Uharamisho Wa Kusimulia Hadith
Sisi tumezungumzia hapo awali vile uandishi wa Hadith ulivyoharamishwa na kile kilichotokea athari yake. Mazungumzo yetu hapa yanaelezea ukweli kuwa kama vile historia inavyoelezea, baadhi ya Sahaba walijaribu hata kuzuia kusimulia Hadith kwa mdomo pia. Wao walizuia uandishi wa Hadith kwa kisingizio cha Qur’an kulindwa, na wao waliharamisha kusimulia kwa mdomo pia kwa kisingizio cha kuwazuia watu wasitilie mkazo mambo mengine isipokuwa Qur’an tu, kama kwamba azma yao ilikuwa kuifanya Hadith ionekane kuwa ni kitu kisicho na maana wala kisipewe umuhimu wowote na vyovyote vile, kuna uwezekano wa kuwapo kwa sababu za kisiasa katika hatua hizo.
Qurzah ibn Ka'ab anasema:
Sisi tuliondoka Madinah kwenda Iraq. Umar alitusindikiza hadi kufikia nje ya Mji. Yeye alituambia, "Je, mnajua kwa nini mimi nimekuja nanyi hadi hapa?" Sisi tulijibu, "Labda umekuja kutuaga, kwani sisi ni Sahaba wa Mtume s.a.w.w." Umar alisema, "Mimi nimekuja kuwaambieni kuwa nyie muuweke mkazo wenu zaidi juu ya Qur’an na kwamba musizisimulie Hadith za Mtume s.a.w.w. kwa zaidi, ila kidogo tu. Sasa endeleeni kwani mimi ni mshiriki wenu katika swala hili."
Qurzah anaongezea katika riwaya nyingine:
Pale mimi nilikuwa nimeketi miongoni mwa watu waliokuwa wakisimuliana Hadith. Ilionekana kuwa mimi ndiye niliyekuwa nikizijua Hadith nyingi kuliko wao. Lakini nilijikalisha kimya pale nilipokumbuka ushauri wa 'Umar.'
Katika mapokezi ya al-Dhahabi, yeye anaripotiwa akiwa amesema, wakati wao waliponiomba kusimulia Hadith za Mtume s.a.w.w., mimi niliwaambia kuwa Umar ameniharamishia kufanya hivyo. 1
Vile vile imeripotiwa kuwa wakati Khalifa alipomtuma Abu Musa al-Ashari kwenda Iraq, alimwambia, "Usiwashughulishe watu katika Hadith. Mimi ni mshiriki wako katika swala hili." 2
Riwaya hizi zinatuonyesha majaribio yaliyofanywa katika kuzuia kuenezwa kwa Hadith za Mtume s.a.w.w., si pekee kwa maandishi tu. Ibn Asakir anaripoti haya yaliyosemwa na Ibrahim ibn Abd Rahman:
Haki ya Mungu, Umar hakufariki kabla ya kuwaita Sahaba wa Mtume s.a.w.w. kama vile Hudhayfah ibn al-Yamani, Abu al-Darda, Abu Dhar, Aqabah ibn Amir na ......Yeye aliwaambia: "Je ni Hadith zipi hizi ambazo nyinyi mnazieneza pembe zote?" Wao walimjibu, "Je, wewe unatuzuia kusimulia Hadith?"
Kwa mujibu wa riwaya iliyorikodiwa na al-Tabarani, Ibrahim ibn Abd Rahman alikuwa na uzoefu wa kusema:
"Umar alimwita Abdallah ibn Mas'ud, Mas'ud al-Ansari na Abu Darda. Yeye aliwaambia, "Je, ni Hadith zipi hizo za Mtume s.a.w.w. ambazo mnazisimulia kwa kupita kiasi?" Na kuanzia hapo aliwazuia Madinah tu hadi kufariki kwake (waliwekwa chini ya kifungo)." 3
Ni dhahiri kuwa watu hawa walikuwa ni miongoni mwa watu maarufu kabisa katika Sahaba wa Mtume s.a.w.w., Ahl al-Sunnah hawana shaka juu ya watu kama hawa juu ya usadikifu wa watu kama Hudhayfah, Abu Darda na Ibn Mas'ud hadi kuwa alipomtuma Iraq, aliwaandikia, "Mimi nimependelea faida yenu kuliko hasara yangu kwa kuwatumieni Ibn Mas'ud kwenu nyinyi." 4
Ibn Sazm amechukizwa mno na shutuma hiyo dhidi ya Khalifa, lakini, hakuthubutu kushutumu tendo la Khalifa, yeye anazusha mashaka kuhusu ukweli wa riwaya. Yeye anasema: "Hadith hii ni mursal, na yenye mashaka kwa sababu ya mmoja wa watu katika mfululizo wa wasimulizi ni Shu'bah. Hivyo haiwezi kuchukuliwa kuwa ni uthibitisho." Lakini sisi twaelewa kuwa Hadith hiyo ipo imepokelewa kwa kupitia mifululizo ya wasimulizi. Zaidi ya hayo, Ibn Haytham, katika Majma al-Zawaid (Vol. 1 uk. 147), baada ya kuitenga Hadith hii ni sahihi, ameandika: "Msemo huo wa Umar ni sahihi (inayosadikiwa) na ipo imesimuliwa kwa kupitia mifululizo ya masimulizi mengi."
Hata hivyo, Ibn Hazm, wakati akiichambua Hadith, anasema:
Riwayah hii kwa uthibitisho ni uongo; kwani aliyesema itatubidi tuseme kuwa amejitoa katika mipaka ya Islam, kwa sababu jitihada zake zililenga katika kufunika na kupuuzia Hadith za Mtume wa Allah swt. 5
Mwandishi wa al-Sunnah qabl al-Tadwin anaandika:
Ukweli kuwa kuwekwa mahabusu (habs) kwa Sahaba (katika Madinah) kulitokana na wao kusimulia Hadith za Mtume s.a.w.w., sivyo sahihi. Kwa sababu Abu Hurayrah alikuwa mmoja wa watu wa aina hiyo, na ambapo yeye hakuwekwa mahabusu (na Umar). 6
Habari ya hapo juu si ya kweli, kwa sababu Abu Hurayrah mwenyewe alikuwa ni mmoja wa wale waliopigiwa marufuku na Umar katika kusimulia Hadith za Mtume s.a.w.w. Abu Hurayrah alitekeleza maamrisho ya Umar na hivyo aliweza kusimulia Hadith kidogo mno katika uhai wa Umar.
Imekamilika, wal hamdu-lillah.
- 1. al-Rihlah fi talab al-hadith, 89; tazama Fath al-Bari , I, 158, 159; Jami’bayan al - ‘ilm , I, 111, 113, al-Majruhun, I, 57; Tadhkirat al-huffadh , I, 108, al-Muhaddith al-fadhl, 215, 223
- 2. Abu Hanifah, 59
- 3. Kashf al - ‘astar al-zunun, II, 1908
- 4. Sunan al-Darimi , 79; Hayat al -Sahabah ,, III, 257, 258; Jami’ bayan al–‘ilm, II, 120; Tabaqat al-Kubra,VI, 7; mustadrak al-Hakim, I, 152 (al-Hakim asema:‘Hadith hii ni isahihi nzima kwa nzima kutokana na sanad’); Tadhkirat al-huffadh ,I,7; Ta'rikh al-fiqh al-Islami, 41.
- 5. Al-Bidaya wa al-nihayah, VIII, 107; mwandishi asema, “Hadith hii ya‘Umar ni mashuhuri”.
- 6. Hayat al -Sahabah ,III, 272; Kanz al-‘ummal, V, 239