read

Aya 1-11

Maana

Kila mwenye kusema: Lailaha illa llah Muhammadur rasulullah (Hapana mola isipokuwa Mwenyezi Mungu, Muhammad ni Mtume wa Mwenyezi Mungu) atastahiki yale yanayowastahiki waislamu, naye atawapatia wanayostahiki waislamu kutoka kwake. Hiyo ni katika maisha ya hapa duniani. Ama maisha ya akhera, hiyo peke yake haitatosha kumpatia thawabu za Mwenyezi Mungu na radhi zake mpaka awe amekusanya mambo yafutayo:-

1. Hakika wamefaulu waumini ambao ni wanyenyekevu katika Swala zao.

Kunyenyekea ni kinyume cha kiburi na kujikweza. Mwenyezi Mungu anasema: "Wananyeyekea kwa udhalili." (42:45). Kunyenyekea katika Swala ni natija ya kuwa na yakini na Mwenyezi Mungu na kuhofia adhabu yake. Swala bila ya yakini si chochote wala lolote. Imam Ali (a.s.) anasema: "Kulala na yakini ni bora kuliko kuswali na shaka."

2. Na ambao hujiepusha na mambo ya upuuzi.
Mumin wa kweli upuuzi na batili haimfanyi aache Mwenyezi Mungu. Imam Ali (a.s.) anasema: "Hakika mawalii wa Mungu ni wale ambao wanaangalia ndani ya dunia wakati watu wanapoangalia nje yake na wanajishugulisha na ya baadaye wakati watu wakijishughulisha na ya sasa." Akasema tena: "Mwenye kuangalia kasoro zake hatajishugulisha na kasoro za wengine."

3. Na ambao kwa Zaka ni watendaji.

Angalia tuliyoyaandika kuhusu Zaka katika Juz. 3 (2:272-274).

4. Na ambao wanazilinda tupu zao isipokuwa kwa wake zao au kwa iliyowamiliki mikono yao ya kuume. Kwani si wenye kulaumiwa.

Makusudio ya iliyowamiliki mikono yao ya kuume ni wajakazi. Hivi sasa hawako tena. Zina ni miongoni mwa madhambi makubwa na uchafu katika sharia ya kiislamu. Kwenye jamii yoyote zina ikienea basi inabomoka.

Lakini anayetaka kinyume cha hayo basi hao ndio wapetukao mipaka.

Yaani atakayetaka kumwingilia asiyekuwa mkewe au mjakazi, basi atakuwa amepituka mipaka ya Mwenyez Mungu na anastahiki ghadhabu yake na adhabu yake.

Unaweza kuuliza kuwa je, kauli yake Mwenyezi Mungu: "Lakini anayetaka kinyume cha haya" inachanganya kujitoa manii kwa mkono kunakojulikana kwa jina la punyeto (Kujipuli)?

Jibu, ndio. Kwa sababu Mwenyezi Mungu amehalalisha mke na mjakazi na akaharamisha kinyume cha hivyo kwa namna yoyote ile itakayokuwa. Ndio maana mafakihi wote wakaharamisha, isipokuwa Hanafi na Hambali wamesema inaruhusiwa kwa yule anayehofia kuingia kwenye haramu. Tazama Ruhulbayan cha Ismail Haqqiy.

Imam Jafar Sadiq (a.s.) aliulizwa kuhusu punyeto (Kujipuli). Akasema ni dhambi kubwa. Muulizaji akamuuliza iko wapi kwenye Kitabu cha Mwenyezi Mungu ewe mtoto wa Mtume wa Mwenyezi Mungu? Imam akasoma: Lakini anayetaka kinyume cha hayo… Kisha akasema: Ponyeto ni kinyume cha hayo.

5. Na wale ambao wanachunga amana zao na ahadi zao.

Tumezungumzia kwa ufafanuzi kuhusu amana na wajibu wa utekelezaji wake katika Juz. 5 (4:58). Ahadi ni kila aliloliamrisha Mwenyezi Mungu na kulikataza. Mwenyezi Mungu anasema: "Na tekelezeni ahadi yangu. Nitatekeleza ahadi yenu" Juz. 1(2: 40).

6. Na ambao Swala zao wanazihifadhi wakidumu nazo kwa wakati wake.

Tumefafanua kuhusu Swala katika Juz. 1 (2:3, 110).

Hao ndio warithi, watakaorithi Firdausi, wadumu humo.

Mumin yoyote atakayekuwa na mambo hayo yaliyotajwa, basi atastahiki Pepo, kama anavyostahiki mrithi mirathi kutoka kwa jamaa yake wa karibu. Wapi na wapi urithi wa dunia unaoisha na mabalaa yake na urithi wa akhera na neema zake za kudumu!

وَلَقَدْ خَلَقْنَا الْإِنْسَانَ مِنْ سُلَالَةٍ مِنْ طِينٍ {12}

Na hakika tumemuumba mtu kutokana na asili ya udongo.

ثُمَّ جَعَلْنَاهُ نُطْفَةً فِي قَرَارٍ مَكِينٍ {13}

Kisha tukamjaalia awe tone katika makao yaliyo makini.

ثُمَّ خَلَقْنَا النُّطْفَةَ عَلَقَةً فَخَلَقْنَا الْعَلَقَةَ مُضْغَةً فَخَلَقْنَا الْمُضْغَةَ عِظَامًا فَكَسَوْنَا الْعِظَامَ لَحْمًا ثُمَّ أَنْشَأْنَاهُ خَلْقًا آخَرَ ۚ فَتَبَارَكَ اللَّهُ أَحْسَنُ الْخَالِقِينَ {14}

Kisha tukaumba tone kuwa pande la damu na tukaliumba pande la damu kuwa pande la nyama, na pande la nyama tukaliumba kuwa mifupa na mifupa tukaivika nyama. Basi ametukuka Mwenyezi Mungu mbora wa waumbaji.

ثُمَّ إِنَّكُمْ بَعْدَ ذَٰلِكَ لَمَيِّتُونَ {15}

Kisha hakika nyinyi baada ya hayo ni maiti.

ثُمَّ إِنَّكُمْ يَوْمَ الْقِيَامَةِ تُبْعَثُونَ {16}

Kisha hakika nyinyi siku ya Kiyama mtafufuliwa.

وَلَقَدْ خَلَقْنَا فَوْقَكُمْ سَبْعَ طَرَائِقَ وَمَا كُنَّا عَنِ الْخَلْقِ غَافِلِينَ {17}

Hakika tumeumba juu yenu tabaka saba. Nasi katika kuumba si wenye kughafilika.