingawaje yeye alikuwa na baadhi ya vitabu alivyovipata wakati wa kampeni ya Yarmuk (kutokea Makanisa ya Kiyahudi).
Abu 'Ubayd anaongezea:
"Ni lazima, uharamisho (wa uandishi na usambazaji) haukuhusiana na Hadith na Sunnah za Mtume s.a.w.w., kwa sababu itawezekanaje kuharamisha uandishi wa Hadith wakati ambapo wengi wa Sahaba wenyewe walikuwa wakinakili Ahadith. 12
Hii inatuonyesha waziwazi kuwa Umar aliharamisha uandishi wa Hadith za Mtume s.a.w.w. na Sunnah zake kwa sababu yeye alichukulia msimamo kama ule wa maandishi yaliyokuwa yametolewa na waalimu wa Kiyahudi. Kwa hivyo, badala ya kuangalia na kuchunga kuenea kwa imani za Israiliyyat, yeye alikuwa ameshawishiwa nayo, ushawishi ambao ulisababisha katika kuangamizwa kwa Sunnah za Mtume s.a.w.w. Vile vile ni lazima iongezwe kuwa
Abdallah ibn Amr mwenyewe alikuwa mmoja wa waenezaji wa 'Israiliyyat’ ambaye kamwe alikuwa si mtu aliyechukiwa mbele yao. Ilikuwa ni kwa sababu ya elimu yake ya Tawrati kwamba watu walimwambia awaeleze tabia ya Mtume mmoja.13
Kile kilichotokea, katika mtizamo wetu, ni hivi: "Hadith za Mtume s.a.w.w. kwa ujumla hazikuandikwa hadi kufikia mwishoni mwa karne ya 1 A.H./7 A.D., ingawaje baadhi ya Sahaba walipendelea uandikaji wake na vile vile wengineo walikuwa na vibao vilivyokuwa vimeandikwa Hadith. Uandikaji wa hapa na pale ulianza kutokea katika karne ya 2 A.H. /8 A.D. , lakini ukusanyaji na uandikaji wa Hadith ulianza kwa nguvu mwishoni mwa karne ya 2 A.H./8 A.D., na hasa katika karne ya 3A.H./8-9A.D. Ingawaje inawezekana kuwa wakusanyaji walikuwa na mkusanyiko usio na utaratibu (kwani walikuwa wakikusanya chochote kile walichokipata bila ya kufanyia utafiti juu ya usahihi wake au ni nani aliyeileza), ni dhahiri kuwa wingi wa Hadith walizozikusanya zilikuwa zimetokana na kutamkwa tu.
Ushahidi uliopo ni kwamba uandishi mdogo kabisa-ambao hauwezi kulinganishwa na kazi kubwa ya ukusanyaji wa Hadith-zipo dalili kidogo kabisa zenye kuonyesha kuwa kulikuwepo na uandishi wa Hadith katika karne ya 2 A.H./8 A.D. Hivyo inaweza kusemwa kuwa Hadith hazikuwa zikiandikwa kwa kipindi kirefu na zilikuwa zikisemwa kwa midomo tu bila ya kuandikwa katika kipindi hicho. 14
- 1. Abu Zuhrah, al-‘Imam Zayd, 167.
- 2. Jami’ bayan al - ‘ilm ,II,82, Fath al-Bari , Muqaddimah, uk.4; Taqyid al-'ilm ,57; Ta'rikh al-fiqh al-Islami, 88.
- 3. Adwa’ ‘ala al-Sunnat al-Muhammadiyyah, 51.
- 4. Adwa’ ‘ala al-Sunnat al-Muhammadiyyah, 51.
- 5. Jami’ bayan al - ‘ilm , I, 81
- 6. Jami’ bayan al - ‘ilm , I, 82
- 7. Taqyid al-'ilm , 57
- 8. Abjad al-‘ulum, 110.
- 9. Al-Sahih min sirat al-Nabi al-‘a’dham (s.a.w.w.), I, 27, maelezo.
- 10. Taqyid al-'ilm , 51; Jami’ bayan al - ‘ilm , I, 64; Kanz al-‘ummal, V, 239
- 11. Sunan al-Darimi , I, 124; Taqyid al-'ilm , 56; tazama Taqyid al-'ilm , 57,
Tadhkirat al-huffadh , I, 296 - 12. Taqyid al-'ilm , 61; Jami’ bayan al - ‘ilm , I, 65; Husn al-tanbih, 92
- 13. Tazama Buhuth ma’a Ahl al-Sunnah wal Salafiyyah, 97; kwa ajili ya habari kutoka Talmud, tazama al-Tafkir al-dini ‘ind al-Yahud, uk. 79, kutoka Talmud Hittin, 60/ bab Tamura, bab 14; Qasim ibn Muhammad ibn Abi Bakr anasema: “Idadi ya ahadith iliongezeka katika zama za utawala wa ‘Umar. Yeye aliwaamrisha kuzileta na akazichoma moto.
Tazama Tabaqat al-Kubra , V, 188 - 14. Gharib al - hadith , IV, 282